TRA yakamata shehena kubwa ya bidhaa za magendo

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukamata bidhaa za magendo kwenye maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na mipakani.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi (TRA) Bw. Richard Kayombo wakati akifanya mahojiano na Mwandishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kuhusu juhudi za operesheni ya kutokomeza bidhaa za magendo nchini.

Bw. Kayombo ameeleza kuwa, mkoani Lindi TRA imefanikiwa kukamata mashua katika bandari ya Lindi ambayo ilisheheni bidhaa za magendo zenye thamani ya shilingi 159,361,046.

Ameongeza kuwa katika operesheni hiyo, TRA imefanikiwa kukusanya kodi ya jumla ya shilingi 10,500,678 kutoka katika bidhaa zilizokuwa katika nyaraka za forodha (manifest) ambapo pia inategemea kukusanya kodi ya shilingi 19,529,500 kutoka katika bidhaa ambazo zilikuwa katika nyaraka za forodha lakini thamani yake ilikuwa chini ya bei halisi.

Akitaja bidhaa hizo za magendo zilizokamatwa katika mashua hiyo ni mifuko 3,725 ya sukari yenye thamani ya shilingi 127,070,562, betri katoni 50, mchele mifuko 3,087, mafuta ya kula madumu 80, majokofu manne ya mtumba, baiskeli 4 za mitumba pamoja na katoni 20 za hamira.

“Mashua hiyo ilikamatwa katika bandari ya Lindi tarehe1 Februari, 2016 baada ya wasamaria wema kutoa taarifa ya kuwepo bidhaa za magendo ndani ya mashua hiyo ambapo upakuaji wa shehena hiyo ulianza mara moja.’’Alisema Kayombo.

Ameongeza kuwa, Jijini Dar es Salaam, TRA kwa kushirikiana na kikosi cha doria cha Jeshi la Wanamaji wameweza kukamata Jahazi lenye jina la ‘Takbiri’ lenye usajili wa namba Z-875 likiwa limesheheni lita 19,700 za dizeli ambapo thamani yake bado haijapatikana kwakuwa imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya Uchunguzi zaidi.

Aidha, majahazi mengine matatu yamekamatwa katika eneo la Kigombe mkoani Tanga ambayo yalikuwa na bidhaa za magendo yenye thamani ya shilingi 99, 682, 273, 48 ambapo ndani kulikuwa na magunia ya sukari, mchele, mafuta ya kula, matairi ya magari, nyavu za kuzuia mbu, jokofu, jiko la umeme, rangi za kupuliza, betri na biskuti.

Majahazi hayo yalitaifishwa baada ya wahusika kujitosa ndani ya maji na kutoroka.

TRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inafanya doria saa 24 kila siku katika maeneo yote yaliyoshamiri upitishaji wa bidhaa za magendo pia imeunda Kanda Maalum katika maeneo ya Mbweni, Msasani, Kunduchi pamoja na Kigamboni.
 
Back
Top Bottom