Udini, ubaguzi na uchaguzi Uingereza

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Na Ahmed Rajab

KESHO ulimwengu utakuwa na Uingereza na Uingereza itakuwa na ulimwengu. Macho ya ulimwengu yataiangazia Uingereza. Masikio yake yatayatega huko na pua zitanusanusa yatayojiri nchini humo.

Kwa zaidi ya karne na nusu Uingereza imekuwa ikijigamba kwamba bunge lake ndilo mama wa demokrasia. Imekuwa ikijinadi hivyo tangu Januari 18, 1865 pale mwanasiasa John Bright alipotoa hotuba mjini Brighton akisema kwamba “Uingereza ni mama wa mabunge”.

Kesho ulimwengu mzima utaingiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua vipi wapiga kura wa taifa hilo watavyoitumia haki yao ya kidemokrasia ya kujichagulia wataowawakilisha katika bunge jipya. Kwa kuwachagua wabunge hao watakuwa pia wanachagua nani aiongoze serikali.

Mchuano halisi utakuwa baina ya chama cha Conservative cha waziri mkuu Boris Johnson na chama kikuu cha upinzani cha Labour, kinachoongozwa na Jeremy Corbyn.

Vyama kadhaa vidogo vitashiriki katika uchaguzi na kutakuwako wagombea huru wasiofungamana na chama cho chote.

Lakini hasa hasa hayo yatakuwa maashindano baina ya Johnson na Corbyn. Johnson anajulikana kwa kusema uongo uliomfikisha hapa alipofika katika siasa za Uingereza. Uongo wake ndio pia ulioifikisha nchi yake katika hii njia panda ya iwapo ijitoe au ibakie katika Muungano wa Ulaya (EU).

Wengi nchini Uingereza wanamuona kuwa ni mtu asiye na uadilifu. Hata hivyo, mbwembwe zake zinawafanya baadhi yao wamuone kuwa ana haiba ya kuendelea kuwa waziri mkuu.

Mshindani wake, Corbyn, ni mtu wa msimamo. Ni muadilifu asiye na mikogo na ambaye kwa miaka mingi amekuwa akiwatetea wanyonge na wanaodhulumiwa Uingereza na kwingineko duniani. Hata hivyo, kuna wenye kumuona kwamba hafai kuwa waziri mkuu.

Adui mkubwa wa Johnson ni Johnson. Licha ya haiba yake haonekani kuwa ni mkweli. Na adui mkubwa wa Corbyn ni Corbyn. Licha ya kuonekana kuwa ni mkweli haonekani kwamba ana haiba ya kuwa waziri mkuu.

Lakini Corbyn ameandamwa na adui mwengine aliye mbaya zaidi na mwenye sumu kali. Adui huyo ni vyombo vya habari vyenye kutumiwa idara za ujasusi wa kijeshi za Marekani na Uingereza. Idara hizo zimekwishaamua kwamba Corbyn hatowafaa akiwa waziri mkuu na hawataki awe waziri mkuu.

Hoja inayotumiwa na isiyo na mantiki ni kwamba eti Corbyn ni kitisho kwa usalama wa Uingereza na nchi nyingine zilizo katika Umoja wa Kijeshi wa NATO.

Kila uchao vyombo vya habari vyenye kushawishiwa au kutumiwa na kampeni za idara za usalama za Uingereza na Marekani humuandama Corbyn. Kampeni hizo zina njama za kumfanya Corbyn aonekane kuwa ni mharibifu au mwangamizi atayetumiwa na Urussi.

Takriban kila siku vyombo hivyo vya habari hutafuta jambo la kuonesha kwamba Corbyn hafai kuwa waziri mkuu. Mara nyingi huwa wanamsingizia mambo yasiyo ya kweli au huupotosha ukweli.

Mfano mzuri ni msimamo wake kuhusu Israel na siasa za Uzayoni za watawala wa huko. Msimamo huo umemponza Corbyn kwa sababu umepotoshwa kusudi na vyombo vya habari pamoja na wenye kumuunga mkono Johnson.

Walianza kwa kumtuhumu kwamba amekuwa akiwadekeza bila ya kuwachukulia hatua wanachama wa chama cha Labour wenye chuki dhidi ya Wayahudi. Halafu wakazikuza tuhuma hizo na kumfanya Corbyn aonekane kwamba yeye binafsi ni mbaguzi mwenye chuki na Wayahudi.

Ajabu ya mambo ni kwamba kuna watu wanaoziamini tuhuma hizo licha ya kwamba Corbyn miaka yote amekuwa akijulikana kuwa anapinga ubaguzi wa aina yoyote, pamoja na ule dhidi ya Wayahudi.

Wanachofanya kwa kusudi adui zake ni kuugeuza upinzani wake dhidi ya Uzayoni wa serikali ya Israel uonekane kuwa ni ubaguzi dhidi ya Wayahudi.

Tuhuma hiyo dhidi ya Corbyn haina hata chembe ya ukweli. Lakini imekuwa ikitajwa na kukaririwa mara kwa mara na imewafanya baadhi ya watu waiamini.

Tuhuma hiyo imeufuata mkondo ule ule wa uvumi kugeuka na kuwa kweli. Na ilipata nguvu mwishoni mwa Novemba alipojitokeza kuhani mkuu wa Wayahudi wa Uingereza na wa Jumuiya ya Madola, yaani ulamaa wao mkuu, Ephraim Mirvis, akisema kwamba Corbyn hafai kuwa waziri mkuu.

Swali la kuulizwa ni: kwa kiwango gani tuhuma hizo zitamuumiza Corbyn kwa kuwafanya wapigaji kura wasiwachague wagombea wa chama chake cha Labour? Kwa maoni yangu sidhani kwamba wenye kuziamini shtuma hizo dhidi ya Corbyn wataweza kuwazuia wapiga kura wengi wasiwapigie kura wagombea wa chama cha Labour.

Inakisiwa kwamba idadi ya Wayahudi wa Uingereza inakaribia 300,000. Lakini Wayahudi hao wa Uingereza si kitu kimoja. Wamegawika kimadhehebu, kisiasa, na kijamii. Kwa hivyo, kuhani mkuu Mirvis hawezi kuwa ametoa maoni yake kwa niaba ya Wayahudi wote.

Miongoni mwa hao Wayahudi laki tatu, labda kasoro ya robo yao ndio waumini wa madhehebu ya kuhani Mirvis. Na hata hao walio madhehebu mamoja na Mirvis si wote wenye kukubaliana naye.

Lakini magazeti, mitandao ya kijamii na taarifa za habari za baadhi ya steshini za televisheni hujaribu kuonesha kana kwamba Wayahudi wote hawamtaki Corbyn.

Ndio maana baada ya kumshambulia Corbyn hadharani, Mirvis mwenyewe naye alishambuliwa na Wayahudi wenzake.

Kuna waliosema kwamba ametumiwa na Mossad, shirika la Ujasusi la Israel, kumchafua Corbyn. Wengine wamekuwa wakisema kwamba Mirvis toka hapo amekuwa akiwaunga mkono waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pamoja na Boris Johnson.

Msimamo wa Corbyn kuhusu Israel unamtapisha Netanyahu kwani Corbyn amekwishaahidi kwamba akiwa waziri mkuu serikali yake itaitambua dola ya Palestina na Uingereza itaacha kuiuzia silaha Israel pamoja na Saudi Arabia.

Bila ya shaka watakuweko wataokipinga chama cha Labour kwa sababu ya hizo tuhuma za kuwa na chuki na Wayahudi. Hata hivyo, siamini kwamba watakuwa na wingi wa kura za kuweza kubadili matokeo ya uchaguzi.

Nionavyo ni kwamba ni watetezi wa chama cha Labour katika majimbo ya uchaguzi mawili au matatu tu wataoweza kuathirika kwa hatua ya kutopigiwa kura kwa sababu ya shutuma hizo.

Mirvis ameungwa mkono na Justin Welby, Askofu Mkuu wa Canterbury ambaye ni mkuu wa kanisa la Kianglikana la Uingereza. Welby hakumtaja kwa jina Corbyn wala chama chake cha Labour, lakini alisema tu kwamba matamshi ya Mirvis yanaonesha hofu kubwa waliyonayo Wayahudi wa Uingereza.

Msemaji wa Baraza la Waislamu la Uingereza pia hakumtaja Corbyn wala chama chake. Hata hivyo, alisema ya kuwa matamshi ya Mirvis yanaonesha hofu iliyotanda miongoni mwa Wayahudi kwa kuwepo chuki dhidi yao nchini Uingereza na kwenye medani ya siasa.

Aliongeza kwamba Baraza hilo linakubaliana na kuhani mkuu kwamba baadhi ya wanasiasa wameonesha ushujaa lakini wengi wamekaa kimya.

Msemaji huyo wa Baraza la Waislamu alikumbusha kwamba chuki dhidi ya Waislamu nayo imeenea nchini na imeshamiri ndani ya chama kinachotawala cha Conservative. Waislamu, alisema, wanakabiliwa na kitisho kutokana na chuki hiyo yenye kuvumiliwa na kupuuzwa ndani ya chama hicho.

Wakati huohuo kumekuwa na kampeni miongoni mws makundi ya Kiislamu ya kuwataka Waislamu wakipigie kura chama cha Labour. Makundi hayo yamechukua hatua hiyo kwa sababu ya chuki dhidi yao inayopaliliwa ndani ya chama cha Conservative na wanayosema inaenezwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwemo waziri mkuu Johnson.

Kadhalika, makundi hayo yanataka Waislamu wakiunge mkono chama cha Labour kwa sababu ya msimamo wake wa kupinga ubaguzi wa aina yoyote na kwa sababu inazipinga sera za Israel kuhusu Palestina.

Pamoja na yote hayo, makundi hayo ya Waislamu pia yamevutiwa na ahadi aliyoitoa Corbyn ya kuzuia kuiuzia silaha Saudi Arabia ili kuinyima uwezo wa kufanya mashambulizi nchini Yemen.

Baraza la Wahindu, kwa upande wake, limejitokeza wazi kuwahimiza Wahindu wasikipigie kura chama cha Labour. Kwenye taarifa ambayo baraza hilo limetoa kumuunga mkono kuhani Mirvis, baraza hilo limehoji kwamba chama cha Labour kinawapinga Wahindu na kinawapendelea Waislamu.

Wahindu wamekerwa na matamshi makali ya chama cha Labour yaliyoilaani hatua ya India ya kuliondoshea jimbo la Jammu na Kashmir hadhi yake maalum ya kuwa na katiba yake ya kujiendesha lenyewe.

Ajabu ya mambo ni kwamba msimamo wa chama cha Labour kuhusu suala la Kashmir hautofautiani hata chembe na msimamo rasmi wa serikali ya Boris Johnson.

Uchaguzi ni uchaguzi lakini huo utaofanywa kesho Uingereza utakuwa wa babu kubwa. Usishangae ukiviona vyombo vya habari vya dunia vikiupa kipaumbele uchaguzi huo kana kwamba hakuna jengine la maana litalokuwa linatokea duniani.

Uzito wa taarifa kuhusu uchaguzi huo utakuwa mkubwa kushinda ule wa matukio mingine ya kimataifa. Majukwaaa ya kijamii nayo yataingia kama upupu utaowawasha wanayoyatumia wasilione jengine la kulizungumzia isipokuwa uchaguzi wa Uingereza.

Uchaguzi huo wa kesho ni uchaguzi wenye umuhimu mkubwa zaidi kushinda takriban chaguzi zote za Uingereza tangu nchi hiyo na nchi washirika wake zilipoishinda Ujerumani na Italia vitani Septemba 2, 1945. Una umuhimu mkubwa kwa sababu utaamua mengi kuhusu mustakbali wa Uingereza na hususan suala la Brexit, la Uingereza kujitoa kutoka Muungano wa Ulaya. Wenye kutaka kujitoa wanauona uchaguzi huo kuwa ni wa kufa na kupona.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Chanzo: Raia Mwema







Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ahmed rajab analia lia baada ya tegemeo lao corbyin kupigwa chini

Corbyin hawezi kuwa kiongozi ndani ya Uingereza na hata Ndani ya chama wamemchoka

Labor wamekuwa wakitumia masikini kujipatia kura ila hawajawasaidia kwa chochote
 
Zote porojo tu, ukweli ni kwamba Corbyn ni Communist, na Wazungu Anglo Saxon hawataki communism, huyo ni taipu ya Bernie Sanders, AOC au Obama.
Communist ni anti christ.

Waingereza wamechagua Johnson sababu hawataki communism kama ambavyo USA wamechagua D.Trump, D.Trump alisema USA will never be a communist country!
 
Unaweza uchambua uchaguzi wa hapa bongo namna hii na kuchambua tabia za mgombea mmoja mmoja na ukavuka 2020?
 
Mbona huyu Rajab hajawahi kuandika chochote kuhusu mateso ya Wakristu huko Pakistan? Mnafiki mkubwa huyu
Yani huyu nilishamgutukia toka mwanzo hana lolote.
Na niliwahi kusema humu jukwaani mpango wa waislamu kushawishiana wapige kura labour mzee Mohammed Said nilimwambia pamoja na Zurri.
.
Kuhani mkuu wa Wayahudi anamwita ulamaa kweli hii ni akili au maugondo?
Hafahamu kipi kiliitoa Labour madarakani
 
Back
Top Bottom