Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Katika kitabu cha Marko 4:35-41, Biblia inaelezea tukio la Yesu kutuliza dhoruba iliyotishia kusambaratisha mtumbwi waliokuwa wakisafiria.
Biblia inasema siku hiyo, ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke, twende ng’ambo ya pili.” Wakawaacha wale watu wakaingia katika ile mashua ambamo Yesu alikuwa amekaa. Pia palikuwa na mashua nyingine.
Pakatokea dhoruba kali, mawimbi yakaipiga ile mashua waliyokuwa wakivukia, ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa amelala akiegemea mto sehemu ya nyuma kwenye ile mashua. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kwamba tuna zama?’ Akaamka, akaukemea ule upepo, akaiambia ile bahari, “Kaa kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari.
Ni wazi kwamba mambo si shwari ndani ya Chadema, kwani kuna dhoruba kubwa inakipiga chama hicho tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho, ambao ulimweka madarakani Tundu Lissu kama mwenyekiti na John Heche kama Makamu Mwenyekiti.
Inaonekana aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kundi lake hawakuyapokea matokeo hayo kwa moyo mkunjufu. Hiyo ni kutokana na kinachoendelea sasa, ambapo watu wa kundi lake sasa wameunda kundi la G55 wakikosoa uongozi uliopo madarakani.
Januari 22, 2025 baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho, Mbowe alihutubia mkutano mkuu, ambapo alisisitiza makundi ya uchaguzi kuvunjwa na uongozi mpya kupoinya majeraha ya uchaguzi.
Baada ya hapo uongozi mpya pamoja na mengine uliunda kamati ya maridhiano iliyoongozwa na baadhi ya wazee wa chama hicho, lengo likiwa ni kupatanisha makundi yaliyokuwa yakisigana wakati wa uchaguzi.
Lakini kinachoendelea sasa ni kinyume, kwani G55 wameibuka wakipinga kila kinachofanywa na uongozi mpya. Wamepinga utekelezaji wa kampeni ya Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi.
Soma pia: Waraka wa G55
Licha ya uongozi mpya kuwaita watia nia Makao makuu ya Chadema Mei 3 kujadili mwenendo wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, G55 hawakufika, badala yake waliandika waraka kwa Katibu mkuu wa chama hicho na baadaye wakaitisha mkutano na waandishi wa habari wakipinga kuzuiliwa kugombea.
Wakati huu ambao Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amekamatwa na kufunguliwa kesi ikiwamo ya uhaini, wakati chama kikiendelea na kampeni ya Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi, G55 wano wanaendelea kupambana na uongozi mpya na sasa wanajiondoa Chadema kwa makundi tofauti kila uchwao.
Ieleweke kwamba G55 wamegawanyika katika makundi mawili; kundi la kwanza linatangaza kujitoa Chadema lakini hawasemi wanakwenda wapi. Kundi la pili ni wale wasiojitoa Chadema lakini wanaendelea kuchokoa uongozi uliopo madarakani.
Miongoni mwa waliopo kundi la pili ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome ambaye amekishitaki chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa akilalamikia uteuzi wa baadhi ya viongozi uliofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu na kuridhiwa na kikao cha Baraza Kuu Januari 22.
Mchome anadai kuwa kikao hicho hakikuwa kimetimiza akidi na kwamba baadhi ya waliopiga kura hawakuwa wajumbe halali. Tayari Msajili amesharidhia malalamiko hayo na ametangaza kuwatangua viongozi hao akiwamo Katibu Mkuu, John Mnyika.
Katika kundi hilo, yupo pia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho upande wa Zanzibar, Said Issa Khamis na wenzake wawili ambao wamekishitaki chama hicho Mahakama Kuu wakidai kuwa hakitendi haki katika mgawanyo wa mali. Hivyo wanaiomba Mahakama isimamishe shughuli za chama hadi kesi hiyo itakaposikilizwa.
Kwa hiyo utaona kundi la kwanza linatangaza kujitoa Chadema na huenda kuna mikakati na ahadi nono huko waendako na kundi la pili linabaki ili kuendelea kuchokonoa uongozi uliopo. Ilimradi wakiache chama hicho kikiwa kimekufa kabisa.
Ukimya wa Mbowe
Ni wazi kwamba chokochoko hizi zote zinafanywa na makada na viongozi wa Chadema waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe katika uchaguzi. Kwa kuwa walishindwa uchaguzi, kuna kila daklili kwamba bado wanaumia, hivyo wanaona bora wakose wote.
Tangu uchaguzi wa Chadema ulipokwisha, Mbowe ambaye ni mjumbe wa kamati kuu, hajaonekana kwenye kikao chochote kilichoitishwa na uongozi mpya. Pia hajazungumza lolote kuhusu vurugu zinazoendelea ndani ya chama.
Je, yeye ndiye anayewatuma G55 kufanya wanayofanya? Kama hawatumi, kwa nini hawakemei au hawatuizi? Maana hao wote walimuunga mkono wakati wa uchaguzi.
Soma pia: Ukimya wa Mbowe
Maana kama aliridhia kushindwa uchaguzi, ilitarajiwa awe wa kwanza kuvunja kundi lake na kuendelea kukijenga chama alichokiongoza kwa miaka 20.
Kipindi hiki ambacho chama kimeingia kwenye dhoruba kali, mawimbi yanakipiga ndani na nje, ilitarajiwa Mbowe aamshwe akemee upepo (G55) ili chama kitulie. Kama vile Yesu alivyoamshwa na wanafunzi wake, yeye aliamka na kuukemea upepo na hali ikawa shwari.
Ukimya wa Mbowe nao ni jibu; kwamba huenda ama anaratibu mvurugano unaoendelea au ameona kama kukosa wakose wote. Kufanya kosa sio lazima ulifanye moja kwa moja; hata kuzuia kosa lisifanyike nako ni kufanya kosa. Mbowe anaweza kabisa kuwazuia G55 wasifanye wanachokifanya, lakini yeye amechagua kukaa kimya, maana yake ameridhia dhoruba iendelee ndani ya chama hicho.
Wapo wanaodai kuwa ukimya wa Mbowe una kishindo kikubwa na kwamba anajipanga kurejea kwenye ulingo wa siasa kivingine, hivyo kwa sasa anatuma vijana wake kumwandalia njia ya kupita.
Wengine wamekwenda mbali wakisema, Mbowe anajutia kuruhusu uchaguzi ulio huru na wa haki uliowawezesha Lissu na Heche kushinda. Watu hao wanadai kuwa, lawama zinatoka kwa baadhi ya matajiri waliokuwa wakikifadhili chama hicho kupitia kwa Mbowe na yeye mwenyewe amewakubalia hivyo, anatafuta ‘plan B’ ambayo sasa ataonyesha mabavu yake akishindana na Chadema aliyoijenga mwenyewe.
Kama atafanikiwa kwa njia hiyo, bado atakuwa na mtihani mwingine wa kukubalika kwa wananchi. Wengi wanahisi kuna fedha chafu zimewekwa kufanikisha mkakati huu, lengo likiwa ni kudumaza upinzani.
Hiyo ni kutokana na mani aliyoijenga ndani ya Chadema kwa zaidi yamiaka 33 aliyotumika ndani ya chama hicho. Anapaswa kuilinda heshima hiyo kwa kukubaliana na matokeo yaliyowaweka wenzake madarakani.