Umuhimu wa kuwasiliana na mwanao.

Umuhimu wa kuwasiliana na mwanao.

Sema Tanzania

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2016
Posts
251
Reaction score
466
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa moja ya mambo muhimu zaidi katika malezi ni fursa ya watu wazima (wazazi au walezi) kuzungumza na kuwasikiliza watoto. Kupitia mwingiliano huu wa kila siku, watoto na watu wazima wanaweza kuendeleza mahusiano ambayo huwasaidia watoto kujifunza kuhusu maisha yao wenyewe na kuing'amua vyema dunia inayowazunguka.

Wazazi na walezi wanaowalea watoto wanao-wajibu wa kujenga na kudumisha mahusiano mema na ya kutegemeana kati yao na watoto wanaowalea. Jambo la muhumu kabisa ni kuhakikisha mawasiliano chanya yapo na yanadumishwa baina yao. Huna haja ya kusubiri migogoro eti ndipo uzungumze na mtoto. Watafiti wanaamini kwamba iwapo wazazi watadumisha mawasiliano na mahusiano ya karibu na watoto wao, hapatakuwa na haja ya kutumia nguvu nyingi kumjenga mtoto kuwa mwenye nidhamu bila hata ya shuruti!

Mafanikio katika kuwasiliana na mtoto huhitaji kuzingatia umri kwani kila hatua ya ukuaji inatoa fursa na uelewa tofauti. Kuelewa jinsi watoto wa umri husika huwasiliana inakupa wasaa wewe kutoa ujumbe mwepesi na stahiki ili ueleweke vyema.

Tenga muda kusimuliana hadithi na mtoto. Watoto wote hupenda kusikia na kusimulia hadithi. Tumia fursa hii kuwasimulia watoto hadithi za chimbuko la familia yao na familia tandaa. Hii itawapa nafasi ya kujivunia utu wao na mafanikio yaliyopatikana toka vizazi na zizazi vya mababu zao. Uzoefu huu unaweza kuwajenga watoto kuwa jasiri katika kupambana na changamoto za kila siku kwani wanajua babu zao waliweza. Mtoto pia atajenga mapenzi ya dhati na ndugu zake wa familia tandaa na kuwachukulia kama watu muhimu katika maisha yake na historia yake.

Elewa hisia za mtoto. Hii itakupa fursa ya ukaribu wa pekee kwani mtoto atakutegemea hata pale anapokuwa na jambo zito moyoni utaling'amua. Vilevile fursa hii itakupa wasaa wa kumweleza mwanao kwamba siku hazifanani. Leo anafurahi lakini kesho anaweza kuamka na msongo wa mawazo na kwamba hayo ndiyo malimwengu. Tafiti zinaonyesha kwamba watoto wanaokulia katika familia ambazo hisia zao zinajengwa namna hii huwa na wepesi katika masomo na mara nyingi hufanikiwa maishani. Yaani hata changamoto za maishani wanaweza kuzikabili kwani walijengewa uelewa mapema.

Jenga tabia ya kuandikiana jumbe za maneno kwenye karatasi. Hii inakupa fursa ya kujua kama mwanao anaweza kusoma na vilevile utapata kuuona mwandiko wake. Njia hii pia itakusaidia kumjengea uwezo katika kupangilia mawazo yake katika maandishi. Unaweza kuanza na ujumbe mdogo tu, mfano, ‘Naomba tukatembee’, n.k.

Mwisho tunahimiza uwe na subira katika maongezi na mwanao. Mvumilie na jitahidi usiwe mwongeaji sana bali toa na jenga fursa za kuwa msikilizaji. Namna hii unaweza kusikia mambo mengi ikiwa ni pamoja vitendo vya kikatili anavyoweza kuwa anafanyiwa pasi yeye mwenyewe kujua. Mawasiliano ni fursa adimu ya kumlinda mtoto dhidi ya udhalimu wa walimwengu wa dunia ya sasa.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.
 
Ok... Japo imekaa kisasa(Kizungu) zaidi..
Hii itaanzs fanya kazi kwa % kubwa kwa vizazi vilivyo zaliwa 2000s ns kuendelea
 
Ok... Japo imekaa kisasa(Kizungu) zaidi..
Hii itaanzs fanya kazi kwa % kubwa kwa vizazi vilivyo zaliwa 2000s ns kuendelea
Habari, Asante kwa kutuandikia. Unayoyasema ni ya kweli na ni kutokana na ukweli kwamba miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto kubwa sana ya malezi na ndiyo maana hata sisi kama wadau wa watoto kazi yetu kubwa ni kuwakumbusha wazazi ama walezi juu ya suala mtambuka la malezi kwa watoto.
 
Tamaduni zetu zinazuia sana hii ya mzazi kuongea na mwanae. Mfano huu ushauri utaonwa na % chache ya wenye access na JF which means itakua ni kundi la watu wachache.

Over time pengine hii tamaduni itafutika as sisi wazazi wapya tumekua influenced na elimu kidogo, internet kidogo, movie kidogo so Mungu tusaidie.
 
Hakika, umezungumza vizuri mno. Endelea kuelimika kupitia makala zetu za kila siku hapa mtandaoni
 
Nilitaka niijue hii org ya "sema Tanzania " kwa kiufupi samaha kwa kua nje ya mada
Kama zilivyo taasisi nyingine, Sema Tanzania hufanya kazi na watoto, kwa kuwawezesha watoto kupaza sauti zao katika nyanja mtambuka, Kupitia huduma ya simu kwa mtoto, namba 116, Sema Tanzania husikiliza na kuyafanyia kazi yale yote yamhusuyo mtoto, kubwa likiwa ukatili dhidi yao, Unyanyasaji na Udhalilishaji. Kupitia simulizi na visa vya kweli vya watoto, Sema Tanzania huandika makala kadha wa kadha zihusuzo mambo mtawalia, SimuliziZa116 pamoja na #Malezi, Wazazi, walezi pamoja na jamii hupata kufahamishwa na kukumbushwa juu ya wajibu wao. Tupigie namba 116 sasa bure kutoka mitandao yate nchini ili tuzungumze!
 
Hawa watoto huwa mnawafikiaje au kupitia simu tu ?
 
Hawa watoto huwa mnawafikiaje au kupitia simu tu ?
Zipo programu mbalimbali zinazotekelezwa nchini kwa minajili ya kuwafikia watoto walio mjini na vijijini. Tafadhali, Usisite kutembelea tovuti yetu na kurasa zetu za mitandao ya kijamii kujionea haya.
 
Back
Top Bottom