Mwanakijiji waapa, kwa tunda uliloonja,
Eti we utalikwepa, kisa wameshalionja,
Kilipata hutoepa, utakula hutoonja,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!
Utamu wa tunda mwana, ulile uridhike,
Liwe limemenywa jana, ile ile ladha yake,
Hata ule mchana, utasema mwake mwake,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!
Tunda ale Amani, au Joni halihusu,
Awe kala Jakisoni, asojuwa shika kisu,
Aonje naye Hasani, haondoi hata nusu,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!
Tunda lataka matunzo, tautunza utamuwe,
Tunda la toka mwanzo, linakifu na ujuwe,
Ka we mtu kwa vikwazo, utakufa kwa kiwewe,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!
Midhali umeridhia, tafaidi utamuwe,
Wako wanolililia, waomba walikamuwe,
Hawajali mabakia, wanataka warushiwe,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!
Tunda ule kwa nafasi, wewe ni mwenye haraka,
Usiwe na wasiwasi, kama tunda walitaka,
Uache huo ukwasi, tunda halina viraka,
Mlaji ni mla leo, mla jana kala nini?!