Uchama kuelekea uchaguzi 2025

Uchama kuelekea uchaguzi 2025

Dr Adam Francis

JF-Expert Member
Joined
Aug 12, 2011
Posts
464
Reaction score
687
Mwaka huu, 2025, bila shaka tutapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Tayari wanasiasa wengi wakongwe na wanaoibuka wameshaanza harakati za kusaka bahati yao kuifikia nchi ya ahadi iliyojaa mishahara mikubwa, maposho makubwa, mafao manono, sifa uheshimiwa na fursa za nafuu zingine mbalimbali.

Katika mazingira ya sasa ya nchi yetu, ambapo nafasi za uongozi wa kisiasa sio tu ni fursa ya kuwatumikia wananchi bali pia ni mchongo ambao ukitiki basi umetusua kimaisha, uchaguzi kwa wanasiasa wetu utegemewe kuwa ni jambo la kufa na kupona. Wapo watakaotaka kutumia makanisa, wengine misikiti, makabila, uzawa, waganga, uchawi, fitna, uongo, uchonganishi na hata uchochezi.

Wakati vurugu zote hizi zikiendelea, ni vyema wasomi, wachambuzi, wanaharakati, viongozi wa dini na wadau wengine kuwasaidia wananchi kuwapa tathmini sahihi ya mambo ili wapige kura zitakazotuletea tija sasa na kwa miaka mia moja au zaidi. Wajibu huu usipofanywa kikamilifu uchaguzi wa mwaka huu hautakuwa na tija yoyote kwa nchi yetu.

Changamoto kubwa ya siasa zetu sasa ni kukua kwa UCHAMA! Huu ni ugonjwa mkubwa sasa ambao umeleta upofu, ububu na uziwi hata katika mambo yaliyodhahiri kuwa hayana tija kwa nchi yetu. Maamuzi ya nani apigiwe kura hayazingatii tena sifa na ubora wa mgombea bali chama chake tu. Uchama wa namna hii umezaa tathmini za jumla jumla za ulaghai. Mathalani utasikia mtu akisema chama fulani wezi au chama fulani wachochezi na hata kusema chama fulani wadini? Mambo ya namna hii yanafanywa kwa makusudi na wanasiasa kuwachanganya wananchi ili watekeleze mob justice kwenye masanduku ya kura.

Kama tukiyatazama mambo katika mizania isiyoelemea upande wowote wa kisiasa, kabla hujakifungamanisha chama fulani na tabia ya mtu fulani, ni kwanini tusifungamanishe tabia hasi za tunayemtuhumu ama na dini yake, au na kabila lake au hata jinsia yake? Ni jambo gani haswa linalotufanya tuzifungamanishe tabia hasi za mtu na chama kizima.

Jambo hili ukiacha ukweli kwamba linapuuza uhalisia kuwa hakuna chama, wala dini, wala kabila linaloweza kusimamia na kuratibu mawazo na maamuzi ya wafuasi wake, pia linawabebesha wasiohusika lawama kwa makosa ambayo hawakushiriki. Ipo hatari ya wananchi kumkosa diwani safi ambaye angewaletea maendeleo na kwasabu ya zogo la hao wezi hao wezi ambalo hata halijathibitika.

Ili kujenga, kudumisha na kuendeleza siasa za ushindani zakistaarabu ni vyema wanasiasa wetu wakajadili maswala ya kisera ya kitaifa, wakatueleza sifa zao za kiutu, kimaadili na kiuongozi kama sababu za kushawishi wachaguliwe badala ya kuongoza mazogo yanayoelekeza wananchi kwenye mob justice.
 
Back
Top Bottom