Norbert Mporoto
Member
- Jul 18, 2020
- 14
- 12
Na: Norbert Mporoto
28.02.2021
“Allah amefaridhisha mambo ya dini kwa hivyo usiyapuuze. Vilevile kaweka mipaka usiikiuke, amekataza baadhi ya mambo kwa hivyo usiyafanye. Yale aliyoyanyamazia ni kwa ajili ya huruma zake kwako wala hakusahau kwa hiyo usiyadadisi”
Ni maneno mazuri yenye kubeba dhamiri ya imani zetu, ili mioyo yetu itulie tukisubiria kuuona ufalme wa mbingu. Naomba nikiuke kidogo misingi ya imani zisizo asili yetu kwa kuanza kufanya udadisi juu ya uhusiano wetu wa kibinadamu na dini hizi, ambazo zinaongozwa na misahafu kama katiba yake.
Kama ilivyo katika uongozi wa taasisi, jamii, au taifa lazima kuna sheria na taratibu ambazo zinatumika kama mwongozo, na asili yake ikiwa ni katiba ambayo ndiyo mkusanyiko wa sheria hizo. Hivyo, imani zetu kupitia dini huongozwa na misahafu anuai kulingana na muktadha wa dini husika. Kuzungumzia dini ya mtu kwa uzuri au ubaya si jambo la kiungwana hata kidogo, lakini kukiuka misingi ya dini ili kukosoa (kulingana na mienendo husika), kuokoa na kurekebisha hatma za waumini katika imani zao ili kutafuta mwafaka mwema katika jamii zao ni jambo sahihi ambalo makala hii inalenga kujadili kwa kina.
Kiuhalisia dini ni jukwaa linalowakusanya watu wa imani moja chini ya mwamvuli unaosimamia na kuainisha sheria, kanuni, miiko, na taratibu ambazo huakisi utamaduni na asili yao wakati wote wanaposimama kuitetea kwa kuabudu, na kuidhihirisha imani yao. Lakini kwa maana iliyopoteza umaana wake katika mapokeo yaliyofanywa na wengi wetu ni ile inayoakisi dini kuwa imani. Awali kabla ya mapokeo ya imani au dini hizi kulikuwapo na imani zetu asilia (kote barani Afrika). Mapokeo ya imani kiukweli hayakuzingatia muktadha na hatma yetu, ila tu wapokeaji hawa waliweza kuzipokea kama m’badala wa imani zao zilizoitwa za kishenzi na zilizojaa uovu na matendo yanayosadikika kuwa ya kishetani. Labda! Kwa kifupi, walianzisha safari isiyoweka bayana mwelekeo wake, na baadae kukosa ufahamu wa kuona mbali kusawili matokeo ya kinachofanyika kwa kivuli cha imani hizo.
Uwezo hafifu wa kung’amua kilichopo ndani ya mapokeo hayo na matokeo yake unatokana na mfumo uliotumika na waliozileta imani hizo. Mbinu hizo zilimdhoofisha mpokeaji na kumuaminisha kuwa hakuna imani ya kweli zaidi ya hiyo, hivyo msingi huu m’bovu umetujenga kuwa na akili fupi za kutoweza kuamua nini hatma yetu dhidi ya mataifa anzilishi ya imani hizi.
Jambo ambalo ni kosa, ni kushindwa kung’amua kuwa imani ya watu fulani hubeba utamaduni wa watu husika, hivyo hata akipewa mtu mwingine aiendeleze imani hiyo hawezi endana nayo kamwe. Ni shughuli ngumu ya kumpaka rangi punda ili ageuke kuwa pundamilia wakati inafahamika wazi kuwa mvua ikinyesha atairejea asili yake ya kuwa punda. Na hivyo ndivyo ilivyo kwetu sisi tuliopokea imani hii, na tumeshindwa kuendana nayo kiasi kwamba imani hizi zimegeuka kuwa zimwi linalotutafuna kila uchao.Lakini upande wa pili kwa waliotuletea imani hizi kwao ni furaha na shangwe mithili ya ngedere waliovamia shamba la mahindi maana hawana uchungu nayo, wala hawaumii kwani hawajui hata gharama na kiasi cha jasho lilichomwagika kufikia hatua hiyo.
Kitendo cha kuridhia kupokea imani zao, ni kuruhusu mataifa yetu yaenende katika mwongozo wa tamaduni mbili tofauti. Lakini tamaduni hizi mbili haziwezi pikika katika chungu kimoja, hivyo chokochoko na mitafaruku inayoendelea barani Afrika kwa namna moja au nyingine inatokana na ugeni wa tamaduni za kiimani tulizobebeshwa, na kuzivaa haswa kanakwamba ni asili yetu, kiasi cha kushindwa kuimudu mihemko yetu juu yake na hata kutizamana kama maadui wa kiimani.
Leo hii Afrika, dini imekuwa mithili ya dawa za kulevya zenye madhara zaidi ya bangi na mirungi (yapasa itumike fikra ili uweze kutambua ukweli huu, na tuweke kando hisia zetu). Imani za dini tulizopokea zimeathiri watu wetu kifikra, zimejenga hofu na woga na zaidi dini hizi zinatafuna mihimili ya mataifa yetu, yaani aliyeleta ukoloni ndiye aliyeleta dini hivyo shabaha ya mkoloni bado iko palepale kupitia mwamvuli wa dini tulizopokea. Hivyo tunautukuza ukoloni katika namna tusiyoielewa!
Kupitia mikononi mwa waanzilishi wa dini hizi, dini zimekuwa zikichochea mapigano baina ya waafrika. Kwa sababu za kutengenezwa, historia ya bara la Afrika inaonyesha namna ambavyo baadhi ya nchi zimekuwa zikikumbwa na kashfa ya mapigano ya kidini. Japokuwa ukweli wake ni kwamba mapigano hayo yanasababishwa na imani ya uadui ambavyo mizizi yake imetokana na mataifa anzilishi wa dini hizo kwa kutizama watu wa dini moja kuwa na uhasama na watu wa dini nyingine, kitu kinachopelekea kuvunjika kwa umoja baina yao na kushamiri kwa mapigano ya kidini.
Mapigano haya hayakuwepo kipindi babu zetu wakisali chini ya mti ama kipindi tunatambika; kipindi ambacho hizo imani zetu zinazoitwa za kishezi na zenye unasaba na ushetani zikiwa zinatumika. Kamwe hatukuwahi kupigana kisa huyu anatambika chini ya mti au yule anatambika juu ya jiwe. Kwanini leo hii kuwe na mapigano? Tumetoa wapi hizi tabia za kishenzi kwenye dini tulizoaminishwa eti ni za watu safi na werevu? Kwanini dini za sasa hazihubiri upendo katika matendo? Kati ya hao na babu zetu nani ni washenzi? Kitu pekee kinachopelekea tuyanyoshee vidole mataifa hayo ni namna ambavyo yamekuwa yakinufaika na kile tunachokiita ‘faida mgogoro’ mara baada ya pande hasimu walizozichochea kupigana, hatimaye kupata madhara. Kinachoonekana baada ya hapo si kusaidia mapigano hayo yaishe, bali ni kuumia kwa rasilimali za taifa husika.
Mapokeo ya kidini katika bara letu yaliandaliwa kwa kipindi kirefu, hakuna mizania inayopima wema au ubaya, usahihi au upotoshaji, au hata mienendo ya dini hizi huku kwetu. Tumekuwa na woga wa kutotaka hata kuhoji tu kwanini dini hizi nyuma yake kuna vitisho vingi, vinavyotuweka mbali na Mungu kwa kuwa tunamwogopa (maana anaadhibu sana tunapokosa, hapendi tukosee, hapendi twende kinyume na kanuni zake). Lakini anatupenda sana pale tunapomtolea fungu la kumi.
Sitaki mnielewe vibaya mkanibatiza majina ya hovyo, lakini ukweli ni kwamba mnamkosea sana Mungu. Mungu hayuko hivyo, yaani mungu wa sisi waafrika sio mnyonge anayetaka tuwe watu wa kupelekwa kama bendera. Wala si dhaifu kushinda Mungu wa wazungu, wala hataki kila siku tumlilie kwa kueleza shida zetu ambazo tumejitakia wenyewe. Mungu katupa akili, ni lazima tuitumie kutafakari mapokeo ya dini hizi. Na panapobidi basi tusimame kuabudu kwa usahihi, tofauti na hizi imani za kibepari zisizo na kweli ya huko tuendako.
NB: Picha imetumika kufasili Makala hii, haina umiliki.