TataMadiba
JF-Expert Member
- Feb 7, 2014
- 9,866
- 5,742
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa wafanyabiashara wa vifaa vya mawasiliano, kuacha kuwahadaa wananchi kwa kutoa punguzo ili kuwashawishi kununua simu bandia na kutishia kuwafunga miaka 10 jela, faini ya Sh30 milioni au vyote kwa pamoja watakaobainika.
Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka hiyo ikiwa katika hatua ya kutekeleza mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi, huku ikitarajia kuzima simu feki ifikapo Juni 16.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Mhandisi James Kiraba alisema kuna wafanyabiashara wajanja wanaobadilisha namba za utambulisho za vifaa vya elektroniki (IMEI) ili kuwahadaa wateja kuwa simu zao siyo feki.
Kwa ujanja huo, namba ya utambulisho inakuwa inatumika na simu zaidi ya moja na kutambulika na mfumo licha ya kuwa ni feki.
Pamoja na kuonekana ni halisi kwa kipindi wanachozinunua, alisema simu hizo zinazobadilishwa IMEI nazo zitazimwa Juni 16 kwa kuwa ni feki.
“Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mikononi (mobile devices), kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 10 au faini isiyopungua Sh30 milioni au vyote kwa pamoja,”alisema.
Alisema kumekuwa na udanganyifu kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu.
Kiraba alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na hilo, huku wakihakikisha kuwa simu zao zimehakikiwa ili kuzuia usumbufu wa aina yoyote, utakaoweza kujitokeza wakati kipindi cha mpito kitakapomalizika.
Alisema idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zimeendelea kupungua kutoka asilimia 30 Desemba mwaka jana hadi kufikia asilimia 13 Machi.
Alisema uchambuzi wa Februari ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia tatu, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 18 huku simu halisi zilikuwa sawa na asilimia 79.
“Uchambuzi wa Machi unaonyesha idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia nne, huku idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 13, uchambuzi huu unahusisha makampuni yote ya simu nchini,”*alisema.
Source: Mpekizi