Serikali Mashirika ya Umma nao wahusika
NHC, TBA, PPF nao kama NSSF?
Wahariri wathibitisha ukihiyo wao sekta ya Majengo
Wananchi wahoji Ni Dk. Dau au kuna jingine?
BAADA ya Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG) kutoa taarifa ya kutohusika na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna ufisadi mkubwa kwenye miradi ya Shirika la Hifadhi ya Jamii(NSSF), mengi zaidi yagundulika yaliopo nyuma ya pazia, imefahamika.
Taarifa za kuaminika ilizozipa gazeti hili imegundulika kuwa kashfa zilizotolewa dhidi ya NSSF kwamba lilinua ardhi kutoka kampuni ya Azimio Housing kwa thamani ya ekari moja sh. milioni 800 ni kashfa ya kutungwa kwa malengo maalumu.
Uchunguzi wa gazeti hili unathibitisha kuwa kilichofanywa na NSSF ndio kinachofanywa na taasisi zote nchini katika sekta ya nyumba ( real estate sector).
Baadhi ya magazeti nchini na mitandao ya kijamii iligubikwa na habari kwamba katika uwekezaji wake NSSF lilipandisha thamani ya ardhi kutoka kwa wawekaji.
Moja ya gazeti la kila siku nchini lenye kuheshimika liliingia kwenye mtego wa kutumika kwa kuthubutu kukokotoa thamani ya mradi dhidi ya mchango wa ardhi wa mbia wa NSSF na kupotosha umma kuwa shirika hilo lilinua ardhi kwa bei ya juu.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa katika sekta ya majengo, ardhi huwekewa thamani kulingana na kiwango cha uwekezaji katika mradi ili wenye ardhi kuweza kufaidika.
Mashirika mbalimbali ya umma na watu binafsi wamefanya hivi na iwapo mifano itawekwa ni dhahiri hata viongozi wakuu wa nchi wangekuwa majipu. Baadhi ya mifano imeanishwa hapa kwa faida ya wasomaji wa gazeti letu.
Miaka ya 90 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liliingia makubaliano na Shirika la Mafuta la Taifa ( TPDC ) kujenga Mafuta House kwenye ardhi inayomilikiwa na NHC katika eneo sasa pamejengwa Banjamin Mkapa Towers.
NHC walipewa asilimia 25 ya thamani ya mradi kwa kutoa ardhi ( Land for Equity ) ambayo mwaka 1995 ilikuwa ni Shilingi bilioni 19 bilioni. Kwa mujibu wa mkataba huo thamani ya ardhi ile mwaka huo ilikuwa shs 4.75 bilioni.
Mwaka 1995 thamani ya ardhi katikati ya jiji ilikuwa ni shilingi 62,500 kwa kila mita ya mraba na kiwanja kile kina mita za mraba 6,221 sawa na ekari moja na nusu.
Kwa kutumia mahesabu ya magazeti yaliyoshupalia sakata hili, thamani ya ardhi ya NHC ingekuwa shilingi 388 milioni na hivyo bei kukuzwa mpaka shilingi 4.8 bilioni sawa na nyongeza ya shilingi 4.6 bilioni.
Ni dhahiri mwandishi na wahariri wa magazeti yaliyoandika habari zile hawana chembe ya ujuzi katika sekta ya ujenzi wa nyumba.
Shirika hilo hilo la NSSF ni mfaidika wa mradi wa ardhi kwa hisa katika mradi wa Umeme Mkuranga ambapo mwaka 2014 NSSF walinunua ardhi kwa thamani ya shilingi 100 milioni jumla ya ekari 100 ili kuweka mtambo wa kufua umeme.
Mwaka 2015 Wawekezaji waliingia ubia na Shirika kujenga Mtambo wa Umeme na mchango wa NSSF ukawa ni ardhi yake na kupewa asilimia 10 ya thamani ya uwekezaji wa Dola za Kimarekani 450 milioni.
Kwa mahesabu ya magazeti na wahariri vihiyo NSSF ndani ya mwaka mmoja iliweza kupandisha thamani ya ardhi ile kutoka shilingi 100 milioni mpaka shilingi 90 bilioni! Kama hesabu za wahariri hao ni sahihi basi NSSF badala ya kuwa na asilimia 10 ya mradi ingekuwa na asilimia 0.06 kwani ndio thamani ya ardhi yake.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa shirika la NHC wameingia makubaliano na Shirika la PPF kujenga PPF Tower Mwanza ambapo NHC walitoa ardhi na kupewa hisa ya mradi asilimia 25. Mradi una thamani ya sh. bilioni 258 na ukubwa wa kiwanja cha NHC ni ekari moja tu. Lakini kamwe huwezi kusikia PPF wamenunua ekari moja kwa sh. bilioni 64 . Huwezi kusikia hivyo kwa sababu ndio sekta inavyoendeshwa.
Shirika la NSSF limejenga jengo la Shirika la Umma la RITA jirani na klabu ya Billicanas ambapo RITA wametoa ardhi tu na kupewa asilimia 25 ya mradi mzima wa sh. bilioni 198. Kiwanja cha RITA ni nusu ekari. Kamwe huwezi kusikia NSSF wamenunua nusu ekari kwa sh. bilioni 49.
Wakala wa Majengo Tanzania ( TBA ) iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi ambayo Waziri wake alikuwa John Pombe Magufuli ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga jengo maeneo ya Ocean Road Hospitali kwa kuingia ubia na kampuni ya Fida-Hussein ambapo TBA wamepewa 25% ya mradi ule wa mabilioni ya shilingi kwa kutoa kipande cha Ardhi tu.
NSSF iliingia ubia na kampuni ya Azimio kwa kampuni ya Azimio kutoa Ardhi na kupata asilimia 20 ya thamani ya mradi wa Dege Eco Village.
Nini tofauti kati ya NSSF na Mashirika hayo mengine kwa mifano iliyoelezwa? Ni dhahiri kuna jambo zaidi ya miradi. Wakati utaeleza nini kilichopo nyuma ya pazia. Gazeti hili litakuwa mstari wa mbele kabisa kueleza ukweli wa suala hilo.
Chanzo: Jamvi la Habari