Uhusiano wa Karume, Seif Sharif wahojiwa

Zak Malang

JF-Expert Member
Dec 30, 2008
5,404
234
Uhusiano wa Karume, Seif Sharif wahojiwa


WAKATI Jumuiya ya Kimataifa ikisifu uhusiano mpya kati ya Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad, wazee waliokuwapo wakati wa kuasisiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wamesema uhusiano huo ni bandia na huenda ukasababisha vurugu za muda mrefu Zanzibar.

Wakizungumza katika mahojiano maalumu na HABARILEO hivi karibuni, wazee hao, Baraka Shamte na Enzi Talib, walisema uhusiano huo unao mwonekano wa muda mfupi ambao ni utulivu na wa muda mrefu ambao ni vurugu.

Katika mwonekano wa muda mfupi, uhusiano huo umeelezwa kuleta utulivu Zanzibar ambapo Talib alitoa mfano wa kukatika umeme kwa miezi mitatu kwamba kama si uhusiano huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ingepata taabu ya kutuliza wananchi na pengine Serikali ya Jamhuri ya Muungano ingelazimika kununua jenereta kukabiliana na hali hiyo.

“Kimsingi maridhiano yaliyofanywa na Rais Karume na Seif yameleta utulivu wa kisiasa tu na hata zile fujo za kupigana na kuchukiana zimeondoka, kuna uvumilivu mkubwa sana,” alisema Talib.

Hata hivyo alibainisha kuwa uhusiano huo katika muda mrefu utasababisha Katiba ya Zanzibar ibadilishwe na baadaye hata ya Muungano, jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu.

Mtazamo huo wa vurugu pia ulitolewa na Shamte, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Chama cha Afro Shiraz, ambaye alisema uhusiano huo ni bandia na kuongeza kuwa ni ujanja wa Seif kuingia serikalini, baada ya mbinu zake za muda mrefu kutaka kuingia kushindwa.

Kwa mujibu wa Talib, baada ya CUF kufanikiwa kushawishi Baraza la Wawakilishi kupitisha Muswada wa Sheria ya Kura za maoni ambayo inamsubiri Rais Karume ausaini iwe sheria, tayari chama hicho kitakuwa kimeshafanikiwa kubadili Katiba ya Zanzibar.

Wananchi wakikubali kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kura hiyo ya maoni ambayo Talib anaamini kuwa watakubali, muundo wa SMZ utabadilika, ambapo Rais atakuwa na Makamu wa Kwanza, ambaye atatoka chama chenye kura zilizokaribia za Rais na Makamu wa Pili wa Rais ambaye atachukua shughuli za Waziri Kiongozi.

Mabadiliko hayo ya muundo wa SMZ, yatailazimu pia protokali ya viongozi ya Serikali ya Muungano kubadilishwa ili kutambua nyadhifa hizo za Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Talib ambaye alikuwa mwandishi wa kwanza wa marehemu Karume, alisema kwa kuwa Seif ameshatangaza nia yake ya kugombea urais na kutokana na historia ya uchaguzi wa Zanzibar, kiongozi huyo wa CUF atakuwa ameshajihakikishia nafasi ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

“Seif ni mzoefu wa siasa na utawala, ameona mengi na chama chake ni cha pili kwa kura (jambo litakalomfanya awe Makamu wa Kwanza wa Rais kikatiba), lazima atashinikiza sera za chama chake katika Serikali,” alisema Talib na kuongeza kwamba kwa kuwa Karume atakuwa ameshamaliza muda wake, Rais atakayekuwapo atakuwa na kazi ngumu kukabiliana na uwezo wa Seif.

Mtazamo huo wa Talib ambaye anaamini Seif katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, anaweza kumfunika Rais ajaye wa Zanzibar, pia ulizungumziwa na Shamte ambaye kwanza alisema haamini kama wananchi kwa ridhaa yao wataipitisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa isipokuwa Serikali hiyo kwa mtazamo wake itapitishwa kimabavu.

Shamte ambaye kwa maoni yake itakayoundwa si Serikali ya Umoja wa Kitaifa bali Serikali ya CCM na CUF, alionya kuwa kitakachofanyika ni kumwingiza mpinzani ndani ya Serikali na hivyo vita ya upinzani itaendelea ndani ya Serikali.

Alionya kuwa ni rahisi kukabiliana na mpinzani aliye nje ya Serikali kuliko aliye ndani na kutoa mfano wa ugumu wa utawala unaoendelea katika nchi za Kenya na Zimbabwe.

Kuhusu sera za vyama hivyo, Talib alionya kuwa moja ya sera ya CUF ni kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali tatu ambayo alisema Seif anaweza kuishinikiza akiwa serikalini.

Mtazamo huo pia ulizungumzwa na Shamte ambaye alishauri kama wanataka kuunda Serikali ya CUF na CCM, vyama hivyo vinapaswa kabla ya hapo, vitunge ilani moja ya uchaguzi ambayo ndiyo itakayotumika kutengeneza sera zitakazotekelezwa na Serikali hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juu ya mtazamo wa wanasiasa hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Saleh Ramadhan Feruz na Mkurugenzi wa Taifa wa Uenezi na Uhusiano na Umma (Taifa), Salum Bimani, walisema japo hayo ni maoni yao, lakini wanapotosha mantiki ya maafikiano ya vyama hivyo yenye lengo la kuimarisha amani Zanzibar.

“Hayo ni maoni yao. Lakini hizo ni ndoto za Alinacha. Hao wengine wana lao walilolificha nyoyoni. Hawapendi kuona amani na utulivu na mshikamano Zanzibar.

Wanapenda fujo na ugomvi viendelee, sababu wanafaidika hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu. Wanaweza kufaidika na kampeni za wagombea wasiokuwa na nia njema,” alisema Bimani bila kuweka wazi wagombea anaomaanisha.

Kwa mujibu wa Bimani, wapo baadhi ya wagombea urais wa Zanzibar kupitia CCM wasiounga mkono maridhiano. Alisema wanaunga mkono hadharani, lakini faraghani hawaungi mkono.

“Sisi tunawaambia siasa za chuki zimeshapitwa. Wazanzibari wanatazama mbele, wanajali maslahi yao na vizazi vyao. Hawatazami tena kwenye ugomvi wala hawarudishwi kwenye ugomvi,” alisema Bimani.

Akieleza kushangazwa na maoni ya wanasiasa hao, Bimani alisema CCM ina viongozi makini, chini ya Rais Jakaya Kikwete ambao walitafakari kabla ya kuamua na wasingeweza kukubali jambo ambalo baadaye litaleta matatizo. Vivyo hivyo, alisema CUF haiwezi kukubali kufanya mambo yasiyo na maslahi kwa Taifa.

Akizungumzia kilichoelezwa kwamba Serikali ya pamoja itabadilisha Katiba na kuathiri Muungano, Bimani alisema marekebisho yatakayofanyika CUF inaamini ndiyo yataimarisha pia Muungano.

“Viongozi kama hao wenye mawazo mgando wamekwishapitwa na wakati. Tunakwenda mbele, tunasubiri kura za maoni, “ alisema na kusisitiza kwamba anaamini asilimia 99 zitakuwa kura za ndiyo.

Feruzi, pamoja na kusema kuwa uamuzi wa chama ulizingatia mengi zaidi ya hoja za wanasiasa hao, alisisitiza kwamba ushirikiano huo si wa Karume na Seif bali ni wa vyama vya siasa. “Hizo ni dhana potofu au kutokuelewa. Karume ana dhamana ya nchi; akiwa Rais anabeba dhamana ya nchi na wote waliomo.

Alisema Karume alikuwa na jukumu la kufanya jitihada kutafuta ufumbuzi wa kurekebisha machafuko ya Zanzibar kwa kukaa na Seif kwa kuwa ndiye alikwa sehemu ya mgogoro huo, na kamwe asingeweza kumwita kiongozi wa chama kingine kwa sababu hawakuhusika.
“Jitihada hizo inategemea ni nani ni sehemu ya hilo tatizo.

Kwa siasa za Zanzibar mtu wa kukutana ni wa CUF na lazima awe Katibu Mkuu, asingeweza kuzungumza na NCCR kwa sababu si mdau.

Hapa hakuna ushirika, urafiki wala udugu zaidi ya kwamba ni watu wawili viongozi walioona wana wajibu na hasa Karume aliyeapa kikatiba kulinda na kutetea wananchi,” alisema Feruz.


Alishutumu watu wanaotaka kugeuza makubaliano hayo kuwa suala binafsi kwa kusema, “mtu anayelifanya hili kama jambo binafsi, ana tatizo la kutoelewa mipaka, wajibu na majukumu ya Rais, katika kutimiza majukumu yake. Sina hakika hao pengine wangefurahi kumwona Karume akipiga raia.”

Akizungumzia kile kinachosadikiwa kuwapo wanaounga na wasiounga mkono Serikali ya pamoja, Feruz alisema, “katika mkusanyiko, hamwezi kuafikiana kwa asilimia 100. Wapo wenye mitazamo tofauti .”

Kama alivyosema Bimani wa CUF, Feruz pia alisema katika uwanja wa siasa, yumkini wapo wanaofaidika na hali ya vurugu. “Wengine wanaweza kufaidika katika hali ya vurugu, lazima wachochee. Wengi tunaamini kuwa siasa inafanyika vizuri katika hali ya maelewano. CCM inasimamia sera ya amani, utulivu na mshikamano.

“Msitarajie nyakati za sasa ikawa sawa na miaka ya 1960, 70 na 80. Sasa si nyakati za siasa za kushupaliana,” alisema na kuwataka Wazanzibari wasikubali ushawishi na kuongeza, kwamba ndani ya kipindi si kirefu wataona faida ya kukaa kwenye amani.

Jana alipokuwa akifunga kongamano la viongozi wa matawi ya CCM katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu Tanzania, Rais Karume aliwataka viongozi katika vyuo kuitumia vyema elimu yao kusimamia umoja, mshikamano, amani na utulivu.

Aliwataka vijana hao kuepuka viongozi wenye lengo la kuondosha amani, utulivu na mshikamano nchini .

Alisisitiza kwamba lengo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wasilifanye sababu ya kugawa wanachama, na wajue kuwa ni hatua ya kuondoa uhasama na kuendeleza amani na utulivu nchini.

Source: Habari Leo
 
CCM na CUF wasaini MoU kabla ya kuunda serikali ili wabainishe mambo watakayoshirikiana isijetokea mgongano wa itikadi za vyama!
 
Back
Top Bottom