Ndio mara yako ya kwanza kusikia chuo kikuu kimezingirwa na ukuta?
Kikwete kuichangishia fedha UDSM
19th January 2011
Rais Jakaya Kikwete , ameandaa hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kituo cha wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), itakayofanyika Ikulu kesho.
Ujenzi wa kituo hicho unalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi wanapojisomea katika maktaba.
Akizungumza na wanahabari jana, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema Rais Kikwete atahamasisha uchangiaji wa ujenzi wa kituo hicho na miundombinu yake.
Alisema wengine wanaotarajiwa kuchangia ujenzi huo, ni wahitimu wa zamani wa UDSM pamoja na wadau wa chuo hicho.
"Ukiwa nje utawaona wanafunzi wengi wanasoma kwenye miti na nyasi kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa maktaba ya kujisomea japokuwa kuna wengine wanapenda kukaa kwenye miti kwa ajili ya kupunga upepo," alisema Profesa Mukandala.
Alisema kwa sasa wahadhiri na wafanyakazi wa chuo wameweza kuchanga na kupata Sh. bilioni 1.34 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho unaotarajiwa kugharimu Sh. bilioni 17.
Profesa Mukandala alisema kukamilika kwa kituo hicho, kutachukua wastani wa wanafunzi 5,000.
Kituo hicho kitakuwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kutolea huduma muhimu kwa wanafunzi, yakiwamo ya kusomea na kupumzika wakati wa mchana, kupata huduma za internet, posta na benki, ofisi za vyama na makundi mbalimbali ya wanafunzi na maktaba kwa ajili ya wanafunzi wa shahada za juu.
Alisema UDSM ina mpango wa kujenga mabweni ya wanafunzi kwa awamu tatu, yatagharimu Sh. bilioni 18 na kwamba, watalipatia ufumbuzi tatizo la wanafunzi kupanga nje ya chuo.
CHANZO: NIPASHE