Tarime waiadhibu CCM, kwa niaba ya Taifa! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tarime waiadhibu CCM, kwa niaba ya Taifa!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Oct 8, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 8, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,489
  Likes Received: 81,786
  Trophy Points: 280
  Tarime waiadhibu CCM, kwa niaba ya Taifa!

  Lula wa Ndali-Mwananzela Oktoba 8, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  SIJUI kitabu wanachotumia Chama cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi kina kurasa ngapi. Dalili zote zilizopo, hata hivyo, zinaonyesha kuwa yawezekana kitabu hicho kina kurasa moja na ina mistari miwili tu ya maelekezo.

  Mstari wa kwanza unasema “shinda kwa gharama yoyote ile” na mstari wa pili unasema “ukizidiwa ita Polisi”. Mstari wa tatu ambao umefutika na unaonekana kwa mbali unasema “ukiona polisi wanazidiwa, angalia mstari wa kwanza na wa pili”.

  Uchaguzi mdogo wa kiti cha Ubunge cha Jimbo la Tarime unatarajiwa kufanyika Jumapili kuziba pengo lililoachwa na Chacha Wangwe. Nimesema unatarajiwa kwani yawezekana kabisa kabla ya mwisho wa wiki kutokana na “sababu za kiusalama” uchaguzi huo ukaahirishwa. Hilo halituombei.

  Lakini kama utaendelea kufanyika kama ulivyopangwa basi kuna kila dalili kuwa CCM watapoteza uchaguzi huo kwa asilimia zisizopungua sitini. Hata hivyo, ushindi wa upinzani huko hautakuwa kwa sababu wanakubalika zaidi au kwa sababu wamefanya makubwa zaidi Tarime. La hasha, ushindi wa upinzani na hapa naamini Chadema, utatokana si na mkakati wao au uzuri wahoja zao bali kutokana na mioyo ya wana Tarime wenyewe.

  Wana Tarime wanatambua kuwa kama CCM na Serikali yake wangetaka kweli kushughulikia matatizo ya Tarime wangeweza kufanya hivyo miaka 10 iliyopita. Kama wangetaka kushughulikia tatizo la mapigano ya koo wangefanya hivyo muda mrefu uliopita. Lakini kwa vile hawakufanya hivyo wana Tarime wamegundua kuwa CCM wanachotaka ni kura tu ili wapate jimbo jingine.

  Hivyo ushindi wa upinzani ambao sitaushangaa ukitokea utatokana na wananchi wa Tarime kukataa ahadi za CCM na wapambe wake. Na zaidi kitu ambacho kinawaumiza wana Tarime ni huu uamuzi wa kupeleka kundi kubwa la polisi hadi Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Kamanda wa Operesheni maalum. Wote hawa wamepelekwa Tarime sasa.

  Wananchi wa Tarime wanakumbuka jinsi Mbunge wao Chacha Wangwe alivyoomba na kubembeleza bungeni ili vikosi maalum vipelekwe kule. Ilikuwa ni hapa mwishoni tu (miezi michache kabla ya kifo chake) ndipo timu ya wabunge ilienda huko na sijui mafanikio yake yalikuwaje.

  Wana Tarime wanakumbuka jinsi kundi la polisi lilivyopelekwa kule Tarime wakati wa sakata la migodini ambapo ilisababisha Wangwe kutiwa pingu na washirika wenzie kufungwa.

  Wana Tarime wanakumbuka mwaka 2003 pale ambapo baadhi yao walikuwa wananyanyaswa na Mkuu wa Wilaya na maafisa wengine ili wakubali malipo kiduchu kutoka kwa kampuni ya madini ya Afrika Mashariki. Wanakumbuka jinsi Tume ya Haki za Binadamu ilipotoa amri (zuio) kwa viongozi hao wa Serikali kutowanyanyasa hao wananchi na kuacha mpango wake huo.

  Wananchi wa Tarime wanakumbuka vizuri jinsi wananchi wenzao walivyouawa kinyama mwaka 2006 kwa kudaiwa kuingia kwenye mgodi wa Barrick kinyume cha sheria. Wanakumbuka jinsi ambavyo nguvu zaidi zimekuwa zikitumika kuwanyamazisha wale wanaopinga au kuhoji masuala ya migodi katika ardhi ya Tarime. Yapo matukio mengine ambayo wananchi wa Tarime wanayakumbuka vizuri na jinsi gani walivyotamani kuona Serikali ikiwatetea bila ya mafanikio.

  Wananchi wa Tarime wanakumbuka hayo yote. Wanakumbuka migongano ya koo mbalimbali. Lakini pia wengine wanajiuliza mbona kuna koo nyingine za Kikurya mkoani Mara na hawapigani? Mbona kuna maeneo mengi tu ambapo Wajaluo na Wakurya wanaishi na hawapigani? Mbona upande wa Kenya wa Wilaya ya Kurya kuna karibu watu wa koo na makabila yale yale lakini hakuna vurugu kama za Tarime? Hivi ni kweli mapigano hayo ni ya “koo” na ya kuwa wanagombana tu kama ndugu na kuchinjana?

  Kwa muda wote huu hakuna uongozi wa kweli ulioonyeshwa na Serikali ya CCM kutafuta suluhisho la Tarime. Viongozi wake wamekuwa wa kwanza kwenda kupatanisha Wakenya na Wazimbabwe; wamekuwa wa kwanza kupeleka majeshi Comoro na Lebanon, kulinda amani, lakini Tarime wanasubiri hadi wakati wa uchaguzi kupeleka mamia ya polisi hadi wengine wanatetewa kwa kufanya vitendo kinyume na sheria. Wananchi wa Tarime wanakumbuka hayo yote.

  Ni kutokana na kumbukumbu hiyo wananchi wa Tarime bila ya hofu, woga au kujali mtu au kitu chochote wataongozana kwa amani, hakuna silaha isipokuwa vidole vyao kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura siku ya Jumapili.

  Watakachopigia kura kwanza ni hukumu kwa CCM na uongozi wake wilayani humo na mkoani humo. Wataihukumu Serikali ya CCM kutokana na kuwasahau na kuwafanya wajisikie wako nje ya nchi yao. Wataihukumu CCM kwa kuleta viongozi wote vigogo kuomba kura lakini kutopelekea viongozi hao wakati watu wanakosa kula kutokana kuuana. Kwamba CCM imeona ni muhimu zaidi kuomba kula kuliko kuja na mkakati wa upatanishi.

  Wananchi hawa wa Tarime watakapopiga kura Jumapili watakuwa wanatumia mizani. Watapima mapungufu ya CCM na mapungufu ya Upinzani; watapima uwezo wa CCM kutatua matatizo yao na uwezo wa Upinzani kutatua matatizo yao. Wataona pasipo shaka kuwa CCM ina mapungufu mengi kama kinachotamba kuwa na dola na kila aina ya uwezo wa kufuatilia mambo. Watatambua kuwa Chadema ni chama chenye mapungufu yake ambayo wao wana Tarime wanayajua wazi kabisa.

  Watakumbuka mgongano wa Wangwe na Mbowe, watakumbuka majibizano yao kwenye vyombo vya habari, na kwa hakika watakumbuka tuhuma zinazotolewa dhidi ya Chadema kuhusu kifo cha Wangwe. Wakikumbuka yote hayo watakumbuka jambo moja kubwa nalo ni kuwa katika mambo yote chama chenye madaraka ya kufanya kazi ni CCM.

  Kama alivyosema Tambwe Hiza ni kweli kuwa viongozi wa Chadema watakamatwa basi ina maana kuwa CCM na Serikali yake wanajua wahalifu na wamewaacha kutembea. Ina maana kuwa vyombo vya dola vinajua watu waliovunja sheria na wamewaachia watambe. Wana Tarime watagundua janja ya nyani. Watawakatalia CCM ujiko huo kwani kama kweli vyombo vya Serikali vilikuwa vinataka kuchunguza kifo cha Wangwe walikuwa na nafasi nzuri na ya wazi.

  Kama kweli Serikali ingetaka kutafuta ukweli wa ajali nzima wana uwezo na njia za kuwasiliana na mashirika ya kimataifa ya upelelezi kama Scotland Yard ya Uingereza, lakini hawakufanya hivyo. Kama wangetaka msaada wa kufanya uchunguzi wa kina kweli wangeweza kuomba msaada hata wa FBI ya Marekani. Hawakufanya hivyo. Na wakati ule kabla ya Wangwe kuzikwa hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyesimama na kuitisha uchunguzi huru isipokuwa ndugu wa marehemu na waandishi ambao tulithubutu kupiga kelele.

  Wana Tarime watakumbuka kuwa ni Chadema kilichosimama upande wao na ni viongozi wa Chadema waliosimama nao wakati wote wa matatizo yao. Watakumbuka kuwa kama kuna makosa basi Chadema wawe wamejifunza sasa na ya kuwa hii ni nafasi ya mwisho ya wao kuaminiwa na wana Tarime. Wana Tarime watasema kati ya CCM na Chadema ni bora kuendelea na Chadema kwani kimejidhihirisha kuwa ni mtetezi wa raslimali za wananchi wa Tanzania na wataongoza kutetea maslahi hayo tena kwa mbunge mpya ajaye. Hili wananchi watalikumbuka.

  Hivyo naamini kabisa kuwa wananchi wa Tarime wakiamka siku ya Jumapili watakuwa wamejawa furaha na matumaini kuwa wataipa nafasi Chadema kumalizia ngwe yao ya kuongoza Tarime hadi uchaguzi wa 2010. Wataipima na kuichuja baada ya kufanya makosa ya hapa na pale. Wataiangalia kwa karibu kama imejifunza kusikiliza makada wake. Ni kutokana na ukweli huo wananchi wa Tarime watairudisha Chadema na mgombea wake bungeni na baadaye mwezi huu watashuhudia kuapishwa kwa mbunge wao mpya.

  Pamoja na hilo wana Tarime watakuwa wametuma ujumbe wa wazi kwa CCM na kwa Chadema. Kwa upande wa Chadema watawaambia kuwa tumewapa nafasi hii mjisahihishe na muendeleze mapambano ya Wangwe. Kwa upande wa CCM watawaambia kuwa tumewakataa kwa sababu mmetukataa lakini mkionyesha kutujali miaka hii miwili iliyobakia na si kutusahau au kulipiza kisasi basi msirudi kabisa huku 2010.

  Hivyo basi, CCM ijiandae kubwaga na ikubali matokeo na ifanye kazi ya kujitengeneza upya kama inataka kura za wana Tarime. Lakini upande mwingine Chadema watakaposhinda wasije kudhania wameshinda kutokana na uzuri wa chama chao, hoja zao au mikakati yao. Ushindi wao utatokana na kitu kimoja tu nacho ni kuwa wana Tarime wanajua chaguo lao. Wana Tarime wameamua kuwapa nafasi moja tu ya kujisahihisha na kuonyesha uongozi wa kutatua matatizo ya Tarime. Hivyo baada ya kutangazwa washindi wanyenyekee kwa wana Tarime na kuwaahidi kuwa watatekeleza ujumbe waliopewa nao ni kuendeleza mapambano waliyoachiwa na Chacha Wangwe, kwani hakuna tena kulala mpaka kieleweke. Kisipoeleweka wana Tarime wana haki ya kuichagua CCM mwaka 2010.

  Nawatakia uchaguzi mwema, na wa amani. Mwenye kushinda na ashinde, mwenye kukosa akose na akubali. Kwani mwisho wa siku, Tarime itaendelea kuwa mikononi mwa wana Tarime.

  Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk
   
Loading...