UKAWA wavurugika ndani ya majimbo matano

UKAWA wavurugika ndani ya majimbo matano

Mazaya

JF-Expert Member
Joined
Apr 9, 2015
Posts
875
Reaction score
771
kilufi.jpg

Aliyekuwa Mbunge wa Mbarali kupitia CCM ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chadema, Dickson Kilufi (aliyevaa suti) akimsikiliza mlinzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali baada ya kuzuiliwa kuingia getini alipotaka kwenda kuchukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, mkoani Mbeya jana

Toka Mikoani. Siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kutangaza mgawanyo wa majimbo, baadhi ya majimbo hayo yamekumbwa na sintofahamu baada ya wanachama kutokubaliana na uamuzi ya viongozi wa kuachiana majimbo.

Vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine, chama chenye nguvu kwenye jimbo husika na kura za uchaguzi wa mwaka 2010.

Tayari Chadema na CUF vimeshatoa orodha ya majimbo vitakavyosimamisha wagombea wake na kuacha baadhi, ambayo yameibuka kutoelewana baina ya uongozi wa juu na wa wilaya.

Moja ya majimbo ambayo hayakuwekwa kwenye orodha ya mgawanyo ya Chadema iliyotolewa mapema wiki hii ni Ngara ambayo iliachiwa NCCR-Mageuzi, lakini uongozi wa wilaya wa chama hicho kikuu cha upinzani umesema utasimamisha mgombea.

Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ngara, Kennedy Staford amesema Kamati Kuu ya Ukawa imewachanganya wananchi wa jimbo hilo kutokana na uamuzi huo wa kuipa NCCR-Mageuzi nafasi ya kusimamisha mgombea.

Staford alisema kitendo cha kuipa jimbo hilo NCCR-Mageuzi bila viongozi wa wilaya kushirikishwa ni kuwakatisha tamaa wanachama kuendelea kuunga mkono Ukawa kupitia Chadema.

Alisema chama kilichopendekezwa kusimamisha mgombea hakina wanachama na wafuasi wanaoweza kutoa ushindani kwa mgombea wa CCM. "Jimbo la Ngara tulishafanya mchakato wa kumpata mgombea aliyepigiwa kura za maoni na tayari amechukua fomu ya kuwania jimbo kupitia chama chetu," alisema Staford.

Majimbo yaliyotangazwa na Chadema kusimamisha mgombea katika Mkoa wa Kagera ni pamoja na Karagwe, Kyerwa, Bukoba Mjini, Muleba Kaskazini, Biharamulo na Muleba Kusini.

Wakati hayo yakitokea Ngara, Ukawa wilayani Kakonko pia imeingia katika mvutano baada ya baadhi ya vyama shirika kuweka wagombea wake kuwania ubunge kwa Jimbo la Buyungu na kukiuka makubaliano. Hali hiyo imejitokeza baada ya Samso Bilago kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya Chadema na kusababisha wasiwasi kwa wananchi kutokana na jimbo hilo kuachwa kwa NCCR-Mageuzi ambayo mgombea wake Mawazo Atanasi pia amechukua fomu.

Akizungumzia hali hiyo, katibu wa CUF jimboni humo, Odasi Kalimanzila alisema msimamo wa Ukawa haujavunjika licha ya kwamba kuna baadhi ya vyama ambavyo vimeonekana kwenda kinyume na makubaliano. Hata hivyo, katibu wa NCCR-Mageuzi wilayani Kakonko, Marco Bajora alisema bado kuna changamoto kubwa katika umoja huo, na kwamba wanachosubiri ni uamuzi wa wananchi kumchagua kiongozi atakayefaa katika kuleta maendeleo.

Ester Bulaya azua balaa

Wakati huohuo, aliyekuwa mshindi wa kura za maoni Bunda Mjini wa Chadema, Pius Masururi ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM huku mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Imanani na wanachama 50 wakiwamo viongozi wakijivua uanachama.

Masururi, aliyepata kura 65 mbele ya wapinzani wake wa karibu, Magembe Makoye (40) na Ester Bulaya (37) katika kura za maoni zilizopigwa Julai 29 mwaka huu, ametangaza uamuzi wake huo jana kupitia kituo cha redio cha Mazingira FM cha mjini Bunda.

Masururi amesema ameamua kukihama chama hicho baada ya kutofurahiswa na kitendo cha Kamati Kuu ya Chadema kupuuza uamuzi wa wanachama kwa kukata jina la aliyeshinda kura za maoni.

Katika jimbo la Bunda Mjini, Chadema imebadilisha matokeo na kumteua mshindi wa tatu, Ester Bulaya kupeperusha bendera ya chama hicho, jambo lililowaudhi baadhi ya makada wake.

Baadhi ya wanachama walioongozwa na mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Imanani wamesema kitendo cha makao makuu ya Chadema kutengua uamuzi wa kura zao za maoni ni udhalilishaji mkubwa, hivyo hawana budi kukihama chama hicho. "Tumeamua kuuachia uongozi wa makao makuu uendeshe mambo yote, nasi tusiwe tena wanachama maana hautusikilizwi," alisema Mashaka Kipili mmoja wa wanachama hao.

Katika tukio jingine, aliyekuwa mbunge Mbarali kupitia CCM, Dickson Kilufi amekumbana na vikwazo kwenye chama chake kipya cha Chadema baada ya uongozi wa wilaya kusema hauna taarifa za kutaka agombee ubunge wa jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Chadema wilayani Mbarali, Peter Mwashiti alisema taarifa za Kilufi kujiunga Chadema anazisikia kwenye vyombo vya habari na mitaani na kwamba suala la kutaka agombee ubunge halipo kwa vile tayari alishapitishwa Liberatus Mwang'ombe kuwa mgombea wa jimbo hilo.

'‘Kama amejiunga na Chadema, tunamkaribisha, lakini kibaya ni kwamba hajawahi kuwasiliana na kiongozi yeyote wa Chadema Wilaya ya Mbarali na cha kushangaza tunasikia ameanza kujitangaza eti kateuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya Chadema. Sisi tuna mgombea wetu na ameshachukua fomu pale halmashauri," alisema.

Kilufi alipoulizwa kuhusu hoja hizo, alisema aliteuliwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye ubunge wa Jimbo la Mbarali.

Wakati mgogoro huo ukiendelea, mwenyekiti wa CCM Mbarali, Mathayo Mwangomo amesema Kilufi alikuwa mzigo ndani ya chama hicho hivyo wanashukuru kujiengua kwake na kujiunga na Chadema.

Pia, Kilufi alijitetea kuwa hakuwa mzigo, bali mzigo ni viongozi wa CCM ambao alidai wanapenda rushwa.

Wafuasi wa Chadema, Kata ya Forest Mbeya waliandamana hadi katika ofisi za wilaya za chama hicho wakipinga shinikizo la uongozi wao kutaka aliyekuwa diwani, Boyd Mwabulanga achukue fomu za kuwania tena nafasi hiyo.

Mwanachama wa chama hicho aliyejitambulisha kwa jina la Mwamakamba, alisema anashangazwa na kitendo cha baadhi ya viongozi kutumia mbinu za kiujanja ujanja kutaka Mwabulanga agombee tena badala ya Henry Mwakikambu aliyeshinda kura za maoni.

Viongozi wa wilaya walilazimika kuwatuliza wandamanaji hao kwa kuwaeleza kwamba kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika aliruhusu Mwakikambaku achukue fomu haraka na kuapishwa mahakamani ili agombeee nafasi hiyo. Pia, katika Jimbo la Handeni Mjini vyama vya CUF na Chadema vimesimamisha wagombea ubunge licha ya mgawanyo wa majimbo hayo kuonyesha kuwa CUF ndiyo kimeachiwa nafasi hiyo.

Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Zaharia Yohana alisema ni kweli wamesimamisha wagombea ubunge na udiwani katika majimbo yote pamoja na kata zote Handeni Mjini na Vijijini ili kushiriki uchaguzi mkuu.

Kuhusu mchakato huo kukiuka makubaliano ya vikao vya Ukawa, alisema hawezi kulizungumzia hilo bali anafuata maelekezo ya viongozi wake.

Chanzo: Mwananchi
 
Changamoto kama hizi zilitarajiwa

Kamati ya Ufundi ya UKAWA shughulikieni haya
 
Isingewezekana kwa mahali kote mambo yaende kama yalivokuwa yamepangwa. Wagombanao ndio wapatanao.
 
Mimi bado naamini watu waliopo huko mashinani level ya wilaya na majimbo ndio wanaoona ni chama gani kina nguvu.

Pamoja na maamuzi ya kitaifa nashauri kama chama kinaona kuwa ndicho chenye nguvu wachukue fomu, mengine yatajulikana huko mbele ya safari...
 
Baada ya chadema kununuliwa na mroho wa madaraka mambo yote ukawa iliyokubaliana yamepoteza mwelekeo. Ndio maana Lipumba aliona ajitoe kutunza heshima yake.
 
Mimi bado naamini watu waliopo huko mashinani level ya wilaya na majimbo ndio wanaoona ni chama gani kina nguvu.

Pamoja na maamuzi ya kitaifa nashauri kama chama kinaona kuwa ndicho chenye nguvu wachukue fomu, mengine yatajulikana huko mbele ya safari...

Mkuu, hizi shaghala baghala ni evidence tosha kuwa hawa watu hawana maandalizi tosha ya kuongoza nchi.
 
Chadema Bunda yabomoka vibaya
-Robo tatu ya viongozi wa kamati tendaji wajihudhuru nyadhifa zao
-Wasema chanzo ni Esther Bulaya kubebwa na viongozi wa juu wa chama hicho
-Wasema wamekitumikia chama hicho na kuwekwa ndani lakini sasa hawathaminiwi
Na Ahmed Makongo, Bunda;
Agosti 20, 2015;

CHAMA cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) katika Wilaya ya Bunda, kimepata mpasuko mkubwa kutokana na jana karibu robo tatu ya viongozi wake kujihudhuru nafasi zao, akiwemo katibu mwenezi wa Chadema jimbo la Bunda Emmanuel Malibwa, mwenyekiti wa jimbo hilo Samwel Alfred na katibu wa Chadema Wilaya Rita Itandilo.

Baadhi ya viongozi hao pamoja na baadhi ya wanachama wa chama hicho walisema kuwa sasa hivi watamuunga mkono mgombea wa CCM katika jimbo la Bunda Stephen Wassira, kwa sababu viongozi wao wamejichanganya sana, kwa kuwafanyia maamuzi ambayo siyo sahihi.

Habari zinasema kuwa chanzo cha viongozi hao kujihudhuru nafasi zao ni aliyekuwa mbunge wa viti maalumu kundi la vijana kutoka mkoani Mara, kupitia tiketi ya CCM Esther Bulaya, aliyejiunga na chama hicho hivi karibuni na kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge katika jimbo la Bunda mjini kupitia tiketi ya Chadema, huku aliyeshinda kura za maoni Pius Masururi akikatwa jina lake.


Viongozi hao walisema kuwa kwa mjibu wa katiba uteuzi wa mbunge huko kwenye kamati kuu, lakini walivyowaletea Esther Bulaya yeye alikuja na uongozi wake bila ya kuwashirikisha viongozi waliokuwepo na kwamba kwa jinsi hiyo wameamua kujihudhuru nafasi zao na kumwachia viongozi aliokuja nao.

Viongozi hao pamoja na wa kamati tendaji na baadhi ya walinzi, wakifuatana na wananchama wa kawaida zaidi ya 70, wamejihudhuru nafasi zao kwa kile walichodai kuwa viongozi wa chama hicho wakiwemo wa ngazi ya juu wameivunja katiba ya chama hicho kwa makusudi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana katika hoteli ya Green Guden, mjini Bunda viongozi hao walisema kuwa wameamua kujihudhuru nafasi zao na kubakia wanachama wa kawaida kwa sababu viongozi wao wa Mkoa, kanda na Taifa wamekiuka katiba ya chama hicho.

“Kwa kile kilichotokea kupitia uongozi wetu wa mkoa, kupitia katibu wetu wa Chama Mkoa Chacha Heche na mwenyekiti wetu wa Mkoa wameshindwa kujua jimbo la Bunda msemaji wa chama au Mkoa ni nani wao badala ya kufuata katiba wameshindwa kujua katiba inasemaje kuhusu malalamiko yoyote.

“Wao badala ya kuona katiba inasemaje na kanuni za chama zinasemaje na taratibu zinasemaje kuhusu malalamiko yoyote kama yalikuweo ili waweze kuyafanyia kazi, lakini kilichofanyika ni udhalilishaji na maamuzi ambayo kamati tendaji ina mamlka ya kuyafanyia kazi, kupitia viongozi hawa ambao leo wanatoa matamko, mimi huwa sikubali kutokuonyesha msimamo.

“Mimi siku zote huwa napenda kuwa muwazi leo nafikia kuchukuwa maamuzi haya magumu, mimi ni mwanchama mwaminifu wa Chadema nimekitumikia chama kwa kipindi cha miaka zaidi ya kumi, lakini leo Bunda imekuwa shamba la bibi, maamuzi ya mtu ndiyo yanayokuja kulitengeneza jimbo la Bunda, kamati tendaji ya jimbo la Bunda ilifanya uteuzi wake wa awali kupitia kura za maoni.

“Walimaliza kura za maoni wakaenda kwenye kamati tendaj,i mimi kama katibu wa Wilaya naletewa mapendekezo ya kamati tendaji ndiyo ninayAfanyia maamuzi, nilichukuwa majina ya wsagombea nikayapeleka kwenye tume kwenda kuyawatambulisha, lakini kilichotokea Mkoa na Kanda na Naibu Katibu mkuu wakatoa maelekezo mengine mbadala, akaletwa mtu ndani ya ofisi yangu bila kunishirikisha wala hata kupewa barua ya kunitambuliusha.

“Lakini kilichofanyika huyo aliyeletwa akaanza kunielekeza lakini mimi kama katibu wa Wilaya ninayejua utaratibu nilikataa, lakini kilichotokea nikiingia ofisini kwangu pale naonekana kama mimi ni mgeni au mtuanayehitaji huduma pale, na kilichotokea wakachonga mhuri mwingine wakatengeneza mhuri ndani ya mhuri mwingine.

“Ndicho kilichopelekea leo hii nimeamua kuchukuwa maamuzi magumu kama mwanamke na nimeamua kujihudhuru nafasi hii ya katibu wa wilaya Chadema nitabaki kama mwanachama wa kawaida isije ikaonekana mimi ndiye nimesababisha chama kushindwa”alisema.

Naye mwenyekiti wa jimbo la Bunda, Samwel Alfred, alisema kuwa “mimi kama mwenyekiti wa Chadema jimbo nimeamua kujihuduhuru uenyekiti wangu wa jimbo la Bunda na nimeamua kujihudhuru uenyekiti wangu wa mtaa, kwa sababu kuna vitu vilivyonikera baada ya kuona kuna watu wanavunja katiba.
“Cha kwanza tulipiga kura za maoni wakapatikana washindi watatu wakiwemo wawili ambao waamekitumikia chama, lakini cha ajabu wakarudisha jina la mshindi wa tatu (Esther Bulaya), hawakuvunja katiba, lakini cha ajabu aliyerudishwa hakuonyesha ushrikiano na viongozi waliokuwepo, kwa kuhofia kuwa walikuwa kambi nyingine kwamba watasababisha ashindwe.” Alisema.

Aliongeza kuwa pia kwa upande wa wagombea udiwani wagombea waliopendezwa na kamati tendaji pia majina yao yalibadilishwa na viongozi wa mkoa, kanda pamoja na Naibu katibu mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, ambapo yaliletwa majina ya wagombea wengine na kuondolewa wale waliokuwa wameshinda na kupitishwa na kamati tendaji ya jimbo.

“Mimi kama kiongozi niliyepigania chama hiki niliyepata kesi nyingi nimekaa magereza, nimenyanyaswa nimepigwa na nimedhalishwasana, leo hii nimeamua kujihudhuru lakini siyo kwamba naondoka peke yangu naondoka na makamanda wakiwemo wajumbe wa kamati tendaji na katibu wa Bavicha, kwa hiyo robo tatu ya kamati tendeji yote tumejihudhuru.

“Hata wenyeviti wa kata, viongozi wa vijiji, vitongoji wote wameamua kujihuduhuru, najua makamanda wataumia sana maana wanakitaka sana Chadema, lakini kiongozi aliyeletwa kugombea ameshindwa kutambua mchango wa viongozi hawa waliokipigania chama na kufikia hatua hii sisi tumeamua tumpishe ili ashinde salama’ alisema.

Katibu mwenezi wa Chadema jimbo la Bunda, Malibwa alisema “ Mimi kama katibu mwenezi wa Chadema jimbo la Bunda natangaza rasmi kuwa nimejihuduru nafasi yangu hiyo ya uenezi, na wafuasi wangu wote ambao niliwashawishi wakaingia Chadema leo watambuwe kuwa nimejihudhuru nafasi hiyo nitabaki kuwa mwanachama wakawaida tu.

“’Na sijaondoka peke yangu kama mnavyoona hapa ndugu waandishi wa habari tunao viongozi wote wa kata 20 za jimbo la Bunda, wakiwemo wenyeviti wa kata, makatibu wa kata, kwa ujumla kamati tendaji ya watu 17, mimi mwenezi, mwenyekiti wangu na wajumbe wengine tumeondoka imebaki na watu watatu tu” alisema.

Alisema kuwa yeye pia alikuwa ni mgombea udiwani wa kata ya Nyamakokoto na alikuwa tayari amechukuwa fomu katika ofisi ya Tume, lakini sasa hatarudisha fomu hizo na kwamba kutokana na utaratibu huo kuvunjwa na viongozi wao kwenye baadhi ya kata kuna wagombea wawili wa Chadema ambao tayari wameshachukuwa fomu za Tume kuwania nafasi hiyo.
Viongozi hao walisema kuwa pamoja na kujihudhuru watapiga kura zao katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakati viongozi hao wakisema wamejihudhuru nyadhifa zao viongozi wa Chadema, akiwemo mmoja kwa niaba ya katibu mkuu wa Wilaya Kaunya Yohana, alisema kuwa viongozi hao wapatao kumi na moja hawajajihudhuru kama walivyodai bali wamesimamishwa uongozi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kupandikiza wagombea bila taratibu, rushwa na kukiuka maadili na kanuni za chama hicho.
image.jpg View attachment 278669
 
Wakati wa mabadiliko vikwazo ni lazima. Wapo wengi watakaopinga ama kushindwa kuendana na mabadiliko.Hata wakati Nuhu akiijenga safina wengi walitokea kumpinga,kumdhihaki na kumtukana.Mwisho wa siku gharika iliwamaliza!!
 
Mimi bado naamini watu waliopo huko mashinani level ya wilaya na majimbo ndio wanaoona ni chama gani kina nguvu.

Pamoja na maamuzi ya kitaifa nashauri kama chama kinaona kuwa ndicho chenye nguvu wachukue fomu, mengine yatajulikana huko mbele ya safari...

UKAWA ni wa viongozi wa juu sio wanachama wa matawini waache kulia lia.Kwani Lowasa alipoingizwa UKAWA walikuwa consulted? Waache kujishebedua wapokee amri na maamuzi kutoka kwa madikiteta watawala viongozi wa juu wa UKAWA hawataki wahame kabla hawajatimuliwa.
 
hakuna jambo lolote lisilo na changamoto! kikubwa ni kusolve kwani ukitofautiana na mkeo ndo uhame nyumba? tunahama nyumba au kuacha kwa wenye sifa za kufanya hivyo pindi mambo yakishindikana kabisa kama jinsi tulivyoshindwa kwenda sambamba na ccm!
 
Changamoto kama hizi zilitarajiwa

Kamati ya Ufundi ya UKAWA shughulikieni haya

We Mjamaa ulienda ugambani kimwili ila roho umeaicha chadema, nakuonaga sometym unashindwa kujizuia kuonyesha mapenzi yako kwa ukawa.
 
Baada ya chadema kununuliwa na mroho wa madaraka mambo yote ukawa iliyokubaliana yamepoteza mwelekeo. Ndio maana Lipumba aliona ajitoe kutunza heshima yake.

Naona unaifanya kazi yako kwa bidii
 
safari ya kuanguka ndio ishaanza, hapo ndio utajua nani kakomaa katika siasa.
siwezi poteza kura yangu kwa UKAWA
Isingewezekana kwa mahali kote mambo yaende kama yalivokuwa yamepangwa. Wagombanao ndio wapatanao.
 
Wakati wa mabadiliko vikwazo ni lazima. Wapo wengi watakaopinga ama kushindwa kuendana na mabadiliko.Hata wakati Nuhu akiijenga safina wengi walitokea kumpinga,kumdhihaki na kumtukana.Mwisho wa siku gharika iliwamaliza!!

umesikia Bunda kimenuka?
 
Back
Top Bottom