Toba hurejesha amani na imani iliyopotea

foroy

Senior Member
May 2, 2018
186
288
Binadamu tumeumbwa kukosea. Na tunafanya makosa mengi mara kwa mara. Huo ndiyo ubinadamu wetu, ndiyo asili yetu, na ndivyo tulivyoumbwa.

Kuna yale tunayomkosea Mungu kwa imani na yale tunayokoseana sisi kwa sisi katika mchakato wa kuendelea kuishi.

Katika mazingira yote mawili; kiimani au kibinadamu, makosa huvunja moyo na kupoteza urafiki ama ukaribu wetu wa asili kati yetu binadamu au kati yetu na Mungu.

Bahati nzuri kuna kitu kinaitwa toba.

Tunapomkosea Mwenyezi Mungu, ni toba ndiyo yenye nguvu ya kurudisha ukaribu na upatanisho wetu na Muumba. Ndiyo maana dini zote zinafundisha umuhimu wa kufanya toba mara nyingi iwezekanavyo, kwasababu tunakosea mara nyingi pia.

Lakini pia tunafundishwa kufanya toba kila tunapokoseana sisi kwa sisi, katika hili au lile. Kwa vile toba hurejesha amani na imani iliyopotea.

Lakini toba ni nini hasa?

Toba ni mchakato wa mambo mawili; ungamo (confession) na kutubu (repentence).

Ungamo maana yake kukiri. Mtu anayeungama, maana yake anakiri na kukubali makosa aliyofanya.

Kitubio kwa upande mwingine unahusisha kuomba msamaha, kujutia kosa na ahadi(dhamira) ya kutorudia kosa.

Hivyo ni sahihi kusema kuwa kutubu hakukamilishi toba bila kuungama. Na kuungama bila kutubu ni kazi bure.

Mtu akikuomba msamaha kwa dhati na kukutaka yaishe, ni lazima akiri pia kwa kinywa chake kuwa ni kweli alitenda kosa hilo.

Kukiri kosa ni jambo gumu kwa binadamu wengi. Lakini kuungama ni jambo muhimu sana katika mchakato wa kusameheana. Kuungama kosa ni ishara ya kujishusha. Anayeungama kosa lake kabla ya kuomba msamaha hufanya hivyo kutoka ndani ya roho yake na kujipambanua kwa laumu na dhamira ya kutokurudia kosa tena.

Anayesisitiza kuomba msamaha bila kukubali au kukiri kosa lenyewe, aghalabu hila bado ipo ndani yake na hana majuto ya dhati. Na mara nyingi mtu wa namna hiyo, baada ya muda mfupi atarudia tena kosa lile lile.

Kwenye mahusiano kwa mfano, uzoefu unaonesha wanawake wengi ni wagumu kukiri kosa kuliko wanaume. Mwanaume akibainika kufanya kosa fulani, ni mwepesi kukiri na kuomba msamaha. Mwanamke akifanya kosa kama hilo na kubainika ni nadra sana kukiri. Wengine huwa wapo tayari kufa au hata kuyatoa sadaka mahusiano yao, lakini sio kukiri kosa husika.

Yawezekana ni suala la kimaumbile. Hilo sijui. Lakini jambo moja la hakika ni kuwa, asiye na utayari wa kukiri kosa, hana majuto wala utashi wa kutokurudia kosa hilo. Hata kama akikuomba msamaha kwa machozi, kama hajakubali na hataki kukiri kosa lake nakuahidi kuwa atarudia tena!

Katika malezi pia, kuna watoto ambao ni wagumu sana kukubali makosa yao. Anaweza kuwa amedokoa kitu, au kuharibu kitu fulani na ukapata hakika kuwa mhusika ni yeye, lakini ukimuuliza anakataa kata kata. Siyo dalili nzuri.

Naelewa, watoto wengi hukataa kukubali makosa yao kwa kuchelea viboko, lakini usimchukulie kawaida mtoto anayependa kujitetea zaidi kuliko kukiri makosa yake. Siyo dalili njema hata kidogo. Hiyo mbegu ikiota na kukomaa, atakuja kuwa kiumbe mwingine.

Mzoeshe mtoto kukiri makosa yake, na akiomba msamaha, muonye hima na kumsamehe.

Mzoeshe mwenzi wako kukubali makosa na mapungufu yake, na akikuomba msamaha, msamehe mara moja. Usimfanye ajutie kuungama kwake.

Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu. Anataka tuungame na kukubali makosa yetu kwanza. Kisha tutubu na kuweka nia ya kutokurudia tena, haidhuru kama ukianguka tena.

Nawakatakia Jumapili Njema
 
Back
Top Bottom