TSD na maswaibu yake

TSD na maswaibu yake

chakachuaz

Member
Joined
Jun 20, 2012
Posts
13
Reaction score
0
MASWAHIBU KATIKA IDARA YA UTUMISHI WA WALIMU (TSD)
Idara mojawapo inayokumbana na maswahibu mazito kutokana na hali hiyo ni idara ya utumishi wa walimu ambayo inazo ofisi hadi ngazi ya wilaya. Idara hii hasa Ofisi za TSD (W) na TSD (M) zinaongoza kwa uduni, yaani ni Ofisi ambazo hazina mwonekano wa kiofisi unaoendana na mazingira ya sasa. Majengo wanayotumia baadhi ya ofisi hizi yamechoka sana, yamejaa vinyesi vya popo na mende ambao wakati mwingine hufanya kazi ya mapokezi, vumbi na halufu za ajabu ajabu ambazo kwa upande wangu niseme kwamba husaidia kuwapa Watumishi wa Ofisi hizo ruhusa za rejareja za ugonjwa wa kikohozi, mafua na macho. Mazingira ya nje yanayozunguka Ofisi hizo yanaongoza kwa uchafu, nyasi ni ndefu, magugu ndio yamekuwa wageni wanaobisha hodi milangoni pa Ofisi hizi.
Hizi ndizo OFISI ZA OFISI YA RAIS, TUME YA UTUMISHI WA UMMA ambazo mwonekano wake hautoi taswira ya Jina lenyewe. Na sijui kama Mheshimiwa Rais katika ziara zake mikoani alishawahi kutembelea Ofisi zake hizi na kuziona jinsi zinavyofanana. Hakika akifanya zoezi hilo la kuzitembelea Ofisi zake hizo, akakutana na mapokezi ya mende na Popo na kisha akabarikiwa kunusa manukato mazuri yanayotokana na mende na popo hao, akapiga chafya ambayo kwa hakika hajawahi kuipiga maishani mwake na inawezekana asiipige tena katika maisha yake, na kama vile haitoshi kikohozi ,mafua na hata maradhi ya macho vikapambana na Amiri jeshi mkuu huyo na kufanikiwa kumshinda kabla mheshimiwa pilitoni, Cofta na wengineo hawajaarifiwa ili wamsaidie, nina hakika hatua za haraka zitachukuliwa ili kuzinusru Ofisi hizi na watu wake.
Maswaibu yote haya yanatokana na kutozithamini ofisi hizi hasa katika swala zima la bajeti. Ni jambo la kushangaza kuona kwamba Ofisi za TSD (W) na TSD (M) zinatengewa shillingi elfu ishirini (20,000/=) kama fedha ya usafi kwa miezi mitatu. Hebu tutafakari kwa pamoja jambo hili, ni Ofisi gani inaweza kutumia Tsh 20,000/= kwa miezi mitatu kama bajeti ya usafi alihali ofisi hiyo haina mfanya usafi aliyeajiriwa, ofisi hiyo ina mazingira yanayoizunguka and then 20,000/= per 3months. Are we realistic? Are we thinking critically? Sabuni yenyewe mche unauzwa Tsh 2000/= kwa mwezi inahitajika miche 4, sabuni ya unga kwa matumizi ya mwezi mmoja ni Tsh 18,000/=, Disinfectant kwa mwezi ni Tsh 15,000/=, Toilet paper ni Tsh 8,000/= kwa mwezi. Huo ni mchanganuo kidogo tu kwa mahitaji machache ya usafi wa mazingira ya ndani ya ofisi na Latrines, na gharama zake kwa hivyo vichache tayari ni zaidi ya Tsh 20,000/= kwa mwezi. Je hao wanaojiita wataalamu wa bajeti ya TUME na Idara zake hawana hata soni machoni pao kupanga bajeti ya Twenty thousand for 3months! Shame on you. Kama huo ni usafi wa mazingira ya ndani, je mazingira ya nje hayahitaji kufanyiwa usafi? Kwa kuwa Ofisi nyingi za TSD hazina wafanya usafi wa kuajiriwa hulazimika kutafuta vibarua wa kusaidia kazi hiyo pale wanapomudu kufanya hivyo na kibarua huyo hulipwa ujira wa Tsh 5000/= kwa siku. Sasa tujiulize 20,000/= itamlipa kibarua huyo kwa siku ngapi? Niliwahi kumuuliza AFISA mmoja wa TUME makao makuu swali hili,kwa nini ofisi zenu ngazi ya wilaya na mkoa mnazitengea bajeti ndogo ya usafi? Bila aibu akajibu, unajua ofisi hizi nyingi zimo ndani ya maeneo ya Wakuu wa Mikoa ama Wakurugenzi kwa hiyo hao ndio watawajibika na usafi wa mazingira yanayowazunguka. Sasa nikajiuliza, hiki kiburi cha kumtegemea mume mwingine ahudumie familia yako kinatoka wapi? Kwa sababu ni jambo la kushangaza, utakuta ofisi ya Katibu tawala MKOA ama ya MKURUGENZI imebeba mzigo wa kulipia jengo,umeme,maji na wavuti(Internent) lakini mtu huyo hana hata soni anataka na usafi wa kuzunguka Ofisi yake nao afanyiwe na Katibu tawala Mkoa au Mkurugenzi. Ama ndo utekelezaji wa dhana ya ushirikiano na wadau wengine kwa kuwabebesha mizigo ya kuhudumia ofisi zenu. Acheni kulazimisha ndoa za mkeka alhali muoaji hataki.
Kama vile hiyo haitoshi, kizunguzungu kingine ni hiki, Ofisi inatengewa Tsh 300,000/= au 500,000/= kwa ajili ya kujiendesha kwa kipindi cha miezi mitatu (yaani hiyo ndiyo inakuwa bajeti ya Robo moja ya mwaka), ambapo fedha hizo nazo hazitumwi kwa muda muafaka na pengine hazitumwi kabisa hata kwa vipindi vitatu vya robo mwaka. Je unatarajia kuwepo na mafanikio katika utumishi wa walimu? Huo ni uongo kabisaaa mbele za mwenyezi mungu. Kwanza huwa nashangaa kuona jinsi tume inavyojifagilia katika ripoti zake ambazo zimejaa udanganyifu na upotoshaji badala ya ukweli. Nawaomba muwe mnasema ukweli kwamba mmetekeleza kwa asilimia tatu (3%) na kufeli kwa asilimia97% kuliko kumfariji Mkulu wa Magogoni. Nadhani hii itasaidia hata Mkulu kushtuka ili kama kuna wanaoionea TUME washughulikiwe ama suluhu ipatikane.

SAMANI ZA OFISI NA VYUMBA VYA OFISI
Kasheshe nyingine iko kwenye samani za Ofisi hizi. Ofisi nyingi za TSD wilayani na mikoani zina fenicha ambazo kwa hakika nashindwa kuelewa kwamba zilitengenezwa wapi, achilia mbali kuwa ni OLD TRADITION WOODEN FURNITURE, kwa sababu utakuta kiti kimoja kina uzito wa kilo 10 hadi 12, meza ndo usiseme kabisa kwa maana hizi hata kuhamishika hazihamishiki kabisa labda pawepo na msaada wa mabaunsa kumi hivi. Sasa huwa najiuliza kwamba , TUME haioni umuhimu wa kuajili mabaunsa wa kusaidia ofisi hizi. Pamoja na uwepo wa fenicha hizo nzito, bado nazo hazitoshelezi kwani utakuta Ofisi ina kiti kimoja au viti viwili na meza moja au mbili alhali watumishi ni wanne. Vifaa vingine hivyo ndivyo aibu kabisa, kwani nyaraka nyingi za serikali zinazagaa zagaa chini ya sakafu zikikojolewa na popo. Hakuna Kompyuta, cabinets, kabati wala files za kuhifadhia nyaraka hizo. Sasa nashindwa kuelewa kama TUME inashughulika na rasilimali watu na kwamba rasilimali watu ni records na nyaraka ambazo zinahitaji kuhifadhiwa kwa uangalifu mkubwa. Kwa sababu hata Gereji zina utaratibu wa kuhifadhi vipuri vya magari ili visipate kutu. Sasa iweje ofisi ya umma ishindwe kuwa na vifaa vya kuhifadhia nyaraka za serikali. Je hili nalo linahitaji kumrudisha mkoloni aje atuchape mijeredi ili tuwajibike?
WATUMISHI KATIKA OFISI ZA TSD MIKOANI NA WILAYANI
Ofisi nyingi za TSD mkoa na wilaya zina watumishi wachache sana. Yaani ni jambo la kushangaza Ofisi ya TSD yenye shughuli nyingi za walimu ati ina Mtumishi mmoja tu. Sasa unajiuliza anamudu vipi kazi hizi. Sasa hili nalo tumrudishe mkoloni awatwange viboko ndo muamke. Duh! Mnatia aibu. Jichangamsheni wenyewe na miaka 50 ya uhuru. Hapa sitaki kuwaambia watu wa kuajiriwa kwani najua mnajua watu wanaotakiwa kuajiriwa kwa sifa na aina ya watumishi na idadi kwa kila ofisi ya TSD mkoa na wilaya. Licha ya uchache wao bado utakuta nao hawajalipwa maslahi yao mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya mshahara kwa miaka hata minne. Je mnadhani mtu huyu anakuwa na amani awapo kazini? Jibu hapa ni hapana, kwa maana mtu huyu atakuwa anawaza udhalimu aliofanyiwa na anaofanyiwa na serikali yake.
VYOMBO VYA USAFIRI
Katika hili sichelei kusema kwamba ni uzembe wa hali ya juu kama siyo dharau, kwani Ofisi nyingi za serikali zimepewa umuhimu na unyeti wa kupewa magari na pikipiki kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Je chombo hiki kinachoitwa TUME YA UTUMISHI WA UMMA si muhimu na nyeti kwa serikali kiasi cha kunyanyapaliwa? Utasikia walimu wakilalama TSD haitufikishii habari zinazohusu utumishi wetu ati mpaka tuwatembelee ofisini kwao kana kwamba Ofisi zao ni CONSULTANT OFFICE. Huyu TSD Officer atawezaje kuwafikishia ujumbe wateja wake alhali hana Usafiri na bajeti yenyewe ni kiduchu. Niliwahi kumuuliza Afisa mmoja wa TUME MAKAO MAKUU, kwa nini Ofisi zenu za TSD Mkoa na Wilaya licha ya unyeti wa shughuli zake hazina vyombo vya usafiri? Jibu alilonipa ni hili, ofisi hizi hazina vyanzo vya mapato ya kuweza kuendesha magari na pikipiki ikiwa watapewa. Kimsingi jibu lenyewe halina mashiko kwani ofisi zote za umma yakiwemo magari huendeshwa na kodi za wananchi. Lakini tujiulize mbunge anapewa gari na anapewa mafuta kila siku, je mbunge huyu ana chanzo cha mapato? Si anapewa na serikali. Sasa iweje Ofisi yenye shughuli kemkem na ambayo kimsingi gharama za kuendesha gari ikiwa itapewa ni ndogo ukilinganisha na za mbuge isipewe gari kwa kuwa haina chanzo cha mapato. Huu kwangu ni unyanyasasaji. Matokeo yake ni kuzorota kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo mashauri ya nidhamu hususani yanayohitaji uchunguzi ambayo mengine yana umri zaidi ya mwaka mmoja na yanaigharimu serikali hiyohiyo yenye kigugumizi cha kutoa vyombo vya usafri kwa Ofisi za TSD mikoani na wilayani. Amkeni msisubiri kuamshwa. Ama mnasubiri kuamka wakati wa giza kama Karunguyeye.
MAANDALIZI YA TANGE YA WALIMU
Kituko kingine kiko hapa, maandalizi ya Tange ya Walimu huchukua Takribani miezi mitatu hadi minne. Lakini shughuli hii pamoja na unyeti wake haitengewi pesa kwa ajili ya kuifanikisha, na kama inatengewa basi huchakachuliwa na Wakulu wa Bajeti. Matokeo yake ni kwamba tange zimekuwa haziandaliwi ipasavyo ama haziandaliwi kabisa. Kwa ufupi tu ni kwamba zoezi hili huanzia ngazi ya wilaya na kisha kukamilishwa katika ngazi ya mkoa. Sasa inashangaza kukuta wakulu wa TUME wamekazana kabisa bila aibu, tutumie Tange ya walimu haraka. Aaaah! bwana oneni aibu. Udhaifu umeanzia kileleni wala siyo kwenye mizizi. Utaombaje kuwaishiwa tange alhali unayemwomba hiyo tange hata compyuta hana. Tena eti iwe kwenye soft copy. Aaaaah! acheni masihala bwana. Jaribuni kutambua shughuli nyeti zinazofanywa na Ofisi hizi na kuzipa kipaumbele katika bajeti hasa huko mikoani na wilayani ambako ndiko utekelezaji unaanzia.
FEDHA ZA VIKAO VYA KAMATI ZA MIKOA NA WILAYA
Fedha za vikao vya kamati za Mikoa na Wilaya zimekua zikitumwa kwa kusuasua ama hata kutotumwa kabisa kwa vipindi hata vitatu. Hali hii imesababisha Ofisi za TSD kwa ujumla wake kushindwa kutekeleza majukumu yake yanayotokana na vikao hivyo na hivyo kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa Walimu na wadau wengine kikiwemo Chama Cha Walimu (CWT). Vikao hivi ni muhimu pamoja na mambo mengine katika kuwapandisha walimu madaraja/cheo, kujadili mashauri ya nidhamu, mirathi ya walimu waliofariki n.k lakini bado havipewi umuhimu kabisa. Sasa sisi tulio TSD mikoani na wilayani tunapouliza juu ya swala hili, Wakuu wa TUME utasikia wanakwambia unajua TUME ilikuwa inashughulikia maswala nyeti kwanza, hivyo vumilieni tu. Sasa hapa najiuliza mwalimu ambaye anasubiri shauri lake lisikilizwe ama apandishwe daraja/cheo anavumiliaje hapa. Saana ni kumwongezea hasira. Na kwa mantiki hiyo kelele za walimu hazitaisha kamwe. Kwa maana vyombo vinavyoshughulilkia maswala ya walimu havitendewi haki kabisaa na hivyo kutowatendea haki walimu.
Fedha za uchunguzi wa mashauri ya nidhamu: hizo ndizo hazitumwi kabisaa na uthibitisho wake ni rahisi tu, angalia mashauri ya nidhamu yenye muda mrefu ambayo hayajafanyiwa uchunguzi, utakuta Mkoa mmoja una mashauri 30 hadi 40 yote haya yana umri kati ya mwaka mmoja na zaidi. Hii inaongeza chuki baina ya TSD na walimu, kwani walimu wengi wasioelewa hili hudhani kwamba TSD ina lengo la kuwahujumu haki zao. Lakini Kwa upande mwingine inaiongezea serikali mzigo wa madeni pindi mwalimu anaposhinda kesi hiyo ya muda mrefu. Sasa nawaombeni muwe makini kushughulikia maswala ya Walimu ambao ni kundi kubwa la wafanyakazi katika utumishi wa umma Tanzania.

USHAURI WA BURE
Hata kama mtautaka ama mtaukataa, mimi napenda kushauri tu kwamba, kwanza TUME YA UTUMISHI WA UMMA itolewe Ofisi ya Rais na ipelekwe TAMISEMI ambako nadhani inastahili. Kama hilo halitawezekana, basi angalau idara ya TSD ipelekwe TAMISEMI.
Pili, badala ya TUME Makao makuu kuendelea kuhodhi mamlaka makubwa ikiwemo bajeti ifanyike COMPLETE DECENTRALIZATION itakayo wezesha Ofisi zilizo mikoani na wilayani kutekeleza majukumu yake inavyopaswa.
Tatu, kila idara iliyo chini ya TUME YA UTUMISHI WA UMMA iwe na VOTE na SUBVOTE yake itakayowezesha idara husika kupata mgawo wake wa fedha moja kwa moja kutoka hazina na hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.
Nne, mishahara ya watumishi wa TUME YA UTUMISHI WA UMMA iangaliwe upya ili iweze kuendana na ile ya TUME zingine za serikali. Mfano, Tume ya mipango.
Tano, madai ya watumishi wa TUME ikiwemo malimbikizo ya mishahara yalipwe haraka kama hatua ya kuongeza morali wa kazi.
Sita, mabango makuubwa mliyoyaweka kwenye Ofisi za TSD yakiwa na maandishi makubwa ya ``OFISI YA RAIS” mkayatoe tu maana hayatoi taswira ya hadhi ya Ofisi zenyewe.
 
Ni kweli mkuu,idara hizi ni kero kubwa!baadhi ya wilaya hazina hata huyo tsd officer,anawekwa just mtu ambaye kiuhalisia mambo ya tsd hana uelewa nayo kabisaaa,au tsd mmoja anatoa huduma ya wilaya zaidi ya moja!
Hii idara ni nyeti kwani inadeal na uhai na mstakabarh wa maisha ya mwalimu,na ndo maana sasa kuna kelele nyingi za vidato,madaraja na marekebisho ya mishahara lukuki!Elimu itashuka kila leo,kero ni nyingi sana.
Hebu wahusika chukueni hatua sasa!
 
Back
Top Bottom