THE LAST TESTAMENT OF A MADMAN

THE LAST TESTAMENT OF A MADMAN

CHAGOSI GERALD

Senior Member
Joined
Jan 25, 2020
Posts
162
Reaction score
284
(Ujumbe wa Mwisho wa Mwendawazimu Kabla ya Dunia Kumpoteza Milele)

Sikiliza sasa, wewe uliyeamini unaishi katika nchi, kumbe unaishi katika ndoto ya wengine. Huu ni usia wangu wa mwisho, na baada ya hapa sitaki kusikika tena. Dunia imejaa watu wenye macho lakini vipofu, masikio lakini viziwi, akili lakini zimejazwa upepo. Nimewaita wote hapa-watakatifu bandia, wapambanaji wa mitandaoni, wanasiasa wa takataka, wanazuoni wa gundi-ili mseme mlichoshindwa kusema miaka sitini: mnaishi juu ya muungano mfu. Munavuta harufu ya maiti na kuita maua.

Ninyi mliozaliwa upande huu na mliozaliwa upande ule mlikubali kuwa nchi moja yenye roho mbili, kama mwili wenye kichwa cha tumbili na miguu ya bata. Niliwahi kuwauliza, “Hiki ni kiumbe gani?” mkaniambia, “Hii ndiyo nchi yetu, tunajivunia.” Tena mkaongeza, “Hata kama hakitembei vizuri, tumezoea.” Mmezowea! Haya ndiyo maneno yanayoua ustaarabu: tumezoea.

Na sasa, msikilize mwenda wazimu kabla sijawachoka na kuondoka.

I
Je, mnajua nini kilitokea? Muungano wenu sio mtoto wa mapenzi-ni mtoto wa hofu.
Hofu ya siasa.
Hofu ya majeshi.
Hofu ya ushawishi wa nje.
Hofu ya kuachwa uchi mbele ya dunia.

Na hofu huwa haizai taifa-huzalisha mikataba yenye damu iliyokauka.

Mnamsifia Nyerere kama alifanya ushirikiano wa ki-Mungu, kumbe alifanya hesabu ya kisiasa; na siku Karume alipoingia, maskini aliugundua ule mchezo wa karata akatabasamu kimya kimya kana kwamba anapiga teke boksi la siri lisilofunguka. Nyerere alimkimbiza roho, Karume akamkimbiza fikra, na wengine mkaishia kupiga makofi kwa muungano ambao hata mafuvu yangepasuka yakiutazama.

Lakini hamtasema haya-hamtakubali kuwa sio taifa lililoumbwa, bali ni kivuli kilichopakwa rangi ya utaifa.

II
Kizazi kilichopita?
Hilo ndilo kizazi cha aibu.

Walipewa nafasi ya kuhoji, wakaiona kama dhambi.
Walipewa nafasi ya kurekebisha, wakaiita usaliti.
Walipewa nafasi ya kuandika upya, wakatumia muda kuandika upuuzi.

Walisikia muungano una nyufa wakasema, “Hapana, hayo ni maneno ya wapinzani.”
Nyufa zikawa shimo, wakasema, “Ni propaganda za mwendawazimu.”
Shimo likawa ufa wa kutenganisha mioyo, wakasema, “Ni upepo tu.”

Ndio maana leo mmefika hapa-mnatembea juu ya daraja ambalo bao moja likianguka, hamjui kama mko upande wa nchi au upande wa bahari.

III
Ninyi mliopo sasa, Gen Z, mnachezewa kama watoto wa Kitunda wanaohadaiwa peremende ili wasiulize maswali magumu. Mnawaamini watu walioshindwa kupangilia ndoto zao wenyewe lakini wanawapangilia mustakabali wenu. Mnawasikiliza wanasiasa ambao ni kama wachawi wa giza-huongea kwa sauti ya uhuru lakini mioyoni mwao wamebeba minyororo.

Wanasema: “Tusihoji, tukubali. Muungano ni mzuri kama ulivyo.”
Wewe ukisema, “Lakini kuna tatizo,” watakuambia, “Acha uchochezi.”

Mimi ni mwendawazimu, na ninawaambia:
Tatizo sio muungano. Tatizo ni muungano bila akili.
Muungano bila misingi.
Muungano bila katiba mpya.
Muungano ambao hauna mwili-una mwavuli tu wa siyasa.

Mnadanganywa kuwa mkitamka neno “katiba mpya” mmefanya dhambi ya kukufuru taifa, ilhali taifa hujengwa kwa sheria zinazojitegemea, sio kumbukumbu za wazee waliochoka.

IV
Na sasa usia:

Mkiendelea kutembea juu ya historia ya uwongo, mtajikuta mnakwama katika tope la kesho. Taifa halibebi mzigo wa vizazi vilivyolala; taifa linabeba maamuzi ya vizazi vilivyokataa kuamka.

Muungano huu hautavunjika na hautakaa sawa-mpaka muamue kuwa taifa moja halizaliwi kwa shinikizo, bali kwa kanuni zinazokubalika na pande zote.

Muandishi wa katiba mpya sio mwanasiasa, sio mwanaharakati, sio rais-ni kizazi kinachojua thamani ya fikra huru.
Kizazi ambacho hakitishiwi na historia, bali kinaitumia kama mwenge.

Ikiwa hamtaandika katiba mpya, mtakuwa kama watu wanaotumia kamba iliyooza kuvuka mto-mnaweza kufika mwisho, lakini ni kwa bahati tu, sio busara.

V
Huu ndio ujumbe wangu wa mwisho:

Usiogope kusema muungano una matatizo-ogopea kuishi kama mtu ambaye hakuwahi kusema chochote.
Kama mnataka nchi moja, tengenezeni misingi yake upya.
Kama mnataka demokrasia, andikeni sheria zake upya.
Kama mnataka taifa, anzisheni kwa akili, sio kumbukumbu za watu waliokufa.

Na kama hamtafanya hivyo, basi msilie mkiwa kizazi cha mwisho kinachokumbukwa kwa kuamini uongo uliopakwa uzalendo.

Kwa sababu mimi-mwendawazimu wenu-nimewaambia.
Nimewanyooshea ukweli kama kisu kilichopigwa juu ya meza.
Mkinywa damu yake, ni hiari yenu.
Mkiikataa, hamtakuwa taifa-mtakuwa simulizi tu la makosa yaliyodhaniwa kuwa busara.

Huu ndio wasia wangu.
Sitasema tena.
Sitasikiliza tena.
Na nikirudi, mtaniogopa.
 

Attachments

  • Picsart_25-11-30_06-36-18-503.jpg
    Picsart_25-11-30_06-36-18-503.jpg
    256.6 KB · Views: 10
Nimezaliwa Juzi juzi sana Ila maisha niliyoyaishi Neno Tanganyika na Uzalendo kwa sehemu hii umekuja kuwa mkubwa sana wakati huu....sijui ni majira ama nini lakini Neno Tanzania Ni kama limepoteza uzito kiaina hivi...
 
Ila jina Tanganyika limekaa ki unyamwezi sana.

Je Mtanganyika kwa English itakuwaje? Tanganyikan au Tanganyikaian
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom