SoC03 Uchafuzi wa mazingira uliokithiri ndani ya Ziwa Viktoria

Stories of Change - 2023 Competition

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,590
2,090
Habari wanajukwaa!
Ni wazi kuwa ustawi ulio imara wa binadamu unategemea kwa kiasi kikubwa mazingira, ikiwa mazingira ni mazuri na bora basi ustawi na maendeleo ya maisha ya mwanadamu huwa yenye Furaha na amani sana, ila mazingira yakiwa kwenye hali mbaya basi hata utamu wa maisha unakuwa unakosekana kabsa. Ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa, utupaji ovyo wa takataka kwenye vyanzo vya maji, yote haya na mengine huchangia maisha ya mwanadamu kuwa ni jehanamu ya ajabu sana.

Hakuna furaha yoyote kuishi kwenye ardhi ambayo ina ukame wakati miaka ishirini iliyopita tu eneo hilo lilikuwa limezungukwa na vyanzo kadhaa vya maji kama mito na mabwawa, hakuna ambaye anafurahi kutokwa jasho kwa jua kali Ubungo kwa kukosekana miti ambayo ingetumika kama vivuli na kupunguza makali ya jua.

IMG_1244.jpg

PICHA KWA HISANI YA BRILLIANT UGANDA.

Siku ya alhamis ya tarehe 4 mwezi wa tano mwaka huu nilipata safari ya kwenda wilaya ya Ukerewe, hivyo ilinibidi kupanda meli moja ambayo ni kawaida yake kufanya safari zake kutoka Mwanza mjini kwenda Nansio Ukerewe. Nikiwa kama mdau wa maendeleo na mtanzania anayeipenda nchi yake niliona sio vyema kukaa kwenye kiti muda wote kutoka Kamanga mpaka Nansio hivyo nilikwenda kutazama uzuri na urembo wa ziwa nyanza maarufu kama ziwa viktoria. Moyo ulikuwa na hamu na Furaha kubwa kutazama injini za meli zikirusha maji kwa fujo huku tukiiaga Kamanga ila punde tu ndani ya dakika 10 nilipatwa na huzuni sana.

Mboni za macho yangu zilishuhudia kiwango kikubwa sana cha taka zikiwa zinaelea katika ziwa hili pendwa ambalo ndo linaipatia sifa Tanzania kwa kutoa samaki aina ya sato. Kuanzia chupa za plastiki za vinywaji baridi, vifungashio vya bidhaa, yaani uchafu wa kila aina ulikuwepo. Niliumia sana kwenye moyo wangu, ila wakati naugulia maumivu baadhi ya abiria wananitonesha zaidi kwani nilishuhudia abiria wakiwa wanakula mahindi ya kuchemsha huku uchafu wakitupa ziwani. Hapo nilishindwa kuvumilia na kuamua kuwafokea na kuwauliza kwa ukali sana kwanini wanakuwa hawajali ustaarabu wa mazingira ya ziwa letu, lakini wao walidai kuwa ni kawaida kufanya vile sio leo, jana au juzi, ni mazoea ya kawaida kwa watu kuona ziwa viktoria kama jalala vile kwa kisingizio cha kuweka mbolea.

Leo natamani kuzungumzia kuhusu uchafuzi mkubwa wa mazingira katika ziwa viktoria kiasi kwamba jiji la Mwanza kukinyesha mvua basi taka zote zinaelekezwa ziwani. Sio sahihi hata kidogo kwani hapo tunazidi kuharibu ziwa letu, na hata kuharibu ekolojia halisi ya asili ya maisha ya viumbe ndani ya ziwa letu.
Ni wangapi wanajua kuwa ziwa viktoria ni uti wa mgongo wa Uchumi wa Jiji la Mwanza na Tanzania, wangapi wanajua kuwa ziwa hili limetoa ajira kwa watu? Je tumewahi kufikiria hata kidogo ni kwa kiasi gani ziwa hili limebeba hatma ya watu katika maisha yao? 55% ya samaki wote hutegemea ziwa kama makazi yao, huku zaidi ya viumbe milioni 1 kati ya viumbe milioni 7.8 wameshapotea, kama hauamini uliza samaki aina ya ningu, domodomo kama bado wanapatikana ndani ya ziwa hili.
IMG_1245.jpg

PICHA KWA HISANI YA INFO NILE

Mwaka 2020, kupitia ushirikiano wa shirika la CIWA wakiongozwa na kitengo cha Benki ya Dunia cha Water Global Pratice waliainisha vyanzo vikuu ambavyo ni mstari wa mbele katika kuchafua ziwa viktoria. Kwanza kabsa walionesha kuwa shughuli za kilimo kando kando ya ziwa zinachangania kwa ukubwa kuharibu mazingira ya ziwa nyanza, tazama maeneo ya Nera utakutana na watu wamelima pembezoni mwa ziwa bila hata tatizo lolote, jiulize vipi kuhusu matumizi ya kemikali ambazo zipo kwenye mbolea hizi zinakwenda kuharibu kabsa ekolojia ya ziwa.
IMG_1251.jpg

PICHA KWA HISANI YA NUKTA HABARI

Uingizwaji wa maji taka kutoka mitaa na viunga mbalimbali vya Jiji la Mwanza, kama wewe ni mkazi wa Mwanza basi utakubaliana na mimi kuwa mto Mirongo unaongoza kwa kuingia maji taka kwa kiasi kikubwa zaidi.

PICHA KWA HISANI YA NUKTA HABARI

Ukitaka kujua namna ambavyo ziwa nyanza linapokea kiasi kikubwa cha taka basi ikinyesha mvua sogea mpaka kituo cha kliniki Pembeni tu kuna ofisi za benki kuu, kando ya ofisi za idara ya maji, utaona maajabu ambayo utachukia maisha ya watu wanaoishi ndani ya jiji hili la Mwanza.

PICHA KWA HISANI YA EATV
Kwa hakika utachukia wakazi wa Mwanza kwa uchafu wa mazingira, kiasi cha maji na taka ambacho kinaingia kwenye ziwa ni kikubwa sana na hapo ni kwa siku moja, bado hatujiulizi hizo taka zinakwenda wapi, kama sio kwenda kuharibu mazalia na ekolojia ya viumbe ndani ya ziwa nyanza.
Na ndo maana mpaka leo vita dhidi ya magugu maji haijapata suluhu kwa kuwa mazingira machafu ndo makazi bora sana ya magugu maji, je nini kifanyike?

1. Serikali kupitia wizara ya mazingira iwaagize Baraza la mazingira NEMC kusimamia vyema zaidi mazingira ya ziwa Victoria, kwa maana huu ndo uhai wa Tanzania na jiji la Mwanza.

2. Uongozi wa jiji la Mwanza wakae chini na kutunga sheria na kanuni maalumu za kulinda hali ya mazingira ya ziwa Victoria.

3. Kuimarisha mifumo ya uzoaji wa taka kila mtaa na kuweka sehemu moja ya kutupa taka kwa kila kata, hii itapunguza mrudikano wa taka ambazo zinasubiria mvua ishuke ndipo watu wafungulie taka ziende na maji mpaka ziwani. Sio sahihi kabsa na ni kitu cha kukemewa vikali.

4. Kuweka mpango maalumu wa kukusanya taka ndani ya ziwa ili kuweka hali ya mazingira ya ziwa nyanza kuwa salama kwa viumbe. Ziwa nyanza ni mkombozi kwa wananchi wa Mwanza, kwani wanahitaji maji hayo kwa ajili ya matumizi ya kila siku, na pia ni kichochezi cha ajira ndani ya jiji letu la Mwanza.


PICHA KWA HISANI YA IPP MEDIA
Mwezi machi mwaka 2022 mkutano wa mazingira wa umoja wa mataifa ulikubaliana kuwa na kauli moja ya kulinda mazingira ya maziwa duniani kote, huku wakiwahimiza nchi wanachama wenye mmiliki ya maziwa kulinda, kurudisha asili ya maziwa na kutumia maziwa hayo kwa ustaarabu, pamoja na kuweka mipango sahihi ya kushirikiana kuyatunza.
 

Attachments

  • IMG_1250.jpg
    IMG_1250.jpg
    11.1 KB · Views: 2
  • IMG_1248.jpg
    IMG_1248.jpg
    42 KB · Views: 2
  • IMG_1247.jpg
    IMG_1247.jpg
    42.3 KB · Views: 3
  • IMG_1246.jpg
    IMG_1246.jpg
    116.3 KB · Views: 3
Back
Top Bottom