Teknolojia ya mawasiliano isambae vijijini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Teknolojia ya mawasiliano isambae vijijini

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Mar 19, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 19, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  Mawasiliano ya uhakika ni moja ya nyenzo muhimu katika viashiria vya maendeleo katika mataifa yote duniani. Kuongezeka kwa Teknolojia mpya na upatikanaji wa mawasiliano ya haraka kumerahisisha kupungua kwa gharama za mawasiliano nchini hasa ikizingatia ushindani uliopo miongoni mwa

  mitandao mingi ya mawasiliano ya simu, ambayo sasa imeboreshwa na kuwafanya watumiaji wa mitandao hiyo kufaidika zaidi.
  Hayo yalikuwa moja ya maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, wakati akifafanua

  utendaji wa taasisi hiyo na kuelezea mkakati wa uboreshaji wa huduma za mawasiliano nchini katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam iliyofanyika katikati ya wiki hii, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Haki ya Wateja Duniani na kauli mbiu yake ilikuwa 'Fedha Yetu, Haki Yetu'.

  Profesa Nkoma alielezea kwa kina namna ugumu wa mawasiliano uliokuwepo mwanzoni mwa karne hii, na jinsi ulivyoathiri maendeleo ya wananchi na kukwamisha upatikanaji wa taarifa zilizochukua muda mrefu kuwafikia walengwa hasa katika maeneo ya vijijini.

  Alisema hiyo ilikuwa changamoto kubwa na ambayo sasa imepatiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa kutokana na mitandao mingi kuingia katika ushindani wa kutoa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

  Tunatambua mabadiliko ya gharama za mawasiliano tangu mitandao ya simu za mikononi zilipoanza kutumika nchini mwanzoni mwa miaka ya tisini, na pia tunathamini juhudi zilizofanywa na serikali kupitia taasisi hii ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa namna walivyodhibiti utoaji wa leseni

  kwa kuzingatia ubora wao na huduma zitolewazo.
  Ingawa ni kweli kuwa upo uhusiano wa karibu sana kwa wadau wa sekta ya Mawasiliano Tanzania, ambapo serikali inategemea watoa huduma hiyo (makampuni) walipie kodi kulingana na mikataba na wakati huo huo watumiaji (wananchi) nao wachangie kwa kununua gharama za mawasiliano,

  bado pato linaweza likaongezeka maradufu kama teknolojia hiyo ikisambaa hadi kwa wananchi wengi walioko vijijini.
  Kinachotia moyo kwa sasa kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA , Profesa Nkoma ni kwamba juhudi zinafanyika kupeleka mitandao vijijini

  ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha watangazaji kuwekeza zaidi vijijini ambako alisema huko ndiko kwenye fukuto la maendeleo ya Watanzania walio wengi.

  Na kwamba ili hayo yaweze kufanikiwa na kutoa tija, TCRA inafanya kazi kwa karibu sana na wadau wa sekta zote kuimarisha mahusiano ya mawasiliano.

  Kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa mawasiliano, Serikali imeanzisha mtandao unaounganisha mawasiliano kwa kutumia kiungo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na ule wa baharini wa SEACOM uliopo Kunduchi Beach Dar es Salaam, zote zikiwa ni juhudi ya kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya Tanzania.

  Wateja wa huduma za mawasiliano pia wanazo haki za msingi ambazo watoa huduma hiyo inawalazimu kuzingatia. Haki hizo ni pamoja na kupata taarifa muhimu kuhusu bidhaa kabla na wakati wa kutumia, kupata huduma bora zilizo kwenye viwango vya kimataifa, kutobaguliwa katika kupatiwa huduma, kupewa taarifa kabla ya kusitishwa kwa huduma na kadhalika.

  Tunaipongeza taasisi ya TCRA kwa juhudi zote zinazofanyika katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini na hasa katika hatua za kumpunguzia gharama mwananchi na kumshirikisha katika kutoa ushauri na maoni ya kiutendaji.

  Tumeshuhudia baadhi ya wananchi wanaposhindwa kupata mawasiliano kwa mitandao ya simu hubaki wakinung'unika wasijue nini la kufanya. Ni imani yetu kuwa TCRA itatoa elimu kupitia vyombo vya habari nchini namna ya kuwasiliana na watoa huduma mara tatizo la kiufundi linapotokea.

  Zipo changamoto nyingi wanazopata watumiaji wa mitandao ya mawasiliano ya simu, lakini tunaamini kwa kipindi kifupi kijacho, Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano itaweka mikakati ya kumaliza matatizo ya kiufundi yanayojitokeza kwa wadau wote, na pia kuwashinikiza makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano nchini kusambaza huduma hiyo hadi vijijini kwa maendeleo ya Taifa.

  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

   
Loading...