Tujifunze yanayotokea Uingereza tudumishe muungano wetu

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
MWEZI uliopita tulishuhudia taifa la Uingereza likipiga kura ya maoni ambayo imeonesha kwamba Waingereza wameamua kujitoa kwenye muungano wa nchi za Ulaya ambako wamekuwa wanachama kwa miaka takribani 50.

Matokeo ya kura hiyo yalikuwa asilimia 52 ya wapiga kura waliotaka Uingereza ijiondoe kwenye umoja wa Ulaya huku asilimia 48 wakipinga. Tukio hilo liliwashangaza watu wengi, kwani hata nchi 27 za Ulaya ambazo zimebaki kwenye umoja huo, hazikutarajia kwamba Waingereza wangeweza kupiga kura ya kujitoa. Hata nchi ya Marekani ambayo ni swahiba mkubwa wa Uingereza haikutegemea.

Athari za matokeo ya kura hiyo ya maoni zimeanza kuonekana kwani mara tu baada ya matokeo hayo, uchumi wa Uingereza umeanza kuporomoka. Thamani ya fedha yake, Pauni inashuka kwa kasi dhidi ya fedha ya umoja wa Ulaya, euro na dola ya Marekani. Aidha, Waingereza waliokuwa wakiishi na kufanya kazi kwenye nchi nyingine za Ulaya, wanafukuzwa kurudi nyumbani kwao halikadhalika raia wa mataifa yaliyo wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaoishi na kufanya kazi nchini Uingereza nao wanafukuzwa.

Kibaya zaidi, nchi za Scotland na Wales ambazo zinafanya muungano wa Uingereza zinatishia kujitoa kwenye Umoja wa Dola ya Uingereza (The United Kingdom) kwa sababu wananchi wengi wa nchi hizo walipiga kura kuunga mkono kubaki kwenye umoja wa nchi za Ulaya. Hivyo wanaona uamuzi uliofanywa na wapiga kura wa nchi ya Uingereza ingawa ndio wengi kwa idadi, lakini wao kama nchi hauwahusu, hivyo ni bora wajiondoe kwenye dola ya Uingereza.

Aidha kuna raia wa nchi hizo wanaotaka kura hiyo ya maoni irudiwe kwa sababu haikuzingatia uwiano wa wapiga kura wa kila nchi kati ya nchi zinazounda dola ya Uingereza. Hakuna uhakika iwapo kura hiyo ya maoni itarudiwa au haitarudiwa. Lakini kikubwa zaidi tunachopaswa kujifunza ni kwamba nchi ya Uingereza imeshapata madhara makubwa ambayo hayawezi kulipika, tofauti na walivyofikiria.

Kwa mfano, uchumi wa nchi hiyo umeporomoka na sarafu ya nchi hiyo kushuka kwa kasi. Pili, hatua hiyo imejenga uhasama kati ya Waingereza na watu wa mataifa mengine ya Ulaya. Tatu, Waingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mataifa mengine watapoteza ajira na kurudi nyumbani. Nne, Uingereza imepoteza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji ambazo ilikuwa inazipata ndani ya Umoja wa Ulaya.

Sasa zile ndoto kwamba Uingereza ikijitenga na Umoja wa Ulaya, itakuwa taifa kubwa kama Marekani, imethibitika kwamba sio za ukweli. Badala yake Uingereza inaweza kuwa taifa dhaifu zaidi. Kutokana na hali hiyo maelfu ya Waingereza wamekuwa wakiandamana kutaka Uingereza ibakie kwenye umoja wa Ulaya, baada ya kugundua kwamba madhara ya kujitoa ni makubwa kuliko faida.

Hivyo ndugu zangu watanzania, mfano huo wa Uingereza uwe fundisho kwetu kwani hapa kwetu kuna watu wanaleta chokochoko za kutaka kuvunja Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar ulioanzishwa mwaka 1964 na waasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amaan Karume. Tukumbuke kwamba Muungano huo, ulitokana na historia ya nchi zetu mbili, kwani ni ukweli kwamba zaidi ya asilimia 55 ya Wazanzibari wana asili ya Tanzania Bara. Na sasa hivi tumeoleana na tunashirikiana sana.

Lakini kwa muda mrefu kumekuwepo na chokochoko za kutaka kuvunja Muungano kwamba Zanzibar itapata neema na maendeleo makubwa (wanadai itakuwa kama Dubai au Singapore) ikijiondoa kwenye muungano. Mfano wa Uingereza umetuonesha kwamba dhana hiyo sio ya kweli, badala yake madhara ya kuvunja muungano yatakuwa makubwa kuliko faida. Kwa mfano, kisiwa cha Pemba nacho kinaweza kudai kuwa nchi huru.

Aidha tukumbuke kuwa kuna wazanzibar zaidi ya milioni 2 wanaoishi na kufanya kazi Tanzania Bara, sasa Muungano ukivunjika watakwenda wapi? Pia, kuna wafanya biashara Wazanzibari waliowekeza huku bara, muungano ukivunjika watakosa fursa hizo. Ni dhahiri kwamba madhara yatakuwa makubwa kuliko faida kama ilivyotokea huko Uingereza. Kikubwa zaidi ni suala usalama, huweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mfano, Sudan Kusini ilipojitenga na Sudan ya Kaskazini, sasa Sudan Kusini wanapigana wenyewe kwa wenyewe. Nchi ya Yugoslavia, ilipotengana na kuwa mataifa matatu ya Serbia, Croatia na Bosnia walianza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo maelfu ya watu waliuawa. Urusi na Ukraine ambazo zamani zilikuwa taifa moja na kutengana hadi leo wanapigana vita kugombea mipaka, maslahi na kadhalika.

Hata huku kwetu Tanzania Bara, hatuko salama kwani kuna baadhi ya wanasiasa wa chama fulani na baadhi ya viongozi wa dini wanazungumzia kitu kinachoitwa Meru Republic, bila aibu tena hadharani. Hivyo iwapo muungano utavunjika watu hawa wanaweza kupata sababu ya kuidai hiyo inayoitwa Meru Republic. Hata hilo wazo la Tume ya Warioba kuwa na Muungano wa serikali tatu, pamoja na kwamba linashabikiwa na Ukawa, mimi na chama changu cha TLP hatuliungi mkono, tuna wasiwasi kwamba huenda ikawa chanzo cha kuvunja muungano.

Maana unapokuwa na serikali ya muungano ambayo haina ardhi, wala vyanzo vya mapato, itakuwa dhaifu isiyo na meno, hivyo ni rahisi nchi mojawapo ikajiondoa na kusababisha madhara kama niliyo yataja awali. Ndugu watanzania, tuelewe kwamba kuna wanasiasa wanaotaka kuvunja muungano kwa sababu za maslahi yao binafsi pamoja na uchu wa madaraka.

Pengine kuna mtu anaona muungano ukivunjika yeye atapata urais wa nchi fulani Wanasiasa hao wameshasema kwamba wakiingia madarakani wanataka Zanzibar iwe na sarafu yake, iwe na jeshi lake na iwe na kiti kwenye umoja wa mataifa sasa tujiulize vyote hivyo vikiwepo, je, muungano utakuwepo? Waswahili walisema ‘Fumbo mfumbie mjinga, mwerevu atagundua’. Hivyo watanzania tuwe macho na wana siasa wa aina hiyo wanaotaka kututenganisha undugu wetu wa tangu enzi na enzi ambao ndio ulizaa muungano wa Tanzania.

Mwisho, somo ambalo watanzania tujifunze kutoka Uingereza ni hili suala la kurudiwa kwa uchaguzi. Tumeona sasa baadhi ya nchi zilizo kwenye dola ya Uingereza zinataka kura ya maoni irudiwe na hata baadhi wananchi wanataka kura ya maoni irudiwe. Hivyo, kurudiwa uchaguzi, sio jambo jipya na geni hapa duniani. Hata taifa la Australia lilirudia uchaguzi.

Nawashangaa baadhi ya wanasiasa na baadhi ya vyama kususa uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na badala yake wanamtaka Rais Magufuli awatangaze kwamba wameshinda, jambo ambalo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na ya Muungano hana uwezo nalo. Nawashangaa kwamba iwapo waliona Tume ya Zanzibar haina uwezo wa kufuta uchaguzi huo, kwa nini hawakulipeleka suala hilo mahakamani.

Mahakama ndio yenye maamuzi ya mwisho kwa mujibu wa katiba zetu. Sasa wanakimbilia kuomba msaada ili mataifa ya Ulaya na Marekani yaingilie kati na kuwapa ushindi, jambo ambalo haliwezekani kwa kuwa sisi ni mataifa huru. Pengine wanataka kuturudisha kwenye ukoloni mamboleo kwa mlango wa nyuma. Watanzania tujihadhari.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa TLP na Mbunge wa zamani wa Vunjo

Chanzo Habari Leo
 
Back
Top Bottom