Ummy Mwalimu: Wenye Bima za NHIF Walipiwe Vifaa vya Usikivu

kirerenya

JF-Expert Member
Aug 27, 2013
1,696
2,251
bima.jpg

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha wanachama wa mfuko huo wanapata matibabu ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa kutumia kadi zao.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Saalam alipokuwa akizindua rasmi matibabu hayo yatakayokuwa yanatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili badala ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Waziri Ummy amesema kuwa uanzishwaji wa matibabu hayo nchini ni moja kati ya mikakati iliyopangwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha nchi inapunguza gharama za matibabu zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.

”Leo tunazindua rasmi matibabu haya hivyo kuanzia sasa ni mwisho kupeleka wagonjwa wa aina hii katika hospitali za nje ya nchi na ili kuhakikisha watu wengi wanapata matibabu haya wananchi wote wenye bima za NHIF watapatiwa matibabu hayo hasa kusaidiwa katika ununuzi wa kifaa husika,” alisema Mhe. Ummy.

Mhe Ummy aliongeza kuwa mbali na wagonjwa wenye bima za NHIF pia aliitaka hospitali kuzingatia Sera ya Msamaha ambapo wagonjwa wasio na uwezo wafanyiwe utaratibu wa kugharamiwa angalau gharama za kununulia vifaa hivyo.

Alisema ili kufanikisha matibabu hayo wizara italazimika kutenga bajeti ya kuwanunulia wananchi vifaa kwa lengo la kuipunguzia hospitali gharama za uendeshaji.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Mseru alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa matibabu hayo hospitali ilianza na uboreshaji wa miundo mbinu, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na kuwapeleka wataalam nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo ili kuhakikisha matibabu hayo yanatolewa kwa ubora na uhakika.

“Hospitali imetumia jumla ya shilingi bilioni 13.6 ambazo zimetumika katika kukarabati na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka vyumba 13 hadi kufikia vyumba 20, Kuongeza wodi za wagonjwa mahututi kutoka vitanda 21 hadi vitanda 40, kwa nyakati tofauti hospitali imepeleka wataalamu kupata mafunzo pamoja na kununua vifaa tiba,” alisema Prof.Mseru.

Prof. Mseru aliongeza kuwa nje ya nchi matibabu hayo yanagharimu kati ya shilingi milioni 80 hadi milioni 100 wakati kwa Tanzania matibabu hayo yatagharimu shilingi milioni 36 ambapo takribani shilingi milioni 31 zinatumika kununulia kifaa na kwamba matibabu yake hapa nchini ni ya gharama ndogo ukilinganisha na nchi za nje.

Prof. Mseru alifafanua kuwa fedha hizo ni majumuisho ya mkopo wa shilingi bilioni 7.2 kutoka NHIF, shilingi milioni 600 kutoka kwa wafadhili, ruzuku kutoka Serikalini shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni 2.8 kutoka vyanzo vya vyanzo vya mapato vya ya hospitali.

Akiwawakilisha wananchi waliowahi kupatiwa matibabu hayo na Serikali nje ya nchi, Hilda Bohela amesema kuwa kuanzishwa kwa matibabu hayo nchini ni jambo la kujivunia kwani litapunguza gharama na usumbufu ambao mgonjwa anaupata wakati akiwa katika mchakato wa kufika nchi za nje kwa ajili ya matibabu.

“Napenda kutoa rai kwa wataalam wa magonjwa haya kutoa elimu kwa wazazi ili waweze kuachana na mila potofu za kuamini kuwa mtoto akichelewa kuongea au kusikia kuwa ni tabia ya kurithi kutoka kwa ndugu zake. Pia nawashauri wazazi wenzangu kuwa makini kuwachunguza watoto wakiwa bado wadogo na kuwapeleka hospitali ili waweze kupatiwa matibabu kwa haraka,” alisema Bi. Hilda.

Matibabu hayo ndiyo ya kwanza kwa Afrika Mashariki kufanyika katika Hospitali ya Umma. Kwa mwaka huu, Hospitali ya Taifa Muhimbili imejipanga kutibu jumla ya wagonjwa 24 kwa awamu sita.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
 
Jambo jema sana hili maana hii bima ya afya bado imebana vitu vingi sana.
 
Ahsanteni!

Ngoja nifiche kilichopo moyoni kwanza nitakilipua baadae.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom