Ukilipenda, Tumia

Jeho

JF-Expert Member
Jul 2, 2011
5,053
5,515
Kwa muda mrefu nimekuwa nikitamani kushirikisha jamii katika mambo mazuri ambayo nimejifunza na mengine yakitoka katika uzoefu binafsi. Tamanio lenyewe linatokana na idea ya inspiration/motivation speeches inayofanywa na watu katika mataifa ya nje.

Lengo ni kukuza uelewa na ufahamu wa wanajamii, hii hasa ikiwa kwa wale wasiojua (ukizingatia, elimu ni kwa wale wasiojua).

Na nimekuwa nikitamani kushirikisha jamii kupitia runinga, lakini kutokana na uhaba wa pesa, kwangu mimi imeshindikana. Lakini kushindikana kwangu hakumaanishi ishindikane na kwa wengine.

Naamini kuna wenye vipaji na uwezo wa kupata pesa za kufanikisha njozi hii, nitafurahi endapo siku moja nitakutana na video yenye maudhui niliyotaka kufikisha kwa jamii.

Kwa kuanza, nilipanga kuanza na masimulizi mafupi lakini yakiwa na ujumbe ndani yake. Nitaambatisha baadhi ya masimulizi hayo mahali hapa. Na baadaye, kadri watu wangekuwa wanaongezeka katika kufunguka kiakili, ningeenda hatua ya mbele zaidi.

Naamini, kuna mtu fulani anayesoma ujumbe huu na anaweza kufanya kazi hii, tena yaweza kuwa kwa ubora mkubwa zaidi, chukua wazo hili na ulifanyie kazi, mimi nimejitahidi kadri inavyowezekana lakini nimeshindwa.
 
Baadhi ya masimulizi hayo ni haya yafuatayo.

KIOO
•Siku moja waajiriwa wote walifika ofisini na wakaona tangazo kubwa kwenye mlango likiwa limeandikwa “jana, mtu aliyekuwa anazuia mafanikio yako ndani ya kampuni hii, amefariki. Tunakukaribisha kuungana nasi katika msiba ndani ya chumba cha mazoezi”
•Mwanzoni kila mmoja alipatwa uchungu wa kuondokewa na mfanyakazi mwenzao, lakini baada ya muda wakaanza kuingiwa na udadisi wa kumjua mtu aliyekuwa anazuia mafanikio ya waajiriwa wenzake na ya kampuni kwa ujumla.
•Msisimko ndani ya chumba cha mazoezi ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, walinzi waliagizwa kudhibiti mkusanyiko uliokuwamo ndani ya chumba hicho.
•Kadri watu walivyozidi kulikaribia jeneza, ndivyo msisimko ulivyoongezeka.
•Kila mmoja alifikiri, ni mtu gani huyu aliyekuwa akizuia mafanikio yangu? Afadhali amefariki.
•Mmoja baada ya mwingine, waajiriwa hawa wenye furaha walikaribia kwenye jeneza, na kila mmoja alipoangalia ndani ya jeneza, ghafla alikosa cha kusema.
•Na baada ya kutazama, kila mmoja alisimama karibu ya jeneza akiwa kimya na aliyetishika, kana kwamba kuna mtu aliyeshika pande za ndani abisa za roho zao.
•Kulikuwa na kioo ndani ya jeneza: kila mmoja aliyetazama ndani yake, aliishia kuiona sura yake, kulikuwa na maandishi pia kando ya kioo yaliyosomeka hivi “kuna mtu mmoja tu anayeweza kuweka kikomo cha mafanikio yako: ni wewe, wewe ni mtu pekee anayeweza kufanya mapinduzi makubwa ya maisha yako. Wewe ni mtu pekee unayeweza kuleta furaha, kujitambua na mafanikio. Wewe ni mtu pekee unayeweza kujisaidia binafsi.
•Maisha yako hayabadiliki pale bosi anapobadilika, marafiki wanapobadilika, mpenzi anapobadilika, kampuni yako inapobadilika.
•Maisha yako hubadilika wakati WEWE unapobadilika, wakati unapokwenda mbele ya Imani zako kinzani, unapotambua kwamba wewe pekee ndiye mwenye jukumu kwa maisha yako. Mahusiano ya maana unayoweza kuwa nayo, ni yale uliyonayo juu yako mwenyewe.
•fundisho
•Dunia ni kama kioo: huakisi mawazo yako unayoyaamini na kukurudishia matokeo yaiyo sawa na Imani yako. Dunia na uhalisia wako ni sawa na kioo kilicholala ndani ya jeneza, kinachoonesha kifo cha kila mtu kiroho katika uwezo wa kuhisi na kutengeneza furaha na mafanikio yake.
•Ni namna unavyokabiriana na maisha ndiyo huleta utofauti.
 
AKAUNTI YA BENKI
•Fikiria kuna benki, ambayo huweka salio la sh 86,400 kila siku asubuhi, na haitunzi salio la siku iliyopita, na huruhusiwi kutunza salio lolote lile, na kila jioni, salio la siku husika uliloshindwa kulitumia. Ungefanyaje? Ungechukua salio lote, bila shaka ungefanya hivyo!
•Vizuri, kila mmoja ana akaunti ya benki ya namna hiyo. Jina lake ni muda. Kila asubuhi, muda hukuwekea salio la sekunde 86,400, na kila usiku, sekunde zote huondoshwa, na huhesabika kama zilizopotea.
•Sekunde yoyote uliyoshindwa kuiwekeza kwa lengo zuri, haibebwi kwa siku nyingine. Kila siku akaunti mpya kwa ajili yako hufunguliwa, na kila usiku, kumbukumbu za akaunti yako huchomwa moto, ukishindwa kutumia salio ulilowekewa siku hiyo, hasara inakuwa kwako
•Hakuna kurudi nyuma, hakuna kutoa salio kwa ajili ya kesho.
•Hivyo hakuna muda unaozidi au usiotosha. Matumizi ya muda huamuliwa na wewe peke yako na si mwingine.
•Kamwe hakuna kesi ya kukosa muda wa kufanya mambo, lakini kesi ni kama tunataka kufanya jambo au la.
 
MAMBO YA MUHIMU MAISHANI
•Profesa wa falsafa, alisimama mbele ya wanafunzi wake akiwa na baadhi ya vitu juu ya meza mbele yake. Kipindi kilipoanza, pasipo kusema neno lolote alitwaa ndoo kubwa na alianza kujaza mawe makubwa ndani ya ndoo hiyo.
•Kisha aliwauliza wanafunzi wake kama ndoo imejaa. Wote waliitikia kuwa imejaa.
•Kwa hiyo, profesa alitwaa boksi lililojaa changarawe na kumimina ndani ya ndoo. Aliitikisa ile ndoo, na changarawe zikapenya katika nafasi wazi katikati ya mawe
•Kwa mara nyingine, aliwauliza wanafunzi kama ndoo hiyo imejaa, walikubali kwa pamoja kuwa imejaa.
•Profesa alitwaa boksi lenye mchanga na kumimina mchanga huo ndani ya ndoo. Mchanga ulipenya katika nafasi wazi iliyosalia kati ya mawe na changarawe
•Aliuliza kwa mara nyingine kama ndoo ile imejaa, wanafunzi waliitika kwa ndiyo yenye mashaka.
•“sasa” alisema profesa, ninahitaji mtambue kuwa ndoo hii inawakilisha maisha yenu. Mawe ni mambo ya muhimu, familia, mpenzi wako, afya yako, watoto wako, kiasi kwamba, kama mambo mengine yote yangepotea, hayo yangebaki na bado ungekuwa umejaa.
•Changarawe ni mambo mengine ambayo nayo yana umuhimu wake kama vile, kazi yako, nyumba yako, gari lako. Na mchanga ni kila kitu kilichobaki, mambo madogo madogo”
•“kama kwanza utaweka mchanga ndani ya ndoo”, profesa aliendelea, “kusingekuwa na nafasi kwa changarawe au kwa mawe. Vivyo ndivyo ilivyo pia katika maisha yako. Kama ukitumia muda wako wote na nguvu zako kuandama mambo madogo madogo, hautakuwa na nafasi kwa mambo ya muhimu kwako. Kuwa makini na mambo ambayo yana athari kwa furaha yako. Cheza na watoto wako, mpeleke mpenzi wako sehemu za burudani, mara zote kutakuwa na muda wa kwenda kazini, safisha nyumba, andaa tafrija ya chakula cha usiku.
•Tunza mawe kwanza, mambo ya muhimu hasa. Weka vipaumbele vyako, mengine yote yanayobaki ni mchanga.
 
NGUVU YA MAWAZO
Mfungwa aliyehukumiwa kufa aliambiwa kuwa, kama angeshinda jaribio na aendelee kuishi baada ya jaribio hilo, angeachiliwa huru. Alikubali kufanya jaribio hilo. Jaribio lenyewe lilikuwa kwamba, walitaka kujua ni kiwango gani cha damu binadamu anaweza akapoteza na bado akaishi. Walipanga kwamba, damu imwagike kupitia sehemu ndogo ambayo ingekatwa katika mguu wake. Alikatwa kidogo sana, kiasi kwamba hakuna damu yoyote ambayo ingeweza kupenya katika tundu hilo. Ndani ya chumba, mliwekwa mfuko uliokuwa na maji, na kukiwa na sehemu ndogo iliyotobolewa kuruhusu maji yapenye. Chumba kilikuwa giza, na kwa vile kulikuwa na matone yaliyosikika yakidondoka, mfungwa alijua ndiyo matone ya damu kutokea sehemu aliyokatwa. Asubuhi yake, mfungwa alikutwa amekufa, na kilichomuua si damu kumwagika toka mwilini mwake, bali hofu ya akili.

Hebu fikiria, ungelikuwa wewe ndiye mfungwa huyo, asubuhi ungekutwa ukiwa hai, au ukiwa umeaga dunia?
 
Kaka hongera sana kiukweli nimependa sana mawazo yako !!!! Yangeifikia jamii nzima hasa tz tena kwa njia ya sauti na sura yako pia !!!! Hongera sana Mungu akusaidie ufanikishe azma yako !!!!
 
MWINDAJI WA NYATI
•Kuna stori inayoelezwa kuhusu mwindaji mashuhuri wa nyati ambaye alikuwa na rafiki aliyetaka mara zote kwenda kuwinda pamoja na rafiki yake mwindaji. Hivyo, siku moja mwindaji alimwambia rafiki yake, nimepata ruhusa ya kwenda kuwinda katika bonde la Zambezi kuwinda nyati, utapenda kwenda nami? Rafiki alifurahia sana mwaliko huo, na akakubali.
•Na aliuliza, ni lini tutakwenda? Na alijibiwa, baada ya miezi sita tangu sasa, lakini kwanza itanilazimu nikufundishe kuhusu uwindaji.
•Kwa miezi sita iliyofuata, wanaume hawa wawili walikutana kila siku na kujadili na kupanga kwa safari hiyo. Rafiki alishangazwa na namna mwindaji alivyo mjuvi katika masuala mazima ya uwindaji.
•Mwindaji alimfundisha rafiki yake kuhusu pori na namna ya kujiponya na hatari yoyote. Pia alimfundisha kila kitu kuhusu nyati.
•Lazima umweshimu nyati alisema, kwa sababu ni mnyama mwenye akili sana na ni mnyama hatari sana pia.
•Alimpatia vitabu vingi sana vya kusoma kuhusu nyati na uwindaji.
•Katika kipindi hicho, mwindaji alimfundisha rafiki yake kuhusu umbali wa kupiga risasi. Na hivyo rafiki alielewa silaha mbalimbali zitumikazo kuwinda nyati, na hiyo ilimshangaza sana.
•Unaweza kufa huko porini kama hauko vizuri, alimweleza.
•alishangazwa sana kwa yale aliyokuwa akijifunza kuhusu uwindaji.
•Kabla ya hapa, nilifikiri yote ufanyayo ni kufika porini na kulenga risasi, lakni sasa naelewa kuna zaidi ya hili alihamanika.
•Siku ilipofika, wanaume hawa waliianza safari yao kwenda kwenye pori la bonde la Zambezi. Kwa muda wa siku tano, walikuwa wanamfatilia mnyama mmoja tu, na rafiki wa mwindaji alichoka sana. Kuna nyakati walitembea kwa masaa mengi na wakati mwingine walikaa, mwindaji mara nyingi aliangalia maeneo ya kuwazunguka akivichunguza vichaka, yote hiyo akimfuatilia nyati mmoja tu.
•Kwa nini asipige risasi ili twende nyumbani? Rafiki wa mwindaji aliwaza.
•Alikuwa anaelekea kuchoka baada ya kutembea umbali wa maili 50 kwa siku. Pia alikuwa na njaa kwa muda mwingi, maana kwa muda mwingi walikula nyama iliyokaushwa na matunda. Mwindaji aliangalia mara kwa mara kupitia kiona mbali kilichokuwa kwa bunduki yake, lakini hakupiga risasi. Wakati mwingine wanyama walionekana karibu sana, lakini bado hakufanya kitu.
•Na siku hiyo ya tano, mnyama alikuwa katika shabaha tena. Rafiki alikaa kwenye kichaka na mara sungura alijitokeza kwa mbele. Na kisha akasema moyoni mwake, sungura huyu nikimuua, leo tutakula chakula kizuri, maana nimechoshwa na nyama zilizokaushwa pamoja na matunda. Na hivyo akafyatua risasi moja kutoka kwenye silaha yae, sungura alitoweka maana alimkosa katika shabaha yake ni hivyo kwa nyati na kwa wanyama wote porini.
•Mwindaji alimwangalia rafiki yake kwa mashaka na kutokuamini kilichotokea, kisha akampigia makelele, kimbia ama utakufa.
•Walinusurika kushambuliwa na wanyama wa porini, maana ghafla tu, simba pia walijitokeza ambao mwanzo hawakuonekana.
•Nyati akawa amekwenda zake, na uwindaji ukafika mwisho.
•Walirudi nyumbani mikono mitupu.
FUNDISHO
MOJA
•Mwindaji hakutaka kumuua nyati tu, bali lengo lake lilikuwa kwenda na nyama yake nyumbani.
•Hapa kwa wafanyabiashara. Mafanikio ya biashara hayaji kwa vile tu una.
•Wazo kubwa la kibiashara
•Kuweka wazo hilo katika vipimo
•Kuanza biashara na kadhalika. Lakini, kuiendeleza biashara hiyo, kutoa huduma bora na kutoa faida nzuri ndiyo jambo la muhimu.
•Ni dhahiri kuwa. Ni jambo moja kuandama lengo lako na la pili ni kumaliza lengo, hivyo kurejea na nyati wako nyumbani. Katika mambo mengi, huhitajika uzoefu ili kuvishinda vikwazo katika njia.
MBILI
•Katika jambo lolote unalotaka kufanya, kwa mfano biashara, uongozi n.k, lazima ujue kuwa kuna washindani katika jambo husika. Hawa ndio simba katika stori yetu. Mwindaji mashuhuri alijua simba walikuwepo, hivyo alitaka kuchagua muda wa kukamlisha kazi yake katika namna ambayo asingeishia kuwalisha simba wenye njaa pekee. Hii huitwa busara ya uwindaji, ni zaidi ya habari ya majira.
TATU
•Rafiki wa mwindaji, hapa anaweza kuwa mwanachama wa timu yako, au mfanyakazi mwenzako. Ni lazima uchague ambao si tu kwamba wanaelewa kwamba uko kwenye uwindaji wa nyati lakini pia wanaelewa inagharimu kiasi gani kutunza ulichonacho. Mara nyingi utaelewa kuwa, watu wengi huelewa njozi yako unapoanza, lakini kadiri mambo yanavyozidi kuwa magumu, wataweka mbadala wa njozi yako kwa njozi zao dhaifu za uwindaji wa sungura. Hawa ni watu wanaoanza kulalamika na kuhoji mbinu zako nyuma ya pazia. Na huchukua uongozi makini kumtunza kila mmoja kuendelea kuwamo kwenye kundi la uwindaji wa nyati.
•Mara nyingi watu wa namna hii huonekana kama wenye suluhu halisi lakini lisiloonekama sawa. Linaweza likafanya kazi, lakini linganisha ukubwa wa sungura kwa nyati. Na usiruhusu wengine wakuharibie malengo yako kwa njia za mkato.
NNE
•Mawasiliano yasiyokoma na maelekezo kwa wanachama ni ya muhimu. Mwindaji mzoefu yawezekana alifikiri maelezo aliyompatia rafiki yake yalitosha. Na yawezekana mwindaji hakuwa na mawasiliano na rafiki yake kujua changamoto zinazomkabili mwenzake. Na licha ya kwamba alijua kuna simba na wanyama wengine, hakumwambia rafiki yake, yawezekana pia hakumweleza jinsi ilivyo hatari kufyatua risasi ovyo ovyo. Hivyo lazima kuwe na maelekezo sahihi kutoka kwa kiongozi kwenda kwa anaowaongoza.
TANO
•Unaporizika na kitu kidogo inaweza kupelekea kupoteza kilicho kikubwa zaidi. Fikiria kile unachotaka kupata maishani mwako, na vitu ambavyo vimekufanya uridhike na hivyo kujikuta ukiona kile kikubwa kama hakina umuhimu tena.
•Tendo moja batili linaweza kuharibu miezi mingi ya kupanga. Hivyo panga kwa umakini na utende kwa uangalifu. Kila fursa huja na hatari zilizojificha, kuna zaidi ya yale unayoyaona katika macho yako kwenye kila fursa. Mara zote, kaza macho yako katika lengo mahsusi na uepukane na mambo madogo madogo yasiyo na ulazima wowote.
•Nusu ya busara iliyopatikana, si busara.
•Malengo hushindwa pale hamasa inapokosekana.
•Kumbuka, daima utakuwa mwindwaji anayewinda nyati “a hunted buffalo hunter”
•Kumbuka, wakati safari inapokuwa ngumu, ni wale wenye nguvu tu ndiyo huweza kuendelea mbele. Usiruhusu wawindaji wa sungura kuharibu safari yako katika jambo lililo moyoni mwako. Iwe ni biashara, kazi au hata safari ya kiroho.
•Na usiondoke katika shabaha yako, kwa vile tu umeona njia nyepesi kando yako. Njia nyepesi haitakuwezesha kupata unachotafuta endelea kusonga mbele, hata kama ukabiliane na magumu kiasi gani, hatimaye utampata nyati wako.
 
Kaka hongera sana kiukweli nimependa sana mawazo yako !!!! Yangeifikia jamii nzima hasa tz tena kwa njia ya sauti na sura yako pia !!!! Hongera sana Mungu akusaidie ufanikishe azma yako !!!!
Nilitamani iwe hivyo, na bado natamani iwe hivyo. Lakini kwa vile lengo ni ujumbe, ndiyo maana nimeweka wazo hili mahali hapa ili atakayeona linafaa aliendeleze.
 
Nimejaribu kuisoma yote na kwa uwelewa wangu mdogo nilioupata kutoka katika nilichokisoma hapo juu unaweza kuwa speaker mzuri Ila unawaweza pia usiwe hivyo kwasababu nawe pia badala ya kuendelea kuwinda nyati ulikatishwa na aliyeftua lisasi kwa sungula, OK basi nami ngoja nisaidie kukumbusha japo unaweza usiwe na hela za kulipia kupata airtime za TV station bado kuna YouTube unaweza fungua Chanel kule na ukatengeneza vipindi na kuvipa airtime ya kutosha na gharama in nafuu sana na affordable kabisa usife moyo always another chance created by you so create new chance for .
 
Back
Top Bottom