SHIRIKA la Usafiri Jijini Dar es Salaam (UDA), limebinafsishwa kwa Kampuni ya Simon Group Limited kwa bei ya kutupwa ya sh milioni 285 badala ya sh bilioni 1.4.
Kibaya zaidi, shirika hilo limebinafsishwa kwa kampuni hiyo bila kuwashirikisha wanahisa kwa sababu zisizojulikana.
Wanahisa wa shirika hilo linalokadiriwa kuwa na mtaji wa sh bilioni 12 ni Jiji la Dar es Salaam (24.5), Serikali (23) na asilimia 52.5, zimechukuliwa na mwekezaji mpya ambaye ni Simon Group Limited.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa Simon Group Ltd, yenye makao yake jijini Mwanza, imeuziwa hisa 52.5 za UDA ambazo zilikuwa chini ya Msajili wa Hazina.
Katika moja ya barua ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Februari 28 mwaka huu, iliyotiwa saini na ofisa aliyejitambulisha kwa jina moja la Mgendera, kwenda kwa Meneja Mkuu wa UDA, ilimuagiza asitishe uuzaji wa hisa hizo kwa madai kuwa shirika hilo la umma lipo chini ya Consolidated Holding Corporation (CHC) wanaosimamia ubinafsishaji wa mashirika ya umma.
Aidha, uchunguzi umebaini kuwa mnunuzi huyo amepewa baraka za ununuzi na bodi ya wakurugenzi ya UDA, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Iddi Simba.
Simon Group Ltd imelipa shilingi milioni 285.6 ambazo ni asilimia 12 ya hisa za UDA zipatazo 15,000,000.
Kwa mujibu wa nyaraka za mauzo ya shirika hilo ambazo nakala zake tunazo, zinabainisha kuwa Machi 4, mwaka huu, kampuni hiyo iliilipa UDA sh milioni 200 kwa stakabadhi namba 16628, na stakabadhi namba 16629 ya sh milioni 85 ikiwa ni sehemu ya malipo ya hisa 7,880,303, sawa na sh 145 kwa kila hisa.
Malipo hayo yalifanyika kwa ahadi kuwa hisa zilizosalia zingelipwa ndani ya siku 120, jambo ambalo halikufanyika hadi Juni 10, mwaka huu.
Badala yake inadaiwa kuwa mwekezaji huyo, alifika katika ofisi za UDA na kujitangaza kuwa ndiye mwekezaji mpya aliyenunua hisa za UDA kwa asilimia 52.5.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group Ltd, Robert Kisena, anadaiwa kuvunja ofisi ya Meneja Mkuu wa shirika hilo, Victor Milanzi na kuchukua nyaraka muhimu zikiwamo hati za umiliki wa ardhi na kutuma ujumbe wa maandishi kwa njia ya simu ya mkononi, akitishia maisha ya Milanzi.
Kwa mujibu wa habari hizo, Meya wa Jiji, Didas Masaburi, alishuhudia siku mwekezaji huyo alipofika ofisi za UDA na kumuondoa meneja wake, Milanzi.
Milanzi alichukua tahadhari ya vitisho hivyo kwa kutoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime na kufungua RB namba 4610/2011, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.
Alipohojiwa na gazeti hili juu ya kuwapo kwa taarifa hizo, Kamanda Misime alikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini alisema wametumia busara kurudisha suala hilo mikononi mwa wahusika.
Ni kweli tumefikishiwa tuhuma hizo nasi tukawashauri wakayazungumze kwa kuwa tumebaini mkataba wa UDA na mwekezezaji una hitilafu zinazosababisha misuguano hiyo, alisema Kamanda Misime.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA, Iddi Simba, alipohojiwa ushiriki wa bodi yake katika sakata la mwekezaji huyo, alisema suala hilo amelipeleka kwa wahusika ambao ni Consolidated Holding Corporation (CHC), hivyo hawezi kulitolea maelezo yoyote kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka.
Mkurugenzi wa Simon Group Ltd, Robert Kisena, alipoulizwa juu ya sakata hili, hakuwa tayari kutoa ushirikiano na badala yake alisema CHC wanatarajia kutolea ufafanuzi suala hilo.
Kwa upande wa CHC, msemaji wake, Joseph Mapunda, jana aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kukiri kuwapo kwa mvutano kati ya UDA na mwekezaji huyo.
Ni kweli kuna mvutano na mwekezaji, hivi sasa hatuna cha kuzungunza kwa vile ametufungulia kesi Mahakama Kuu ya biashara inayohusu madai. Mshitakiwa namba moja UDA na sisi washitakiwa namba mbili. Kesi hiyo ilifunguliwa Desemba 22, mwaka jana na kupewa namba 100/2010, alisema Mapunda.
Meya wa jiji alipohojiwa juu ya ushiriki wake kumngoa Milanzi, alisema alihusika kwa kuwawakilisha wana hisa upande wa jiji, baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mwekezaji huyo kuwa fedha alizonunulia hisa zimetumika vibaya.
Ni kweli nilihusika kumsimamisha meneja wa UDA kwa kuwa mwekezaji alilalamika namna fedha alizotoa zilivyotumika vibaya, nikachukua hatua za awali ili kunusuru hali hiyo, ikiwamo kufunga akaunti zote, alisema Masaburi.
Akizungumzia mkataba uliotumika kuruhusu mwekezaji huyo kumiliki shirika hilo la umma, alisema mkataba huo aliukuta umeshasainiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa UDA, hivyo asingeweza kuingilia kati kwa kuwa mahakama ndiyo inaweza kuutengua.
Unajua mwandishi, ule mkataba nimeusoma, kuna vitu vingine kama vile hisa alizouziwa Simon Group ni zile ambazo hazijagawiwa ambazo ni asilimia 52.5, jiji linamiliki asilimia 24.5 na serikali inamiliki asilimia 23, ukiangalia mwekezaji anaunda timu ya utawala, alisema.
Aidha, alisema hivi karibuni madiwani watafanya kikao ambapo pamoja na mambo mengine watachambua kuona kama mkataba huo una maslahi kwa taifa au la
Kwa upande wake, Milanzi alisema hakutendewa haki kwani bodi iliyomwajiri, ndiyo yenye mamlaka ya kumwachisha kazi.
Mimi niliajiriwa na bodi ya wakurugenzi wa UDA na ndio wanaopaswa kunipa barua ya kuniondoa kazini, haiwezekani dhamana niliyopewa ya kuongoza na kusimamia shirika la umma nikabidhi bila maandishi, alisema Milanzi.
UDA ina mtaji unaofikia sh bilioni 11.7, yakiwemo mabasi 20, wafanyakazi 120 samani za ofisi, maghala na maeneo ya wazi.
|
| |