Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,314
- 33,108
Diwani wa Kata ya Machame Mashariki, Rajabu Nkya, akiwa karibu na mti ulioangushwa na wapasuaji haramu wa mbao katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika mlima huo.
Uhalifu wa ukataji miti na upasuaji wa mbao katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ambao umefumbiwa macho na mamlaka husika, umezidi kudidimiza Mkoa wa Kilimanjaro katika lindi la umaskini.
Wataalamu wa maji mkoani humo wanaeleza kwamba kiwango cha maji ardhini (water table), kinazidi kushuka wakati ambao pia chanzo kikuu cha maji ambacho ni Mlima Kilimanjaro kikiendelea kuteketezwa.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya mlima huo walisema katika miaka ya hivi karibuni wameshindwa kuendesha kilimo cha mbogamboga kwa kuwa mito na mifereji imekauka hivyo wanakosa maji ya kumwagilia mashamba yao.
Mkazi wa Kijiji cha Kifuni, Kata ya Kibosho Magharibi, Peter Boniface, aliiambia NIPASHE kwamba hali hiyo inaongeza umaskini kwa wananchi ambao wanategemea kilimo kama njia kuu ya uchumi.
Kwa sababu mifereji yote imekauka, kwa sasa tunaziba maji kwenye mto unaotiririsha maji kidogo kazi hiyo inafanyika usiku kucha halafu alfajiri mwanakijiji anayekuwa ameziba maji hayo anaenda kuyafungulia kwa sababu yanakuwa mengi kiasi ndipo anamwagilia shamba lake, ijapokuwa haitoshelezi uwamgiliaji, alisema.
Alisema hata maji ya kutumia nyumbani wanalazimika kununua ya bomba kwa kuwa vyanzo walivyokuwa wakitegemea vimekauka.
Katika maeneo mengine hali ni hiyo hiyo ambayo imesababisha mgawo wa maji katika Manispaa ya Moshi hususan kwa wakazi wa Pausa na Soweto ambao hawapati maji kwa saa 24 kama ilivyokuwa imezoeleka.
Ofisa Maji wa Bonde la Pangani, Philipo Patrick, alisema maji yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Alitoa mfano kwamba mwaka jana mvua zilinyesha chini ya wastani hivyo kuathiri mtiririko wa maji hadi kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu linalotumika kuzalisha umeme.
Wiki ya 38 ya mwaka jana hadi wiki ya pili ya mwaka huu, maji katika bwala la Nyumba ya Mungu ni mita za ujazo 683.53 kiasi ambacho kinaweza kuzalisha umeme, lakini tumewaandikia wadau wa bwawa hilo ikiwemo Tanesco kuwajulisha juu ya hali hiyo, tumewaandikia pia wakulima kupitia vyama vyao juu ya kuendelea kupungua kwa maji ili pengine kupunguza migogoro baina yao na wafugaji, alisema.
Alisema upungufu wa maji unaendelea kusababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa kuwa wananchi watashindwa kulima kwa uhakika.
Hata hivyo, alisema upungufu huo unaongeza uharibifu zaidi kwa kuwa wananchi wanalima hadi kwenye vyanzo vya maji jambo ambalo ni hatari.
Akizungumzia Ziwa Jipe, alisema linakaribia kabisa kutoweka kwa sababu limemezwa na magugu maji.
Akizungumza na NIPASHE, Meneja Umwagiliaji wa Kiwanda cha Sukari cha Tanganyika Plantation Company (TPC), Mhandisi Brighton Nyamgege, alisema upungufu wa maji unaongeza gharama za uzalishaji kwa kuwa kiwanda kinatumia megawati tano za umeme kila siku kwa ajili ya kuendesha pampu zinazovuta maji yanayomwagilia mashamba ya miwa.
Alisema mito mingi imekauka hivyo kiwanda kinalazimika kutumia maji ya chumvi yanayotokana na mto Kikuletwa unaotoka Arusha ambayo wanayachanganya na maji ya visima yanayochimbwa na kiwanda ili kupunguza chumvi.
Hata hivyo, pamoja na kwamba kiwanda kinajiendesha kwa kutegemea pampu; mwenendo wa maji wa kila siku unaonyesha kwamba kiwango cha maji ardhini kinapungua.
Kwa hivyo tumeanza kuchimba visima vidogo vidogo ili tuvute maji kidogo ambavyo vinamwagilia hekta 50 hadi 60 awali tulikuwa tunatumia visima vikubwa vilivyokuwa vinatumia pampu za kuvuta lita za ujazo 500 kwa saa, alisema.
Alifafanua kwamba kiwanda kimekuwa kikifuatilia hali ya maji kila siku ili kuepuka athari zozote zinazoweza kutokea.
Alisema mito mikubwa iliyokuwa tegemezi kwa TPC kama Kikavu, Karanga na Weruweru, inatiririsha maji chini ya kiwango ambapo mita za geji zinazoruhusu umwagiliaji ni 498, lakini hivi sasa ni 456 ambazo hazifai kwa shughuli za kilimo.
Wakati hali ikizidi kuwa mbaya, mamlaka zinazosimamia Mlima Kilimanjaro zimeshindwa kudhibiti wahalifu wanaoingia msituni na kukata miti ovyo kwa ajili ya kupasua mbao, ambayo imekuwa ni biashara ya baadhi ya viongozi wa meneo yanayopakana na msitu.
CHANZO: NIPASHE