SoC02 Umuhimu wa kutunza mazingira na kupanda miti

Stories of Change - 2022 Competition

Bigabo Ezra

New Member
Sep 3, 2022
3
1
Mazingira yanayozunguka yana umuhimu kwetu kama binadamu katika maisha yetu ya kila siku. Mazingira hayo yapo katika makundi mawili tofauti. Kuna mazingira asilia ambayo hayajatengenezwa na binadamu ambayo yanajumuisha miti, mimea na maua ya asili, wanyama pori, ndege pori, vijito vya maji na mengineyo na pia kuna mazingira yaliyoundwa na kutengenezwa na binadamu kama nyumba, barabara, madaraja, vifaa vya moto na mengineyo. Mazingira haya yote yanapaswa kuwekwa safi na salama ili tuendelee kuishi maisha ya kuridhisha.

Athari za kutotunza mazingira

Changamoto mbalimbali hujitokeza iwapo kumetokea uzembe katika utunzaji wa mazingira na madhara yake ni makubwa.

Mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa ambapo misimu ya joto na baridi hupishana na kusababisha mvua kubwa sana au kidogo sana. Mvua kubwa huharibu mazao na mimea na kubomoa madaraja ya maji na pia kuharibu miundombinu ya umeme na barabara. Mvua kunyesha kidogo hupelekea joto na kukosekana kwa maji ya kutumia katika umwagiliaji na kunywesha mifugo. Hivyo afya ya mifugo na mimea huzorota na kufa. Mapato ya wakulima na wafugaji yanakuwa madogo.

Ukataji wa miti bila mpangilio hupelekea kukosekana kwa hewa safi ya Oksijeni ambayo inatengenezwa na miti pamoja na mimea ituzungukayo. Binadamu yupo katika hatari ya kupata magonjwa ya kupumua ikiwa hali ya hewa ina carbon dioxide na haya magonjwa yanachangia watu kupoteza maisha.

Maafa au majanga ya njaa na ukame ni mmoja ya athari ya kutojali mazingira na kukata miti kupitiliza. Mvua hukosekana na matokeo yake mazao kukosa maji na kufa au kunyauka. Janga la njaa hujitokeza hivyo ni muhimu sana kutunza mazingira.

Wanyama pori katika mazingira na watuzungukao wapo hatarini kupotea au kuhamia katika hifadhi za nchi nyingine ili kupata chakula na maji. Hifadhi zetu zina hatari ya kupungukiwa vivutio. Hatari nyingine ni uharibifu unaofanywa na hawa wanyama katika jitihada ya kupata malisho kama tembo kuingia makazi ya watu na kuharibu mashamba. Wanyama hawa wanapaswa kuwekewa mazingira salama kwa chakula na maji.

Kama mazingira hayatunzwi ipasavyo, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza. Magonjwa haya ni pamoja na malaria kutokana na mbu wengi kuzaliana katika maji yaliotuama na maeneo ya majitaka na uchafu. Kipindupindu ni kiashiria kingine kwamba mazingira yanayozunguka sio salama. Kipindupindu hujitokeza mvua za masika zikiwa nyingi na matunzo ya usafi wa misingi, madaraja na mashimo ya taka yanapokosekana. Magonjwa haya huleta vifo katika jamii.

Upepo mkali ni mmoja ya changamoto katika jamii ambapo kama upepo haujadhibitiwa na miti na mimea, upepo unaovuma kwa kasi unaweza kuharibu nyumba na makazi ya masoko na kusitisha kazi za kila siku. Upepo usipodhibitiwa, unaweza kueneza magonjwa ya kupumua kama mafua.

Watu wanafanya uhalifu na wizi wa mali asilia kama hazijathibitiwa na kulindwa. Uhalifu hujitokeza na mali huporwa na wageni wasiojulikana. Watu huchukulia kama fursa na kuanza kukata miti katika mapori, kupora meno ya tembo au ndovu na kukata mkaa.

Serikali inaweza kushindwa kutimiza ahadi zake kwa jamii iwapo itatumia mapato mengi katika matengenezo ya miundombinu kama umeme, barabara na madaraja yalioharibika kutokana na utunzaji mbovu wa mazingira. Gharama za kufanya matengenezo inasitisha mipango ya maendeleo mengine kama chanjo kwa watoto na madawa hospitalini.

Umuhimu wa mazingira kwa binadamu

Mazingira yana mchango mkubwa katika maisha ya binadamu na yanapaswa kupewa kipaumbele na kila mmoja wetu kwa kuyatunza vizuri na kuyaendeleza.

Mazingira hutupatia nishati za kuwasha kwa matumizi ya ndani ya nyumba na pia viwandani. Viwanda vingi hutumia nishati ya makaa katika kazi za uzalishaji kama njia mbadala ya umeme. Watu wa kawaida pia hutumia miti kama kuni na mkaa kwa matumizi mbalimbali.

Mazingira yanachangia kutupatia vifaa vya ujenzi wa majengo ya umma. Vitu vingi vya ujenzi vinatoka katika mazingira yetu kama mawe, mchanga, maji, na miti au magogo ambayo hutumika katika kutengeneza nyumba, barabara na misingi ya madaraja.

Mazingira huchangia kutupatia hali ya hewa safi na kutoa hewa chafu kutoka viwandani. Hewa ya moshi kutokana na magari na viwanda hutumiwa na mimea pamoja na miti na kurejesha hewa safi kwa matumizi ya watu na wanyama.

Mazingira yanahifadhi wanyama na ndege na ni makazi ya viumbe wengine. Viumbe wanajihifadhi katika mazingira mbalimbali kama maporini, katika vyanzo vya maji na maeneo mengine. Hifadhi hizo zinapaswa kupewa kipaumbele na kutunzwa.

Mazingira yetu yanahusika kikubwa katika zoezi la kutengeneza mvua na hatimaye maji kupatikana. Mvua hutengenezwa kutokana na miti na husaidia katika kilimo na kwa matumizi ya umwagiliaji. Mvua zinasaidia pia kumwagilia mashamba ya wakulima.

Mazingira ni mmoja kati ya vivutio vya utalii na yanachangia kuongezeka kwa pato la taifa kupitia vivutio vya hifadhi kama Serengeti, manyara na ngorongoro. Utunzaji wa mazingira unaweza kutuletea wageni kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi.

Kutunza mazingira na kupanda miti kunasaidia kuhifadhi ardhi na kusitisha mmomonyoko wa udongo unaotokana na mvua kunyesha kupitiliza. Kupanda miti husaidia kupunguza maafa yatokanayo na upepo mkali unaoweza kuangusha majengo na mazao mashambani.

Jinsi au mbinu za kutunza mazingira

Jamii inapaswa kuelekeza nguvu zake zote kuhakikisha mazingira yanayoizunguka ni safi na salama. Huduma ya matunzo kwa mazingira ni muhimu ili kupata manufaa ya kimaendeleo na afya njema kupitia mazingira yetu.

Zoezi la kupanda miti linapaswa kupewa kipaumbele ambapo jamii husika ni lazima kujishughulisha na upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ndani ya jamii. Miti inamanufaa ya kupunguza hewa chafu , kupunguza upepo ambao huleta uharibifu na pia miti inapunguza joto litokanalo na jua.

Zoezi la umwagiliaji linapaswa kuhamasishwa na ni kipaumbele katika utunzaji wa mazingira. Miti, maua na mimea asilia inahitaji huduma ya maji ili ikue ipasavyo. Umwagiliaji wa miti unahitajika misimu ya joto na jua. Mimea inaweza kunyauka na kufa kwa kukosa maji. Zoezi la umwagiliaji
lipewe kipaumbele.

Kutumia njia mbadala za nishati ili tulinde mazingira. Nishati zinazo tumika majumbani na viwandani zinapaswa kubadilishwa hasa matumizi ya mkaa na kuni. Njia mbadala ni pamoja na gesi, biogas, na matumizi ya solar systems. Kutumia njia mbadala za nishati itasaidia kikubwa kutunza mazingira.

Elimu ya utunzaji wa mazingira inapaswa kutolewa shuleni na katika jamii. Uhamasishaji juu ya umuhimu wa kutunza mazingira unaofanywa unapaswa kupewa kipaumbele. Elimu ya utunzaji wa mazingira unaweza kufikia jamii kupitia vyombo
vya habari, magazeti na ofisi za mitaa na vijiji.

Sheria za usalama wa mazingira lazima zipewe kipaumbele. Jamii inapaswa kutambua na kuheshimu sheria za kutunza mazingira na umuhimu wa mazingira. Jamii inapaswa kuhusishwa katika zoezi la kuweka sheria za kulinda mazingira yanayoizunguka. Jamii inapaswa kutambua hatua zitakazochukuliwa kama itajihusisha na uharibifu wa mazingira.

Jamii inapaswa kujishughulisha na miradi ambayo ni rafiki kwa mazingira na kuepukana na miradi ambayo inaharibu mazingira. Miradi ya kutengeneza mabwawa, ufugaji wa nyuki na samaki na kilimo cha umwagiliaji huongeza tija katika kutunza mazingira na ustawi wa mazingira. Miradi inayoharibu mazingira inapaswa kusitishwa.

Jamii inapaswa kutambua na kuthamini siku ya mazingira duniani na kuzingatia mafunzo yanayotolewa
katika jamii yetu. Siku ya mazingira duniani inatukumbusha kujali mazingira pamoja na viumbe wengine watuzungukao.

Usafi wa mazingira ni muhimu sana katika jamii bili kuondoa na kuepukana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko. Mazingira yanapaswa kuwa katika hali ya usafi wakati wote ili yavutie wageni. Mazingira safi hupunguza magonjwa na hutupatia hewa safi ya kupumua.

Jamii inapaswa kutambua uwepo wa viumbe wengine katika mazingira yanayoizunguka. Viumbe hao ni pamoja na wanyama kama ndege, tembo, nyati, vifaru na wengine hupatikana katika mabwawa kama samaki. Jamii inapaswa kutambua umuhimu wa viumbe vyote na kuwapa matunzo ipasavyo ili waendelee kupatikana na kuzaliana. Matibabu na chakula kwa hawa viumbe yanahitajika pia.

Miradi mikubwa ya maendeleo ya serikali lazima izingatie umuhimu wa mazingira kama ujenzi wa barabara na reli zinazopitia maporini na maeneo yenye miti mingi. Miradi inayoweza kuleta uharibifu katika mazingira na athari zake kufikia jamii lazima zisitishwe ili kuweza kulinda mazingira ya binadamu.

Jamii inayojihusisha na biashara zisizo halali kama kuchoma mkaa na uwindaji wa wanyama pori bila vibali ni lazima udhibitiwe na vyombo husika. Matumizi ya mali asilia lazima yadhibitiwe ili raia wazingatie umuhimu wa kutunza mazingira na mali asilia.
 
Back
Top Bottom