Uchaguzi wa Yanga sarakasi

Pistol

Senior Member
Oct 13, 2015
194
86
WAKATI Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikisogeza mbele uchukuaji fomu ya uchaguzi wa Yanga, uongozi wa Yanga klabu hiyo umejitangazia mchakato wao wa uchaguzi tofauti na ule wa TFF.

Uongozi huo wa Yanga umeenda mbali zaidi na kudai kuwa wana ushahidi wa wazi kuwa baadhi ya viongozi wa serikali, TFF na baadhi ya wanachama wao wana nia ovu ya kuhakikisha Yanga inasambaratika.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deosdedit, alisema hawaitambui Kamati ya Uchaguzi ya TFF wala mchakato ulioanza na kuwashangaa wanachama ambao tayari wamechukua fomu TFF na kwamba uchaguzi wa Yanga utafanyika Juni 11 mwaka huu.

“TFF haina leja ya Yanga, inajuaje hao waliochukua fomu kuwa ni wanachama halali wa Yanga, hawatambui uongozi Yanga, lakini TFF hiyohiyo imeomba fedha Sh milioni 11 kwa ajili ya usimamizi wa uchaguzi wa Yanga. “Yanga hatuwezi kuwapa fedha hizo na badala yake tutazielekeza kwenye kamati yetu ya uchaguzi, ambayo Mwenyekiti wake atateuliwa na Bodi yetu ya wadhamini muda wowote kuanzia kesho, ” alisema Baraka.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema: “TFF imemwaga mboga, basi sisi tutamwaga ugali, tunawaambia wasithubutu kuingilia uchaguzi huu.'

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja kuitaka TFF kumuwajibisha ofisa wake kabla serikali haijaangusha rungu lake kwa ofisa huyo aliyedaiwa anahujumu uchaguzi wa Yanga. BMT inadai ofisa huyo amekuwa na mkakati wa kuhakikisha uchukuaji fomu unakwama na wanaotaka kuwania uongozi wananyimwa fomu.

Kiganja alisema uchaguzi wa Yanga utafanyika kwa tarehe waliyopanga na si tofauti kwa kutumia kadi za mwaka 2010 na sio kadi mpya za Yanga.

Baraka alitangaza uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utafanyika Juni 11 mwaka huu, ambayo ni tofauti na Juni 25 iliyotangazwa na TFF. Baraka alisema fomu za wagombea zitaanza kutolewa leo huku kwa zile za Mwenyekiti na Makamu wake ni Sh 200,000, wakati zile za wajumbe ni Sh 100,000.

“Kuchukua fomu ni kesho (leo) na kesho kutwa ni mwisho wa kuchukua fomu, Juni 4 mchujo wa awali kwa wagombea na kuwajulisha wagombea, ikiwa ni pamoja na kubandika kwenye mbao za matangazo orodha ya wagombea. “Juni 5 kipindi cha kupokea pingamizi, Juni 6 na 7 pingamizi zote zitapitiwa na kufanya usaili wa awali, na kupeleka majina TFF ili kuhakikiwa na kutolea maamuzi kwenye Kamati ya Maadili na kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF,” alisema na kuongeza kuwa Juni 7 hadi 10 ni kampeni na siku inayofuata uchaguzi.

Hata hata hivyo, mchakato huo ni tofauti na uliotangazwa mapema na TFF, ambapo tayari wanamichezo tisa wamejitokeza kuchukua fomu kuomba nafasi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, waliochukua fomu kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Aaron Nyanda na Tito Osoro, wakati wajumbe ni Edgar Chibura, Pasco Laizer, Mohamed Mattaka, Omary Said, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Mchafu Chakoma.

Nafasi ya Mwenyekiti hakuna aliyejitokeza. Lucas alisema jana kuwa Kamati ya Uchaguzi katika kikao chake cha kufanya tathmini kilisogeza mbele mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mpaka Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya TFF, Aloyce Komba alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa Yanga alisema: “Mimi naendelea na mchakato wangu kama kawaida, huo uchaguzi wao wa chapuchapu mimi siufahamu, watajijua wenyewe.”

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Sina taarifa zozote za Yanga, wajitangazie tarehe wasijitangazie watajuana na wanachama wao.”


Chanzo: Habari Leo
 
Back
Top Bottom