Tunahitaji Taifa lenye Mizizi ya Maendeleo

Hamatan

JF-Expert Member
Nov 10, 2020
3,183
7,645
Kitu chochote kisichokuwa na mizizi/msingi imara, kikitikiswa tu kidogo kinayumba au kuanguka kabisa.

Maisha ni shule kubwa kuliko ile ya chuo kikuu. Kila tunapoishi kuna nafasi ya kujifunza na kuelimika, labda ukatae mwenyewe kuwa hutaki kujifunza.

Serikali ya awamu ya 5 imekuwa darasa kubwa sana, darasa chungu, ambalo tukilitumia vizuri, linaweza kutusaidia sana, kama Taifa, kurekebisha msingi wa Taifa letu ambao ni dhaifu sana.

Sote tunafahamu, jinsi awamu ya 5 ilivyotumia muda mwingi kubana uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa maoni, haki za kidemokrasia, haki za kiraia, kuibuka kwa makundi ya watu wasiojulikana walioua, kushambulia na kuwapoteza watu, n.k.

Lakini kutokana na kufanikiwa kuviziba midomo vyombo vya habari na raia, tulishuhudia jinsi propaganda nyingi zilivyofanywa na vyombo vya habari vya serikali katika kuwahadaa, kuwadanganya na kuwapumbaza wasio na ufahamu.

Wananchi wengi wenye uelewa mdogo, kwa sababu hakuna aliyekuwa na uwezo wa kuwaambia ukweli, walilishwa propaganda za ajabu, hata wakaamini ambayo hayakuwepo. Wakaamini kuwa nchi hii haijawahi kupata serikali nzuri kama ya awamu ya 5. Wakaaminishwa kuwa awamu zote zilizopita ziliongozwa na Marais ambao hawakuwa wazalendo.

Ukweli ni upi? Nini cha pekee ambacho utawala wa awamu ya 5 ulifanya ambacho awwmu zilizotangulia hazikufanya?

1. Wastani wa pato la mwananchi

Utawala wa Mkapa na Kikwete, kila mmoja uliweza kuongeza wastani wa pato la mwananchi kwa kiasi cha dola 300 - 400. Utawala wa awamu ya 5 uliongeza kwa dola 80 tu.

2. Uwekezaji
Uwekezaji wakati wa awamu ya Kikwete, ukuaji wake ulifikia mpaka 28%. Awamu ya 5 ilishusha mpaka 4%

3. Utalii
Utalii ambao, pamoja na madini, ndiyo sekta zinazoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, wakati wa awamu ya Kikwete ulikuwa unakua kwa 15%, wakati wa awamu ya 5 ulianguka mpaka 3.6%

4. Thamani ya Mauzo ya Mazao ya Kilimo

Thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo, awamu ya 5 iliyaangusha kwa 50%

5. Dhahabu
Wakati wa awamu ya Kikwete, Tanzania ilikuwa nchi ya 3 kwa uuzaji dhahabu, awamu ya 5 imeishusha hadi kuwa nchi ya 6 kwa uzalishaji dhahabu barani Afrika. Na kwa sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kwa mazingira mabaya ya uwekezaji kwenye sekta ya madini Duniani. Hakuna anayefanya utafiti wowote wa madini Tanzania. Serikali inahangaika namna ya kuiokoa sekta isife.

Watu wanaongelea miradi, kwa maelezo kuwa awamu ya 5 wamejenga reli, bwawa la umeme, ndege, n.k.

1) Reli
Reli ni muhimu. Wakati wa awamu ya kwanza, kulijengwa SGR ya TAZARA, zaidi ya kilometa 3,000. Kulikuwa na mipango thabiti, ndiyo maana ilikamilika. SGR ya awamu ya 5, hakuna anayejua kama itakamilika, na itakimilika lini. Kwa hiyo awamu ya 5, siyo ya kwanza kujenga reli.

2) Ndege
Kwa sasa, naambiwa tuna ndege 11, kati ya hizo, naambiwa zenye jet engine ni 4. Nyingine zote ni pangaboi. Wakati wa awamu ya kwanza zilinunukiwa ndege mpya, za kisasa kwa wakati wake, ndege 13. Kwa hiyo awamu ya 5, siyo ya kwanza

3) Elimu Bure

Waliosoma kioindi cha huko nyuma, hasa wakati wa Mwalimu na Mwinyi, ndio wanaoelewa maana ya elimu bure, siyo hii ya kisanii ya sasa hivi. Pale UDSM tulikuwa tukipewa travel allowance, high education allowance, stationery allowance, field allowance, special faculty requirements allowance. Wengine mpaka waliwatunza wazazi wao, wengine tuliwasomesha wadogo zetu shule za private, kwa allowance ya chuo kikuu. Je, UDSM, Sokoine, Muhimbili, UDOM, Chang'ombe, Mkwawa, Uyole, n.k. vilijengwa awaku gani?

4) Afya
Nani asiyeijua Muhimbili, Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete, hospitali ya Benjamini Mkapa? Hizi zilijengwa wakati gani? Sijaongelea hospitali za Wilaya na mikoa zilizotapakaa nchi nzima. Thamani ya vituo vyote vya afya vilivyojengwa nchi nzima wakati wa awamu ya 5, thamani yake havifikii gharama ya ujenzi na vifaa tiba vya hospitali 2 tu, Mloganzila na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

5) Barabara

Barabara za lami, kilometa zilijengwa wakati wa awamu ya 5, hazifikii hata 25% ya zile zilizojengwa wakati wa awamu ya Kikwete.

6) Madaraja

Hivi daraja la Kigamboni, daraja la Umoja, na mengi madogo ya kawaida, yalijengwa awamu gani?

7) Viwanda

Hivi mnajua tulikuwa na viwanda hapa vya kuunganisha malori aina ya Scania pale Kibaha? Mnajua tulikuwa na kiwanda cha kuunganisha matrekta bora kabisa aina ya valmet? Mnajua tulikuwa na kiwanda cha kutengeneza baiskeli aina Swala? Mnafahamu kuwa tulikuwa na viwanda vingi vya nguo vilivyokuwa vikizalisha nguo zenye ubora, na siyo takataka hizi za China, India na Thailand? Mwatex, Mutex, Mbeyatex, Urafiki, n.k. Viwanda vingine kama vile vya kutengeneza transformer, Maturubai, viatu, matairi, n.k. Hivi kuna maajabu gani kwenye sekta hii yaliyofanywa na awamu ya 5?

8) Vituo vya Utafiti

Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila utafiti. NIMRI, TAFIRI, CAMARTEC zilianzishwa lini? Ni taasisi gani za utafiti zilanzishwa awamu ya 5?

Hii ni mifano michache sana katika kutaka kuwaelimisha watu wale wanaopumbazwa kuwa awamu ya 5 ndiyo pekee iliyofanya mambo makubwa ya kimaendeleo.

Kwa upande mwingine, wakati tunapiga hatua kwenye maendeleo ya uchumi, kulikuwa na jitihada kubwa sana za kuhakikisha tunajenga nchi yenye msingi mzuri na imara. Msingi imara wa Taifa ni umoja, na haiwezekani kuwa na umoja kama kuna ubaguzi, upendeleo, udikteta na uminyaji wa haki za msingi za raia. Katika hili, Serikali ya awamu ya 5, iliharibu sana. Na serikali ya Rais Mama Samia ifanye kazi kubwa sana kurekebisha maeneo yote yaliyoharibiwa, na ihakikishe tunapiga hatua kuanzia pale ambapo awamu ya 4 iliishia. Cha kwanza, ambacho ndiyo utakuwa mwongozo wetu mkuu, ni KATIBA MPYA.
 
Back
Top Bottom