Tumeuona utakatifu wa “Mama” Teresa, Je, wa Julius Nyerere umefikia wapi?

Mdanganywa

JF-Expert Member
Jun 15, 2009
620
342
Neno "mtakatifu" linatokea kwenye magazeti mengi na hii ni makala mojawapo iliyoonekana juzijuzi
- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
HEADLINE: Tumeuona utakatifu wa “Mama” Teresa, Je, wa Julius Nyerere umefikia wapi?
TAREHE: OCTOBER 13, 2016
GAZETI: RAIA MWEMA, pg. 07
MWANDISHI: JOSEPH MAGATA
- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
Nakushauri kabla ya kuanza kuisoma na kushambulia hakikisha kwenye hiyo website, ya RAIA MWEMA kama kweli ndiko ilikotoka, sasa makala inasema kama ifuatavyo:

LEO ni siku ya 39 tangu Teresa wa Calcutta kutangazwa Mtakatifu pale Roma, wakati jana (Oktoba 11, 2016) tumetimiza miaka 30 tangu ndege yake ilipopata ajali katika kijiji cha Hombolo mkoani Dodoma. Na keshokutwa ni “Nyerere Day” ambaye naye Kanisa Katoliki linaendelea na utaratibu wa kama aliopitia Mtakatifu Teresa.

Sikujadili na yeyote na mtandao wowote siku Mama Teresa anatangazwa pale Vatican zaidi ya kuombwa na mhariri mkuu Godfery Dilunga niandike chochote kuhusu ninavyojua masuala ya utakatifu.

Utakatifu ni jambo refu, naamini kwa leo inaweza kuwa siku nzuri kueleza uelewa wangu kuhusu hili.

Je, utakatifu ni hali gani? Chimbuko la utakatifu ni aina ya maisha baada ya kifo.Yesu, alitoa mfano wa maisha ya tajiri mmoja na masikini aliyeitwa Lazaro kabla na baada vifo vyao (Luka 16:19-31). Pia, biblia inasema: “Yesu akamwambia, mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Anisadikiye mimi, hata kama atakufa, ataishi” (Yohana 11:25-26).

Wakati Yesu anafufuka, biblia inasema,“…makaburi yakafunuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala. Nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi: (Mathayo 27:52-53). Kwa kifupi huu ndiyo msingi wa dhana ya Watakatifu.

Kumtangaza mtu mtakatifu ni jambo refu na la kihistoria. Pale Golgotha, Yesu alimjibu Dismas hivi: “Amin, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradisini”: {Luka 23:43}. Hivyo, Dismas alitangazwa utakatifu na Yesu dakika chache kabla ya kifo chake na sasa anaitwa Mtakatifu Dismas.

Ukatoliki ulipoanza kusambazwa na mitume wa Yesu na wafuasi wao, serikali ya Roma ilikuwa inatawala eneo kubwa la Ulaya.

Ukatoliki, ilichukuliwa kama dini mpya kutoka Israel, lakini isiyopendwa na jamii na hasa kwenye suala la kutotii kwa serikali ilipokosa uadilifu.

Nguvu ya serikali nyingi nyakati hizo ilikuwa ni kuwa na askari, silaha na wapelelezi. Wakatoliki hawa hawakuogopa nguvu hiyo, waliendelea kuongezeka, maana hata kifo hawakukiogopa kwa sababu ya kusimamia imani yao.

Ilifika mahala hata maafisa wa serikali, wanajeshi na wapelelezi kidogo kidogo nao wakawa wanabatizwa wanakuwa wakatoliki.

Hili likaiogopesha serikali. Hivyo mwaka 303 serikali iliagiza wakatoliki wauawe kwa kuliwa na simba kwenye uwanja uitwao “Colosseum” huku umati ukifurika kuona wanavyoliwa na simba. Hadi leo uwanja wa “Colosseum” bado upo pale Roma.

Bado, wakatoliki waliendelea kuongezeka, tena na wale waliouawa wakafanywa mfano wa kuigwa kwenye jamii yao kwamba ni “watakatifu mashahidi wa imani”. Makaburi yao yaliyoitwa “catacombs” yakawa sehemu ya kuhiji, kuwaenzi na kuwaiga ujasiri wao.

Utakatifu huo ulitangazwa na wakatoliki wenzao. Kutangazwa kwa aina hii kunaitwa “acclamation”. Ikawa ndiyo njia ya kwanza ya kutangazwa mtakatifu, ukiacha aliyotumia Yesu kumtangaza Dismas pale msalabani.

Mwaka 325serikali ilisalimu amri kwamba imeshindwa kuwateketeza wakatoliki, kwani kadiri unavyowaua ndivyo wanazidi kuongezeka.

Matokeo yake serikali ikafanya mambo mawili. Kwanza akatangaza ukatoliki uwe ndiyo dini rasmi ya dola yote ya Roma. Kisha, mwaka 330, akiamini kwamba Roma hapatawaliki tena anayeheshimiwa ni Papa kuliko serikali, akahamisha serikali yote kutoka Roma kwenda Constatinople. Constatinople ndiyo Instabul ya sasa nchini Turkey.

Kuanzia hapo, mtawala wa dunia hii alijaribu tena kumvuruga Papa, kama alifaulu ni kwa muda tu, kwani aliishia kuondoka madarakani au utawala wake au dola yake kuanguka.

Sasa kukaibuka aina ya pili ya utakatifu, uliopatikana kwa kuishi maisha ya ujasiri wa kiimani uitwao “heroic virtue”. Hii aina ya watakatifu ikaitwa “Confensors”. Hivyo hadi leo kuna aina hizi mbili za watakatifu, yaani “mashahidi” na hawa “Confensors”.

Tangu mwanzo, makaburi ya watakatifu yalithaminiwa kwa hadhi kubwa. Mara nyingine juu ya kaburi lake ikajengwa altare ya kanisa au kanisa likajengwa pembeni ya kaburi lake.

Kaburi lisilofikika masalia yake (relics) yalihamishiwa panakofikika. Hadi wakati huu neno “canonization” lilikuwa halijaanza kutumika. Kitendo cha kuhamisha masalia kiliitwa “translatio”.

Wenzako kwa kushirikiana na askofu wa jimbo lao, kama walikuona unaishi maisha ya kitakatifu, basi ukifa, iko siku au hata kabla ya mazishi wanakutangaza kuwa “mtakatifu”, yaani njia ile ile ya “acclamation”.

Ilifika wakati askofu akaachiwa mamlaka ya kumtangaza mtu mtakatifu. Maaskofu walipoanza kudhibiti zoezi ndipo neno “canonization” likaanza kutumika, badala ya “acclamation.

Kitendo cha jamii au taifa kukubali kuwa fulani ni mtakatifu, hata bila askofu kukibariki kinaitwa “cultus”. Hivyo, wapo wafu waliopewa utakatifu na wenzao kwa kuamini hii “cultus” na askofu akaikubali baada ya miaka mingi.

Kazi ya kuwatambulisha watakatifu nje ya jimbo ilikuwa ngumu, hivyo ilihitaji askofu mwenye sifa ya kimataifa ambaye Papa tu.

Jimbo la Augsburg (Ujerumani ya sasa), likawa la kwanza kumuomba Papa amtangaze Ulrich kuwa “mtakatifu”. Papa John XV akakubali mnamo Januari 31, 993, Mtakatifu Ulrich akawa wa kwanza kutangazwa na Papa kwa njia ya “canonization”.

Utakatifu ni suala zito kuliko mali yoyote ya kanisa, hata kama ina thamani ya jumla ya pesa zote zilizoko duniani. Kutudanganya ulimwengu wote kuwa “fulani” ni mtakatifu, huku umedhamiria, wakati sivyo, ni zaidi ya ujambazi.

Hivyo, mwaka 1587, Papa alianzisha nafasi ya kisheria ya mtu aitwaye “Promotor Fidei” ili kazi yake iwe kulinda maslahi ya kanisa yanapokuja masuala ya utakatifu pale Roma. Masuala ya watakatifu yakaundiwa “tribunal”, yaani mahakama, yakaendeshwa kwa mtindo wa kesi.

Ukidai kuwa “fulani” ni mtakatifu na unapenda kanisa limtangaze, basi kanisa linaiona hiyo sasa ni kesi. Kinachofuata, kanisa linakuita kwenye “tribunal” yake pale Roma, uapishwe kusema ukweli, wewe utakuwa mtetezi (petitioner), lakini “Promotor Fidei” atakuwa mpinzani wako mkuu pale mahakamani.

Hivyo, ili mtu wako atangazwe kuwa mtakatifu ilikuwa ni lazima upangue hoja na maswali ya “Promotor Fidei”.

Januari 22, 1588, Papa Sixtus V alianzisha jopo lisaidiane na “Promotor Fidei” kwenye kesi hizi. Jopo hili siku hizi linaitwa “Congregation for the Causes of Saints” yaani “Jopo linaloendesha kesi za Watakatifu”. Huwa kuna makosa ya kuliita “Idara ya Kutangaza Watakatifu”.

Nikirudi kwa “Promotor Fidei”, alikuwa anatafuta tu upenyo (objection) ili akwamishe kesi kama wanavyokwamisha mawakili unaowajua.

Mfano ni wa mashahidi wa Uganda. Ilichukua miaka mingi kuwatangaza kutokana na vipingamizi vya “Promotor Fidei”. Kwanza alitaka wamtangaze Charles Lwanga tu, halafu wengine baadaye.

“Promotor Fidei” pia alihoji, kwa nini mashahidi wote 22 watangazwe, wakati baadhi kama Mukasa Kiriwawanvu hawakuwa wamebatizwa?

Hayati Askofu Joseph Kiwanuka wa Rubaga alipangua hoja hizi kwa kusema, haikuwa na mantiki kumtangaza Charles Lwanga peke yake, wakati mashahidi wote 22 waliishi kipindi kimoja, walisali pamoja na serikali iliwaua kwa pamoja.

Hoja ya ubatizo inajibiwa kwamba Charles Lwanga aliwabatiza wenzake usiku kabla ya kifo, na hata kama asingewabatiza, tayari walikuwa kwenye mafundisho, hivyo wamefia imani ya kanisa katika ngazi iitwayo “ukatekumeni”, hivyo nao wanapaswa kutangazwa: {Katekism ya Kanisa Katoliki, 1258-1260, 1281-1283}.

Hatimaye, Oktoba 18, 1964 mashahidi wote 22 wa Uganda wakatangazwa watakatifu: {‘The Observer’ (Uganda): Juni 01, 2014} au {www.observer.ug/news-headlines/32035–how-the-uganda-martyrs-passed-canonization-test}

Mfano huu wa mabishano, katika kesi kati ya “Promotor Fidei” na maaskofu wa Uganda, unakuonyesha jinsi “Promotor Fidei” alivyokuwa na nguvu, lakini pia alivyochukiwa hadi akaitwa “advocatus diabolic”, yaani mtu “mtetezi wa shetani”.

Hivyo, hadi leo, Kanisa Katoliki linapoanzisha shughuli ya kumpata mtakatifu, maana yake linakaribisha mabishano kutoka pande mbili duniani. Upande mmoja unaamini kuwa “huyu ni mtakatifu”, upande wa pili hauamini.

Mabishano yale ndani ya ile “tribunal” au kokote yatakatopokea, na ndivyo inavyotakiwa, yatakuwa ndiyo sehemu ya kujua ukweli unaotafutwa.

Kwenye mambo ya utakatifu, katika kiingereza, hawatumii neno linalomaanisha “mchakato”, yaani “process” au “procedure”, wala katika kilatini hukuti maneno “processus” au “procedendi”.

Ukisoma mambo ya utakatifu kiingereza, utakutana na maneno “cause”, “causes”, na katika kilatini, ambacho ndicho humaliza ubishi wa tafsiri, utakutana na maneno “causae”, “causis”, “causa” , “causas”, “causam”, “causarum”, ambayo kwa kiswahili ni “kesi”.

Hivyo, si sahihi kutamka “mchakato wa kumtangaza Sista Bernadeta kuwa Mwenyeheri”. Ukitafsiri kutoka kilatini, na hata kutoka kiingereza, tamko sahihi ni “Kesi ya Bernadeta Mbawala”.“Kesi” si neno geni kwani hata ninapohudumiwa hospitalini, hawasemi “leteni faili lenye mchakato wa kumponyesha Jose”, wanasema “leteni faili lenye kesi ya Jose”.

Kuanzia mwaka 1983, Papa alibadilisha sheria kwa kesi za utakatifu. Majina ya hizi sheria mpya ni haya,“Divinus Perfectionis Magister” inayofupishwa humu kama “DPM”. Nyingine ni “Normae Servandae”, inayofupishwa kama “NS”, na nyingine ilitoka Mei 17, 2007 iitwayo “Sanctorum Mater” inayofupishwa kama “SM”.

“SM, 4(2)”, inasema “Marehemu ambaye kesi yake imeanza kusikilizwa anaitwa “Mtumishi wa Mungu”. Sifa ya “Mtumishi wa Mungu” ni kwamba yumo katika uchunguzi ili kuthibitisha maombi ya walioanzisha kesi.

Askofu anaweza kuikwamisha mapema kesi kama ina matatizo kwa kutumia kifungu “SM, 44(2)”. Ninaposema “SM, 44(2)” hicho ni kifungu au ibara ya 44(2) ya “Sanctorum Mater”. Hivyo, wanaowaza kuwapata watakatifu ni muhimu wajue vikwazo huanzia wapi na lazima wasome sheria zile tatu.

“DPM, 13(1)”, inasema askofu akishatuma kesi yake kule Roma kwenye “Congregation”, kazi ya kwanza ni mtu aitwaye “Undersecretary” kukagua kama jimbo halikukosea taratibu za kisheria. Kisha, anawasilisha ripoti yake kwenye “Congregation”.Taarifa ya Jimbo la Songea kufaulu vigezo vya kisheria ilitoka Oktoba 17, 2013.

Sheria, “DPM, 13(2)” na “DPM, 7” inasema “Congregation” ikiona ripoti ni safi, inateua mtu aitwaye “Relator” ili aandae taarifa ya wasifu wa kikanisa yaani “heroic virtues” wa au jinsi mtu alivyouawa kwa kutetea imani. Taarifa hiyo inaitwa “positio”.

Hatua hii ndiyo Sista Bernadeta Mbawala wa Songea amefikia, kwani “Congregation” ilishamteua Profesa (Padre) Zdzisław Kijas, awe “Relator” wa kesi yake pale Roma tangu Januari 17, 2014.

Sheria ya Kanisa, “DPM, 13(3)” inasema, “positio” inatakiwa kwanza ipitiwe na kitengo cha wataalamu, hasa wa historia ambao husifika kwa kutunza kumbukumbu hata zisizofikika, zilizofichika, zisizosikika, zilizosahaulika, zisizohimizwa, zisizohamasishwa au zilizopindishwa.

Ilidhihirika wakati wa kesi ya Mary Stuart, malkia wa Scotland, aliyeuawa mwaka 1587 na kuanza kujadiliwa mwaka 1887 (miaka 300 baadaye), kwamba, ili kufanikisha kesi ya mkuu wa nchi na hata za zamani sana, ni muhimu kushirikisha wataalamu wa historia duniani.

Bila mabingwa hawa wa historia za dunia hii, Roma itataabika kupata maelezo ya kutosha kama anayoyasema Polycarp Kardinali Pengo aliponukuliwa hivi: “Licha ya Mwalimu kuwa mcha Mungu, lakini katika uongozi wake kulikuwa na dosari, kwa hiyo ukiangalia katika hilo kwa viongozi hao kutangazwa kuwa watakatifu ni lazima kuwe na maelezo ya kutosha na viambatanisho ambavyo kweli vinaonyesha kuwa anastahili”: {TUMAINI LETU: Oktoba 14, 2011, uk. 02, aya ya 7}.

Sheria, “DPM, 13(4)” inasema “Positio” ikishakubaliwa na magwiji wa historia na taaluma zingine, ndipo sasa anaichukua “Promotor Fidei” ili aongoze timu ya wataalamu wa imani ya kanisa katoliki (theologians) kuichambua kiimani.

Utaona kwamba hapa “Promotor Fidei” aliyekuwa kikwazo mwaka 1587 hadi 1983, sasa hana nguvu za uamuzi kama zamani na hafanyi peke yake. Kila mtu katika mfumo mzima anajitahidi kutafuta ukweli, si kupinga tu.

Kama kesi inahusisha muujiza, sheria “DPM, 8” na “DPM, 14(1-2)” zinasema lazima “Relator” atayarishe “positio” tofauti inayoelezea muujiza tu, lakini itapitia mkondo ule ule, isipokuwa ile sehemu ya wataalamu sasa watakuwa ni madaktari-bingwa wa ugonjwa uliopona kimiujiza, kama muujiza wenyewe ni ugonjwa.

Kesi ikishamiliza haya, ambayo ni ya kitaalamu, kwa vigezo vya kisayansi, basi kwa mujibu wa“DPM, 10(2-3)” ndipo “Promotor Fidei” anaiwasilisha “positio” kwa makardinali na maaskofu wa “Congregation”.

Hii ndiyo hatua itakayofuata kwa kesi Sista Bernadeta Mbawala kama kesi yake ngazi ile ya msururu wa wataalamu iliko sasa.

Makardinali wakishaichunguza “position”, iwe ni kwa mabishano au mjadala, kwa sababu hii ni kesi, wakiiridhia, ndipo mkuu wa “Congregation” aitwaye “Prefect” anaipeleka kwa Papa.

Ikifika kwa Papa, yeye naye kwa muda wake, na namna yake ya kuhakikisha anaitathmini. Akiiridhia, basi Papa anampandisha hadhi kutoka “Mtumishi wa Mungu” kuingia ngazi ya inayofuata iitwayo “Venerabilis”, sijui kwa kiswahili inaitwaje. Wengi hukosea wakieleza kwamba ukitoka “Mtumishi wa Mungu”, hadhi inayofuata ni “Mwenyeheri”.

Kwa ujumla kazi kubwa inakuwa imeishia hapa, kwani sasa “Venerabilis” anaheshimika na kanisa zima duniani, na anaweza kuigwa maisha yake, tunasema ana “heroic virtues”.

Kazi iliyobaki kwa kiasi kikubwa si ya duniani bali ya mbinguni, maana kinachosubiriwa sasa ni miujiza tu ambayo ikithibitishwa kama nilivyosimulia, basi wa kwanza unampandisha hadhi kuwa “Mwenyeheri”, na wa pili unampandisha hadhi ya kuwa “Mtakatifu”, ambapo Papa anafanya kile kitendo, “canonization”.

“Mwenyeheri” ni hadhi unayopewa na Papa, lakini siku hizi si lazima misa yake ifanyikie Roma. Polycarp Kardinali Pengo aliongoza maadhimisho ya kumtangaza Sista Irene Stephan wa Nyeri nchini Kenya kuwa “Mwenyeheri” mnamo Mei 23, 2015.

“Utakatifu” ndilo tendo linalolazimika kufanywa na Papa.Tofauti ya msingi kati ya “Mwenyeheri” na “Mtakatifu” ni historia kama nilivyoeleza. Kutangazwa “mwenyeheri”, hakuna tofauti na kile nilichoeleza kwamba ni sawa na wakati ule “mtakatifu” anathaminiwa kwenye eneo fulani tu.

Hata sasa, kuna kiwango fulani tu cha kumtumia hadharani “mwenyeheri” yaani “public veneration”, na mara nyingi ni kwenye jimbo alilotoka au shirika la wamisionari (religiuos) alilokuwa.

Tofauti nyingine ya msingi ni idadi ya miujiza. Anapofika hatua ya “mwenyeheri” unahitajika muujiza mwingine kumvusha kuingia hatua ya “utakatifu”.

Hivyo ukizipanga hatua ziko hivi: (1): “Mtumishi wa Mungu”, (2): “Venerabilis”, (3): “Mwenyeheri”, (4): “Mtakatifu”.

Miujiza inapojitokeza inapitia hatua zile zile za kesi, ila muujiza kama kuhusu Julius Nyerere ukitokea , si lazima umponye Mtanzania. Muujiza unaweza kumtokea mtu yeyote duniani. Sheria, “NS, 5(b)” inasema askofu anayeanza kushughulikia kesi yenye muujiza ni yule ambaye muujiza umetokea kwake.

Hivi ndivyo hatua zinavyokwenda. Tumeona historia ya jinsi zilivyobadilika tangu enzi za “acclamation” hadi sasa. Lakini dunia huwa inasahau kwamba, hizi sheria na haya mabadiliko hayamhusu Papa. Hivyo, hata leo, kama Papa ana uhakika na taarifa za marehemu, anaweza kumtangaza kuwa mtakatifu hata ndani dakika kumi baada ya kifo chake.

Akifanya hivyo, kihistoria tunasema amefanya ile “acclamation”, lakini siku hizi kuna neno jipya limekuja wanasema amefanya “Equipollent canonization”.

Mara nyingi, Papa hutumia sehemu ndogo sana ya “Equipollent canonization”, pale anapoondoa kizuizi cha miaka mitano cha kuanza kesi. Wakati mwingine anaiharakisha iishe kwa kuiendeleza pale ilipokwamia.

Desemba 17, 2013 Papa Francis alimtangaza mjesuit mwenzake Peter Faber kuwa mtakatifu. Hapa aliimalizia kesi kwa kutumia “Equipollent canonization”, baada ya Peter Faber kukwamia kwenye “Uenyeheri” kwa miaka 141 bila kutokea muujiza wowote.

Je, kesi ya utakatifu inaanzishwaje jimboni? Sheria za Kanisa, “SM, 10(2)” na “NS. 1(a)” zinamruhusu mkatoliki yeyote kutuma maombi ya kuanzisha kesi ya utakatifu wa marehemu, maadam awe tayari kulipia gharama zote.

Baada ya kuanzisha, Sheria “SM, 12(1)” na “NS, 2(a)” zinakuruhusu kupendekeza mtaalamu wa dini ambaye atasimama badala yako.

Mtu wa tatu unayetakiwa kumjua ni askofu unayepaswa kuifikisha kesi yako kwake.Tumeona kuwa hadi leo “acclamation” ipo, isipokuwa imebaki kwa mtu mmoja tu ambaye ni Papa, ikiitwa kwa jina jipya “Equipollent canonization”. Kihistoria tumeona kuwa jimbo lililoendesha “acclamation” ni lile alilofia marehemu.

Hivyo, maadam bado “acclamation” ipo, japo kwa mtu mmoja tu (Papa), bado jimbo linalostahili kuendesha kesi ni lile alilofia marehemu. Sheria ya Kanisa, “NS, 5(a)” imetungwa kwa kuheshimu hili inapoelekeza kwamba, askofu mwenye haki ya kushughulikia kesi ya utakatifu, ni yule wa kwenye jimbo alilofia marehemu.

Julius Nyerere alifia katika Jimbo Katoliki la Westminster. Hivyo Westminster ndiyo walikuwa na haki ya kuendesha kesi yake tangu alipofariki Oktoba 14, 1999. Kama ndani ya siku moja, Papa John Paul II angemtangaza mtakatifu kwa njia ya “acclamation”, ambayo wengine huiita “Equipollent canonization”, basi leo hii tungekuwa tunamwita “Mtakatifu Julius wa Westminster”.

Askofu aliyetaka kuhamisha kesi yake kutoka Westminster, alitakiwa atume maombi na sababu za kufanya hivyo. Hivyo askofu Justin Samba aliiomba Roma ihamishe madaraka ya kesi yake kutoka kwa Westminster, kwenda Musoma aliruhusiwa hivyo Mei 13, 2005.

Sijui askofu Samba alitumia kanuni gani naamini ilikuwepo kwa sababu kanuni “SM, 22” inayoelekeza hivi kutoka kwenye “Sanctorum Mater ” imetolewa Vatican mwaka 2007 wakati kesi imekwishaanza.

Baada ya askofu kupokea ombi, kwa kutumia sheria, “SM, 47”, askofu anaunda timu ya uchunguzi inayojumuisha wafuatao: Mwakilishi wa askofu, “Promotor Justitiae” na mtunza- kumbukumbu (Notary).

Hii maana yake ni nini? Maana yake, watakaohojiwa watarajie kukutana na hoja nyingi za “Promotor Justitiae”, cheo kipya kilichoanzishwa mwaka 1983, sikijui jina lake kwa kiswahili.

Sheria, “NS, 17” na “SM, 98” zinasisitiza mashahidi wanaotakiwa kwenye kesi kuwa ni wale wenye ushahidi wa moja kwa moja au walioishi au kufanya naye kazi moja kwa moja, wanaitwa “eye witnesses”, huku ndugu wa damu na wa ndoa ndiyo wakipewa kipaumbele zaidi.

Uchunguzi unapoisha jimboni, kuna hatua kadhaa za kupitia, kama vile wataalamu wa imani, madaktari-bingwa kama kuna suala la miujiza ya uponywaji. Mambo mengine yanayofuata ni kufunga kesi jimboni ili ianze hatua ya kule Roma niliyokwishaieleza.

Hapa Tanzania, Jimbo la Songea tu ndilo lililoweza kuivuka hatua hii mnamo (Januari 14, 2013).Mahakama ya Songea ilipata mashahidi zaidi ya 60 waliojitokeza kuthibitisha maombezi kupitia kwa Bernadeta na vitabu nane vikisimulia maisha yake.

Hebu tuzitazame kesi tatu zinazosimamiwa na “Postulator” anayeitwa Dk. (padre) Waldery Hilgeman, akisaidiwa na Br. Reginald Cruz, yaani kesi ya Julius Nyerere (Musoma), Bernadeta Mbawala (Songea) na Maurice Otunga (Nairobi).

Kesi zao zilianza majimboni katika tarehe hizi: Julius Nyerere (Januari 21, 2006), Maurice Otunga (Novemba 11, 2011), Bernadeta Mbawala (Januari 26, 2012). Kesi hizi zimeondoka majimboni humo kama ifuatavyo, Sista Bernadeta Mbawala (Januari 14, 2013), Maurice Kardinali Otunga (Septemba 28, 2013), Rais Julius Nyerere (Mei 01, 2014).

Utaona kwamba, kesi ya Bernadeta imetumia siku 303 tu jimboni Songea, ikaisha, ikaenda Roma. Kesi ya Julius Nyerere taarifa zinaonyesha imekwishahamia Dar es Salaam tangu Mei 02, 2014, kuendelea na ngazi ya jimbo.

Je, ni nini kuchelewesha kesi? Tumeona uzoefu wa “promotor fidei” wa zamani, lakini hata mfumo kesi wa sasa, bado si lelemama. Nimeeleza kifupi sana, ukiusoma wote utaona ulivyo mrefu lakini kila hatua inalazimika kukamilika.

Ziko sababu zingine hujitokeza. Gazeti la TUMAINI LETU, (ISSN: 0856-9606, Na. 00383) la Oktoba 14, 2011, kwenye ukurasa wa pili liliandika hivi “WANASIASA WAKWAMISHA NYERERE KUWA MWENYEHERI”.

Ukilisoma ndani utakutana na kauli za Polycarp Kardinali Pengo ambapo amenukuliwa hivi: “Tunasikia Rais wa Uganda na Rais wa Tanzania wanakutana na kujaribu kujadiliana kuhusu kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyeheri, wao inawahusu nini?”: {TUMAINI LETU: Oktoba 14, 2011, uk. 02, aya ya 4}.

Kesi ya Julius Nyerere ilipoanza, gazeti la KIONGOZI liliutangazia umma likisema “Taarifa zote zipelekwe kwa askofu wa jimbo la Musoma, Mhashamu Justine Samba, au kwa askofu wa jimbo lako ambaye atazifikisha Musoma na hatimaye zitakwenda Roma”: {KIONGOZI: Septemba 10, 2005}.

Wale ambao hawakuweza kufika Musoma kutoa ushahidi wa jinsi walivyoishi na Rais Julius Nyerere, ilitungwa sala maalumu na askofu Justin Samba ili iwasaidie na wao kupata ushahidi kama wataiheshimu ile sala iweze kupata miujiza kuthibitisha kesi ya Julius Nyerere.

Mwanzoni ndivyo ilivyokuwa. Kadi zenye sala ya Julius Nyerere zilisambaa majimbo yote Tanzania.

Ingawa Polycarp Kardinali Pengo alinukuliwa hivi mwaka 2011, wanaofuatilia dalili mpya zilianza kujitokeza tangu mwaka 2009. Yeye mwenyewe ananukuliwa hivi: “Kardinali Pengo alisema kipingamizi kikubwa ambacho kimejitokeza hadi mchakato huo kusuasua licha ya kuwa vipo vigezo ambavyo hayati Mwalimu Nyerere anastahili kuwa Mwenyeheri ni kuingiliwa na wanasiasa na makundi ya watu wanaotaka kujipatia umaarufu”: {TUMAINI LETU: Oktoba 14, 2011, uk. 02, aya ya 8}.

Zile juhudi za Polycarp Kardinali Pengo za mwaka 2011 ni kama vile hazikusaidia. Ilibidi gazeti la DAILY NEWS nalo litoe maoni kama ya Polycarp Kardinali Pengo, kuhusu mwenendo huo iliposambaa habari kwamba kuna mpango wa viongozi fulani kujiandaa kwenda Vatican kushawishi (to lobby), ili Vatican impe utakatifu Julius Nyerere kwani anastahili kuitwa mtakatifu: {DAILY NEWS: July 02, 2014, pg. 06}. Ukizitafuta habari hizi hata leo bado ziko mitandaoni.

Msomaji, yanayotokea si mageni duniani. Kesi ya Sista Bernadeta imeenda kwa utulivu na spidi ya ajabu, siku 303 tu jimboni.

Naurudia mfano wa nchini Scotland kwenye kesi ya Mary Stuart, wao wanamwita “Mary Queen of Scots”. Mwaka 1887, maaskofu hao wa Scotland walipendekeza kesi ile ishughulikiwe moja kwa moja na Papa.

Roma iliporudisha ile kesi ianzishwe na hao hao huko Scotland, basi kutokana na siasa na historia ya Britain kesi hiyo ikaishia kukwamia jimboni tangu 1887 hadi leo.

Huu ndiyo ugumu tunaotakiwa kuujua, kwa kesi za utakatifu za wakuu nchi hapa duniani. Wapo wanaobisha kwamba mbona, kuna wafalme duniani waliwahi kutangazwa watakatifu.

Nimeeleza “congregation” imeanzishwa mwaka 1588. Mtakatifu Edward tunayeadhimisha kesho alikuwa mfalme wa England alifariki mwaka 1066, alitangazwa utakatifu Januari 05, 1161. Mtakatifu Wenceslaus “Duke” wa Bohemia tunayemwimba wakati wa Krismas, alipata mwaka 938 enzi za “translatio”.

Wafalme Edmund (England), Hermenegild (Visigoths) na “Mwenyeheri” Humbert (Savoy) waliaminiwa na wananchi wao kwa muda mrefu kwamba ni watakatifu ikawa ni desturi iitwayo “cult”, hatimaye Papa akawatangaza utakatifu moja kwa moja kwa kitendo kiitwacho “cultus confirmed”.

Hivyo, katika Kanisa Katoliki, hakuna mkuu wa nchi hapa duniani, aliyewahi kutangazwa mtakatifu kwa kupitia njia hii ya kuanzishiwa kesi yake kutokea jimbo la nchi aliyoitawala.

Kupitia mfano wa “Mary Queen of Scots” na Julius Nyerere, kwamba Roma inapeleka kesi ya mtawala ianzie alikotawala, basi dunia imeshuhudia kuwa ni kuwapa taabu maaskofu wa nchi hiyo, kuanza kupambana na hamasa za kisiasa zinazoichelewesha au hata kuisitisha kabisa kesi yenyewe.

Tumeona sentensi kadhaa za Polycarp Kardinali Pengo akipambana na uanasiasa, nyingine hii hapa amenukuliwa akisema, “Tusianze kusema Mwalimu akiwa Mwenyeheri maana yake sisi CCM tumetangazwa watakatifu. Hii si shughuli ya kisiasa, wala akitangazwa usiseme sisi familia ya Nyerere tuko kwenye heri. Wapi, nani kakwambia, wote mko kwenye heri? Nayataja mambo haya kwa sababu yanajitokeza sana”: {TANZANIA DAIMA: Januari 14, 2012, uk. 01, aya ya nne}.

Hivyo, kama Roma wataona inafaa, ni bora kesi za hawa wakuu wa nchi duniani, ziwe zinasubiri karne kadhaa baada ya kifo chao, ili kizazi kilichoishi nao, kiwe chote kimekwishaondoka miaka mingi duniani.

Ikifanyika hivyo, haimuathiri marehemu, kwani, kama kweli ni mtakatifu, atabaki kuwa mtakatifu hata bila kutangazwa Roma. Haiwaathiri ambao tayari wanaamini kuwa ni mtakatifu kwani, wataendelea kuamini kama wanavyoamini baba, mama, mjomba, shangazi, babu, bibi na ndugu zao kuwa wako mbinguni.

Wala Kanisa Katoliki halitaathirika. Halijawahi kukumbwa na uhaba wa watakatifu. Watakaoathirika ni wale waliotarajia manufaa mengine tofauti na yanayojulikana na Kanisa Katoliki.

Cell: 075-4710684 Email: josephmagata@yahoo.com
 
Asante kwa Elimu hii murua. Binafsi nimeipenda: Venerabilis. Nilikuwa sijawahi kuisikia.
 
Heshima kwako sana Joseph! Hakika wewe ni kisima cha maarifa kwenye masuala mengi sana!!! Mungu akubariki tuko pamoja daima!!

wakimpa utakatifu nyerere nahama kanisa , huu uhuni wa ccm , nyerere hawezi kuwa mtakatifu
 
Back
Top Bottom