Makanyaga
JF-Expert Member
- Sep 28, 2007
- 11,544
- 7,484
Tufute mfumo wa vyama vingi
Na Deodatus Balile
Ni wiki mbili sasa sijawa katika safu hii kutokana na matatizo yaliyo nje ya uwezo wangu. Naomba uniwie radhi msomaji. Katika ‘Sitanii’ mbili zilizotangulia, niliahidi kuzungumzia mbinu bora za kufanya biashara na nikagusia wenzetu wa Morocco walivyogeuza mwelekeo kwa kuruhusu uwekezaji wa kuanzia dola 15,000 (yaani Sh milioni 35 hivi) na jinsi walivyoweka mazingira wezeshi katika biashara.
Sitanii, wiki iliyofuata ikaja ndege ya Dreamliner, ambayo ilizua mjadala, nami nikasimama kidete kusema bayana kuwa ununuzi wa ndege una faida kubwa kwa taifa hili kuliko hasara. Ukiacha suala la heshima kwa taifa, usafiri wa ndege ni injini ya utalii. Hakuna mtalii atakayekuwa tayari kukamuliwa fedha ndefu kuja Tanzania na kutumia muda mwingi kwenye viwanja vya jirani Bujumbura na Nairobi, kisha useme tutajenga utalii.
Kwa sasa utalii unachangia asilimia 17 ya pato la taifa, na hii ni kwa wastani wa watalii milioni 1.5, tunaowapata kwa tabu sana kwa mwaka. Leo nauli ya ndege ya kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya ambako ni mwendo wa saa moja inalingana katika kipindi cha msimu wa tiketi za punguzo na nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda London, Uingereza.
Wakati Kenya Airways ikiwatoza watalii wastani wa Sh 600,000 kwa safari ya Nairobi – Dar – Nairobi, ambao ni umbali wa saa 1, Kenya Airways hiyo hiyo inakuwa na tiketi za punguzo za hadi Sh 800,000 kwa safari ya Nairobi – London – Nairobi, umbali
ambao mtu anakaa hewani kwa saa 9. Hii ina maana inakatisha tamaa watalii wenye nia ya kuja hapa Tanzania kwa kuona nauli inatisha. Ndege za Air Tanzania zitamaliza kadhia hii.
Sitanii, wiki hii wakati nahangaika huku na kule, nikasikia taarifa zilizonishtua. Nikasikia kuwa Mbunge wa Ukonga (CHADEMA), Mwita Waitara amejiuzulu ubunge na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nasikia na mwingine yuko njiani. Hatua hii ya Waitara imekuja siku chache baada ya wabunge Dk. Godwin Mollel wa Siha (CHADEMA) na Abdallah Mtulia wa Kinondoni (CUF), kuwa wamevihama vyama vyao wakajiunga na CCM, kisha wakateuliwa kugombea majimbo hayo hayo kwa tiketi ya CCM na sasa wamo bungeni.
Mimi sina tatizo na uamuzi binafsi wa mtu kujiuzulu uanachama wa chama chake na kujiunga na chama kingine. Napata tabu uamuzi huo unapotugharimu sisi walipa kodi katika mazingira yanayotiliwa shaka. Gharama tunazozitumia katika uchaguzi
mdogo iwapo tungezitumia kuchimba visima vya maji, Watanzania wengi wangeneemeka.
Si hilo tu, kinachokera zaidi ni kuona mtu anaacha ubunge kisha anagombea ubunge katika jimbo hilo hilo. Zimekuwapo tuhuma za michezo michafu yenye lengo la kuua ushindani wa kisiasa. Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, alifanya kosa hilo hilo la kujivua ubunge wa CCM na kuingia kwenye upinzani (CHADEMA). Naye akaliingiza taifa katika gharama ya uchaguzi mdogo.
Sitanii, sababu zinazoelezwa na wabunge husika wanaohama haziniingii akilini. Najiuliza, tuna sababu gani ya kuendelea na
mfumo wa vyama vingi? Kwa nini kwa mtindo huu tusifute mfumo wa vyama vingi tukawa kama China? China wana chama tawala cha CPC na vyama vya ushauri (upinzani) vinane. Ushauri wa vyama hivi unafanyiwa kazi bila kubezwa.
Tatizo ninaloliona hapa kwetu, inawezekana elimu ya siasa hatujaielewa vema. Tumechukulia ushindani wa kisiasa kama
uhasama, badala ya harakati za kuliletea maendeleo taifa letu. Lakini pia nadhanai wakati umefika kama nchi tuwe na utaratibu wa kuwachunguza hawa wabunge wanaohama vyama. Tuwachunguze hawa kina Nyalandu, Mwita, Mtulia na Mollel.
Tuangalie akaunti zao zina fedha kiasi gani? Tuangalie mali walizokuwa wanamiliki kabla ya kuwa wabunge na mali wanazokuwa nazo hadi wanajiuzulu, kisha tulinganishe na mshahara wanaopata kama vinaendana. Tukiendelea na utaratibu huu wa watu kujiengua kwenye vyama tukaenda kwenye uchaguzi mdogo, na pengine utakuta mtu kama Mwita naye anagombea tena kwa tiketi ya CCM, nadhani tutakuwa hatuna sababu ya kuendelea na vyama vingi nchini. Tuufute mfumo huu.
Source:Tufute mfumo wa vyama vingi | Gazeti la Jamhuri

Last edited by a moderator: