Umati wamlaki Lipumba, Dom wazidi kutimka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Umati wamlaki Lipumba, Dom wazidi kutimka

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Mar 13, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 13, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  Umati wa wafuasi wa Chama cha CUF umejitokeza kumpokea Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipowasili akitokea Marekani ambapo aliongoza jopo la wataalamu wa uchumi lkutoka nchi mbalimbali.  Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akipokewa kwa kishindo jijini Dar es Salaam jana, wanachama 828 wametangaza kukihama chama hicho kwa madai kuwa kimepoteza mvuto.

  Profesa Lipumba aliwasili nchini jana saa 9.30 alasiri akitokea nchini Mrekani na kupokewa na maelfu ya wanachama wafuasi wa CUF kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa shamrashamra na kila aina ya mbwembwe.

  Profesa Lipumba alikuwa Marekani kwa zaidi ya miezi mitano mfululizo kwa kazi maalum baada ya kuchaguliwa na Shirika la NED la Marekani kuwa miongoni mwa wachumi 16 duniani wanaoshughulikia kuporomoka kwa uchumi wa dunia.

  Wafuasi hao waliongozwa katika mapokezi hayo na viongozi wakuu wa kitaifa wa CUF, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

  Viongozi wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Julius Mtatiro, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, Salim Bimani. Mapokezi hayo yalihudhuriwa pia na viongozi

  wa kidini, akiwamo Amiri wa Shura ya Maimamu Tanzania, Mussa Kundecha, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Baraza Kuu), Sheikh

  Ramadhan Sanze na Katibu wa Kamati ya Siasa ya Baraza hilo, Sheikh Ponda Issa, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa nchini.

  Hata hivyo, mapokezi hayo yaliingia dosari baada ya wafuasi 16 wa CUF kujeruhiwa na baadhi yao kukimbizwa hospitali kufuatia gari aina ya FUSO walilokuwa wamepanda kupata ajali.

  Pia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa akitokea safarini, alishangiliwa na wafuasi wa CUF waliofurika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kusubiri kumpokea Profesa Lipumba.

  Dk. Slaa alishangiliwa na wafuasi hao baada ya kupeperusha bendera ya CUF aliyoichukua kutoka kwa mmoja wa wafuasi hao muda mfupi baada ya kutua uwanjani hapo. Haikuweza kufahamika mara moja nchi au mkoa aliokuwa ametokea.

  Wafuasi hao wakiwa wamevalia mavazi ya rangi za CUF na fulana zenye picha za Profesa Lipumba, huku wakipeperusha bendera za chama hicho, walianza kumiminika uwanjani hapo kuanzia saa 4 asubuhi.

  Baadhi walifika uwanjani hapo wakiwa kwenye ma-FUSO, mabasi makubwa na madogo, magari madogo, Bajaj, pikipiki na wengine baiskeli, zilizokuwa zimepambwa picha za Profesa za Lipumba.

  Hadi kufika saa 9 alasiri, barabara zote za kuingia na kutoka uwanjani hapo kuanzia kwenye kona ya kuingia katika barabara hiyo kutoka Barabara ya Nyerere pamoja na eneo lote la nje ya uwanja huo, zilikuwa zimetawaliwa na wafuasi hao wa CUF.

  Muda wote watu waliokuwa katika eneo lote la nje ya uwanja huo wakisubiri kumpokea Profesa Lipumba, walipata burudani ya ngoma na nyimbo za kizazi kipya zilizopamba shughuli ya mapokezi hayo.
  Hata hivyo, watu waliokuwa wamejipanga nje ya uzio wa jengo la watu mashuhuri uwanjani hapo kwa ajili ya

  kusalimiana na Profesa Lipumba, walivuruga utaratibu huo baada ya kuondoka katika maeneo walikokuwa wamejipanga na kumvamia, huku kila mmoja akitaka kumpa mkono.
  Hali hiyo ilisababisha vurugu kubwa na hivyo kuwafanya askari polisi, maofisa usalama wa taifa, walinzi wa Maalim Seif

  na wale wa CUF, maarufu kama ‘Blue Guard’, kulazimika kuvunja utaratibu huo na kumrudisha Profesa Lipumba ndani ya eneo la jengo hilo.

  Akiwa ndani ya eneo hilo, Profesa Lipumba alizungumza na waandishi wa habari wachache. Waandishi wengi, wakiwamo wapiga picha wa vyombo mbalimbali vya habari walizuiwa na walinzi wa uwanja huo pamoja na wale wa CUF kuingia ndani ya eneo hilo kwa ajili kumsikiliza Profesa Lipumba.

  Akizungumza na waandishi hao wachache, Profesa Lipumba alisema alikwenda Marekani kufanya utafiti wa mambo ya kufanya ili kuweza kujenga nchi yenye demokrasia na itakayokuwa na uwezo wa uchumi utakaoongeza ajira na kuondoa umaskini ulioktihiri nchini.

  “Tumepata uhuru miaka 50 iliyopita, lakini mpaka hivi sasa tatizo la umaskini bado kubwa nchini,” alisema Profesa Lipumba ambaye aliahidi kuzungumza kwa kina na waandishi wa habari leo.

  Mara baada ya kuzungumza na waandishi hao wachache, Profesa Lipumba alipanda gari maalum aliloandaliwa ambalo lilisukumwa na wafuasi na wakereketwa wa CUF kutoka uwanja wa ndege hadi Ubungo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari barabarani.

  Msafara wake uliosindikizwa na msururu mrefu wa magari, Bajaj, pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu walikuwa wakikimbia mchakamchaka, ulipita katika Barabara za Nyerere, Mandela, Morogoro, Msimbazi na Uhuru, huku kiongozi huyo akisalimiana na wananchi wa Dar es Salaam.

  WANAVYUO 828 WAJIENGUA

  Wanachama 828 wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Vyuo vikuu vya mkoa wa Dodoma, wameamua kukihama Chama hicho kwa madai kuwa kimekosa mvuto.

  Waliokihama ni 46 kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana (Sjut), 723 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), 32 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na wanachama 27 wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP).

  Akitoa tamko hilo kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CUF tawi la SJUT, Mohamed Abdullah Rashid, alisema wameamua kukihama chama hicho kutokana na kukosa mvuto kwa wanachama wake kila kona ya nchi.

  Hata hivyo, Wanachama hao hawakueleza wanahamia chama gani, lakini walidai kuwa endapo hawatapata sehemu ya kuhamia watabaki kuwa wanaharakati wa kupingana na ubaguzi na ukandamizaji wa kisiasa au kiuchumi.

  Alisema wao kama wasomi, wameona kuna sababu ya kukihama chama hicho kutokana na viongozi wa juu wa chama hicho kukiuka madhumuni ya chama.

  Alizitaja sababu nyingine kuwa ni kupoteza kura 336 katika Jimbo la Uzini hali iliyoonyesha chama hicho kimepoteza mvuto kwa wanachama wake kiasi cha kupitwa na Chama cha Demokrasia na Maendele (Chadema). Nyingine ni kauli

  chafu za Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismal Jussa Ladhu, kwamba kushindwa katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi Jimbo la Uzini kulitokana na wapiga kura wengi kuwa Wakristo.

  “Bwana Jussa amekiuka ibara ya 8 ya katiba ya CUFna katiba ya 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayomtaka kiongozi kuwa ni mtu mwenye kuheshimu watu na uhuru wao wa kibinadamu, serikali halali za nchi, Bunge

  au Baraza la Wawakilishi na Mahakama zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ya nchi,” alisema.
  Pia alizitaja sababu nyingine kuwa ni kukosa wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki na kushindwa kusimamisha mgombea.

  Wanafunzi hao walisema wapo pamoja na wanachama wa chama hicho waliofukuzwa, akiwemo Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na kudai kuwa wanawaunga mkono katika kipindi hiki kigumu.

  “Tuna amini kuwa kipindi hichi ni kigumu, lakini ni kipindi cha ushindi na tuna waunga mkono katika utekelezaji wa demokrasia ya kweli katika kufanikisha kupinga ubaguzi, udhalilishaji, ukandamizaji wa kisiasa na kiuchumi ili kuliletea maendeleo endelevu taifa letu,” alisema.
  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Daudi Mchambuzi

  Daudi Mchambuzi JF-Expert Member

  #2
  Mar 13, 2012
  Joined: Nov 25, 2010
  Messages: 31,797
  Likes Received: 36,826
  Trophy Points: 280
  CUF ni maiti iliyoanza kuoza.
  Lipumba kaja kuzika mzoga huu.
   
Loading...