Tuanzishe idara maalum za ushauri shuleni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tuanzishe idara maalum za ushauri shuleni

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by PERECY, Mar 18, 2012.

 1. PERECY

  PERECY Member

  #1
  Mar 18, 2012
  Joined: Jan 11, 2012
  Messages: 29
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  (Wana JF, makala hii ilitoka katika gazeti la Jamhuri J4 ya Machi 13, tafadhali mawazo yenu ni muhimu sana, kwani elimu yetu imekuwa bandia):

  Tumeshuhudia matokeo mabya ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2010 na 2011. Mshtuko umeongezeka kwa wazazi, na watoto wenyewe. Hatma haijulikani. Hakuonekani maono yenye kujenga matumaini na mabadiliko ya hali hii karibuni.


  Darasa la wanafunzi 252 waliomaliza katika shule fulani Iringa manispaa, wamekosekana wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili, 13 daraja la tatu, 98 daraja la nne, na 141 daraja sifuri. Matokeo ya shule nyingi yana taswira hii, kwa shule nyingi za watoto wa familia maskini. Tuendelee ‘kutafakari'? Tutachukua hatua lini?

  Dira ya Tanzania 2025 inajielekeza katika kuwezesha jamii yote kupata elimu ya msingi, kuondoa ujinga na kufikia elimu na mafunzo bora ya ngazi ya kati, kwa kuwajengea stadi na maarifa stahiki. Kwamba, elimu ni wakala, nyenzo na mkakati muhimu wa kubadili mitazamo na fikra za watu, ili kujenga taifa la wasomi, waliopandikizwa maarifa kwa ufanisi na umahiri wenye kulenga mahitaji ya ushindani kutatua changamoto zinazolikabili taifa.

  Hivyo, mfumo wa elimu umeumbwa kulenga ubora; mbiu ya kipaumbele ikihimiza sayansi, hesabu na teknolojia kuanzia ngazi za chini – kwa watoto wote wa kuanzia umri wa miaka 6 – 15. Sayansi na hesabu zinapewa umuhimu kwa kuzingatia uhitaji wa soko la teknolojia mpya, bila kupoteza mwelekeo katika mambo ya kijamii. Jamii maskini zikihakikishiwa kupatiwa elimu bora ya msingi. Rasilimali na mahitaji ya elimu yakiongezwa na kusimamiwa vizuri.Ufadhili wa kutosha kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu. Elimu ya awali haikuachwa.

  Mikakati imetajwa. Miongoni mwake ni kupunguza kwa kiwango - wezeshi gharama za elimu na mafunzo ya chuo kikuu; kuhimiza mahusiano miongoni mwa wadau na taasisi; sekta binafsi na jamii ishiriki utoaji wa elimu; kurekebisha mitaala kwa kulenga zaidi sayansi na teknolojia; kuhimiza uwiano kati ya vifaa na watumishi/wafanyakazi (walimu); kuhimiza sekta binafsi kuwekeza elimu katika jamii za chini ili kuchota uwezo wao wa ubunifu; kuanzisha program maalumu zitakazolenga kaya maskini zinafikia elimu ya msingi, n.k.

  Sera ya Elimu na Mafunzo haikubaki nyuma. Imebeba zaidi ya sentensi 125 za kisera kuhusu mfumo wa elimu, usawa wa kufikia, usimamizi wa sekta, mfumo rasmi wa elimu na mafunzo kwa ngazi zote, mitaala na mitihani, mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya kati, elimu isiyo rasmi, na ugharamiaji mafunzo.

  Sera inasema malengo ya pamoja ya elimu ni kuendeleza wasifu tegemeana za utu wa mtu (integrative personalities); kuendeleza na kufurahia utamaduni wa taifa na Katiba ya nchi; kujenga taifa la watu wenye kupenda kujifunza na kutumia stadi na maarifa waliyopata kuboresha hali za maisha yao; kuwajengea kujiamini, na akili ya udadisi, na mtazamo wa kulenga maendeleo; kuwapa elimu inayoendana na mabadiliko ya dunia ili kuweza kukabili changamoto mbalimbali; kuhimiza kupendana, tabia ya kuheshimu kazi ya aina yeyote na kuongeza uzalishaji; kupandikiza tabia ya maadili, umoja wa kitaifa,mahusiano ya kimataifa, amani na haki; kusimamia taifa na matumizi ya mazingira, na kuboresha ufanisi wa elimu katika soko la ajira na mafunzo ya ufundi stadi. Je tunaenda sawa katika malengo haya ya elimu?

  Shule za sekondari kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne zina changamoto kubwa. Kwa mtazamo wangu, hakuna hatua ngumu katika maendeleo ya mtu (kibaolojia na ukuaji wa kiakili) kama katika umri wa mwanafunzi anapoingia kidato cha kwanza mpaka cha nne. Ni hatua ya muhimu ya kielimu yenye kuweza kumsaidia mtu kujua mwelekeo wake kimaisha (kusimama au kuanguka). Kwa matokeo kama hayo hapo juu kwa shule moja katika manispaa ya Iringa, malengo mahsusi ya elimu yanasiginwa!
  Tanzania ilikuwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) 2002 – 2006, na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) 2004 – 2008. Mipango hii ililenga pamoja na malengo mengine, kuongeza uandikishaji shule za msingi na wanaojiunga na sekondari. Mafanikio makubwa yameonekana. Madarasa yamejengwa, na kumekuwepo jitihada za kuzipatia shule walimu. Tukisuasua katika maabara na vifaa vya kutosha. Changamoto ni kubwa na hasa kwa shule za maeneo ya vijijini.

  Taarifa za utafiti, zinaonyesha kwamba, kwa ujumla, mabadiliko makubwa ya kielimu yalishuhudiwa kwa miaka mitano iliyopita (2002 – 2006). Baada ya serikali kukwepa kwa muda mrefu, jitihada hizi ambazo zilitakiwa siku nyingi. Taarifa inasema utashi wa kisiasa wa serikali ulikuwa mfano mzuri – kutoka kipindi cha pili cha utawala wa Rais Mkapa kuelekea kipindi cha utawala wa Rais Kikwete, Waziri Mkuu Lowasa na Waziri Sitta (Magreth) walionyesha mafanikio.

  Idadi ya uandikishaji imeongezeka katika shule za msingi hivyo kulazimisha kupanua elimu ya sekondari. Uhitaji wa mikakati sahihi ya kisera utaonekana ili kutoa mwongozo katika vipaumbele, matumizi ya rasilimali na utekelezaji wake. Ushauri ukitolewa katika maeneo muhimu matano ambayo yalionyesha changamoto kubwa, ikiwepo serikali ionyeshe malengo mahsusi katika elimu ya sekondari; kulenga katika matokeo na si idadi; walimu na miundombinu sahihi kwa walimu; kipimio cha mafanikio – mitihani inalenga kupima nini; na, lugha ya kufundishia – kiingereza kutumika katika elimu ya msingi, na lugha zingine za kimataifa kufundishwa sekondari, (Suleman Sumra & Rakesh Rajan, (2006), Working Paper No. 4, Secondary Education Tanzania: Key Policy Challenges, HakiElimu).

  Tunajifunza kwamba maisha ya mtu yana hatua ambazo zimefuatana na zinahusisha mawazo, tabia, mihemko na mahusiano. Kila hatua hudumu kati ya miaka 20 – 25; ambapo kuna mambo ambayo ni lazima mtu uyamudu katika hatua husika. Chochote ambacho mtu atashindwa kukimudu katika hatua ya umri husika, baadaye huwa ni changamoto kubwa sana ya kimaisha kwa mtu, katika umri na hatua ambayo si wakati wake (Herbert Harris , (2004), The 12 Universal Laws of Success).

  Tunapoiangalia miaka 20 -25, ya kila hatua ya mwanadamu, mambo yafuatayo ni lazima yafikiwe. Moja, ni elimu (education),tangu miaka 0 – 25. Mbili, ni hisia na uzoefu (feeling & experience), miaka26 – 50. Tatu, nguvu (power) kufanya mambo kutokea, miaka 40-60 au 50–75. Nne, umilele (immortality) – kutathimini mafanikio na maanguko, miaka 60 – 75, au 75 – 100 ukifanikiwa kufika.
  Ni katika umri wa miaka 0 – 25 wa maisha ya mwanadamu ambapo mtu anatakiwa kuwa na uhakika kuhusu elimu yake (awali, msingi, sekondari, kati na chuo kikuu). Ndani ya hatua hii mwanadamu anajifunza kanuni na misingi ya maisha. Unajenga na kupokea mifumo ya maisha. Unapata maelekezo kwa kusoma, kufundishwa, kuandika, kuhesabu, kuwaza ki-maantiki, na kufanya maamuzi. Katika hatua ya elimu unajenga msingi wa mawazo, tabia, mihemko na mahusiano – ambapo maisha yako yote mengine yataegemea. Katika hatua ya elimu mtu anajenga tabia ya msingi – ya kujitambua, mtazamo wake kuhusu wengine, na dunia kwa ujumla. Katika hatua hii mtu anajenga kuajiamini au hofu; imani au mashaka; ujinga au uelewa; mtazamo chanya au hasi; utegemezi au kujitegemea.

  Utegemezi wa elimu toka kwa watu wengine ni changamoto ya hatua ya elimu. Mhusika anatambulika kama mtoto – mwanafunzi hivyo hana mchango mkubwa katika hatua hii. Hivyo, mawazo, tabia, mihemko, uzoefu, na mitazamo chanya na hasi ya wazazi wake, walimu wake, viongozi wake, au watu wa kuigwa katika jamii humjenga mhusika katika mitazamo chanya au hasi ya umri wake wa utoto na utu-uzima-mchanga.

  Katika hatua hii kama msingi haukujengwa sawasawa, ni lazima, katika umri fulani wa maisha ya mhusika, mipasuko itaonekana. Mtu hatakuwa na amani, afya bora, furaha, wala hatajikubali. Hataipenda serikali. Anaweza kuwa katili kwa kila kitu. Lakini endapo msingi huu utajengwa kwa dhati, upendo, uaminifu, imani, nidhamu, ujasiri, huruma na mitazamo yote chanya; mtu katika hatua hii atakuwa ameandaliwa vizuri kushuhudia hatua zingine tatu za maisha yake kwa mafanikio makubwa. Hali ikoje? Tunajenga watu 141 kwa daraja sifuri dhidi ya wanafunzi 252 katika Hatua ya Elimu, je tunalenga kweli Dira ya Tanzania 2025 na malengo ya Sera ya Elimu na Mafunzo?

  Mosi, tunaporejea kuitafakari Dira ya Tanzania 2025 kwamba elimu ni wakala, nyenzo na mkakati muhimu wa kubadili mitazamo na fikra za watu, ili kujenga taifa la wasomi, waliopandikizwa maarifa kwa ufanisi na umahiri wenye kulenga mahitaji ya ushindani kutatua changamoto zinazolikabili taifa. Pili, tunaporejea kuangalia malengo ya Sera ya Elimu na Mafunzo mathalani kujenga taifa la watu wenye kupenda kujifunza/kujieleimsha na kutumia stadi na maarifa waliyopata kuboresha hali ya maisha; kuwajengea kujiamini, na akili yenye kujiuliza maswali na kutafuta majibu sahihi, na mtazamo wa kulenga maendeleo; kuwapa elimu inayoendana na mabadiliko ya dunia ili kuweza kukabili changamoto mbalimbali. Je ni kwa hali hii ya wanafunzi 141 kupata daraja sifuri katika shule moja?

  Napendekeza Idara Maalumu za Ushauri Shuleni ili zifanye kazi ya kushauri na kumsaidia mwanafunzi kwa kina katika Hatua ya Elimu, tofauti na sasa mwalimu ndiyo anakuwa kama mshauri. Napendekeza kiwepo kitengo maalum katika kila shule, kitengo ambacho kitakuwa na wafanyakazi wenye elimu nzuri ya ushauri, stadi za kazi, saikolojia na elimu ya ujasiriamali, wakifanya kazi ya kumjenga mwanafunzi kufikia maono yake zaidi ya mitihani ya darasani. Kwamba, katika ratiba ya masomo ya shule husika, iwe ni mkakati wa serikali kwamba katika siku maalumu, darasa fulani litaingia katika chumba maalumu, wanafunzi wa darasa husika na walimu mahiri wa maeneo tajwa hapo juu wanaingia na kufanya majadiliano ya kawaida, urafiki na mazingira au mifano halisi ya mada ambayo itawekwa na kujadiliwa kwa pamoja ili kuibua ubunifu, na kujua mitazamo chanya, vipawa na mienendo ya wanafunzi.

  Idara Maalumu za Ushauri Shuleni zifanye kazi ya kujenga nidhamu na maadili ya wanafunzi kwa ufanisi, kwa kulenga kuthibiti tabia za matumizi ya simu yasiyo na mipaka; uvaaji wa nguo wenye kichefuchefu; kuwajengea wanafunzi uelekeo sahihi wa vipawa na ubunifu wao – hata kama ni katika uimbaji, iwe ni uimbaji wenye faida kwa maisha ya kijana husika hata katika hatua zingine za maisha, tofauti na sasa kila kijana wa sekondari ‘analazimisha kuchana mistari ya bongo fleva', ambayo baada ya umri fulani, muhusika hopotea katika ramani ya muziki.

  Huu ni uchokozi. Mjadala unaendelea. Mawazo yako ni muhimu sana kuhusu Idara Maalumu za Ushauri Shuleni!


  Perecy Paulo Ugula,
  Rafiki wa Elimu,
  Simu: 0766 082388
   
Loading...