Tutaraji nini kwa waziri aliyeghushi cheti? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tutaraji nini kwa waziri aliyeghushi cheti?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Magezi, Nov 6, 2009.

 1. M

  Magezi JF-Expert Member

  #1
  Nov 6, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  [​IMG]
  Tutaraji nini kwa waziri aliyeghushi cheti?  Johnson Mbwambo
  Oktoba 28, 2009


  WIKI iliyopita mwanasafu mwenzangu wa gazeti hili, Lula wa Ndali Mwananzela, alinikuna alipoandika kwa uchungu kuhusu gharama tunazolipa kwa kuukubali ufisadi kuwa rafiki yetu wa kweli badala ya kuwa adui wetu wa haki.

  Naungana naye katika shaka yake kwamba hakuna maendeleo yoyote ya maana tutakayofikia kama tutaendelea kuukubali ufisadi kuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku; na hasa kama tutaona ni sawa tu kuongozwa na viongozi ambao ni mafisadi au walioingia madarakani kwa njia za kifisadi.

  Wiki hiyo hiyo ya jana, mwanaharakati mmoja wa Dar es Salaam ambaye pia ni mwanasheria, Kainerugaba Msemakweli, alijenga ujasiri wa kutangaza hadharani majina ya vigogo kadhaa, wakiwemo mawaziri na wabunge, ambao wamegushi vyeti na kuudanganya umma kuhusu viwango vyao vya elimu.

  Orodha hiyo ni nzito, tena ina vigogo ambao baadhi yao walikuwa watu muhimu katika kampeni ya Rais Jakaya Kikwete ya mwaka 2005.
  Katika nchi nyingine zenye raia wenye mwamko, tukio la mwanasheria huyo kuanika hadharani orodha ya vigogo hao lingewasha moto wa aina yake nchi nzima. Lakini si Tanzania.

  Ingekuwa ni nchi nyingine (hata hapo Kenya tu), yangetokea hata maandamano ya kuwataka vigogo hao waliotajwa ama kuthibitisha kuwa madai hayo ni ya uongo au kujiuzulu nyadhifa zao. Lakini si Tanzania.

  Hapa Tanzania ni business as usual. Hakuna anayetishika. Hakuna anayejali, na hakuna anayetaka vigogo hao wawajibishwe. Kwa nini? Kwa sababu tumefikia hatua ya kuukubali ufisadi kuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

  Kwa maneno mengine, tunaliona tendo la mtu aliyeghushi vyeti kuteuliwa kuwa waziri au kugombea ubunge, ni tendo la kawaida tu – nothing to write home about!
  Hata Rais wetu, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda ambao, katika hali ya kawaida, kutuhumiwa kughushi vyeti kwa mawaziri wao wangekuona ni sawa na kuchomwa mkuki moyoni, wamekaa kimya!

  Si wao wenyewe wala wasaidizi wao walioonyesha kukerwa na madai hayo, na hivyo hawakuona busara ya kuchukua hatua zozote. Wameamua kukaa kimya. Ni business as usual.

  Ni kama vile madai hayo mazito dhidi ya mawaziri hayaathiri credibility ya serikali na ya rais mwenyewe aliyewateua katika nafasi hizo za uwaziri.
  Na pengine ni kweli kwamba madai kama hayo hayawezi kuathiri credibility ya serikali. Yaathiri credibility ya serikali kwa nani? Kwa Watanzania ambao wamefikishwa mahali wakaukubali ufisadi kuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku?

  Baadhi yetu tunaoshangaa ni kwa nini madai hayo mazito dhidi ya mawaziri hao hayajafanya kope za kina Kikwete na Pinda zipepese, tunaonekana kama vile tumetoka sayari nyingine!

  Hapa ndipo tulipofikishwa. Sijui kiongozi wa Tanzania sasa atende ufisadi wa aina gani mkubwa ndipo kope zetu zipepese na hatua zichukuliwe; maana tumeukubali ufisadi kuwa ni sehemu ya maisha ya viongozi wetu.
  Kwa hakika, katika hili la mawaziri na wabunge walioghushi vyeti na kujiita madokta wakati si madokta, nawakumbuka wabunge wa Iran namna walivyoushughulikia ufisadi kama huo.

  Ilikuwa ni Oktoba mwaka jana wakati ilipobainika kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Kordani alikuwa na PhD feki ya Oxford – chuo kikuu cha Uingereza chenye heshima kubwa duniani.

  Wairan walikitilia shaka cheti hicho kwa sababu, si tu hawakuamini kwamba waziri wao alikuwa na bongo za kuweza kuwa mhitimu wa PhD wa Oxford, lakini hata Kiingereza alikuwa hajui kukizungumza vizuri; achilia mbali ukweli kwamba cheti chenyewe kilikuwa na makosa kadhaa ya lugha.

  Shaka hiyo iliwafanya waandishi wa habari na wanaharakati waingie kazini! Wakachunguza hadi Oxford kwenyewe ambako ilibainika Ali Kordan hajawahi kusomea shahada yoyote katika chuo hicho. Ilibainika pia kwamba maprofesa aliowataja kuwa ndiyo waliokuwa wasimamizi wake wakati akiwania shahada hiyo, hawakuwahi kuajiriwa na chuo hicho – yaani ni feki.

  Ushahidi huo ulipowekwa hadharani, Bunge la Iran likachachamaa. Ali Kordani akawekwa kitimoto bungeni, na hatimaye akakiri kuwa PhD hiyo ni feki. Wabunge wakapiga kura kumtimua ubunge na uwaziri. Hata uswahiba wake na Rais Ahmednejad haukumsaidia kitu.

  Kwa hiyo, hata Iran, ambayo demokrasia yake ni changa kama yetu, imetushinda katika hilo. Wairan waliona wamevunjiwa heshima mno kuwa na waziri aliyeghushi PhD ya Oxford, wakamtimua kazi. Lakini si Tanzania ambako tuna kigogo anayeaminika kughushi PhD ya Havard, na bado anadunda!

  Niseme pia kwamba katika hili la mawaziri wetu kughushi vyeti na kujiita madokta wakati si madokta, namkumbuka class mate wangu wa Mzumbe Sekondari, Alfred Ngotezi.
  [​IMG]

  Samuel Mchele Chitalilo

  Alfred Ngotezi alipata kuwania ubunge wa jimbo la Buchosa akipambana na mbunge wa sasa, Samuel Mchele Chitalilo. Ingawa Chitalilo alishinda, rafiki yangu Ngotezi aliletewa dossier iliyoonyesha kuwa mbunge huyo alidanganya kuhusu kiwango chake cha elimu, na kwamba cheti alichowasilisha wakati akiomba kuwania ubunge kilikuwa feki.

  Rafiki yangu Ngotezi, akiongozwa na mshawasha wa kuuonyesha umma kwamba Chitalilo hakuwa na uadilifu wa kustahili kuwa mbunge, akalivalia suala hilo njuga. Akasafiri hadi Uganda kwenye shule ambayo mbunge huyo alidai alisomea. Akathibitishiwa kwamba hakupata kusoma katika shule hiyo.

  Akarudi nyumbani na ushahidi wote. Akafikisha dossier nzima ya udanganyifu wa mbunge huyo kwa vyombo vinavyohusika, ikiwa ni pamoja na Bunge na chama chake cha CCM, lakini hakuna kilichotokea. Jamaa anadunda bungeni mpaka leo, na rafiki yangu Ngotezi hana raha mpaka leo kuona mtu aliyedanganya akiitwa “Mheshimiwa Mbunge.”

  Naamini kilichomvunja zaidi nguvu na kumkatisha kabisa tamaa, ni pale Rais Kikwete alipokwenda kwenye jimbo hilo na wakati akihutubia mkutano wa hadhara akawaambia wananchi: “Kuna kelele kelele nyingi dhidi ya mbunge wenu, lakini zisiwakoseshe usingizi.”

  Hebu fikiria: Madai mazito kama hayo yanayomkabili mbunge wa CCM, lakini Rais, ambaye ndiye pia mwenyekiti wa chama, anayapuuza kwa kusema; “kuna kelele zinapigwa dhidi ya mbunge wenu…zisiwakoseshe usingizi”.

  Hivi rais anayetoa kauli kama hizo kwa jambo zito kama hilo anaweza kweli kusimamia uadilifu wa watendaji wake? Na kwa kauli yake hiyo, alituma ujumbe wa aina gani kwa wapiga kura wale wa Buchosa na Watanzania kwa ujumla?
  Kwa hiyo, juhudi zote za rafiki yangu Ngotezi za kuuanika ufisadi wa mbunge, pamoja na pesa zake nyingi alizotumia, ziliishia ukingoni kama ambavyo juhudi za mwanaharakati Kainerugaba Msemakweli zitakavyoishia ukingoni.

  Nina hakika Kainerugaba alitumia muda na fedha zake nyingi kufanya utafiti wake huo wa miaka mitatu kuhusu madai ya elimu ya vigogo hao. Lakini nina hakika pia kwamba hakuna kitakachotokea; kwani mpaka sasa hakuna kope zilizopepesa. Ni business as usual. Ndivyo tulivyo, na ndipo ufisadi ulipotufikisha!

  Hebu jiulize: Hivi waziri anayedanganya hata katika masuala yanayohusu elimu yake mwenyewe, anaweza kuaminika katika mambo makubwa yanayohusu pesa na siri za serikali? Lakini ni nani wa kumnyooshea kidole wakati wengine wote nao wanaogelea katika ufisadi wa aina moja au nyingine?

  Hata hivyo, nimshukuru na kumpongeza Kainerugaba kwa kazi hiyo aliyojitolea kuifanya. Hata kama haitazaa matunda kwa sababu ya kuukubali ufisadi kuwa ni kitu cha kawaida katika maisha ya mawaziri na wabunge wetu, lakini yeye ametimiza wajibu wake wa kiraia.

  Angalau hatutahukumiwa na vitukuu vyetu kwamba sote tulikuwa mazezeta na majuha. Ukweli ni kwamba sote hatukuwa majuha. Walikuwepo kina Lula na kina Kainerugaba na wengine wengi waliojaribu kutufumbua macho, lakini hatukuweza kuyafumbua; kwa vile tulishaaminishwa kwamba ufisadi ni rafiki wa haki.

  Je, kuna jema lolote kubwa tunaloweza kulitaraji kutoka kwa waziri au mbunge aliyeghushi cheti? Jibu langu ni “hakuna”. Sana sana akili yake ataielekeza zaidi kwenye kughushi hati mbalimbali ili kuiba fedha za walipakodi (fedha za umma) kama ilivyotokea kwenye EPA.

  Halafu eti tunapaswa kuwakubali na kuwaheshimu kama viongozi wetu. Na si tu hao waliowateua kuwa viongozi; bali pia hata hao wenyewe walioghushi! Mimi moyo wangu unasita kwa hilo.

  Uko wapi ule utaratibu wa zama za Nyerere wa Vetting ambapo mtu alichunguzwa na Usalama wa Taifa historia yake, elimu yake, hulka yake, mienendo yake, uadilifu wake kabla hajapewa uongozi serikalini?

  Tafakari!!
   
 2. nguvumali

  nguvumali JF Bronze Member

  #2
  Nov 6, 2009
  Joined: Sep 3, 2009
  Messages: 4,864
  Likes Received: 143
  Trophy Points: 160
  hapo chakutaraji ni haya ya kina Sofia SIMBA na Makongoro Mahanga.
  Kwanza jiulize aliemchagua Waziri aliefoji Cheti hana vyombo vya uchunguzi ? au ni ule mfumo wa kupendeleana, na urafiki katika maswala yanayogusa mustakabali wa taifa, na jamii pana.
  Naamini kosa analo zaidi alie wateua, na ndio maana anawaonea haya kuwang'oa.
  Nchi inayumba, uchumi uko duni, watu wanakufa njaa, ujinga unaongezeka, hatutashangaa hata mauaji ya ushirikina ya hawa ALBINO chanzo ni aina hii ya watawala.
   
 3. C

  Choveki JF-Expert Member

  #3
  Nov 6, 2009
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 35
  Sasa kama viongozi wenyewe wapo hoi ki fikra utategemea nini? Binafsi sintoshagaa kama kuna baadhi ya hao viongozi ambao nao ni wanunuzi wa hivyo viungo vya maalbino ili waendelee kuwa kwenye uongozi(kutokana na watakavyoshauriwa na waganga wao)
   
Loading...