Toka kwa muuza mihogo mpaka SGR

Toka kwa muuza mihogo mpaka SGR

DUMIZI

Member
Joined
Apr 23, 2019
Posts
16
Reaction score
13
Naamka asubuhi na mapema nikiwa na njaa. Nachemsha chai nakumbuka kitafunwa sina. Natoka barabarani namwona mama muuza mihogo.

"Niuzie ya mia tano!"
"Subiri kidogo, ndiyo kwanza nimeiweka motoni."

Naamua kuketi juu ya jiwe kuisubiria.
Moshi mseto wa vifuu na kuni za kuokoteza, unasambaa hewani na kuleta kadhia nyingine.
Mteja wa kwanza mie, acha nivumilie.

"Bado kidogo itakuwa tayari..." nasema na roho yangu, nikichezea simu yangu.

Baadae nasikia sauti ya mtu chakaramu, ni mswahili mwenye maneno mengi mdomoni, "We mama Aisha hebu nipe mihogo ya elfu mbili. Fanya haraka basi njaa itaniua..."

Mama Aisha anapokea hela yake na kumfungia mihogo. Kufumba na kufumbua mihogo imeisha. Nauliza, "Mimi vipi?"

"Oh... Nisamehe baba'angu nafsi ilighafirika. Subiri kidogo nimeinjika mingine... "

" *** you! " Inanitoka kwa hasira.

Nakinga mkono arudishe hela yangu.
Nimesubiri zaidi ya dakika kumi nikila moshi wako. Anakuja mwingine unamuuzia kabla yangu? Ni dharau ama uchawi?

Naondoka nikisonya.

Kama imekuuma basi ndiyo hali halisi, kote imesambaa hulka ya ubinafsi.

Hata dukani kwa Mangi halikadhalika. Unasubiri huduma wengine wanakuja, wanapitisha mikono juu ya bega zako.

"Mangi naomba sigara!"
"Mangi nipe unga robo!"

Huwa najiuliza kwani hamnioni? Au nimekuwa mweusi mfano wa kivuli? Au ninyi mna haraka zaidi yangu?

Na hii kasumba wala si ya mmoja.
Nenda Stendi ya Mbezi Magufuli utaikuta. Nimeishudia pia Stendi ya Msamvu.
Nikadhani SGR itasaidia kuleta ustaarabu...

Thubutu!

Ama hakika tabia ni ngozi. Watanzania na ubinafsi ni chanda na Pete. Kwanini hatuna ustaarabu wa kufuata foleni?

Kuprint tiketi abiria wanajazana, ukipanga foleni wanakuona wakuja. Utabaki umesimama peke yako kama sanamu.

Hata zoezi la ku-scan tiketi, hali ni moja. Watu wazima wanalundikana kama nyumbu. Mtoa huduma hajui aanze na yupi. Mikono yenye tiketi inamuandama mpaka puani...

Hata barabarani ni vivyo hivyo. Hakuna anayetaka kufuata foleni. Kila dereva anaamini kutanua ndiyo ujanja. Sasa tukichepuka wote nani atabaki njia kuu?

Ustaarabu wa "Pita nami nipite" ni neno la kigiriki kwenu, huh?

Ni nani katuloga tusiheshimu foleni? Inagharimu bei gani kusimama nyuma ya uliyemkuta na isitoshe safari yenu ni moja? Au kumtangulia aliyekutangulia ndiyo ujanja?

Jambo moja tukubali, hii kasumba ni alama ya ubinafsi; kudhani unastahili kuliko wengine.

Ni kweli, ubinafsi ni hulka ya asili kwa kila binadamu. Lakini hugeuka kuwa janga unapokosa kiasi; unapopuuza utu wa wengine, unapohalalisha kuvunja foleni, kuhodhi haki au kula na kuvimbiwa kuliko jirani....ndipo ubinafsi unapogeuka sumu na laana.

Tuikumbuke roho ya Mwalimu Nyerere leo, aliyehubiri habari za utu na usawa kwa vitendo: na si kwa maneno matamu yasiyoakisi dhamiri.

Taifa linalosongwa na ubinafsi, haliwezi kuendelea, kwani linajimaliza lenyewe polepole, kama mihogo inayochomwa kwa moto wa vifuu. Hapa inaiva, pale mibichi.

Waffaqaka-llāh
 
Hamia Burundi mkuu tuachie bongo yetu, tunaimudu na kuijulia sisi wenyewe.
 
Back
Top Bottom