TUKUMBUSHANE KIDOGO KUHUSU SIMBA NA EAG GROUP

Jeff Gemo

Member
Jul 11, 2015
34
26
(Unapoletewa mihogo kwenye box la Pizza)

Mambo mengi huja na kupita na tunasahau, lakini kuna muda kwakweli unapotaka suluhisho la tatizo lazima utazame ni wapi umeanguka. Ahsante sana Radio Times FM kupitia kipindi cha Wizara ya Michezo segment ya “Dokodoko”, ninaweza kusema hiki ni kipindi bora kabisa cha michezo kwa hivi sasa, hongereni sana kwa kuamua kujivika “mabomu”, nilipenda sana kipindi cha Alhamis mlipowakumbusha wasikilizaji wenu kuhusu EAG Group na Simba Sports Club.

Tangu Aveva alivyoingia madarakani kwa mbwembwe na vishindo, alikuwa hajafanikiwa jambo lolote kubwa kati ya yale aliyokuwa ameahidi. Kwahiyo wakawa wanaparanganika kuonesha kwamba wapo na wanawatumikia wapiga kura wao. Ndio sasa baada ya karibu mwaka hivi wakaja hawa EAG Group Limited kama mkombozi wa Simba Sports Club.

Nakumbuka ule Mkataba wa Simba na EAG Group ulisainiwa pale Southern Hotel kama kumbukumbu zangu zipo sahihi, ilikuwa tarehe 1/04/2015 (Siku ya wajinga Duniani) mbele ya wanahabari huku ukigubikwa na maneno matamu ambayo kila aliyetoka aliamini Simba inakwenda kubadilika na haitatokea timu itakuwa kama Simba.

EAG Group Limited kupitia Mkurugenzi wake Bw. Imani Kajula alisema ataendesha shughuli za kimkataba na Simba kwa kutumia uzoefu wa Timu ya Arsenal ambayo alidai kuna “biashara” wanafanya nayo, kwahiyo Simba ingekuwa kama Arsenal (Yaani Arsenal ya Uingereza.. Kajula mungu anakuona)

Kajula akasema Simba itakuwa na nguvu kubwa za kiuchumi, itakuwa na wadhamini wa kutosha na fedha nyingi tu ili waache kutegemea mapato ya getini pekee, hili lilishangiliwa sana na wanachama baada ya mkutano ule (hapa mpaka mimi nilikuwemo wala nisijitoe kwakweli, tulipigwamo changa la macho)

Aveva yeye alisema kwa mkataba huo wa EAG angeweza kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Bunju na kuboresha jengo la klabu lililopo kariakoo, sasa kumbuka wakati huo ulikuwa hutwambii kitu kuhusu Bunju, na ndio tunasuka timu yetu wenyewe, obviously angeeleweka sio kesi sana.

Baada ya hapo tukashuhudia Tigo wakiingia mkataba pia na Simba kuhusu SIMBA NEWS, ambayo hata hivyo sikumbuki kama tuliwahi kuambiwa inaingiza kiasi cha fedha kwenye klabu, lakini tarehe 22/06/2015 tukazindua website yetu wenyewe na picha za kutosha pale (si unajua kama Arsenal babu), ile event ikapita.

Sasa hivi ni mwaka mmoja na miezi saba tangu “ndoa” ya EAG Group na Simba Sports Club, Klabu anajiandaa kuingia kwenye mabadiliko (ambayo hayatatokea, sorry for that) huku inaendelea na mkataba wake na EAG ambao wameshindwa kutekeleza majikumu yao katika mkataba.

Simba imemamaliza mzunguko wa kwanza bila mdhamini, hii ni kazi ya EAG na walitakiwa kuhakikisha Simba ina wadhamini wa kutosha tangu wakati ule wa Kilimanjaro. Lakini pia hatujaona progress za Bunju kutoka kwa EAG, jambo kubwa labda ni wakati ule waliwapeleka wachezaji wetu “Tanzania Vijijini” kufanya branding ya jina, mbaya zaidi hakuna bidhaa iliyopelekwa katika maeneo hayo waliyofanya branding, sasa sijui walikwenda kufanya nini mungu wangu wa Israel.

Haya achana na hilo, wachezaji waliahidiwa Simu mpyaaa Huawei flani hivi maana nao pia waliingia mkataba na Simba, sina hakika kama hili lilitokea, wakasema mchezaji bora sijui atapewa gari, sijui mchezaji kijana mwenye kipaji, mambo chungu mbovu lakini ndio yameishia kwenye laki tano sijui, hakuna gari wala pikipiki, na EAG bado wapo tu.

Sasa Simba ni kwanini inaendelea kuwakumbatia EAG ikiwa sote tunaona hakuna la maana wanalofanya? Hii kampuni ililetwa na nani hapo Simba? (usiniambia habari za zabuni tafadhali) kwahiyo huyo aliyeileta ndio anaendelea kuicha ikae hapo bila kufanya kazi? Ni suala la aibu kabisa kwa uongozi mzima wa Simba, shame on you!! SHAME ON YOU!!!

Mabadiliko gani mtayapata na kuwaletea tija ikiwa mnashindwa kuwawajibisha EAG kuwa kutotekelesha ahadi zao (na labda masharti ya mkataba)? Simba imeshindwa kuuza jezi zake kama ilivyopanga awali, pale pale Klabuni chini kuna jezi fake kibao.. Sasa imagine mtu anauza jezi fake hapo hapo kwenye jingo la Klabu halafu unakuja unatuletea habari za Arsenal sijui nini, what do you know about merchandise business? Simba ilivyo na mtaji mkubwa hivyo unataka kusema jezi hazilipi?

Hivi hawa EAG wananufaika vipi na Simba Sports Club? Na sisi tunanufaika vp na wao? Naona ni mazingaombwe tu, Simba bado hawajielewi na ninadhani hii inatosha kuwapima katika safari ya mabadiliko, inawezekana Simba hatuhitaji mabadiliko ya mfumo wa Hisa, yawezekana hawa viongozi nao wakakimbilia kwenye Hisa ili kuficha makosa waliyoyafanya.

Mimi nadhani turejee mkataba wetu na EAG, tunaweza kusimamisha mchakato wa mabadiliko au kuhairisha kabisa kubadilisha mfumo uliopo na kwenda mfumo wa Hisa, yawezezekana sio hitaji letu na tukafanya kwa presha na sifa za kijinga ikaja kutugharimu. Simba wanaweza kupata fedha kupitia udhamini na haki za matangazo ikiwa watavunja mkataba na EAG na kutangaza zabuni upya ili tupate mtu makini anayeweza kutekeleza mipango kwa kutumia rasilimali zilizopo na ubunifu uliopo ndani ya uwezo wetu.

Simba bado haijajaribu kufanya jambo lolote kwa ukamilifu na kwa kutumia wataalamu, kabla ya kuwaza mabadiliko hebu kwanza tujaribu kujichunguza na tutazame tunapotoka, tujiridhishe na tuamini kweli bila mfumo wa Hisa klabu haiendesheki ndipo tuamue nini cha kufanya.

Tunaposema tunataka mabadiliko ya mfumo, sio lazima yawe ya kiuendeshaji, yawezekana ni mfumo wa kiutawala, kwanini Aveva sasa hivi anakimbilia mfumo wa uendeshaji badala ya kujipima yeye na watu wake katika utawala? Inawezekana labda tukipata mtu tofauti na Aveva mambo yanaweza kuwa sawa. Hapa ninachochajaribu kusema ni kwamba tufanye tathmini ya kweli ni wapi tumekosea, tusipelekeshane kama magari mabovu.

Simba imeikumbatia EAG kana kwamba ndio kampuni yetu ya masoko, mkataba hauna tija lakini hauvunjwi, Simba inakufa njaa lakini EAG hatuoni wanasumbuka, hawa ni kina nani? Rafiki yangu mmoja alinitania wakati Fulani akasema “EAG maana yake ni Evans Aveva Group ndio maana hawaondoki pale pamoja na kwamba hawana wanachokifanya” ni maneno ya utani lakini unaweza kuona pengine kuna ukaribu wa EAG na Simba zaidi ya huu tunaofikiria sisi.

Bado muda wa kubadilika tunao tunaweza kufanya hivyo ili kuiokoa timu yetu, matatizo yetu tuna uwezo wa kuyamaliza wenyewe, tuambiwe mafanikio ya EAG Group kwa Klabu yetu au basi tuwaombe watupishe ili tutafute watu wengine.

Nasisitiza siamini katika kuyakimbilia mabadiliko kwa pupa, hasa huu mzuka walio nao viongozi wetu ambao unanipa mashaka makubwa, ni lazima tukatae kuburuzwa na tusimamae imara tuwahoji ni kwa namna gani wanatumia rasilimali zetu, na tunafikiwa kwa kiwango gani?

Nimepitia maktaba kwangu na nimekutana na hotuba ya Aveva aliyoitoa siku ya wanasaini mkataba na EAG.

[[[[[[HOTUBA YA RAIS EVANS EVEVA 01/04/2015]]]]]]]

“Ndugu Imani Kajula, Mkurugenzi Mtendaji EAG Group LTD
Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club,
Wanachama wa Simba Sports Club,
Wageni waalikwa,
Waandishi wa habari,

Awaliyayote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwenu waandishi wa habari na waalikwa wote kwa kufika asubuhi hii kuja kushuhudia hatua kubwa Simba inayopiga leo. Napenda nianze kwa kuwaeleza Simba hana mzaha, kwahiyo mkutano wetu hauendani na umaarufu wa siku hii, kwani sisi tuko serious!

Wakati wa kampeni ya uchaguzi, Wananchama wengi na wapenzi wa Simba walizungumzia umuhimu wa timu yetu kujenga mfumo imara wa uchumi na mapato. Sisi ni viongozi wasikivu na tumelifanyia kazi agizo hilo kwani lina mantiki pana sana katika mpira wa leo.

Ndugu wanahabari,

Ni jambo lililowazi kuwa uwezo wa kifedha wa timu unamchango mkubwa sana katika kuleta ufanisi na maendeleo ya mpira na klabu yeyote. Wote tunatambua kuwa uendeshaji wa timu wenyetija ni aghali mno, na muhimu zaidi ikiwa timu inataka kujenga mfumo bora na kuifanya iwe tishio Nchini na Nje ya Tanzania, ni lazima iwe na misingi imara ya uchumi na vyanzo vya matapo. Hivyo niukweli usiopingika kuwa umuhimu wa kubadilika na kujenga uwezo wakifedha wa klabu yetu ya Simba ni suala muhimu sana ili kufikia malengo ya kuboresha kiwango cha uchezaji, motisha kwa wachezaji, ufundi na vifaa.

Wote mnatambua kuwa kuendesha timu ya mpira wa miguu kwa ufanisi ni gharama kubwa na pia ili kupata wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kushindana ni aghali zaidi, haya yote yanahitaji timu yenye mfumo na msingi imara wa fedha. Mpira wa vijana ni nguzo imara ya timu na kuendeleza soka katika Nchi yeyote duniani, pia ili hili nalo lifanikiwe ni lazima uwezo wa timu kuanzisha, kuhudumia na kuendeleza vipaji uwe mzuri.

Ndugu wanahabari,

Najua nyinyi ni watu makini wa kunukuu na kunusa, nadhani mmeona wazi kuwa mkutano wetu wa leo si kuhusu ufundi bali kujenga mfumo bora, wa uhakika na imara wa mapato ya klabu yetu ya Simba.

Mwezi uliopita, Simba Sport Club ilitoa zabuni ya kutafuta kampuni mshauri na mtekelezaji wa mkakati wa kuongeza mapato na biashara ya Simba Sports Club. Napenda kutumia fursa hii, kuwaeleza rasmi kuwa baada ya kupokea zabuni Simba Sports Club imeridhika na wasifu, weredi na uzoefu wa kampuni ya EAG Group LTD na hivyo kuipa kazi ya kuwa Washauri watekelezaji wa mkakati wa kukuza, kuanzisha na kuendeleza mapato ya klabu yetu ya Simba.

Tunafurahi kwamba mikakati hii ikitekelezwa tutaweza kukamilisha malengo makuu ya Simba ikiwemo;

•Kujenga uwanja wa Bunju,

•Kupata mapato yatokanayo na uuzaji wa jezi na vifaa vyenye nembo ya Simba,

•Kuongeza wanachama na ukusanyaji wa ada za kila mwaka

•Kuanzisha zawadi kwa mchezaji bora watimu, mchezaji kijana mwenye kipaji na pia mchezaji mwenye nidhamu wa timu. Hili tunalianza mwaka huu na mchezaji bora wa Simba atapata gari, Mchezaji bora kijana atapata Sh: 5,000,000 na Mchezaji mwenye nidhamu 2,000,000.

•Wachezaji hawa pia watapata simu ya mkononi aina ya HUAWEI yenye thamani ya Shillingi 1,100,000 kila mmoja.

•Pia mwaka huu tunaanzisha Tuzo ya mchezaji aliyetukuka yaani Hall of Fame ili kuenzi wachezaji wetu wa zamani.

•Pia ili kuwapa taarifa mashabiki na wanachama wake Simba Sports itaanzisha mfumo wa taarifa rasmi kwa ajili yao.

•Sherehe maalum ya Simba kwa ajili ya kuzawadia na kuchangisha fedha yaani Simba Gala, itayofanyika wiki maarufu wa Simba yaani Simba Day.

Haya ni machache mno kati ya mambo mengi ambayo yataanza kutekelezwa na kampuni ya EAG Group LTD.
Waswahili husema, matendo ni bora zaidi kuliko maneno. Lengo letu kubwa leo hii ni kuwashirikisha na kuwaeleza juu mikakati yetu, tuna uhakika salam na kishindo kitafika mtaa wa pili.

Napenda kuwashukuru sana kwa kunisikiliza na napenda kumkaribisha rasmi Mkurugenzi Mtendajiwa EAG Group LTD, Imani Kajula kuzungumza nasi.
Simba Oyeee!”

[[[[[[[[[[[[[[[MWISHO]]]]]]]]]]]]]]

Jeff Gemo Mnyama Machine
The One Man Army
Affirmative Gemo The Great

[HASHTAG]#SeriesFreeLife[/HASHTAG]
Season Two | Episode six
 
ngoja waje..
utasikia tuachie simba yetu..
sijui mwenye simba ni nani na asiye nayo ni nani
 
Mkuu nenda kwenye mkutano utoe maoni yako. Yatasikilizwa na utapata ufafanuzi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom