Ukurasa wa 570: Kazi na ajira

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Watu wengi wamekuwa wakichanganya kazi na ajira. Utasikia mtu akisema sina kazi ya kufanya, akimaanisha hajaajiriwa. Hii siyo sawa. Wacha tuliweke hili sawa ili tujue ni kipi hasa tunachohitaji.

Ajira ni pale unapoambiwa nini ufanye. Mtu anakuajiri na kukupa majukumu yako ya kazi, ambayo unatakiwa kuyatekeleza. Hapo una ajira. Una mtu wa kukuambia ni kipi cha kufanya.

Kazi ni kile kitu unachochagua kufanya, unafanya hata kama hakuna anayekuambia ufanye. Unafanya kwa sababu unajua kuna watu wanahitaji au kuna mabadiliko unayoweza kuyaleta.

Ajira inatoka kwa mwingine, kazi inatoka ndani yako. Kwa kufanya ajira unatekeleza malengo na ndoto za wengine. Kwa kufanya kazi unatoa mchango wako kwa wengine.

Unaweza kuwa na ajira na ukafanya kazi pia, na hapa ndipo unapojitofautisha na waajiriwa wengine, na kujiweka kwenye nafasi ya kupata mafanikio makubwa. Kazi hii unaweza kuifanya kwa kuweka ubora zaidi kwenye ile ajira yako, au ukawa na kitu cha pembeni unachofanya.

Usiseme huna kazi kwa sababu hujaajiriwa, chagua kitu unachoweza kufanya ambacho kina mchango kwenye maisha ya wengine.

Usiridhike tu na ajira uliyonayo, bali angalia namna ya kuongeza thamani zaidi kwa kwenda hatua ya ziada, kufanya zaidi ya unavyopangiwa kufanya. Pia fanya kitu nje ya ajira yako, hata kama ni kwa hatua ndogo.

SOMA; JINSI YA KUANZISHA NA KUKUZA BIASHARA YAKO UKIWA BADO UMEAJIRIWA.

Kwa vyovyote vile hakikisha una kazi, iwe umeajiriwa au la. Hakikisha una kazi unayofanya, kazi inayotoka ndani yako, kazi inayoongeza thamani kwenye maisha ya wengine, na hapo ndipo mafanikio yako yalipo.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
 
Back
Top Bottom