Hii ilitoka kwenye Nipashe la 27/08/08
TRL wajipanga kugoma nchi nzima kudai mishahara mipya
2008-02-27 08:48:31
Na Karama Kenyunko
Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), wanatarajia kugoma nchi nzima ili kumshinikiza mwajiri wao kuwalipa nyongeza ya mshahara mpya uliotangazwa na serikali.
Mgomo huo umepangwa kuitishwa baada ya utaratibu wa wafanyakazi wa mikoani kupiga kura za siri kukubali kugoma au kukataa.
Kwa upande wa wafanyakazi wa TRL makao makuu jijini Dar es Salaam, jana waliunga mkono mgomo huo baada ya wafanyakazi 483 kupiga kura.
Matokeo ya kura hizo ni kwamba wafanyakazi 481 walikubali kufanyika kwa mgomo huo wakati kura moja ilikataa na nyingine moja iliharibika.
Wafanyakazi hao wanataka nyongeza ya kima cha chini cha mshahara cha angalau Sh. 200,000 kwa mwezi tofauti na wanacholipwa hivi sasa cha wastani wa Sh.100,000
Kwa mujibu wa sheria za kazi kuhusu migomo, wafanyakazi watapiga kura na ikiwa theluthi mbili ya wafanyakazi wataafiki kufanyika kwa mgomo basi mgomo huo utakuwa halali.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Nchini (TRAWU), Bw. Sylvester Rwegasira alisemahatua ya kwanza ilikuwa kumwomba mwajiri nyongeza kama ilivyotangazwa na serikali.
Alisema baada ya mazungumzo na mwajiri hakuafiki kuongeza kiwango hicho na badala yake aliongeza asilimia 15 tu ya mshahara.
Alisema baada ya kushindwa kuelewana na mwajiri wao walikwenda katika Baraza la Usuluhishi kama Sheria ya Kazi inavyoelekeza.
Alisema Baraza la Usuluhishi baada ya kukutanishwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi na mwajiri imeshindikana kufikia makubaliano.
``Baada ya baraza la usuluhishi kushindwa kupata suluhu alitupa hati inayoonyesha kuwa ameshindwa kutusuluhisha hivyo sheria inatutaka baada ya hatua hiyo kwenda mahakamani ama kugoma, sisi tumechagua kugoma,`` alisema.
Alisema baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika katika mikoa yote ambako kuna matawi ya TRL na wafanyakazi wote wakaafiki kugoma watafanya hivyo.
Alisema kabla ya kugoma, wafanyakazi hao watampa mwajiri muda wa saa 48 ili kama anaweza kutekeleza madai yao vinginevyo watatangaza mgomo nchi nzima.
Alisema wakati hayo yakiendelea, mwajiri aliiandikia serikali kuomba asamehewe kulipa mishahara hiyo lakini Serikali ilikataa.
``Ndugu wafanyakazi wenzangu tunatakiwa kuwa na mshikamano katika kipindi hiki, ukitaka kufika peponi ni lazima kwanza ufe,`` alisema.
Aliongeza`` ni lazima tushikamane ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana.``
Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza kabla ya zoezi hilo, walisema inasikitisha kuona kuwa wakati kampuni hiyo imeongeza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria lakini inashindwa kulipa mishahara mipya kama ilivyoelekezwa na serikali.
Alisema inasikitisha kuona wafanyakazi wenye asili ya kiasia wanalipwa mishahara minono kwa kazi zilezile zinazofanywa na wafanyakazi wa kawaida.
``Wakati dereva mwenye asili ya kiasia analipwa Sh. milioni tatu kwa mwezi, uongozi umeshindwa kutulipa sh. laki mbili kwa mwezi,`` alisema.
Mgomo huo ukiachwa uendelee utaathiri zaidi sekta ya usafirishaji hasa kwa wananchi wa mikoa ya Kaskazini kwa kuwa ndiyo usafiri pekee wa uhakika unaotegemewa zaidi na wananchi hao.
Aidha, mgomo huo utaziathiri zaidi nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda ambazo zinategemea zaidi njia hiyo kwa kusafirisha mizigo.
Uganda ambayo ilikuwa ikisafirisha mizigo yake kupitia bandari ya Mombasa nchini Kenya ilisitisha kutokana na vurugu inayoendelea nchini humo na hivi karibuni imeanza kutumia bandari ya Dar es Salaam jambo linaloweza kuwa pigo ikiwa mgomo huo utaachwa ufanyike.
Wakati huo huo TRL, imeingiza injini tisa za kukodi zilizotengenezwa miaka 10 iliyopita kutoka nchini India ili kuboresha usafiri wa reli nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bw. Jayaram Rarasimhaswami, alisema injini hizo zitasaidia kuongeza huduma na kukuza usafiri wa treni.
Alisema kila mwaka, shirika litakuwa linailipa kampuni ya Rites ya nchini India dola milioni sita za Kimarekani pamoja na matengenezo iwapo zitaharibika na ununuzi wa spea.
Aidha, Bw. Rarasimhaswami, alisema kuwa, injini nyingine tano ambazo zilitakiwa kuwasili jana, zimekwama katika bandari ya Shadya, Falme za Kiarabu kutokana na kukosa usafiri.
Alisema injini hizo zitaongeza huduma ya usafiri kutoka asimilia 30 hadi kufikia ongezeko la tani 15,000 za mizigo.
Alisema vichwa vingine 10 vyenye uwezo wa kubeba mabehewa mengi, vinatarajiwa kuingia nchini baada ya miaka miwili ili kutoa nafasi ya kutangaza zabuni kwa kampuni zitakazotengeza vichwa vinavyoendana na reli za hapa nchini.
Naye Mjumbe wa Bodi wa shirika hilo ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini, Bw. Silaju Kaboyonga, alisema shirika hilo lina mpango kazi wa ongezeko la huduma za usafiri ili ziwe nzuri.
Alisema shirika limeagiza mabehewa 23 ya kukodi ambayo yanatarajiwa kufika Machi, mwaka huu ambayo yatasaidia kuongeza safari nyingine kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kuzifanya kuwa mbili.
Bw. Kaboyonga alisema kuwa, TRL ilipoingia madarakani ilikuta vitendea kazi kutoka TRC vikiwa vibovu.
Alisema miaka ya nyuma wakati wa TRC, kampuni ilikuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo ya tani milioni 1.4 na TRL ilitaka kuongeza lakini badala yake ilipungua na kufikia tani 700,000.
Alisema TRL imepanga kufanyia marekebisho injini zote za zamani ili ziweze kubeba mabehewa na mizigo mingi kwa wakati mmoja.
Aidha, Bw. Kaboyonga alisema dola milioni 77 za Kimarekani zinatarajiwa kutolewa na mashirika mawili kwa ajili ya kutengeneza reli na kununua spea, mabehewa pamoja na vipuri.
SOURCE: Nipashe