tunasubiri mabomu maandamano ya uvccm

nyabhingi

JF-Expert Member
Oct 12, 2010
15,513
19,998
Samson Mwigamba

KUNA habari kwamba eti Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wanaandaa maandamano ikiwa masharti waliyoipa Bodi ya Mikopo hayatatekelezwa.

Lakini hawatoi masharti kwamba kina JK wakiilipa Dowans wataandamana nchi nzima.

Kama nchi hii ina maajabu basi, hayo maajabu ni ya chama kinachotawala na serikali yake. Eti siku hizi UVCCM wanatokeza mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kuelezea kutoridhishwa kwake na mambo kadhaa yanayoendelea hapa nchini?

Sikumbuki ni lini lakini nakumbuka nimewahi kuandika makala moja nikaelezea ujanja wa kitu kinachoitwa CCM.

Nilielezea jinsi ambavyo CCM inaweza kujidai kusurrender ili kumsoma adui ili wasonge mbele.

Nikasema wanatumia mbinu za kijeshi zile za kurudi nyuma na kujipanga upya kabla ya kusonga mbele.

Wakati ule nilikuwa nikiongelea kitendo cha baadhi ya wana CCM kujidai wanapiga vita sana dhidi ya rushwa kiasi cha kumlazimisha waziri mkuu wao wa wakati huo Edward Lowassa kujiuzulu. Nilisema CCM walishasoma hali wakaona wakilazimisha kusonga mbele wakiwa na Lowassa walikuwa wanaanguka anguko kuu tena la ghafla. Wakarudi nyuma wakajipanga na kumtoa kafara Lowassa ili wao wasalimike.

Napenda niwaase wanavyuo vya elimu ya juu na wanafunzi wa vyuo vingine na hata wale sekondari.

Kwamba kile kinachotangazwa na UVCCM kwa sasa ni usanii wa hali ya juu. Umoja huo wa vijana wa chama tawala wamegundua kitu.
Wamegundua kutokana na kauli ya kada mmoja wa chama chao aliyesema kwamba chama hicho kimeadhibiwa na vijana kwenye uchaguzi wa mwaka jana. Kwamba chama chao kimeonekana kuwasahau vijana, hakihangaiki na maendeleo ya vijana.

Mwaka 2005 kilitoa ahadi ya jumla ya maisha bora lakini ndani ya ahadi hiyo kulikuwa na ahadi mahsusi kwa vijana. Walisema kutatolewa ajira milioni moja kwa ajili ya vijana lakini walipofika 2010 wakaripoti kwamba hata wale wanaookota makopo na chupa chakavu za maji ya kunywa na kwenda kuziuza kwa shilingi 20 kwa chupa nazo ni ajira zilizotengenezwa na CCM.

Sisi tukawauliza wananchi kwamba hapo CCM imeongeza ajira ama imeongeza idadi ya vichaa wanaotembea majalalani wakiokota makopo?

CCM iliahidi kuwawezesha vijana na wanawake. Sikufikiri kama kuwawezesha ilikuwa ni kuwaita tu vijana na kuwagawia shilingi elfu 50 kila mmoja. Sisi tulidhani chama hicho kilikuwa kinakwenda kuandaa mazingira mazuri ya kukuza uchumi shirikishi.

Uchumi ambao unazibeba sekta zote rasmi na zisizo rasmi na kuweka mazingira bora ya yatakayomfaa kila mwananchi awe mfanyabiashara, mfanyakazi na hata mkulima.

Akili ya wana CCM ikaishia tu kwenye kuchukua mabilioni ya serikali na kuyaita mabilioni ya JK utadhani yametoka mfukoni mwake na kisha kuanza kuwagawia wananchi elfu hamsini hamsini ili wafanye biashara eti kwa namna hiyo wamewawezesha vijana na kina mama.

Kwanza kiwango hicho hakikuweza kuwa mtaji wa maana kwenye mfumo wa uchumi wa Tanzania wenye mfumko mkubwa wa bei na uliotawaliwa na manyanyaso makubwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na urasimu wa kufa mtu katika kuanzisha biashara.

Biashara ambazo zingeweza kufanywa na mtu aliyekopeshwa kiasi kidogo hivyo kwenye hayo mabilioni ni umachinga tena ule wa kutembea na soksi barabarani, umama lishe tena kwa mtu ambaye alikuwa na pesa nyingine ambayo ameshalipia kibanda cha kufanyia huo umama lishe, na biashara nyingine kichaa kama ile ya kununua chupa na makopo kutoka kwa vichaa wanaoyaokota majalalani na baadaye naye akayauze kiwandani ili kiwanda kiya-recycle na kuyatengeneza mapya.

Lakini mambo matatu yakatokea. Kwanza waliopata hizo pesa wakawa ni vigogo wa serikali na mabenki ambamo pesa hizo zilipitishiwa.

Wanyonge hawakuziona na hatimaye tukatangaziwa kwamba kati ya watanzania zaidi ya milioni 30 wanaoishi kwenye umaskini uliopitiliza eti ni 47 elfu tu ndio waliopata hizo hela. Umaskini utaondokaje?

Lakini tatizo la pili ni lile nililoliezea hapo juu kwamba pesa hiyo haikutosha kuanzisha biashara ya maana yenye kuinua maisha ya mtu.

Na la tatu ni kwamba wale wale akina mama lishe na wamachinga waliotumia visenti hivyo kuanzisha biashara ndogo ndogo ndio walewale waliokuwa wakikamatwa kila leo na wanamgambo wa JK huyo huyo wakidai eti wanakuwa uchafu kwenye majiji yetu kama Dar, Arusha, Mwanza, Mbeya, na miji mingine.

Wakawa wanakamatwa na kunyang'anywa bidhaa zao na hatimaye kushindwa kufanya biashara.

Hapa Arusha siku ya Alhamisi nimetokea maeneo ya AICC Complex kuelekea Usa-river nikaombwa lift na binti ambaye huwa namwona nje ya geti la ofisi zetu akiuza karanga za kukaanga. Binti yule kumbukumbu zangu zinaonyesha kwamba amekuwa akiuza pale karanga tangu 2008 ndiyo biashara inayompa kupeleka tonge la ugali kinywani. Anasema hana mume na ana mtoto mmoja.

Pale anapouzia karanga zake kuna vijana wenzake wa kike na wa kiume ambao wanafanya biashara ya kuuza vocha za simu na magazeti.

Wale wanaouza vocha, kampuni mojawapo huwapa faida asilimia 10. Kwa maana kwamba akiuza vocha ya shilingi elfu moja anapata faida shilingi 100.

Nilipowafuatilia sana nikagundua kwamba siku mambo yamekuwa mazuri sana muuzaji mmoja anaweza kuuza vocha za shilingi elfu 20.

Faida yake ni 2000. Na hapo zingatia kwamba makampuni mengine hutoa shilingi 700 kwa kila elfu kumi.

Hii ina maana kwamba kama muuzaji huyu atapata bahati ya siku zote anazokwenda kijiweni kuwa nzuri basi kwa siku sita za wiki ambazo huuza vocha kwa wiki nne atapata shilingi elfu 48 ambazo ni za kudunduliza kila siku siyo kwamba zinakuja mara moja kila mwezi.

Hapo sijamzungumzia muuza magazeti ambaye katika kila nakala moja ya gazeti linalouzwa shilingi 500 yeye huambulia shilingi 70. Fuatilia wakuambie wanauza nakala ngapi kwa siku ili uone wanaingiza kiasi gani wale wanaopakata nakala chache mkononi.

Wadundulizaji hawa hawawezi kula chakula chao cha mchana kwenye canteen ambazo zinayazunguka maeneo ya AICC ambapo bei ya chini kabisa ya chakula kwenye canteen hizo ni shilingi 2000 na kwa kina mama ntilie wa vichochoroni ni 1500.

Wakifanya hivyo kipato chao kimeishia kwenye lunch. Nimeshuhudia, siandiki habari za kutunga.

Kwamba vijana hawa mlo wao wa mchana ni pakti tatu tatu za karanga kutoka kwa kijana mwenzao ambaye naye yuko pamoja nao akiuza vipakti vya karanga shilingi mia mia. Kijana huyu ndiye aliyeniomba lift kwamba anashukia mbele kidogo ya eneo la Sanawari.

Alipoingia kwenye gari mimi na wenzangu tuliokuwa kwenye gari tukagundua kwamba alikuwa ana huzuni, amechanganyikiwa na machozi yanamtiririka machoni.

Akatuuliza ofisi za Mtendaji Kata ya Sekeiaziko wapi. Kabla ya kumwonyesha tukamuuliza kulikoni? Akatuambia mgambo wa jiji wamemnyang'anya karanga zake zote pamoja na vyombo vyake wakimwambia anachafua jiji. Maisha bora kwa kila mtanzania na vijana watawezeshwa!

Ni kada hii ya vijana ambao sasa wameishtukia CCM. Mimi sina uhakika wala sijawahi kumwuliza lakini nimeambiwa kwamba kwenye kata moja ndani ya Jiji la Arusha aliyeshinda udiwani kupitia CHADEMA alikuwa mfanyabiashara ya kupakia abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda.

Wengi hawakutarajia lakini kijana alishinda kwa nguvu ya wenzake hao hao wanaofanya biashara ya pikipiki, vocha, karanga, kupakia abiria kwenye baiskeli, na kadhalika. Huyu leo ni mwakilishi mzuri wa vijana hawa maana anaijua vema shida yao.

Diwani aliyegombea na kijana huyu kupitia CCM amesikika akisema kwa mwendo huu hapo 2015 hakuna CCM. Akadai kwamba hakuamini kama vijana wa leo wanaweza kupiga kura na kumchagua kijana mwenzao ambaye hata nyumba ya kupanga ni ya shida kuwa diwani wao. Akaeleza bayana kwamba huko tunakokwenda kwa vizazi vya vijana hawa wanaoendelea kufikisha umri wa kupiga kura, CCM haina chake.

Ahadi za CCM za 2005 hazikuwaacha wanafunzi hasa wa elimu ya juu. Waliambiwa kwamba mikopo kupitia bodi ya mikopo itaboreshwa. Niliwahi pia kuliandika hili. Kwamba bodi ya mikopo ya elimu ya juu ilianza mwaka wa masomo 2005/2006 wakati tunaingia kwenye uchaguzi wa tatu wa vyama vingi.

Mwaka huo mikopo iligawiwa kama karanga. Ilikuwa mwanafunzi akipata tu barua ya kukubaliwa kuingia chuo kikuu chochote chenye usajili ama chuo chochote cha elimu ya juu chenye usajili anapeleka maombi bodi akiambatanisha ile barua na kupewa mkopo asilimia 100.

Kuna habari zilizokuja kuthibitishwa baadaye na serikali kwamba kiasi cha shilingi bilioni 30 zilipotea kwa kuwakopesha wanafunzi mara mbili mbili. Na bado JK akawaita wanafunzi wa vyuo vikuu pale Diamond Jubilee na kuwaahidi kwamba ataboresha zaidi mikopo na wanafunzi watafurahi.

Nikajiuliza ni nini anakwenda kuboresha. Je, ni kuongeza kiwango cha mikopo mara mbili ama ni kutoa mikopo hata mitatu kwa mwanafunzi mmoja? Baada ya kuwa rais waulize wanafunzi leo jinsi gani mikopo yao imeboreshwa watakupatia jibu zuri zaidi kuliko la kwangu.

Sasa vijana nchi nzima wameigeuka CCM. Wanafunzi wa elimu ya juu wanaikimbia CCM kama ukoma.

Matawi ya CHADEMA yanazidi kufunguliwa vyuoni kila kukicha. Maandamano ya kuipinga serikali yamezidi, kuandamana kupinga uchaguzi feki wa umeya Arusha, kuandamana kupinga kulipwa kwa Dowans, kuandamana kupinga kucheleweshewa pesa za mikopo ya wanafunzi, kuandamana kupinga mwenzao kuuawa na polisi, wamachinga kuandamana kupinga manyanyaso, kuandamana kudai katiba mpya na kukabidhi rasmu ya katiba mpya, na kadhalika.

Na katika makundi yote vijana ndio wanaoongoza katika maandamano hayo. CCM haijalala, inasoma alama za nyakati. Inaangalia Tunisia na Misri, Yemen na Algeria, inashtuka. Inaona jinsi anguko lao linavyoharakisha. Na mkumbuke kwamba lengo kuu la CCM ni kushinda uchaguzi na kuunda dola na limerudiwa vizuri zaidi juzi na Katibu Mkuu wao Yusuph Makamba.

Kwa lugha nyingine bila kushinda uchaguzi hakuna CCM. sasa wanabuni mbinu namna gani wapate kura mwaka 2015. Hakuna namna zaidi ya kuwateka vijana waikubali tena CCM. wafanyeje sasa? Waitumie UVCCM.

Haijapata kutokea Tanzania hii tangu kuumbwa kwa dunia hii. Eti vijana wa CCM wataandamana kuipinga serikali yao ili na wao wapigwe mabomu kama walivyopigwa wanafunzi wa UDOM. Naomba niwakumbushe wanafunzi wa elimu ya juu na vijana wa nchi hii kwa ujumla.

Kwamba sababu inayotangazwa na UVCCM itakayofanya waandamane ni ile ile waliyokuwa nayo wanafunzi wa UDOM, Makumira University, Ardhi, na wengineo.

Na kila walipoandamana walipigwa mabomu na virungu na polisi kwa sababu walikuwa wakiipinga serikali ya CCM na taasisi yake moja inayoitwa Bodi ya Mikopo. Sasa niwaulize, Je, ni kweli kwamba UVCCM imedhamiria kuandamana kwa sababu hiyo hiyo ya kuipinga serikali ya chama chao na kwa sababu hiyo kukipinga chama chao, na hatimaye na wao wapigwe mabomu na virungu? Swali lingine, Je, walipotangaza kwamba serikali isiilipe Dowans shilingi bilioni 94 na kumtaka rais wao ambaye pia ndiye mwenyekiti taifa wa chama chao achukue maamuzi magumu, lakini badala yake Kamati Kuu ya chama chao iliyoketi chini ya uwenyekiti wa rais wao yule yule, ikatoa tamko kwamba lazima Dowans ilipwe, walifanya nini?

Je, waliandamana kupinga maamuzi hayo? Je, leo serikali ya chama chao ikijitokeza na kudai kwamba bodi yake ya mikopo ya elimu ya juu inafanya kazi nzuri katika mazingira magumu, bado wataandamana tena tamko hilo litolewe na rais wao kwenye hotuba zake za kila mwisho wa mwezi, bado wataandamana?

Nawatahadharisha vijana wa vyuo vikuu msidanganyike. Kinachofanywa na UVCCM ni usanii uliokubuhu wa kisiasa. Wanataka kuwarubuni kwamba UVCCM iko pamoja na Watanzania isipokuwa kuna wazee wachache ndani ya CCM ndio wanaoharibu sifa ya chama na serikali. Mtaingia mkenge mrejee CCM kwa kudanganywa kwamba muingie humo muwapige vita hao wazee ili vijana mshike hatamu na nchi inyooke. Uongo mkubwa!

Kama UVCCM inapiga vita ubabaishaji na inapinga Dowans kulipwa, mbona wanawashambulia akina Sitta na Mwakyembe ambao pia wanapinga Dowans isilipwe na Sitta kasikika pia akiikoromea Bodi ya Mikopo?

Vijana UVCCM ikifanikiwa kuwadanganya kama ilivyowadanganya 2005 na nyinyi mkaungana nao na mkavalishwa kapelo za kijani na T-shirt za kijani mkaandamana nao na kujidai kuilaani bodi ya mikopo, mmeliwa. Mtairejeshea CCM madaraka 2015 na lengo lao litakuwa limetimia na mateso mtakayoyapata baada ya uchaguzi wa 2015 hamjapata kuyashuhudia. Muda utasema!

Vinginevyo mimi nasubiri nione UVCCM ikihamasisha vijana wale wale wa vyuo vikuu vile vile, waandamane kwa sababu zile zile za mikopo kwa wanafunzi, dhidi ya serikali ile ile iliyoko madarakani, katika kipindi hiki hiki cha mwaka 2011, kukiwa na jeshi lile lile la polisi, chini ya IGP yule yule Said Mwema, ma-RPC wale wale kama yule wa Arusha Thobias Adengenye na yule wa Dodoma Zelothe Steven, ma-OCD wale wale kama yule wa Arusha Zuberi Mwombeji, halafu waruhusiwe kuandamana.

Na kama hawataruhusiwa eti wasonge mbele na kuandamana, na kama wataandamana eti wasipigwe mabomu wala virungu, wala risasi za baridi wala za moto. Na kama kweli wameamua naomba kweli waandamane kama walivyoandamana UDOM na Makumira na wapigwe kweli kama walivyopigwa vijana wetu kwenye vyuo hivyo, na tuone uongozi mzima wa UVCCM ukitimliwa kwa kwenda kinyume na chama chao na serikali yao. Hapo ndipo nitaamini kwamba walikuwa wameamua kweli. Tunayasubiri kwa hamu maandamano ya UVCCM!
 
Back
Top Bottom