UKEREWE: Zana haramu za uvuvi, zenye thamani ya zaidi ya bilioni 1 na milioni 106 zateketezwa

Queen V

JF-Expert Member
Jan 19, 2012
775
1,332
nyavuuu.jpg


Zana haramu za uvuvi, yakiwemo makokoro 365 ya samaki aina ya Sangara na nyavu za timba 2,764 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni 106 zilizokamatwa na idara ya uvuvi katika halmashauri ya wilaya ya ukerewe mkoani Mwanza zimeteketezwa chini ya usimamizi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.

Zoezi la kuteketeza zana hizo haramu za uvuvi, zilizokamatwa kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana hadi Mei 31 mwaka huu katika mialo mbalimbali ya ziwa victoria, limefanywa na mkuu wa wilaya hiyo Joseph Mkirikiti katika kijiji cha Bukongo, ambapo amewataka viongozi wa serikali za vijiji na kata wanaomiliki makokoro hayo kuyasalimisha kwa hiyari yao kabla ya hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ukerewe pia ametangaza mkakati wa serikali katika vita dhidi ya uvuvi haramu, ikiwemo kuwapata waingizaji wa makokoro pamoja na nyavu za makila na nyavu za timba.

Afisa uvuvi wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Aboubakary Rutabanzibwa mbali na kueleza baadhi ya changamoto zinazojitokeza wakati wa uteketelezaji wa zoezi hilo, zikiwemo za wananchi kushindwa kuwataja wamiliki wa zana haramu za uvuvi na mahali wanapojificha, amewahimiza wavuvi kuanza kufikiria kufuga samaki kwenye mabwawa badala ya kujihusisha na uvuvi usioendelevu unaochangia kupungua kwa samaki wachanga katika ziwa Victoria.

Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa wilaya ya Ukerewe, inayoundwa na visiwa 38 wanajishughulisha na shughuli za uvuvi. Sekta hii ya uvuvi imeajiri zaidi ya watu 80,000 wilayani hapa na pia inatoa ajira na riziki kwa wananchi wengi wa wilaya hii.


Chanzo: ITV
 
Back
Top Bottom