Tumieni vizuri mitandaoni ya Kijamii

Tumieni vizuri mitandaoni ya Kijamii

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,741
Reaction score
25,681
22090169_1812053552170382_1815354537811334383_n.jpg

Bado huwa ninashangaa kuhusu watu wanaojimaliza kwa sababu ya mitandao ya kijamii, yaani kwa kuwa watu wamemsema sana, kesho kajiua, anakuwa na stress mpaka wengine wanalia huku wakiwa wamejifungia vyumbani mwao.

Wengi wamekuwa wakijiamini kwamba wao ndiyo wao, linapokuja suala la kuonyesha utofauti tu wanahangaika usiku na mchana. Hutakiwi kuonyesha kwamba wewe ni dhaifu hasa kwa watu usiowajua. Ni mara ngapi umekuwa kwenye matatizo? Je, marafiki zako wa mitandaoni walionyesha kukuunga mkono? Ni mara ngapi umekuwa ukiumwa, je, marafiki zako wa mitandaoni walikuja kukuona?

Kwa nini leo ukose raha kwa sababu ya watu hao? Kwa nini leo uogope kwa ajili ya watu hao? Ni lazima uwe na msimamo kwamba hutoyumbishwa na watu usiowahi hata kuwaona kwa kuwa unafanya vitu huku ukiwa umesimama peke yako. Kuna watu wakisikia kwamba unaumwa, wanafurahi na kukupiga vijembe, inakuwaje leo uwaogope watu hao?

Unatakiwa kuwa mwanaume au mwanamke wa chuma, usiyeyumbishwa kwa lolote lile. Huwa simsikilizi mtu wa mitandaoni, huwa sijawahi kuchukua ushauri kutoka kwa mtu wa mitandaoni na sijawahi kuwa na hamu ya kukutana na mtu wa mitandaoni na ndiyo maana nakuwa bize na muda wangu, ukitaka tuonane, kwanza subiri ubize uishe ambao siamini kama utaisha miaka hii mitano.

Ni lazima ifike muda ujitambue wewe ni nani, ni lazima ifike muda ujue kwamba watu wa mitandaoni si wote wazuri, si wote wanaotaka usimame, si wote wanaokuombea mema, wengine ukisema nimenunua nyumba, wanaumia moyoni, wengine ukisema nimepata kazi wanaumia moyoni.

Jaribu kuwaepuka watu wa mitandaoni, tena wakati mwingine fanya jambo kuwachukiza, waumie kwa sababu ya msimamo wako. Unapotaka kufanya kitu kumfurahisha kila mtu, hutoweza kabisa. Yesu alikuja duniani, akaponya watu, akafufua lakini mwisho wa siku akasulubiwa na Waisraeli wenyewe. Mtume Muhammad alisambaza Uislamu, akafanya kila lililo jema lakini amini kuna wengine walimchukia, kama hao wawili walichukiwa kwa mambo yao mema, wewe utapendwaje bwana? Kama watu wengine hawakuwasapoti kwa waliyoyafanya, wewe utasapotiwa vipi?

Hiyo ni mifano inayotakiwa kukuweka imara, ni mifano inayotakiwa kukushtua kwamba upo peke yako na hakuna mwingine. Leo ukisema nisifanye kitu fulani kwa sababu wakina fulani mitandaoni wataumia, kuna siku wao watafanya pasipo kujali kama utaumia au la.

Mwingine hawezi kuweka hata picha za wazazi wake kwa kuwa watu watawaona wamechoka, wengine hawataki kuweka hata picha za nyumbani kwao eti kisa kubaya, wengine wanashindwa kusema kwamba wanaishi Tandale, Tandika,Mbagala au Mwananyamala na sehemu nyingine za uswahili eti kwa kuwa kuna watu watawacheka. Ndugu yangu, unawaogopa watu wa mitandaoni? Unawaogopa watu wasiokuwa na makucha ya kukurarua? Unaogopa watu ambao hata ukiumwa hawatoweza kuja kukuona? Unawaogopaje watu ambao hata ukiwa na njaa hawatoweza kukupa chakula?

Kuwa na msimamo, anza na wewe mwenyewe. Ni lazima leo usimame na useme kwamba “Mimi nina msimamo na sitoyumbishwa”. Kwangu, nilijiwekea msimamo wa kuwasapoti watu. Mtu wa kwanza kabisa kumsapoti ni mimi mwenyewe, mtu akinishindanisha na mimi, nitajiweka kwenye ubora kuliko mtu yeyote duniani.

Baada ya hapo nitamsapoti mtu ninayeishi naye nyumbani, hata akishindanishwa na nani, nitasema wa nyumbani ni bora, baada ya hapo nitamsapoti ninayeishi naye mtaani au niliyewahi kuishi naye, nikimaliza nitamsapoti mtu wa Wilaya ya Kinondoni kwa kuwa ndipo ninapotoka, nikimaliza nitamsapoti mtu wa Dar, yaani leo ukisema wanamuziki wa Dar na Mwanza wakali nani, nitasema wa Dar. Baada ya hapo nitamsapoti mwanamuziki wa Tanzania hasa akiwa anapambana na wa kutoka nje ya Tanzania.

Ni msimamo ambao nimeuweka, huwa hauyumbishwi, huwa hauhitaji ushauri wa mtu mwingine. Katika maisha yangu ninajua kitu kimoja tu kwamba si kila mtu atakupa ushauri mzuri, wengine watakupa mbaya kwa kuwa wanatamani kuona ukianguka.

Si kila kitu naweka mitandaoni, si kila kitu ninatakiwa kumuonyesha mtu. Si kila mtu anatakiwa kujua ni gari la aina gani ninaendesha, si kila mtu anatakiwa kujua mshahara kiasi gani ninapokea kwa sasa, na si kila mtu anatakiwa kujua ni msichana gani mrembo niliyekuwa naye.

Ni muda ambao unatakiwa kufanya vitu wewe kama wewe, simamia kitu ambacho unakiamini. Wengi wamefeli kwenye mitandao kwa kuwa waliwaamini watu waliokuja kuwaangusha baadaye, si kila rafiki unayekuwa naye kwenye mitandao basi ndiye rafiki wa kudumu, mkubwa ambaye atakusaidia, wengine wapo kwenye sura za kutabasamu lakini nyuma wameshika visu kukuchoma.

Usiogope kuandika kitu chochote mtandaoni endapo tu ukijua huvunji sheria za nchi. Leo mtu wa Mwanza akilalamika, wa Mbagala akilalamika, wa Temeke au Tandika, sehemu nyingine ya nchi huku nikiwa sijawahi hata kuona sura zao ana kwa ana, huwa ninacheka, mtu akilalamikia kitu fulani, ninaongeza kingine ili azidi kulalamika kwani najua mwisho wa siku hatomwambia bosi wangu anipunguze mshahara, hatomwambia Mungu asinibariki, hatofanya kitu chochote kunirudisha nilipokuwa.

Wengine wanaandika posti kwa kuwa wanataka LIKES nyingi ambazo haziwezi kuongeza chochote, hazitowapa pesa wala kuwafanya kutoka walipokuwa. Ndugu yangu, kitu kimoja kitakachokufelisha maishani mwako ni kuwaamini watu wa mitandaoni kwa kutaka kuwafurahisha kwa kila kitu.

Ukishindwa kabisa, fanya kama ninavyofanya, ukiweka kitu watu wengi kikawauma, usiache, andika kingine ili kuwachoma vizuri, wakikasirika, usirudi nyuma, andika kingine kuwachoma zaidi, hayo ndiyo maisha yanavyotaka kuwa hasa kwa watu ambao huwajui na ambao unajua kabisa hakutotokea siku nikaonana nao au hata kunitumia pesa ya chakula.

Kama unaishi kwa kuogopa watu wa mitandaoni, ndugu yangu hilo ni kosa kubwa, kuna siku unaweza kujiua eti kisa Nyemo kasema kuhusu picha yako wewe ni mtu mbaya na sura yako inastahili kuogopesha watoto wasiotaka kunywa uji.

YOU HAVE TO REMEMBER, YOU CANT PLEASE EACH AND EVERYONE, SO DO WHAT YOU CAN DO TO PLEASE YOUSELF. (KUMBUKA KWAMBA HUWEZI KUMFURAHISHA KILA MTU, FANYA UWEZAVYO KUJIFURAHISHA WEWE MWENYEWE)
 
Ni kweli...

Tatizo binadamu wa siku hizi ni wabishi sana...

Ngoja niseme kile nachokiamini, tatizo lako kumbe ni hizo likes nyingi...



Cc: mahondaw
 
Mtandaoni ndio gengeni siku hizi tuangalie pia tusiwaudhi wengine kiasi cha kuwafanya wakose raha.
 
Back
Top Bottom