Siku na tarehe kama ya leo mwaka 2008 majira ya saa 2:30 asubuhi ndio siku ambayo baba yetu mpendwa mzee RK ulipoiaga dunia ukiwa na umri wa miaka 76. Ilikuwa ni Ijumaa ya terehe 4/1/2008 ndiyo siku ambayo baba yetu mpendwa alipoiaga dunia baada ya kuugua kansa ya koo kwa takriban mwaka mmoja.
Ulikuwa ni msiba mkubwa sana kwetu kutokana na juhudi zako za kutulea ukiwa peke yako baada ya kifo cha mama yetu hapo mnamo tarehe 1/8/1982 akikuachia jukumu la kulea watoto 8, watatu wa kike na watano wa kiume. Ingawa kaka zangu 3 na dada zangu 2 walishakuwa wakubwa kwa umri na kimo, ni mimi na wadogo zangu wawili, mmoja wa kike na wa mwisho wa kiume ndio tulioachwa na mama tukiwa na umri wa chini ya miaka 11.
Tunakumbuka kauli yako baada ya kifo cha mama yetu kwamba hutaoa mke mwingine mpaka hapo utakapotulea na kuwa watu wazima na kujitegemea na hiyo ilitokana na hofu yako ya malezi ya mama wa kambo kutokana na imani kwamba malezi ya mama wa kambo yana walakini. Sina uhakika sana na jambo hilo lakini huo ulikuwa ndio uamuzi wako.
Kwa juhudi zako na kwa kusaidiana na kaka na dada zangu ulimudu kutulea mimi na wadogo zangu hadi tukafikia umri wa kujitegemea. Ni mapenzi yako na malezi yako mahiri ndiyo yaliyoifanya familia yako ya watoto 7 tuliobaki, kushikamana hadi leo bila kusambaratika, baada ya dada yetu mkubwa na mlezi wetu aliyechukua jukumu la mama kufariki hapo mnamo tarehe 5/5/1994 kwa kifafa cha mimba.
Tumejifunza mengi sana kwako, lakini lililo muhimu sana kwetu ni kutusisitiza kujiamini na kujitegemea kwa kila kitu. Nakumbuka msemo wako kwamba mtegemea cha ndugu hufa masikini, msemo huu ndio ulikuwa kama kauli mbiu yako ya kutuchagiza kila mtu kujitegemea bila kutegemea msaada kutoka kwa ndugu.
Leo hii imetimia miaka mitano tangu ututoke, na tunakukumbuka sana kwa hekima na busara zako. Ulikuwa mcheshi na mwenye furaha wakati wote na hata pale ulipokuwa umezongwa na jambo, bado tabasamu lako lilikuwa halikuishi usoni pako, ilikuwa ni vigumu kwetu kujua ni wakati gani ulikuwa na huzuni, ulikuwa ni mwerevu wa kubadili jambo lililokukera na kuliweka katika mzaha na hivyo kutokukuumiza kihisia. Lakini hata hivyo, hukusita kuonyesha hasira zako pale ilipobidi.
Tumeendelea kufuata nyayo zako na hivi sasa familia yetu imezidi kushikamana na kuwa imara, na wote tunatamani kama ungekuwepo leo hii na kushuhudia kile ulichokipanda maana sasa ndio tunaona matunda ya malezi yako. Tumejijengea heshima mbele ya jamii sio kwa sababu ya mali wala fedha, bali kwa sababu ya hekima na busara ulizotuachia kama moja ya nguzo muhimu katika maisha.
Tunaomba Mwenye enzi Mungu aiweke roho yako mahali pema peponi, amina.