Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,756
- 40,930
Sielewi kwanini serikali inapojaribu kusimamia mabadiliko na nidhamu katika utumishi wa umma inajigongelea misumari yenyewe. Ninavyoona ni sawa na fundi seremala mashuhuri anayejaribu kutengeneza samani nzuri lakini haishi kujigonga nyundo vidoleni yeye mwenyewe! Anataka tuone uzuri wa samani zake ili tuzipende lakini wakati huo huo hatukosi kumuona anavyolia kila nyundo inapotua kwenye kidole ambacho angeweza kukiepuka kama angekuwa makini. Anajigonga mwenyewe kwa sababu wakati huo huo anafanya ufundi wake bado anazungumza mambo yasiyohusiana, mara ashike kitabu kusoma, mara asikilize muziki n.k kiasi kwamba anaonekana hana focus.
Binafsi ningependa sana serikali ya Magufuli ioneshe nidhamu yenyewe (self discipline) na kutulia mkazo wanachofanya(focurs) badala ya sasa ambapo hadi baadhi ya vitu hatujui vinaendelea vipi kwani mazungumzo ya kitaifa yamebakia kwenye mambo yasiyo ya msingi au ya lazima (irrelevant issues).
Kuna msemo kuwa "neno la muungwana ndio dhamana yake". Msemo huu unamaanisha tu kwamba mtu muungwana akisema neno, au akitoa ahadi fulani basi haitaji kuweka rehani kitu chochote ili kuaminika; yaani neno lake ni rehani tosha kwa yeye kupewa dhamana. Mtu muungwana anapotoa ahadi basi anaaminika kwa sababu neno lake linaaminika.
SIKUMBUKI (na nimeweka herufi kubwa kwa mkazo tu) kama Magufuli wakati anatoa ahadi mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 alisema jambo lolote ambalo liliashiria kuwa ama angekuwa na ugomvi wa kudumu na wapinzani au kwamba atajaribu kuingilia au kushawishi mihimili mingine ya dola. NINACHOKUMBUKA ni kuwa aliahidi kati ya vitu vingi (hasa kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni pale Jangwani mwezi Augusti 2015) kwamba ataheshimu mawazo ya watu mbalimbali hata kama ni upinzani na kuwa ataheshimu uhuru wa mihimili mingine.
Sasa inapotokea kuwa vyombo vya dola vinahangaika sana na vitu ambavyo vinaangukia kwenye himaya ya uhuru wa maoni au mawazo inasikitisha. Nimewahi kusema hapa miaka karibu kumi sasa kwamba haki ya uhuru wa maoni na uhuru wa mawazo hailindi mawazo mazuri au yenye kufurahisha. Mawazo mazuri na yenye kufurahisha hayahitaji kulindwa; kinacholindwa ni mawazo mabaya, mabovu, ya kuudhi na wakati mwingine ya kukera kabisa. Magufuli alipokubali kutaka kugombea Urais na kusimama kugombea maana yake ni kuwa alikuwa tayari kusemwa, kukejeliwa, kufanywa kituko, kuchorwa vibaya, na hata kufikiriwa vibaya. Alikubali kwa sababu aliaminisha umma kuwa ana ngozi ngumu (tough skin). Na sisi tuliomuunga mkono na ambao bado tunamuunga mkono tunaamini ana ngozi ngumi hivyo tunaposikia ati mtu kakamatwa kwa sababu kamsema vibaya Rais, au sijui kasema jambo lenye kumkera Rais inatuudhi!
Sasa inawezekana ni watu wa chini tu ambao nao wanafikiria wanamtendea Rais hisani kwa kufuatilia watu wanasema nini juu ya serikali au nini. Hizi ni distractions! Leo hii sijui kuna kesi ngapi zinahusiana na mambo ya kipuuzi na watu wazima na akili zao kuchwa kucha wamekaa wanahangaika hadi kama ni burudani inaanza kufanya watu wasinzie. Watu gani hawachoki kutafuta kesi za kila namna, asubuhi na mchana, hadi watu kwenye mitandao wanaanza kutunga vitu vya uongo ili kuwajaza watu hofu! Juzi kuna message inatembea ati serikali inarekodi mazungumzo yote ya kwenye simu na watu wanaanza kuhofia hata kuzungumza kwenye simu, huu ni upuuzi gani?
Kama kweli Magufuli anaumia sana moyoni, anakereka kirahisi rahisi, anakwazika na kila kibaya kinachosemwa juu yake kiasi kwamba anaona wanamzuia kutekelezas wajibu wake au anaona kuwa kazi hii ni ngumu sana kwake kuifanya binafsi nina ushauri mzuri tu; Katiba imeweka utaratibu wa hiari kwa Rais akujiuzulu. Si LAZIMA awe Rais. Kwa sababu tunaomuunga mkono tunaamini yeye ni Rais ambaye Tanzania ilimhitaji sasa na tuliamini kuwa akiweka mkazo (focus) na kusimamia nidhamu (self discipline) ya serikali yake basi katika miaka hii mitano mambo makubwa yanaweza kufanywa kuliko yaliyofanywa miaka hamsini iliyopita!
Hivyo basi, ushauri wangu ni kuwa Serikali ikae chini na kujiuzuli kwanini inachekelea hizi distractions? Kwanini inazunguka zunguka kwenye mambo yasiyo na msingi badala ya kuwashawishi wananchi kwa uongozi wake kuonesha mambo makubwa yanayofanywa au yanayopangwa kufanywa?
Magufului ni lazima ahakikishe mambo yafuatayo nayatokea:
a. Kuheshimu mahakama kwa gharama zote - demokrasia na utawala wa demokrasia vinasimama au kuanguka na uhuru wa mahakama. Kama kuna viongozi wanaitwa mahakamani ni LAZIMA watii! Na binafsi hilo peke yake ni sababu tosha ya kumfukuza mtu kazi kwa kutokutii mahakama. Na Rais mwenyewe aepuke kwa nguvu zake zote undue influence ya mahakama.
b. Rais atumie ushawishi wa nguvu za hoja kuliko ushawishi wa hoja za nguvu. Watu ni lazima waone mantiki ya kinachosimamiwa kuliko hofu ya kutokukisimamia. Katika hili ni lazima Rais ajioneshe kuwa ni mtu wa tafakari na siyo mtu wa munkari. Ukali uliopo ni wa lazima na binafsi naamini kati ya vitu vilivyokosekana kwa muda mrefu ni viongozi wakali; lakini ukali hauondoi ushawishi.
c. Kesi dhidi ya wapinzani na ambazo zinaonekana ni za kisiasa zifutwe ili taifa lirejee kwenye mijadala ya kisiasa bila hofu ya kumuudhi Rais. Na labda hili litawafanya polisi wafocus na wenyewe kwenye mambo ya msingi - kama vita dhidi ya madawa ya kulevya, ufisadi n.k Sasa hivi ni kana kwamba vita dhidi ya ufisadi imeenda picnic! Magufuli aliungwa mkono na baadhi yetu kwa sababu alikuwa ni chaguo sahihi kupambana na ufisadi kwani tulijua ana uthubutu wa kuugusa ufisadi. Hadi hivi sasa kasi ya kupambana na ufisadi haijaleta matumaini sana. Na kinachosikitisha ni kuwa kesi kadhaa hadi hivi sasa zinaonekana haziendi popote kwa sabbabu hazioneshi kama zimefikiriwa vizuri na mawakili wa serikali wanatia aibu! Ni rahisi zaidi kumkamata mtu kuliko kuthibitisha kwanini umemkamata! Watu wakamatwe pale ambapo kuna uthibitisho wa uhalifu hasa lakini hizi kesi nyingine zinafanya serikali ionekane haina mawakili wabobezi au wenye ujuzi wa kusimamia kesi nzito matokeo yake tunatengeneza precendence za ajabu sana!
d. Wakati umefika kwa Magufuli kulihutubia taifa na kulishawishi (persuade) lielewe anataka kufanya nini na anafanya nini vitu hivyo. Ni hotuba ya kuliamsha taifa pia ili kila Mtanzania afanye nini katika nafasi yake. Kitu kibaya ambacho kimetokea (na nilidokeza kwenye makala yangu wiki mbili nyuma) watu wanaitegemea sana serikali hakuna moyo wa kujitolea (kwa kiasi kikubwa). Ni lazima kuamsha roho ya kujitolea katika taifa badala ya watu kusubiria serikali ifanye. Magufulia anatakiwa kuamsha roho ya ujenzi wa taifa; watu wajitolee kulijenga taifa lao kuliko kusubiria kila kitu serikali ifanye. Je, ni vitu gani Watannzania wanaweza kufanya wenyewe bila serikali kuwafanyia? hii ndio changamoto ya kiuongozi!
Kwa ufupi, tuachane na distractions na vitu vinavyopoteza mwelekeo au hata mjadala wa kitaifa. Ni muhimu serikali ioneshe ina nidhamu katika watendaji wake ikibidi hata kupangua baraza la mawaziri kwani kuna watu wanapwaya kupita kiasi sasa hadi inakera. Kama kuna jambo lolote Rais anaona haliendi sawa au linahitaji sheria ngumu ni muhimu serikali iende Bungeni na mabadiliko ya sheria ili jambo hilo lishughulikiwe kisheria.
Tunaomuunga mkono Magufuli tunataka uwajibikaji, utawala wa sheria, kuheshimu tunu za kidemokrasia, ushawishi wa hoja, kuwa makini na wenye mkazo na kuepuka kupoteza muda kwenye mambo yasiyo ya msingi. Muda uliobakia na mchache na tusipoteze nafasi kwa mambo yanayopoteza fedha za umma na muda wa wananchi kujadili mambo ya msingi.