UN na Usalama wa Raia toeni taarifa

John Mnyika

JF-Expert Member
Jun 16, 2006
712
1,240
Haja ya kutaka tamko rasmi toka UN inatokana na taarifa zinazoendelea kusambaa kwa njia ya mtandao zinazoonyesha kwamba tayari vikao rasmi vya UN vimeshaijadili taarifa hiyo. Baadhi ya taarifa hizo ni pamoja na Ripoti Maalumu(Special Report) ya jarida la kimataifa la Africa Confidential ya hivi karibuni(inayopatikana kupitia www.africa-confidential.com) taarifa hizo zinaonyesha kwamba Baraza la Usalama limekaa Novemba 20; Novemba 25 na mwezi Disemba kupitia taarifa husika.

Ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kutoa tamko hivi sasa kwa kuwa mwanzoni mwa mwezi Disemba UN kupitia ofisi yake ya Tanzania ulieleza kwamba taarifa ya timu ya wataalamu haikuwa rasmi mpaka baada ya kujadiliwa na vikao hivyo; sasa kama tayari vikao hivyo vimeshakaa kama inavyodokezwa katika vyanzo hivyo vya kimataifa ni wakati wa umoja wa mataifa kutoa tamko rasmi kuhusu maudhui ya ripoti yake rasmi.

Pia kwa kuwa serikali ya Tanzania ilitoa kauli kupitia Balozi wetu wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Dr Augustine Mahiga kwamba ingewasilisha taarifa ya ufafanuzi wake kuhusu tuhuma zilizomo kwenye ripoti hiyo zinazoitaja taasisi za Tanzania na baadhi ya watanzania; ni wakati muafaka wa ripoti hiyo ya Serikali ya Tanzania kama imeshawasilishwa nayo kuwekwa hadharani na Wizara ya Mambo ya Nje au UN.

Wakati huo huo: Wizara ya Usalama wa Raia inapaswa kutoa kauli kuhusu hatua zilizofikiwa katika kumchunguza Bande Ndagundi na wengine wanaotajwa kwenye mtandao wa biashara ya silaha wanaoishi Tanzania.

Itakumbukwa kwamba mwanzoni mwa mwezi Disemba Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Jeshi hilo(IGP) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) walitoa kauli kwamba jeshi hilo limeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu wote waliotuhumiwa kwenye ripoti hiyo.

Mwezi unaelekea kumalizika bila taarifa kutolewa kuhusu kuendelea kwa uchunguzi huo; pamoja na kuwa masuala ya uchunguzi mengine ni ya siri, lakini hatua za mchakato wa uchunguzi ni jambo la kawaida kuelezwa ili kujenga imani kwa umma na wadau wote kwamba serikali imezipa uzito unaostahili tuhuma hizi kwa lengo la kusafisha taswira ya taifa letu kwa wananchi wake na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa kuwa linafanya uchunguzi wa kina lakini baada ya hapo uchunguzi unaishia hewani ama matokeo yake hayawekwi hadharani. Mathalani mpaka sasa Jeshi la Polisi halijaeleza hatua zilizochukuliwa katika sakata ya Dr Wilbroad Slaa(Mb) kuwekewa vinasa sauti chumbani kwake; tuhuma za kushambuliwa kiharahamia viongozi wa CHADEMA zinazohusisha viongozi wa CCM katika chaguzi ndogo za Kiteto, Busanda na Biharamulo; nk.

Chanzo na maelezo zaidi: http://mnyika.blogspot.com/2009/12/un-na-usalama-wa-raia-toeni-taarifa.html
 
Back
Top Bottom