Tunapambana na mafisadi gani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunapambana na mafisadi gani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Sep 24, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Na Sauli Giliard

  WIKI iliyopita, safu hii ilijikita zaidi katika kujadili iwapo kweli tunapambana na ufisadi ama ‘ufisadi' umeshakuwa kichaka cha kujijengea umaarufu wa kisiasa na hasa ikizingatiwa tuendako kuna uchaguzi mkuu.

  Wiki hiyo hiyo, lilitokea jambo jingine katika ‘vita' hiyo pale alipoingia ‘mpiganaji' mwingine kuendeleza kibwagizo cha vita dhidi ya ufisadi.

  Huyu ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, ambaye kwa upepo ulivyo, ‘Kama hawawezi (wapambanaji), ameamua kuungana nao.' Alimuunga mkono Spika Samuel Sitta, kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na si mafisadi na mianya inayowatengeneza.

  Hapa, baadhi ya vyombo vya habari viliona hayo ni mapinduzi makubwa kwa Katibu huyo na hata kusema, ‘Makamba azaliwa upya'. Kuzaliwa kwake upya, kunatokana na msimamo wa kiongozi huyo ambaye mara kwa mara alikuwa akisema, hakuna fisadi ndani ya chama.

  Baada ya wanasiasa kutofautiana naye, alikiri kuwa kuna mafisadi ndani ya chama chake ila chama kama taasisi si fisadi bali hiyo ni hulka ya mtu mmoja mmoja.

  Kwa maana nyingine, kuna wanachama wengine ambao ni wasafi, hivyo uchafu wa mtu mmoja usiharibu sura ya CCM.

  Ni katika mkanganyiko huo, Makamba alibaki na msimamo kuwa, mahakama ndiyo ina mamlaka kisheria kusema kuwa, huyu ni fisadi, na yule siye, hivyo, wapambanaji wafikie wakati wawe na subira hadi wakati utakapofika.

  Ilhali akiwa na misimamo hiyo, ithibati inaonyesha kuwa, mipango mingi ya serikali haifanikiwi kutokana na kuwepo watendaji wasio waaminifu katika ofisi za umma.

  Bajeti ya serikali inamegwa na wachache, huku taifa likilia njaa, wajawazito wakishindwa kufika hospitalini kutokana na vituo vya afya kuwa mbali nao.

  Kwa haya, ufisadi uwe wimbo na mtaji wa kisiasa ama tupambane na chanzo cha ufisadi? Tugeuke, tujipange.

  Tukirudi kwenye sakata la Makamba, suala halikuwa kwenda kumuunga mkono Samuel Sitta tu, bali alijikuta akitamka siri iliyojificha chini ya mwamvuli wa vita hiyo ya ufisadi pale ambapo alipoingilia programu za mwakani alipowaambia wananchi wa Urambo Mashariki katika Jimbo la Sitta kwamba, wamchague, ni kiongozi mzuri.

  Katika moja ya mikutano yake na wanahabari, Makamba amekuwa akiwaonya wanasiasa kutowavuruga wananchi kwa kupiga kampeni, kwani muda bado. Alisisitiza kuwa, hiyo ni shughuli ya mwakani pale ambapo milango ya kujitangaza kisiasa itakapofunguliwa.

  Ilibidi ‘azaliwe' kwa kuungana na wapambanaji wa ufisadi baada ya kuona kuwa, kama kiongozi mwanadamizi ndani ya chama chake, anayepaswa kuhakikisha kuwa, chama chake hakishindwi katika chaguzi mbalimbali, ni bora achague lililo jema, licha kwa nafsi yake hakutaka kuitumia njia hiyo kama misingi ya CCM.

  Huu ni uashirio ya kwamba, CCM imeamua kujirudi na kuwatumia baadhi ya wabunge waliojipambanua kuwa ni wapinga ufisadi kuwa ni njia yao kuelekea mwaka 2010.

  Imekuwa hivyo kwa sababu, wananchi kwa sasa wameshalewa mvinyo wa mapambano dhidi ya ufisadi.

  Ufisadi kwa sasa si tena kupambana na mfumo, kwani hata mfumo wenyewe unaimba wimbo uleule kwamba ‘tunapambana' na ufisadi.

  Mafisadi wapi? Waliokalia ofisi za umma ama nje? Hii inatuaminisha ya kwamba, kama ilivyo vigumu kwa mtu kuubeba mtungi alioingia ndani yake, ndivyo ambavyo wana CCM watakavyoshindwa kuwalewesha wananchi mvinyo wa vita ya ufisadi.

  Yamkini Makamba amechagua lililo jema kwa kuangalia mustakabali wa chama chake na changamoto zinazokikabili. Kwamba vita dhidi ya ufisadi ni mbinu na mkakati wa CCM kurudisha imani kwa wananchi baada ya upinzani kutaja orodha ya mafisadi.

  Baada ya orodha ile kutolewa, ni dhahiri ya kwamba, chama tawala na serikali kwa pamoja vilitikisika kutokana na kile kilichokuja kujidhihirisha baadaye.

  Baada ya orodha ile ya watu 11, ilikuja kugundulika kuwa, kuna makampuni yenye utata katika uandikishaji wake, wizi katika Akaunti ya Malipo ya Nje katika Benki Kuu (EPA), Commodity Import Support (CIS), achana na Kagoda na Deep Green na mengineyo.

  Kwa uchafu huo huo, CCM inataka kuutumia kujitakasa kwa kuungana na kikundi kidogo cha watu na kusisitiza kuwa, hiyo ni ajenda. Sawa, ipo kwenye ilani, ulikuwa wapi utashi wa kuzuia na kudhibiti hayo?

  Taifa limekwisha kujichafua machoni mwa wananchi wake, wafadhili pamoja na jumuiya ya kimataifa.

  Kuingia kwa makundi haya katika ulingo wa vita dhidi ya ufisadi ni kipimajoto kingine kwa wananchi, hasa ikizingatiwa, nguvu yao katika siasa za nchi hii iko tu pale kunapokuwepo uchaguzi.

  Sasa taifa linaelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya ule mkuu hapo mwakani.

  Kwa wananchi, hiki ni kipimajoto kinachowataka kupambanua ni nani mkweli katika ufisadi huu.

  Ni nani wenye nafasi ya kuzuia na kukabiliana nao na hakufanya hivyo. Je, wananchi wadanganyike kwa wakati mmoja kila mara. Nguvu ya kidemokrasia katika uchaguzi ulioko mbele yetu ndiyo hatima ya maisha ya Watanzania.

  Nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, kuwajibika kwa kiongozi ni suala gumu. Ukiondoa sakata la Richmond, umiliki wa mabilioni ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, hakuna mtuhumiwa mwingine aliyethubutu kujiuzulu kwa lengo la kupisha uchunguzi kufanyika.

  Hata pale ambapo mabomu ya Mbagala yalipolipuka na kuharibu nyumba na kusababisha vifo kwa wanajeshi na wananchi, Waziri mwenye dhamana, Hussein Mwinyi, alinukuliwa akisema, endapo uchunguzi utabaini ya kwamba, tukio hilo lilitokea kutokana na uzembe, atajiuzulu.

  Hili lilikuwa ni onyo kwa wachunguzi wa tukio hilo, kuwa, wawe makini kwani ripoti yao inaweza kumsababishia mabadiliko makubwa ya kisiasa maishani mwake, kwa kulazimika kujiuzulu. Kwa kasumba kama hizi, narudi katika hoja kwamba, wananchi wanayo fursa moja tu katika nafasi zinazojitokeza mbele yao; kuamua lililo jema. Si kwa kukubali kurubuniwa kwa maneno ya vita dhidi ya ufisadi, bali kwa ukweli wa mambo. Waanze na maisha yao, huduma wanazopata katika maeneo yao. Kwa wananchi wa kawaida, wanaweza kuona jambo gumu sana kuamini kuwa, EPA ina mahusiano ya moja kwa moja na maisha yao. Watashindwa kuamini kuwa, vyeo vya kisiasa ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa matabaka kati yao na watawala lakini ni rahisi kutambua ya kwamba, hawana barabara nzuri kama walivyosatahili kuwa nayo.
   
 2. Dr. Chapa Kiuno

  Dr. Chapa Kiuno JF-Expert Member

  #2
  Sep 24, 2009
  Joined: Sep 11, 2009
  Messages: 445
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  ufisadi huu ni hatari
   
 3. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #3
  Sep 24, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Duh na wewe Dr. Chapa Kiuno, Balaa na kwa kuwa mamlaka zinazohusika zinashindwa kuwajibisha watu na watuhumiwa mbalimbali sasa kuna uwezekano wa watu hawa kuambua na kuficha dhambi nyingi sana
   
Loading...