Tume ya Uchaguzi yaandikisha wapigakura milioni 21 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tume ya Uchaguzi yaandikisha wapigakura milioni 21

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, May 13, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 13, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,611
  Likes Received: 4,601
  Trophy Points: 280
  [​IMG] Yasema vifaa vingi vya kura vipo tayari  [​IMG]
  Baadhi ya wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakihakiki majina ya wapigakura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika ofisi za tume hiyo zilizopo kando kando mwa barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam jana.  Hadi sasa watu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK) ni milioni 21.8, ikiwa ni asilimia 86 ya lengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
  Kutokana na idadi hiyo, watu milioni 3.5 ndio waliobaki ili kufikia asilimia 100 ya lengo linalotarajiwa na NEC la kuandikisha wapigakura milioni 25.3 nchini kote katika daftari hilo.
  Lengo hilo la NEC linaweza kufikiwa katika muda ulioongezwa na NEC wa kuandikisha wapigakura mkoani Dar es Salaam, iwapo idadi ya watu ambao hawakuandikishwa wakati wa uboreshaji wa awali wa daftari hilo, itafikia ile ya waliobaki. Muda huo umeongezwa kwa siku mbili mfululizo; Mei 22 na 23, mwaka huu.
  Idadi ya watu walioandikishwa hadi sasa, ilitangazwa na Naibu Katibu Mkuu wa Uandikishaji Wapigakura wa NEC, Sisti Cariah, mbele ya Mwenyekiti wa Kundi la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UN) na Mtawala Mkuu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Helen Clark, alipotembelea kituo cha kuratibu shughuli za tume hiyo jijini Dar es Salaam jana.
  “Hadi sasa watu milioni 21.8 wameandikishwa na kuhusu elimu imekuwa ikitolewa kwa wapigakura, lengo ni kuhakikisha uchaguzi bora na makini ulio huru na wa haki,” alisema Cariah.
  Aidha, alisema vifaa vyote kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu, viko tayari isipokuwa karatasi za kupigia kura na kwamba, tume kwa sasa imejiweka vizuri katika mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT).
  Aliipongeza UNDP kwa ushirikiano mzuri iliyouonyesha kwa NEC tangu ilipoanza mwaka 2004.
  Naye Clark alisema UNDP imeridhishwa na utendaji mzuri wa NEC na kuusifia ushirikiano kati yao kwa kusem, tume imeonekana kufanya vizuri katika shughuli zake.
  Hata hivyo, aliishauri NEC kuhakikisha inaongeza elimu kwa makundi yote ya wapigakura, wakiwamo wanawake na watu wenye ulemavu nchini.
  Kabla ya kutembelea kituo hicho, Clark alipata fursa ya kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana na baadaye alikutana na watendaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, John Haule.
  Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, katika mazungumzo na Rais Kikwete Ikulu, Clark alisema uchaguzi wa kweli wa kidemokrasia siyo lazima ubadilishe chama tawala kwa vile maana halisi ya demokrasia siyo kubadilisha vyama tawala, bali kuwawezesha wananchi kuwa na haki ya kuchagua baina ya vyama vinavyowania madaraka.
  “Linalotakiwa ni kuwa na uchaguzi wa amani, ulio huru na wa haki kwa sababu maana halisi ya demokrasia siyo kubadilisha chama kilichoko madarakani, bali kutoa nafasi kwa wananchi kuchagua chama wanachokitaka,” alisema Clark.
  Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alitumia muda kumweleza Clark hali ya kisiasa na kiuchumi ilivyo nchini, na jinsi Tanzania inavyojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
  Katika mazungumzo hayo, Clark alimweleza Rais Kikwete kuwa ipo mifano mingi hata katika nchi zilizoendelea na za kidemokrasia ambako chama kimoja kilibakia madarakani kwa miaka mingi.
  “Chukua mfano hata wa Marekani ambako chama kimoja kinaweza kubakia madarakani kwa vipindi hata vitatu…ama chukulia mfano wa Japan ambako chama kimoja kilibakia madarakani kwa miaka mingi sana. Suala siyo kubadilisha vyama bali kutoa nafasi kwa wananchi kuchagua chama wanachokitaka,” alisema Clark.
  Viongozi hao pia walijadili hali ya kisiasa ya Zanzibar na maendeleo ya mchakato wa maridhiano, ambapo Rais Kikwete alisisitiza kuwa hali ya sasa ya kisiasa visiwani humo ilihitaji majawabu ya makubaliano na maridhiano.
  Kuhusu hali ya uchumi nchini, viongozi hao walikubaliana kuwa umaskini barani Afrika utapungua tu baada ya kuanza kukua kwa sekta zinazogusa moja kwa moja wananchi na hasa kilimo.
  Rais Kikwete alisema kuwa katika Tanzania, sekta ambazo zinakuwa kwa haraka zaidi, yaani sekta za mawasiliano, ujenzi na madini ni sekta muhimu lazima haziwagusi wananchi wengi zaidi moja kwa moja kwa karibu zaidi kama kilivyo kilimo.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...