Tundu Lissu please, acha kumuibia Lowassa!

Tundu Lissu please, acha kumuibia Lowassa!

Interest

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2015
Posts
3,434
Reaction score
7,091
UKIWA na mtoto mdadisi ni tatizo, yeye hajui upo kwenye hali gani, linalokuja kichwani kwake anakushirikisha utake usitake.

"Baba eeeh," mtoto wangu aliniita.

"Naam Captain Nyambo" niliitka.

"Siku hizi ma-Lowassa hayapo barabarani, sijui nani kayaondoa. Ma-Lowassa yalikuwa mengi baba."

Nikamuuliza: "Ma-Lowassa ndiyo nini?".

Captain Nyambo: "Yale yalikuwa barabarani juu, yalikuwa mengi, nikiwa naenda shule au nikirudi nilikuwa nayaona yamening'nizwa juu, siku hizi hayapo".

Nikamwambia: "Ngoja nikwambie yale siyo ma-Lowassa, zile ni bendera, usije kuniaibisha mwanangu."
Akasema: "Aah bendera!" Kikafuata kimya kidogo, akaibuka na kingine:

"Hivi baba yule Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, unampenda au humpendi?"

"Kwa nini unaniuliza hivyo?" nilimuuliza.
"Mimi najua utakuwa humpendi tu," Captain Nyambo alisema.
"Nisimpende kwa lipi"?

Nilipomuuliza hivyo akacheka, akasema: "Mfano Jecha angekuwa tunakaa naye hapa nyumbani unafikiri ningekuwepo? Anapenda kubadilisha matokeo yule, noma sana, mimi mwenyewe namkubali kwa kubadili matokeo."

Nilinyanyuka kuelekea chumbani ili nimwache peke yake pale sebuleni, maana stori zake nilikuwa sizielewi na ukizingatia nilikuwa na yangu yananivuruga kichwa.

Nilifungua mlango wa chumbani kwangu vizuri, ile nimeingia nageuke nifunge, Captain Nyambo naye huyo, kumbe alikuwa ananifuata kwa nyuma kimyakimya.

"Baba wewe unanipenda sana, sasa Jecha anavyopenda kufuta matokeo, angeweza hata kuamua hata nirudi tumboni kwa mama yangu, sasa hapo ungenionaje? Ungeumia mwenyewe baba yangu unavyonipenda", alisema Captain Nyambo.

"Captain nasikia usingizi, naomba nilale tutaongea baadaye, wewe nenda kaendelee na katuni zako sebuleni," nilimwambia.

"Sawa baba yangu, nipe dakika tano halafu nitakuruhusu ulale, wewe ndiye Capteni Mkuu, nisipojadili mambo ya nchi na wewe, niende nikajadili na nani?"

Nikamwambia sawa, kisha akaendelea: "Hivi baba, Lowassa si anatamani Jecha ndiye angekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)? Maana yake sasa hivi tungekuwa hatujampata Dk John Magufuli na hapo ndipo utajua kuwa baniani mbaya kiatu chake dawa."

Akaniuliza: "Mbona naongea hunijibu?" Nikamwambia namsikia vizuri, aendelee, akasema: "Na kule Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad anaombea Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva ndiye angekuwa Mwenyekiti wa Zec, sasa hivi zamani angekuwa anafanya kazi kama Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar."

Captain Nyambo: "Baba amini usiamini, hakuna mtu mbaya kwa asilimia 100. Si unaona Jecha alivyo, Chelsea wanatamani ndiye angekuwa bosi wa Chama cha Soka England (FA), sasa hivi angekuwa ameshafuta matokeo yote ya ligi ya premier, hivyo kuanza upya. Chelsea wana hali mbaya baba, wanaweza kushuka daraja, bora Jecha aende akawaokoe."

Aliniangalia kwa jicho linalolengwa na machozi, akaniambia: "Jecha angekuwa refa wa mechi ya Algeria na Taifa Stars nisingeumia sana. Angefuta matokeo ya 7-0 ili mechi irudiwe. Haiwezekani tufungwe kikatili, namtaka Jecha. Naamini Watanzania wengi wanatamani refa angekuwa Jecha."

"Ila baba.." akaendelea. "Kuna matokeo mengine Jecha hana ubavu wa kuyafuta. Mfano kifo, mwamuzi ni Mungu. Hata mimi saa zile nilikuwa nakutania tu, Jecha hawezi kufuta uamuzi wa mimi kuzaliwa, mimi nimepangiwa na Mungu kuja hapa duniani".

Nikamwambia ni kweli, hilo la kifo na kuzaliwa linamhusu Mungu, Jecha hana uwezo nalo. Akasema: "Ila hii dunia haina usawa kabisa. Hata pamoja na dosari zinazosemwa zilijitokeza kama Dk Ali Mohamed Shein ndiye angekuwa ameshinda, CCM wangekubali kweli kirahisi kurudia uchaguzi"?

"Hapohapo jiulize, kama matokeo ya sasa yangekuwa yanaonesha Dk Shein ameshinda, hivi kweli Cuf wangekuwa wanasisitiza uchaguzi ulikuwa huru na haki kama ilivyo sasa wakisema dosari hazikuwepo, hivyo mshindi atangazwe?


"Usiache kujiuliza na hili, Lowassa anasema Zanzibar uchaguzi ulikuwa huru na haki, wakati huohuo analalamika Bara ameibiwa kura. Mwaka huu mnalo mliopiga kura."


"Sasa Captain Nyambo nadhani umemamiliza," Nilijaribu kukatisha mazungumzo lakini mwenyewe akaja na lingine: "Mimi naamini baba yangu kilichokuwa kinatafutwa siyo ridhaa ya wananchi, kila upande ulitaka tu goli la ushindi."


"Baba unamjua Maradona?"

"Namjua, anaitwa Diego Maradona".

"Hapo baba kama ingekuwa shindano ungejishindia pipi ya kijiti, baba wewe noma, nitakununulia pipi ya kijiti, sawa?"


Hapa sasa niliona mtoto ananitengeneza akidhani mtoto mwenzake, pipi ya kijiti ya nini mimi? Ila nilishachoka na stori zake, ikabidi nimkubalie ili mambo yapite.

"Maradona alikuwa fundi wa soka hasa, yule jamaa alikua anajua. Ila pamoja na uwezo wake aliopewa na Mungu bado hakuwa muungwana, mwaka 1986 aliwafunga England goli mkono, mwenyewe akajisifu ni Goli la Mkono wa Mungu, hivi ameshawahi kuuona mkono wa Mungu?".

Niliwaza kuwa pengine hapo ndipo ningeweza kumtuliza aachane na stori zake, nikamwambia Captain Nyambo: "Wewe huyo Maradona umemjulia wapi na goli lake la mkono? Mtoto umeanza kukaa vijiweni na umri huo, wewe Nyambo wewe!"

Akanijibu bila presha yoyote: "Baba mimi huwa naangalia vitu kwenye kompyuta, mambo ya intaneti, ukiandika kwenye google maneno football legends, utawaona wengi tu akina Garincha, Pele, Duncan Edwards, Eusebio na wengineo, hapo unaweza pia kumwangalia mmoja baada ya mwingine ndiyo maana niliona vitu vya Pele na kuvikubali."

Nikawa mpole ghafla, maana mtoto ndiye huyo amenikalisha mzimamzima. Kwa hapo sikutaka kuongeza neno, naye hakuwa na shida ya neno langu, akazidi kutiririka:

"Basi baba, vyama vyote vilikuwa na tabia za ki-Maradona. Kulazimisha goli hata kama ni la mkono. Hiyo ndiyo sababu kila upande unakuwa hauna imani mwenzake.

"Japokuwa wewe huwa unanichukulia poa unaniona mtoto, ila kaa na pointi hii. Mwizi huwa hamuamini mwenzake. Hii hali ya hivi vyama vyetu kushutumiana kuwa vimezidiana ujanja, maana yake haviaminiani. Captain Mkuu wewe ni kichwa, utakuwa umeshanielewa."

Akanitazama kama anataka kupokea kitu kutoka kwangu, nikaitika. Niseme ukweli hapo niliitika maana kuna kitu kipya alikuwa amekiingiza kichwani kwangu, kwamba mwizi hamuamini mwizi mwenzake.

Captain Nyambo: "Baba kuna mambo nashindwa kuyasema utanibana niseme nimeyajuaje, ila tambua ukweli kuwa mtu ambaye siye mwaminifu hudhani na mwenzake ni mvunja uaminifu. Mwanandoa mtoka nje, mwenzake akichelewa kurudi nyumbani tu ugomvi. Anawaza kusalitiwa kwa sababu naye anasaliti.

"Mtu asiyeujua usaliti hawezi kumuwazia mwenzake kama anasaliti, weka kichwani halafu usiniulize nimejuaje baba. Ongezea kuwa vyama vyetu vipo kama wafanyabiashara wa madawa ya kilevya, kila kimoja kinataka kumzidi mwenzake ujanja, kuna shida hapo jamani."

Captain Nyambo aligundua kama mahali alipofika alinipata, akataka nimpe uhakika kama baada ya mazungumzo nitampa simu yangu acheze game. Nami mwanangu tena, hata bila stori nampa, naye anajua.

Akasema: "Wauza madawa ya kulevya huwa hawaaminiani kabisa. Hata makubaliano ya biashara zao huyafanya kwa tahadhari kubwa, huyu ana mzigo, mwenzake anazo fedha, kila upande una bunduki, wanajuana kuwa wote ni majambazi, ukizubaa unapoteza mzigo na fedha.

"Mwaka 2015, naona vyama vyote viliingia kwenye uchaguzi, huku kila kimoja kikiwa hakina imani na mwenzake, ndiyo maana mambo yanatokea kama yalivyo. Waangalizi wa ndani na kimataifa wanasema uchaguzi ulikuwa huru na haki, sisi wenyewe kwa wenyewe tunakataa, tunasema tumeibiana."

"Baba eeh!" Captain Nyambo aliniita kama kunishtua. Nilipoitika akacheka halafu akasema: "Baba sisi ni Maradona, si unajua alifunga goli la mkono refa na wasaidizi wake hawakuona? Walikuja kuona kwenye video. Kumbe na sisi tumefungana magoli ya mikono, waangalizi wa kimataifa na wa ndani hawajaona. Sis Maradona baba."

Hapo sasa nami nilicheka, "Sisi Maradona!? Nikacheka tena, nikamwambia anakua vizuri, anazungumza pointi nzuri sana, akajibu: "Eeeh baba, mimi mwenyewe mjanja ndiyo maana najua. Mimi mwenyewe Maradona."

Captain Nyambo akasema: "Baba yule Nape Nnauye siyo Maradona." Nikamtolea macho, akasema tena: "Hata Edward Lowassa siyo Maradona."

Siwezi kusema uongo, maneno yake wakati mwingine yalikuwa siyapati sawasawa, sijui alikusudia kufikisha ujumbe upi?

Akasema: "Freeman Mbowe siyo Maradona. Maalim Seif siyo Maradona. Wanapenda u-Maradona lakini hawauwezi."

Nikamuuliza kwa nini? Akanijibu: "Wewe upo unapasha mwili joto kabla hujaingia kwenye mechi unatangaza kuwa utafunga goli la mkono. Nape alisema watashinda hata kwa goli la mkono.

"Lowassa akasema aachiwe yeye masuala yote kuhusu matangazo ya tume. Mbowe akapiga makelele mengi kuhusu mita 200. Seif asubuhi na mapema, kabla hata Zec hawajajumuisha matokeo, akajitangaza mshindi.

"U-Maradona una kanuni zake. Unakwenda kimyakimya kisha unasherehekea goli, siyo kelele nyingi kabla ya mchezo".

"Baba nina maswali kadhaa, ukinijibu sawa ila ukiamua usiponijibu itakuwa sawa tu," Captain Nyambo alizungumza kibabe sana, nikamwambia nikiweza kujibu nitampa jawabu, nikishindwa nitamkabidhi mji. Akasema hataki mji, nikishindwa nimtoe out, nikamnunulie milkshake.

Akasema: "Hivi baba CCM Zanzibar si ndiyo walikuwa viongozi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa? Kama madai kuwa kura Pemba ziliongezwa ni kweli, huoni kama wameonesha udhaifu mkubwa? Kama wamepigwa changa la macho namna hiyo, vipi uimara wao wa kuwalinda wananchi?

"Serikali makini haiwezi kuibiwa kwa staili ile kama ni kweli. Kwa maana hiyo tukubali kuwa CCM Zanzibar kwa kukiri kuibiwa, maana yake ni wazembe. Jecha pamoja na kufuta matokeo ni mzembe, yeye ndiye bosi, alikuwa wapi kuukabili udhaifu unaosemwa? Anasubiri kila kitu kinakamilika mpaka mtu anajitangaza mshindi ndiyo anafuta matokeo. Huoni kama alihatarisha amani ya Wazanzibar?".

Huku akitikisa kichwa, akasema: "Mungu inusuru nchi yetu, kwa kawaida goli la mkono likishaingia refa akiweka kati limepita hilo. Jecha alisubiri watu wanashangilia ndipo akasema hapana lile halikuwa goli.

"Upande wa pili najiuliza, kama kweli Seif alishinda, wapigakura si ni walewale? Ina maana haamini kama waliompigia kura watampa tena? Kama hakuna mambo ya chinichini, anaogopa nini kurudia? Baba yangu kwa kweli nisikuchoshe, wala usijibu, nipeleke nikapate milkshake, niburudike, nikirudi unisaidie kufanya homework, tulale, kesho shule."

Nilifikiri amemaliza, nikataka kuinuka, Captain Nyambo akasema: "Baba yangu kuna kitu ni vizuri ukizingatie, vyama vinagombana kwa sababu ushindi siyo wa wananchi. Kwa kawaida uchaguzi unapofanyika, wale wagombea wanakuwepo kama sababu ya kupata matokeo, wenye uamuzi ni wapigakura.

"Yeyote anayeshinda, mwenzake anakuwa hana budi kumpongeza, kwani washindi ni wananchi wanaofanya uamuzi kupitia sanduku la kupigia kura. Ninyi mliwekwa picha zenu tu kwenye karatasi ya kupigia kura, wananchi wameamua, ugomvi wa nini?

"Picha iliyo wazi ni kuwa mgogoro unasababishwa na ubinafsi. Kila upande unafikiria kushinda, hauwazi kuwa washindi ni wapigakura. Tuna kazi kubwa kuufikia uungwana wa kidemokrasi walionao Wamarekani, Waingereza na mataifa mengine."

Nilinyanyuka, nikamshika mtoto wangu tukawa tunaongozana kwenda nje, nimpeleke kwenye milkshake, Captain Nyambo aliniuliza: "Lakini baba, hivi kwa nini watu wanamuibia Lowassa? Kwa nini Tundu Lissu na utaalamu wake wa sheria anasema eti Rais Magufuli hatahutubia bunge? Kwamba watamfanyia fujo mpaka aondoke.

"Wanasiasa wanaongea yasiyowezekana. Bunge lina taratibu zake, kuna walinzi. Akishakuwepo Spika wa Bunge, maana yake yeye ndiye mwamuzi na msimamizi wa shughuli zote. Ukimfanyia fujo ukumbini, atamuamuru mkuu wake wa usalama na protokali (Sergeant at Arms) kuwatoa nje."

Nilitabasamu kuona Captain Nyambo anajua mambo mengi, akaendelea: "Najua wanachokifanya ni kumdanganya Lowassa aone watu wanampigania, ila mimi ninazo taarifa kuwa hata mwaka 2010 mambo yalikuwa hivihivi, wakasema hawamtambui Dk Jakaya Kikwete mwisho ikawaje?

"Unakwenda bungeni kama nani kama humtambui Rais Magufuli? Unakwenda bungeni kumfanyia fujo aliyefanya hilo bunge liwepo. Uamuzi wa busara kama huitambui serikali ni kususia bunge kabisa.

"Kazi ya bunge ni kuisimamia serikali, unakwenda kuisimamia serikali ambayo huitambui? Watu lazima wajue kuwa kauli ya Lissu ni kichekesho. Halafu ni aibu kuwa na wabunge ambao wanajitangaza kuwa wafanya fujo. Wamuache Lowassa apumzike, wasiendelee kumuibia kwa maneno yasiyobeba maana".

By Luqman Maloto
 
Maloto umekaaa katikati ya mstali pande zote hazina nia njema na wenyenchi!! Wote wapigaji tuu
 
Ah! Ni ndefu mno nimeachia njiani.
Huo muda niliochoropoka wote ingeishia hapa, ngoja nisome na nyengune kwanza.
 
Daaah hili gazeti nimeshindwa kulisoma.Jaribu kufupisha kama inawezekana.
 
Unafaa kutengeneza mashairi kwa ajili ta taifa la kesho.
Ongeza lugha iwe ya kisanaa.
 
Huu uzi watakao usoma kwa kutaka kuelewa wengi watakuwa wasio na ushabiki wa vyama,ila wale wenye vyama vyao wapo watakaosoma ili kuja kubishana na wapo watakuja kubisha bila hata kumaliza kusoma uzi wenyewe.
 
Hii inadhihilisha kuwa watanzania wengi hawana kazi za kufanya.

Kama una kazi usingepoteza muda kwa kuandika utumbo mrefu kiasi hicho
 
Shukuru umeweka sanaa kwenye maandishi yako vinginevyo wala nisingesoma.....btw umefanya uchambuzi mzuri japo umeegemea zaidi kwa watawala
 
Back
Top Bottom