TCRA bora wakaishi sayari ya Jupiter

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
KINACHOTENDEKA sasa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kinanikumbusha alichokisema aliyekuwa rais wa Marekani mwaka 1801-1809, Thomas Jefferson.

Akitambua umuhimu wa vyombo vya habari na mchango wake kwa serikali au serikali ikosayo mchango wa vyombo vya habari, Jefferson alichagua vyombo vya habari bila serikali.

Alitafakari mchango wa serikali na vyombo vya habari kwa jamii, na akasema: “Ningetakiwa kuchagua kuwa na serikali bila ya vyombo vya habari au vyombo vya habari bila ya serikali, ningechagua vyombo vya habari.”

TCRA wiki iliyopita ilitoa taarifa kwa umma kuhusu mtindo unaoshamiri wa vyombo vya habari kutoa taarifa za siri kutokana na mawasiliano ya kielektroniki ya watu mbalimbali.

Utangulizi wa taarifa unasema: “TCRA imegundua kuzuka tabia ya uvunjaji wa kanuni za utunzaji wa siri za mawasiliano…. Mawasiliano hayo yamefikia hatua ya kuchapishwa katika vyombo vya habari.”

Nina imani kubwa TCRA imechagizwa na habari za uchunguzi zilizoandikwa katika gazeti hili katika siku za karibuni zilizohusisha mawasiliano ya mwanasiasa kijana nchini, Zitto Kabwe na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS), Jack Zoka.

Lakini, MwanaHALISI katika kutekeleza majukumu yake inatoa taarifa zozote – iwe za maandishi au za mazungumzo ya mdomo – iwapo watendaji wake wamezithibitisha kuwa ni halali na zinahusu watu wenye mamlaka inayogusa maslahi au mustakabali wa nchi.

Ni kweli kila mtu anahitaji faragha na ana haki ya faragha. Lakini ni ukweli pia kwamba faragha ya mtu hupungua kwa kiasi chake mara tu anapoamua kuwa kiongozi katika taifa. Kusemwa mabaya ya kiongozi wa aina hiyo huchukuliwa kuwa ndio gharama yake kuwa kiongozi.

Ukienda mbali, hata mtu asiyekuwa kiongozi wa aina hiyo lakini akawa anayo familia, basi faragha yake huisha pale kitendo alichokifanya ndani ya familia yake, kinapogusa hadhi za faragha za mtu mwingine. Ndipo mwanafamilia anapokabiliwa na mashitaka ya jinai kwa kubaka, kujeruhi au kuua.

Upo utaratibu wa kisheria nchini petu kwa viongozi wote wa nafasi za kisiasa – kwa maana ya wale waliochaguliwa na wananchi – kutangaza mali zao kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Utaratibu huo hauwahusu wanafamilia.

Taarifa ya TCRA ilinukuu kifungu cha 98 na cha 123 (1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta inayoelezea kosa la kutoa taarifa za watu na adhabu inayoweza kumpata mtu aliyethibitishwa kisheria kuwa ametoa taarifa husika.

Lakini, katika taarifa yake hiyo, TCRA haikunukuu baadhi ya vifungu vya sheria maarufu inayoeleza dhana ya kilimwengu kwamba haki ya mtu mmoja huishia pale inapoanzia haki ya mtu mwingine (Law of Torts)

Hii ni sawa na kusema kwamba hata ile faragha ya mtu mmoja au kundi, nayo inaishia mara tu anapotenda lolote na likatafsiriwa kuwa limeingilia faragha ya mtu au kundi jingine.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho taarifa ya TCRA imeacha kukinukuu. Nayo ni Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania inayozungumzia uhuru wa watu kutafuta na kupata habari.

Na kama sote tunaamini kuwa Katiba ndio sheria mama, ni lazima wakuu wa TCRA wafahamu kuwa haki ya kupata habari ni haki kubwa kuliko vikwazo vyovyote vinavyowekwa na sheria nyingine – kama hiyo ya mawasiliano – kwa lengo la kuzuia haki hiyo.

Kama kuna mtu au watu ambao mazungumzo yao ya siri yanaingilia faragha ya watu wengine, elimu ya kawaida inathibitisha kuwa mawasiliano yao yametoka katika kuwa ya faragha. Hapo hakuna tena siri kati yao.

Mfano, hivi TCRA watasemaje iwapo gazeti hili limekuja hewani na mawasiliano ya simu au imeili yaliyohusisha watu fulani wenye lengo la kumdhuru kiongozi mkuu wa nchi?

Watu wanaopanga kumdhuru kiongozi wa nchi nao wanahitaji kutunziwa hicho kinachoelezwa kuwa ni “Siri yao?” Kama TCRA wataamua kukaa kimya wanapokuta hali hiyo na baadaye tukio baya likamtokezea kiongozi yule aliyelengwa, wakubwa wa TCRA wataingia matatani.

Ni imani yangu kwamba makachero wa Tanzania wataelekeza nguvu zao za uchunguzi kwa watendaji wa TCRA. Wanaweza wasishitakiwe lakini wanaweza kuwa mashahidi muhimu wa namna taarifa hizo zilivyovuja.

Katika nafasi yangu ya kuwa mwandishi wa MwanaHALISI, nimepata bahati ya kufanya kazi iliyohusu habari ambazo TCRA imezitolea taarifa kuwa zimetolewa kinyume cha sheria, ingawa TCRA hawakutaja gazeti hili.

Taarifa hazikuzungumzia mambo binafsi baina ya wahusika bali zilihusu mustakabali wa makundi ya watu ambayo yangeathiriwa au yameathiriwa tayari moja kwa moja na wahusika.

MwanaHALISI haliandiki habari kuhusu nani anavaa nini au anakula wapi. Lakini kama utakuwepo ushahidi wa taarifa za kielektroniki kuhusu waziri aliyenunua nyumba ya thamani ya Sh. 5 bilioni nchini Marekani, zitachapishwa.

Waziri si mtu binafsi. Ni kiongozi katika taifa anayetarajiwa kuonyesha kwa vitendo alivyo mwadilifu; na ndio maana yumo katika viongozi wanaobanwa na sheria kutangaza mali zao kwa utaratibu unaosimamiwa na Ofisi ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Taarifa zake zinatolewa ili kujulisha umma tabia ya kiongozi wao na washinikize mabadiliko. Kutolewa kwa taarifa hizo pia kunashawishi serikali kumshughulikia kisheria.

TCRA na wengine wanaolalamika wafahamu kuwa haki ya wananchi kupata habari haiwezi kuzuiwa au kuminywa katika zama za sasa.

Uandishi wa habari umekua kwa sababu ya maendeleo na mabadiliko makubwa ya utandawazi na teknolojia ya habari na mawasiliano. Kubuniwa kwa mtandao wa WikiLeaks na raia wa Australia, Julian Assange, kumesukumwa na mapinduzi hayo ya kihabari.

Sasa wanahabari wanaandika yasiyofikiriwa zama zilizopita. Wanaandika mambo mazito na kuachia wananchi wajadili na kuamua. Na hiyo ni haki yao ya kikatiba. Hili ndilo tawi jipya la uandishi wa habari. Wenyewe wanaita Scientific Journalism (Uandishi wa Habari wa Kisayansi).

Isingekuwa aina hiyo ya uandishi, leo tusingejua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hoseah, aliwahi kukutana na kachero na mwanadiplomasia wa Marekani, D. Purnel Delly, na kusema aliyosema kuhusu Rais Jakaya Kikwete na mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Hakuna tena nafasi ya kuficha taarifa zinazohusu umma. Wakati hauruhusu siri kwani ni hizohizo huleta machafuko hasa katika nchi za Afrika. Ni waandishi wasiotambua wajibu wao tu kwa jamii wanaweza kuficha taarifa za kuvuruga uchaguzi au kuhujumu chama cha siasa.

Nini maana ya mitandao kama Facebook na Twitter kama usiri ungekuwa na maana? Mara ngapi watumiaji wa imeili wamejikuta wamevamiwa na hawana pa kukimbilia?

Kuna wataalamu wanapenya kwenye imeili za watu na kufanya watakacho. Hawa wanaitwa Hackers na kanuni moja kuu ya hackers ni kuwa dunia hii haipaswi kuwa ya siri.

Miaka 20 iliyopita, wimbo wa marehemu Dk. Remmy Ongalla wa Mambo kwa Soksi ulionekana haufai; ni wa mambo ya sirini yasiyofaa kutamkwa hadharani. Kuna siri gani leo hii kwenye wimbo ule?

Hata Muhidin Ngurumo akiwa na Msondo Ngoma waliwahi kuimba “Mambo Hadharani” kuashiria sasa kila kitu kifahamike.

Hata kama TCRA na Polisi watashika mwandishi wakimtuhumu kueneza siri na hatimaye kumfunga, hawatamzuia kuipeleka taarifa hiyo facebook, twitter au WikiLeaks.

Iwapo wanadhani ni haki kutunza wanachoita “siri,” ipo njia moja tu: kuhamia sayari nyingine. Ya Jupiter, sayari kubwa kupita zote, ni nzuri zaidi, huko watajitanua.

TCRA bora wakaishi sayari ya Jupiter | Gazeti la MwanaHalisi
 
Back
Top Bottom