Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba sasa uchaguzi umekwisha, hakuna tena mikutano wala maandamano wala shughuli za siasa. Mbowe alimuuliza bungeni katika maswali kwa Waziri Mkuu, maana hasa ya kauli yake. Jibu la Waziri Mkuu lilikuwa la kutatanisha. aliruka maili mia, akisema kwamba hayo aliyasema kwenye jimbo lake wala hakuwa na maana ya nchi nzima.
Lakini haukupita muda, Rais Magufuli "akawaomba" wanasiasa, akimaanisha wa upinzani, wamwache afanye kazi, yaani wasifanye kazi za siasa. hilo halikueleweka, maana vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni, na kazi zake ni za kisheria, kikanuni na kikatiba. Haiwezekani kuvizuia kufanya kazi zake na ukawa hujavunja katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa, na zinginezo. wadau walipinga kauli hii, lakini haikusaidia kitu. wakati akipokea ripoti ya uchaguzi mkuu kutoka kwa Tume ya Uchaguzi, Magufuli sasa alitoa amri kwamba hakuna mikutano ya siasa. siasa zimekwisha na uchaguzi, na wanasiasa wasubiri 2020. Ilionekana kama jambo ambalo haliwezekani kwa nchi inayojinasibu kuwa ni nchi inayofuata "Demokrasia ya Vyama vingi", na ambayo katiba inahakikisha kwamba raia wana uhuru wa KUTOA MAONI, KUKUTANA NA KUBADILISHANA MAWAZO. Lakini Magufuli alisimamia amri yake hiyo haramu, na mpaka leo miaka mitatu baadaye inaonekana tunazoea kwamba vyama vya upinzani haviruhusiwi kufanya mikutano wala maandamano.
Mwanzoni ilikuwa mikutano ya hadhara. Lakini baadaye hata ile ya ndani ilikatazwa. ila sasa cha ajabu kabisa ni kwamba kauli ya Magufuli kwamba siasa zimekwisha mpaka 2020 haieleweki. maana tumeshuhudia chaguzi za marudio moja baada ya nyingine. kwa Rais aliyejinasibu kutotaka siasa tena, huu ulikuwa wakati wa kuchapa kazi kweli. hili wimbi la wabunge na madiwani "kukunwa" na utendaji wa JPM, linaonekana wazi kwamba linachagizwa na chama tawala, tena kwa hongo ambayo inafanya ile kashfa ya TAKRIMA enzi za akina Sumaye, ionekane ni cha mtoto. sasa hivi ni hongo na rushwa waziwazi kabisa, na kisha "uchaguzi wa marudio" unafanyika kwa gharama kubwa. hii haionekani kwamba ni siasa, kwa sababu inaonekana inaisaidia ccm ya JPM.
Magufuli alitoa amri nyingine, kupiga marufuku "Bunge Live". Mwanzoni alijificha nyuma ya Waziri wa habari wakati huo, Nape Nauye. lakini baadaye akatamka wazi kwamba ni yeye aliyetoa amri hiyo. Mwanzoni ilionekana kama vile haiwezekani, lakini taratibu tumezoea kuwa na bunge la gizani. Sababu ni wazi kabisa kwamba ni kudhibiti upinzani. Wabunge wa upinzani ni hodari katika kujenga hoja. hata makamu wa Rais mama Samia anajua hili, na aliwahi kuwataka wabunge wa CCM wapewe mafunzo namna ya kujenga hoja kama wale wa upinzani. alisema waziwazi: "mbunge wa upinzani akiwa anaongea utatamani kumsikiliza". Badala ya kuwanoa wa CCM nao wajenge hoja, ikaonekana njia rahisi ni kufuta bunge live, kwa visingizio vya gharama kubwa. lakini baadaye visingizio pembeni, amri moja.
Mwanzoni watanzania walizoea kusema maoni waziwazi. taratibu tumefundishwa kwamba katika utawala wa Magu, watu washone midomo yao. aliposema anatamani malaika waifunge mitandao, watu hatukuelewa. lakini sasa, baada ya watu mamia kukamatwa kwa kutoa ya moyoni katika mitandao mbalimbali, somo linaeleweka kwamba sasa ni SHUT UP!
Alikuwa ni Mkapa aliyeibuka na mbinu ya kumhoji uraia mtu "anayeleta za kuleta". Alianza na rafiki yake kipenzi, Jenerali Ulimwengu, pale alipomtangaza kwamba si raia. Hii ilikuwa baada ya Ulimwengu kuanza kuhoji baadhi ya hatua za Mkapa wakati huo. Ila hata Nyerere mwenyewe aliyempigia kampeni na kumweka madarakani, alihoji pia hatua hizo. kifo chake ndio kikamfunga mdomo.
Utaratibu huu wa kutumia kete ya uraia umepamba moto wakati wa JPM. kama ambavyo Magufuli hapepesi macho kuvunja makanisa na misikiti kisa kupanua barabara, kadhalika hapepesi macho kuwakaba koo Maaskofu, kutumia kete ya uraia. Hayo yalimkuta Askofu NiweMugizi wa Jimbo la Rulenge. Hilo la kuvunja misikiti na makanisa ni zito kiasi cha kutosha, lakini amevunja pia magorofa, kwa gharama kubwa, tena katika mazingira ambayo uvunjaji huo ungeweza kabisa kuepukwa.
Tukashuhudia watu ambao wanampinga kwa bidii sana Magufuli, wanafikwa na zahama kubwa. kuna waliopotea kama Ben Saanane, aliyehoji PhD ya Magufuli. ilikua ni rahisi tu kutoa maelezo kumjibu Saanane. lakini akapotea. akaja Tundu Lissu. mpinzani mkubwa wa Magufuli, ambaye alielimisha taifa kwamba tunaingia kutawaliwa na Dikteta. Tundu Lissu aliponea chupuchupu mvua ile ya risasi. Yuko ulaya kwa matibabu, lakini huku nyumbani tunashuhudia kutimia kwa maneno yake.
Baada ya ripoti ya Twaweza ikieleza kushuka kwa kasi kwa umaarufu wa Magufuli, mengi yalitokea. kwa hakika kabisa, lile la kuandikiwa barua na COSTECH, ambapo watanzania tulifundishwa kwamba kumbe hata choo cha kulipia kinaweza kutumiwa kutoa amri kwa mtu "anayeleta za kuleta", pale COSTECH walipotoa tishio la kuchukua hatua kwa TWAWEZA, Na hili la Eyakuze wa TWAWEZA kuchunguzwa uraia, na kunyang'anywa Paspoti, ni mambo mawili yanayofahamika. lakini naamini kuna mengi ambayo TWAWEZA wamekutana nayo tokea walipotoa ripoti hiyo mpaka hivi sasa.
Hayo yaliyompata Tundu Lissu, Ben Saanane, Azory Gwanda, Askofu Kakobe, Askofu NiweMugizi, viongozi wa CHADEMA ambao wana kesi takriban 400, na hili la TWAWEZA, na mengine mengi, yanatunyoosha watanzania: watu wanaogopa, wanatishika, wanafuata reli. lakini haitakiwi iishie hapo.
Naamini kwamba Mungu ni mwenye haki. atainua watanzania wengine ambao hawataogopa mabavu ya Magufuli. na kwa mwendo huu anaokwenda, haitashangaza kama kwa kauli ya CCM ITATAWALA MILELE, tayari ana matamanio mabaya zaidi ndani ya uovu wa moyo wake.