Tungo huru si mashairi

Idd Ninga

Verified Member
Nov 18, 2012
4,936
2,000
TUNGO HURU SI SHAIRI
Msiojua kutunga, leo nawapa salamu
Tungo mnazozitunga, siyo tungo mfahamu
Mnapaswa kujipanga, na mtunge kwa nidhamu
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Mashairi bila vina, si shairi mtambue
Nitasema mkinuna, mkitaka mjiue
Hapo utunzi hakuna, rukeni mjibenue
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Ushairi ni mizani, siyo lugha kubadili
Hili usipobaini, kwenye fani we jahili
Bora urudi shuleni, usije angushwa chali
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Wala beti hamjui, limradi kuandika
Na vichwa hamsugui, hamtaki kusumbuka
Lakini siwashangai, hampendi taabika
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Mnatungaje kitoto, ihali watu wazima
Acha niwatie joto, kuwasema ni lazima
Ninawapa mkong’oto, sina budi kuwasema
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Bora ubaki shabiki, kama kutunga huwezi
Hii fani ni mkuki, haushikwi na malezi
Nenda kwa mshika chaki, mwambie hujui wazi
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Watu hovyo mnaghani, mnasema ni utenzi
Nataka ruka vichwani niwapige na makwenzi
Hivi mnaghani nini, bora muimbe mapenzi
Leo naimwaga mboga, tungo huru si shairi.

Mkitaka cha kujibu, nijibuni kishairi
Ka vipi bakia bubu, bure usilete shari
Bure nikakusulubu, nikupige msumari
Asiejua kutunga, hutunga shairi huru.


SHAIRI -TUNGO HURU SI SHAIRI
MTUNZI-Idd Ninga,Tengeru Arusha.​
+255624010160​
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom