Umma ukiungana, si rahisi kuushinda/Raia Mwema, Oktoba 23, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,241
BARAZANI

Umma ukiungana, si rahisi kuushinda

Na Ahmed Rajab

TANGU Alhamisi iliyopita hali ya mambo imechafuka nchini Lebanon. Si shuwari tena. Maelfu kwa maelfu ya wakazi wa huko wamekuwa wakijitokeza barabarani tangu siku hiyo katika mji mkuu Beirut na katika miji mingine wakiandamana dhidi ya serikali ya waziri mkuu Saad al Hariri.

Waandamanaji wamekuwa wakimtaka Hariri ajiuzulu pamoja na serikali yake ya mseto. Serikali hiyo imeundwa kutoka vyama tofauti na mapande mbali mbali ya kidini na ya madhehebu tofauti. Kwa bahati mbaya, siasa za Lebanon zimeingiliwa na udini kiasi cha kuuingiza udini ndani ya mfumo wa utawala wa nchi kwa upande wa ugawaji wa madaraka.

Kwa mfano, kwa mujibu wa Mapatano ya Kitaifa ya 1943, Rais wa taifa hilo lazima awe Mkristo wa madhehebu ya Maronite, waziri mkuu lazima awe Mwislamu wa madhehebu ya Sunni, Spika wa bunge anatakiwa awe Mwislamu wa madhehebu ya Shi’a na kaimu wa Spika wa bunge pamoja na kaimu wa waziri mkuu lazima wawe Wakristo wa madhehebu ya Greek Orthodox.

Katika hali hiyo, inakuwa taabu kuzijadili siasa za nchi hiyo bila ya kuitaja mivutano ya kidini.

Maandamano yaliyoibuka tangu Alhamisi iliyopita yamewajumuisha wafuasi wa vyama tofauti vya kisiasa na waumini wa dini na madhehebu tofauti za kidini. Hii ni mara ya mwanzo katika historia ya Lebanon maandamano ya aina hiyo kushuhudiwa nchini humo. Umeibua mshikamano mkubwa wa wananchi walioziweka kando tofauti zao za kiitikadi, za kisiasa na kidini, na badala yake wameungana kuwa na msimamo mmoja wa kuitaka serikali ijiuzulu.

Maandamano hayo yanayoitwa mitaani kuwa ni “Intifada” ya kodi, yalichochewa na hatua ya serikali ya kuongeza kodi zilizokuwa zimepangwa zitozwe mafuta ya petroli, tumbaku pamoja na simu za mitandaoni kama vile zile za kupitia WhatsApp. Mara tu yalipoanza maandamano ya kulalamika kuhusu nyongeza hizo za kodi, serikali iliifuta mipango yake ya kutoza kodi zaidi kwa huduma na bidhaa nilizozitaja.

Lebanon ina wakazi milioni sita na wengi wao wamekuwa wakilalamika kwamba hali zao za maisha zinazidi kudidimia. Wanasema wamechoka na wanasiasa wao.

Rais Michel Aoun amesema kwamba ingawa madai ya waandamanaji ni ya msingi hata hivyo hakubaliani nao kwamba wanasiasa wote ni mafisadi. Aoun ambaye ni Mkristo wa madhehebu ya Maronite ni kiongozi wa chama cha al Tayyar al Watani al Hurr (Vuguvugu Huru la Kizalendo).

Ughaibuni kuna Walebanon wanaokaribia milioni 14 wanaoishi katika nchi mbali mbali duniani. Nao pia wanasema wamechoka na kwamba lazima pafanywe mageuzi ya kiuchumi nchini humo.

Hao Walebanon wa ughaibuni nao pia, Jumamosi na Jumapili, waliandamana waliko kuipinga serikali yao na wanasiasa wao. Mitandao ya kijamii ilifanya kazi ya kuwahamasisha na kuwajumuisha.

Jumamosi waliandamana London (Uingereza), Madrid (Uhispania), Montreal (Canada) na katika miji ya Marekani ya Washington, Los Angeles, New York na San Francisco.

Jumapili waliandamana Lagos (Nigeria), Brussels (Ubelgiji), Paris (Ufaransa), Sydney (Australia), Mexico City (Mexico) na Tampa, Florida (Marekani).

Wamezilenga hasira zao kupinga nyongeza za kodi na zaidi dhidi ya ufisadi ambao wanasema umezagaa katika ngazi mbali mbali za serikali.

Miongoni mwa wanaolaumiwa kwa ufisadi mkubwa na kwa kuitumbukiza nchi hiyo katika nakama ya kiuchumi ni wapenzi wawili wa mataifa ya Magharibi Riyad Salameh, gavana wa Benki Kuu ya Lebanon (Banque du Liban) tangu 1993, ambaye ni Mkristo wa madhehebu ya Maronite, na Fu’ad Sanyura, aliyewahi kuwa waziri wa fedha na pia waziri mkuu.

Sanyura aliushika kwa mara ya mwanzo wadhifa wa uwaziri mkuu mnamo 2005 na akauacha 2009 akimpisha Saad Hariri, mtoto wa waziri mkuu aliyeuawa Rafik Hariri. Wote ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni na ni wanachama wa chama cha Tayyar al Mustaqbal (Vuguvugu la Mustakbali). Saad Hariri ameushika uongozi wa chama hicho baada ya kuuawa baba yake, Rafik, na Sanyura ndiye anayewaongoza wabunge wa chama hicho.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa za Lebanon wanawaona wote wawili, Salameh na Sanyura, kuwa ni vibaraka wa Marekani.

Mishale ya lawama amerushiwa pia Nabih Berri, spika wa bunge la Lebanon. Berri, ambaye ni Shi’a, ana historia yenye kuvutia. Alizaliwa 1938 huko Bo, mji ulio wa pili kwa ukubwa nchini Sierra Leone, ambako wazazi wake walikuwa wakiishi. Ni mji wenye wakazi waliogawika nusu kwa nusu baina ya Waislamu na Wakristo.

Nakumbuka wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon, vilivyodumu kwa miaka 19 hadi 1990, tukifuatilizia sana na kuziandika harakati za Berri katika vita hivyo na juhudi zake za kukusanya michango ya fedha iliyokuwa ikitolewa na Mashi’a wenye asili ya Lebanon waliokuwa wakiishi Sierra Leone na katika nchi nyingine za Afrika ya Magharibi.

Berri amekuwa akikiongoza chama cha Harakat Amal (Vuguvugu la Matumaini) tangu 1980 alipochaguliwa kiongozi wake. Kwa sasa Harakat Amal ndicho chama cha Kishi’a chenye wabunge wengi (16) kuliko cha Hizbullah chenye wabunge 13. Wakati mmoja katika siku za vita vya wenyewe kwa wenyewe vyama hivyo viwili vya Kishi’a vya Amal na Hizbullah vilitwangana kwa risasi.

Berri alizidi kupata umaarufu alipowaongoza wanamgambo waliokuwa wamesimama kidete kupinga uvamizi wa jeshi la Israel kusini mwa Lebanon na katika Bonde la Beqaa. Kwa muda mrefu amekuwa akishirikiana na Walid Jumblatt, kiongozi wa chama cha Kisoshalisti cha PSP.

Siku mbili hizi shujaa huyo aliyekuwa akiwapigania wanyonge wa Kishi’a amekuwa akilaumiwa kwa ufisadi hata na waandamanaji wa mji wa Kusini wa Tyre wenye Mashi’a wengi.

Shujaa mwengine wa Lebanon, Sayyed Hassan Nasrallah, kiongozi wa chama cha Hizbullah, hakunusurika na lawama za baadhi ya waandamanaji. Nasrallah alimejitolea kuwa mbele kupambana na uchokozi wa Israel nchini humo na ni mwenye kuwatetea wanyonge.

Jumatatu waziri mkuu Hariri na mawaziri wake walikubaliana hatua kadhaa za kuwatuliza waandamanaji. Miongoni mwa mengine serikali imeamua kwamba badala ya kuwatoza wananchi kodi zaidi sasa mabenki na mashirika ya bima ndiyo yatayoongezewa kodi. Mishahara ya mawaziri, watumishi wakuu wa serikali, pamoja na ya mawaziri wastaafu na ya viongozi wengine wastaafu itapunguzwa kwa asilimia hamsini.

Mawaziri wa chama cha Kikristo cha Al Quwwat al Libnaniya (Majeshi ya Kilebanon), kinachoongozwa na Samir Geagea, walijitoa kwenye serikali Jumamosi. Geagea amekuwa akihoji kwamba serikali lazima ijiuzulu.

Hadi sasa ninapoyaandika haya haielekei kwamba Hariri ameweza kuwatuliza waandamanaji. Wameshikilia uzi wao ule ule wa kuitaka serikali ijiuzulu na badala yake wateuliwe majaji huru kuiendesha nchi kwa muda.

Wapo pia wenye kutaka viongozi wote wa kisiasa wakamatwe na waweze kizuizini na walazimishwe kuzirejeshea fedha wanazotuhumiwa kuziiba serikalini.

Shirika la Fedha la Mataifa (IMF) limeitaka serikali ichukue hatua kali zaidi za kubana matumizi na kuongeza kodi na ushuru juu ya mafuta ya petroli. Serikali ikikubali kuchukua hatua hizo itazidi kuupalilia moto mgogoro uliopo sasa.

Lebanon ni muhimu sana kwa eneo zima la Mashariki ya Kati licha ya udogo wa ardhi yake kulinganishwa na nchi nyingine katika ukanda huo. Ikiripuka ikawa haitawaliki eneo zima huenda likaripuka.

Nchi inatawaliwa vibaya, uchumi wake umeporomoka, miundombinu yake haifanyi kazi sawasawa na mingine inakosekana. La muhimu ni kwamba umma umesimama imara kudai mageuzi. Kwa sasa dalili zinaonesha kwamba kwa kuwa wamoja wanaweza wakafanikiwa.


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
 
Back
Top Bottom