Ufisadi na biashara ya fedha haramu

The Genius

JF-Expert Member
May 29, 2018
673
1,000
UFISADI NA BIASHARA YA FEDHA HARAMU

...Mei 1998, Andrew Chenge, akiwa mwanasheria mkuu alihalalisha (Authorized) malipo ya dola 600,000 kwenda kwenye akaunti ya kampuni iliyoitwa Langley Investments Limited, kampuni iliyomilikiwa na aliyekuwa gavana wa benki kuu ya Tanzania, Dr. Idrissa Rashidi. Gavana Dr. Rashidi ndiye alikuwa na jukumu la kuidhinisha (Approve) fedha za malipo ya rada, ambayo masharti yake yalikuwa kwamba; kuifanya hazina ya dhahabu zilizopo benki kuu ya Tanzania kama dhamana ya mkopo huo kutoka Barclays. Dr. Rashidi alikubali pia kwamba, ikiwa Tanzania itakiuka masharti ya mkopo huo, basi sheria zitakazotumika katika mgogoro utakaoibuka, ni za Uingereza na sio za Tanzania. Septemba 20, 1999, Andrew Chenge, yeye mwenyewe alihalalisha kuhamisha fedha kiasi cha dola 1.2 milioni kutoka katika akaunti ya kampuni aliyomiliki ya Franton Investments Limited kwenda kwenye akaunti yake binafsi katika benki iliyoitwa ‘Royal Bank of Scotland’ ya hukohuko kisiwani Jersey, Uskochi.
Taarifa hizi zilipovuja, Chenge hakuonesha kuguswa na tuhuma hizo badala yake aliziita fedha hizo vijisenti. Wanasheria wa Andrew Chenge kutoka Uingereza na Marekani walikiri kwamba, mteja wao alihusika kutoa ushauri wa kisheria katika mradi wa manunuzi ya rada, lakini walikataa kwamba Chenge alisisitiza manunuzi hayo. Hata hivyo, haifahamiki ni vyanzo gani vya mapato alivyonavyo Andrew Chenge, vilivyomuwezesha yeye kuajiri wanasheria nguli na ghali kutoka Uingereza na Marekani.

Wakati wa majira ya vuli ya mwaka 2006, uchunguzi juu ya uhusika wa Andrew Chenge katika mradi wa rada, ulipamba moto. Norman Lamb alikutana na mawakala wa SFO na Wizara ya Ulinzi, katika jengo la Port Cullis ambalo linahodhi ofisi za baadhi ya wabunge wa Uingereza. Mpelelezi kutoka SFO alipendekeza kwamba mkutano huo ufanyike kwenye chumba tofauti na ofisi ya Lamb, kwa kuhofia kwamba ofisi hiyo inaweza kuwa imewekewa vifaa vya kunasa mawasiliano. Kusikia hivyo, Norman Lamb alighadhibika sana na tangu hapo akawa na hofu. Tarehe 5 juni 2008, Lamb alimuandikia wakala yule wa SFO, Bw. Carl Brown akimkumbusha kauli yake wakati uchunguzi ukiendelea. Lamb aliandika; ‘Ulisema kuwa wakati uchunguzi ukiendelea, kampuni ya BAE ilikuwa ikijua kinachoendelea na kwamba walikuwa na taarifa zako na mashahidi uliokuwa ukikutana nawo. Ulionesha kuwa maofisa wa BAE system wanaweza kunasa mazungumzo yako ya siri uliyofanya na mashahidi’.

Wakala wa SFO alijibu kuwa; si kweli kwamba alikuwa akifahamu kuwa BAE wananasa mazungumzo yake, isipokuwa alishauri kutotumia ofisi na maeneo rasmi ya mashahidi kwa ajili ya mahojiano, kama angalizo tu katika taratibu za kiuchunguzi, ilikuwa jambo la busara kuchukua tahadhari. Mbunge Norman Lamb, alijibu kuwa, matumaini yake ni kuwa hakukuwa na vinasa mawasaliano katika ofisi yake. Na kwamba hakuwa akifanya usafi katika ofisi yake mara kwa mara kwasababu hakutaka kuoenekana kuwa ana hofu ya kuwekewa vifaa vya kunasa mawasiliano.

Hata hivyo baadae taasisi ya SFO, ilidai kuwa, kampuni ya BAE iliajiri majasusi wa kufuatilia uchunguzi ule. Lakin kampuni ya BAE ilikana na kuita tuhuma hizo kuwa ni uzushi.

Inafahamika namna kampuni ya BAE system inavyofuatilia maadui zake, hasa katika biashara za silaha. Na hofu aliyokuwa nayo Norman Lamb inafanana na hofu aliyokuwa nayo Edward Hosea, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) nchini Tanzania. Mwaka 2007 Hosea aliwaambia wapelelezi kutoka Marekani kwamba; ‘Maisha yangu yapo hatarini’ na kuongeza kuwa ‘wanasiasa wa Tanzania hawagusiki katika sakata la mradi mchafu wa rada’. Hosea alikata tamaa ya kuwafikisha mahakamani vigogo waliohusika na ufisadi kwenye mradi wa rada lakini alikuwa na uhakika kwamba, wakuu wa vyombo vya ulinzi nawo walihusika katika kashfa hiyo. Hosea aliongeza kuwa anapokea vitisho kupitia ujumbe wa simu na barua, akitaarifiwa karibu kila siku, kuwa anapambana na watu matajiri na wenye nguvu. Hosea alieleza kuhusu mikutano nyeti ya serikali inavyosheheni ubabe na vitisho; ‘Unapoingia katika mikutano yao, wanataka ujione kuwa mdogo na wao uwaone kama miungu. Wanataka ufahamu kuwa wao ndio wamekuweka hapo. Usipokubaliana nawo, kuna hatari’- Alisema Hosea.

Mh. Hosea aliendela kutanabaisha kuwa kama vitisho vitaendela juu yake, atahama nchi. Wakati huo hali ya siasa za nchi ya Tanzania ilikuwa tete hasa katika uwanda wa demokrasia na imani ya wananchi kwa serikali yao ilikuwa ikipungua siku hadi siku. Usalama wa Hosea na baadhi ya wanasiasa waliokuwa mbele kutaka wahusika wachukuliwe hatua, ulitegemea zaidi nguvu ya taasisi ya SFO na vyombo vya kisheria vya Uingereza badala ya vyombo vya ndani ya Tanzania.

Dr. Christopher Cyrilo
FB_IMG_1631780855672.jpg
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom