Tanzia: Mohamed Mlamali Adam afariki Dunia

Tanzia: Mohamed Mlamali Adam afariki Dunia

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
22,474
Reaction score
33,015
TAAZIA: MOHAMED MLAMALI ADAM

MIMI NA MWALIMU WANGU

Mohammed Said



Siku moja nimepita ofisini kwa Bwana Ally Sykes na katika mazungumzo yetu akaniambia kuwa alikuwa siku ya pili anasafiri anakwenda London. Palepale ikanijia fikra nimpe Bwana Ally makala yangu ambayo nilikuwa nimeandika kuhusu historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika aifikishe jarida la Afrika Events. Hili lilikuwa gazeti lililokuwa likichapwa London na Mhariri Mkuu wake alikuwa Mohamed Mlamali Adam na waandishi wengi katika gazeti hili na wafanyakazi wake walikuwa vijana kutoka Zanzibar kama Ahmed Rajab na wengine - ‘’birds of a same feathers...’’ na wachangiaji walikuwa kama Prof. Ali Mazrui, Abdilatif Abdallah, Prof. Mohamed Hyder, Prof. Mohamed Bakari, Fuad Nahdi wote kutoka Mombasa, Prof. Haroub Othman, Prof. Hamza Njozi kutoka Dar es Salaam na waandishi wengine. Africa Events lilikuwa gazeti la Waswahili ingawa likiandikwa kwa Kiengereza. Uzuri wa mkusanyiko huu ni kuwa hawa wote hawakuwa ‘’fellow carpetbaggers,’’ wakiliandikia gazeti kwa mahaba makubwa kwani kwa mara ya kwanza tulikuwa tumepata gazeti letu wananchi wa Afrika ya Mashariki. Kama kulikuwa na kasoro katika jarida hili ni kuwa likiendeshwa na hao ‘’birds of the same feathers.’’ Hii ikafanya jarida kwa baadhi ya watu lisionekane kama jarida la Watanzania wala jarida la Wazanzibari wala la watu wa Afrika ya Mashariki. Lakini kama alivyosema William Shakespeare, ‘’What in a name?’’ Ukipenda, rangi ya paka ina umuhimu gani madhali paka anakamata panya?

Bwana Ally Sykes akaifikisha ile makala kwa Mlamali Adam na siku zile wengi tukiandika kwa mkono na mimi makala yangu ilimfikia Mlamali katika hali hiyo. Nakumbuka ilikuwa haina hata kichwa cha habari. Mlamali aliipa kichwa, ‘’In Praise of Ancestors,’’ na Mlamali ni ‘’wordsmith,’’ muhunzi wa kufua maneno na misemo sisi wanafunzi wake tukimjua mwalimu wetu Mlamali kwa utaalamu huu. Makala hii Mlamali kwa mkono wake mwenyewe akaiandikia utangulizi na akaichapa. Utangulizi wake ulikuwa huu:

There is a large body of Tanzania’s political history which has the effect, if not the avowed goal, of writing down the role of Muslims in the fight for independence. Yet it is a fact that their enterprise were not only crucial but daringly imaginative. Names like Mzee Saadani Abdu Kandoro and the Sykes brothers: Abdu and the ever-youthful Ali come easily to mind. In a forthcoming book, Mohamed Said concentrates on these forgotten founders, what follows is a chapter from his work.’’

Mlamali alikuwa ‘’marksman,’’ mlenga shabaha bingwa ambae kwenye sare yake ya jeshi ukosini anavaa alama ya mkasi medali makhsusi anayotunukiwa mwanajeshi mwenye shabaha kali ambae siku zote anapiga ‘’bull.’’ Si kama hakujua maneno aliyoandika hayatakiwi na kwa miaka imekuwa hivyo kiasi historia za hao aliowataja zilikuwa zimepotea hazipo tena katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika. Mlamali alikuwa anajua fika lakini nilikuwa nimemsogezea bango la kulenga shabaha na vidole vyake vilikuwa vinamuwasha kwa kutaka kuitumia bunduki yake. Si Abdul wala si mdogo wake Ally na Saadan Abdul Kandoro walikuwa wanafahamika na kutambulika kama waasisi wa TANU na wapigania uhuru wa Tanganyika achilia mbali kutaja mchango wa Waislam. Huu utangulizi alioandika ulikuwa utangulizi uliovunja mwiko mkubwa ambao wengi hawakutamalak kuuvunja huo mwiko.

Utangulizi huu ndiyo uliomghadhibisha Dr. Mayanja Kiwanuka kutoka CCM Dodoma akarudisha majibu makali sana lakini majibu yale yalielekezwa kwa mwandishi wa makala ile si kwa Mlamali mhariri wa gazeti. Majibu ya makala yangu yalikuwa makali yaliyojaa kejeli na vitisho. Jarida lile la mwezi March/April 1988 lilikusanywa lote nakala chache sana ziliwahi kuuzwa kabla kwa kifupi wasomaji walikosa nakala ya mwezi huo.

Mlamali alikuwa kanifungulia mlango wa uandishi na watu kunifahamu na pia kufahamu historia ambayo tayari ilikuwa imeshaanza kupotea kwa kupotezwa kwani kuanzia hapo Mlamali akawa anachapa kila makala niliyokuwa nampelekea. Nami nikawa na kazi moja tu. Kusoma kila alichoandika Mlamali na kuiga staili yake. Kwa wale wanaoijua kalamu ya Mlamali hawawezi kukosa kuiona alama yake kwangu mimi ninavyojitahidi kutabaruku na mwalimu wangu kwa kugeza staili yake bila mafanikio makubwa kwani Mlamali alikuwa gwiji umahiri wake wa lugha ya Kiswahili, Kiarabu na Kiengereza ulikuwa ukimfanya akiandika moja ya lugha kati ya hizo tatu utastaladha.

Lakini kabla ya utangulizi huu alioniandikia Mlamali kabla aliandika maneno kama haya kama utangulizi katika makala, ‘’Hero or Humbug,’’ aliyoandika katika kifo cha Sheikh Thabit Kombo:

‘’The death of Thabit Kombo reminds one of other old grand venerable founding fathers of the ruling party in Tanzania. The good Samatitan John Rupia whose property was later nationalised. The nice cheerful Mzee Sampat who toiled for measly wages and died a poor man. The Sweet Abdul Sykes who risked his job as Market Master under colonial government in order to set up the party. And others. They have passed away, their dedication and love of country not quite fully requited. Thabit, however, has all along had it good. Neither his power and reputation nor his immense wealth were ever assailed. How did he do it?’’

(Africa Events October 1986)


Mlamali alikuwa mshambuliaji hodari mwepesi wa kupokea pasi na kuelekeza mashuti golini. Angalia alivyoitoa kutoka kusikojulikana historia ya Thabit Kombo na alivyoipenyeza katika historia ya TANU kiasi msomaji anajiuliza hii ni makala au ni taazia ya Thabit Kombo? Kwa ufundi mkubwa sana makala ile ilikuwa mfano wa ufupisho ‘’absract,’’ ikieleza historia nzima ya Zanzibar kabla na baada ya mapinduzi. Ikieleza raha na karaha zilizokuwako nyakati zile. Makala hii msomaji ukimaliza kuisoma lazima utashusha roho. Hakika mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964 yalikuja na mengi. Kwangu mimi hii ni taazia na inanikumbusha taazia aliyoandika Erika Fiah mwaka wa 1940 baada ya kifo cha Martin Kayamba ambae kama Thabit Kombo alikuwa jirani ya milango ya watawala lakini yeye kuwapo kule hakukumnufaisha yeyote zaidi ya yeye mwenyewe na kuongeza machungu kwa wale waliodhani kuwa yeye angekuwa mkombozi wao. Ajabu kuwa baada ya nusu karne ya taazia ya Fiah, Mlamali anaandika maneno yaliyofanana na maneno ya Fiah kama vile Mlamali na Fiah ni wanafunzi wawili watukutu, wezi wa mtihani waliochunguliana majibu ya maswali ya mtihani darasani. Hakika historia hujirudia lakini bado hubakia kuwa historia.

Msomaji hebu msikilize tena Mlamali anavyozungumza kupitia kalamu yake. Mlamali anaanza kama hadithi kichwa cha tahariri kinasema, ’The Old Man of the Forest.’’:

‘’All know him, who once were avid readers of a thousand – and – one – nights’ fables. He was a man of unaccountable years, his eyes laden with so many crow – feet as to drive to despair all but the most ardent face – lifter. He had a cavernous orifice where the mouth should have been.’’

(Africa Events December 1987).


Usitafsiri ukautoa ladha mchuzi. Ukifanya hivyo utaondoa utamu wote. Acha soma kama ilivyoandikwa kwa Kizungu na mwalimu wangu bingwa wa ung’eng’e na pia lugha ya Kiarabu. Mlamali anawazungumza viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania madaraka ambao kawatumbukiza ndani ya hadithi ya Sindbad Baharia na safari zake saba, Sinbad akiwa kambeba Mzee wa Porini aliyemkaba shingo sawasawa asiyetaka kuteremka mabegani kwake ije jua ije mvua. Hapo Mlamali kachaganya, ‘’satire,’’ na ukweli wa siasa za Afrika. Lakini ukipita katikati ya mistari ya Mlamali utagundua kuna mengi anayozungumza ni kuliko hayo yaliyo machoni pako kwenye kurasa za jarida. Kwa uandishi huu Mlamali aliwaudhi viongozi wengi ambao walijiona katika kurasa za kila alichoandika ndani ya jarida la Africa Events lakini hawakuwa na la kufanya. Huyu ndiye mwalimu wangu miye Mohamed Mlamali Adam.

Sasa baada ya mashambulizi na vitisho vile kutoka Dodoma Mlamali akanipa nafasi ya mimi kujibu yale niliyoshutumiwa kuwa nilikuwa nimepotosha historia ya TANU. Mwezi September katika kumbukumbu ya ya miaka 20 ya kifo cha Abdul Sykes Mlamali alichapa makala yangu katika ukurasa ‘’column,’’ ‘’Once Upon a Time,’’ ‘’Founder of a Political Movement: Abdulwahid K. Sykes (1924 – 1968).’’ Makala hii ilisisimua wasomaji wengi sana kwa kuwa ilikuja na mengi ambayo hayakuwa yanajulikana katika uasisi wa chama cha TANU. Wasiomjua Abdulwahid Sykes wakawa wanauliza waliomjua, ‘’Nani huyu Abdulwahid Sykes mbona historia yake inaingiliana na historia ya Julius Nyerere?’’ Mbali ya maswali ya pembeni hakuna kutoka Dodoma aliyegusa makala ile. Hii ndiyo makala iliyomtoa machozi Mzee Ahmed Rashad Ali alipoisoma kisha siku ya Eid tukakutana Msikiti wa Kitumbini kwenye sala ya Eid akanikumbatia kunipongeza kwa makala ya rafiki yake huku akibubujikwa na machozi kwani nilikuwa nimemkumbusha kipenzi chake na mengi katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika ambayo yeye akiwa mtangazaji wa Radio Free Africa ikitangaza matangazo yako kutoka Cairo katika miaka ya 1950. Rashad alikuwa akifanyia propaganda kulielezea bara la Afrika lilivyokuwa chini ya ukoloni. Mlamali alikuwa kila kukicha akichapa makala zangu na kwa kufanya hivyo kujenga jina langu na wasomaji wangu wakiniona njiani wataniuliza, ‘’Vipi Mohamed mwezi huu tutegemee kitu gani katika Africa Events?’’

Ilikuwa Ahmed Rajab ndiye aliyenipokea London na kuwa mwenyeji wangu. Nilitoka Dar es Salaam nikiwa na barua kwa Mlamali iliyoandikwa na Mwanadiplomasia Ahmed Maulid ambae ndiye aliyenijulisha kwa Ahmed Rajab alipokuja Dar es Salaam na tukakutana nyumbani kwa Mwanadiplomasia Maulid Masaki. Nilikuwa namfahamu Ahmed Rajab kwa kumsoma na kumsikia kwenye radio ya BBC Idhaa ya Kiswahili nakumbuka tulikuwa sote tumealikwa kwa Mwanadiplomasia Maulid. Mwanadiplomasia huyu alikuwa rafiki yangu na jirani yangu tukizungumza mengi katika siasa na historia ya Tanganyika na Zanzibar. Ahmed Rajab siku ile alikuwa kaongozana na marehemu Ali Said mmoja wa vijana wa mrengo wa kushoto kutoka visiwani. Nilifahamiana na watu wengi sana kupitia kwa Mwanadiplomasia Maulid na kitu kimoja ni kuwa kila mtu aliyenifahamisha basi akawa rafiki ndugu kuanzia Ahmed Rajab hadi Salim Himid aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa visiwa vya Ngadzija na sasa anaishi uhamishoni katika mji wa Paris nchini Ufaransa. Salim kila akija Dar es Salaam lazima atanitafuta na mimi nimemtembelea jijini Paris miaka michache iliyopita.

Hivi ndivyo nilivyokuja kujuana na Ahmed Rajab na Ahmed akanifikisha kuonana na mwalimu wangu uso kwa macho kwenye uradi nyumbani kwa Sheikh Mohamed Abubakar, Mwanasayansi wa Kizanzibari katika taaluma ya Fizikia ya Nuklia ngazi ya kimataifa.

Nilipokwenda kumuaga Sheikh Aboud Maalim kuwa nakwenda Uingereza alinambia nijitahidi wenyeji wangu wanifikishe nikaonane na Sheikh Mohamed Abubakar. Sikuuliza sababu ya msisitizo huu adabu ilikuwa inanizuia ndio mila zetu zilivyotuelekeza. Nilizijua sifa zake kutoka kwa Ahmed Rajab hata kabla sijakutananae na ikasadifu kuwa ni nyumbani kwa Sheikh Mohamed Abubakar ndipo nilipokutana na mwalimu wangu wa masafa marefu Mohamed Mlamali Adam. Lakini wakati huo Mlamali alikuwa hayupo tena Africa Events. Lakini furaha yangu ilikamilika siku Ahmed Rajab aliponichukua BBC Idhaaa ya Kiswahili na kwa mipango yake nikapewa fursa ya kuandika na kufanya kipindi ambacho Mlamali alikuwa akikifanya kila juma, ‘’Barua Kutoka London.’’ Mimi kwa kuwa nilikuwa napita njia London kuelekea Glasgow Scotland kipindi changu nilikifanya katika studio za BBC Glasgow na anuani yake ikawa, ‘’Barua Kutoka Glasgow,’’ na kwa hakika sikuwa na lolote ndani ya ile studio ila kumuiga mwalimu wangu Mlamali nikiweka mguu wangu pale ulipobandua wake huku nimeshika kanzu na koti lake kwa nyuma nikiogopa kuteleza na kuanguka.

Allah amweke mahali pema Mohamed Mlamali Adam mtu ambae Allah alimpa vipaji vingi na yeye akavitumia kwa faida ya umma na nchi yake Zanzibar aliyoipenda sana inagawa alihajiri tangu mwaka wa 1968 na kutokukanyaga tena ila mapenzi yake palipozikwa kitovu chake yalimzunguka hadi kufariki.

Tunamuomba Muumba ampokee mja wake huyu na amjalie kati ya wale watakayoipata Janatul Firdaws, Amin.

8 Oktoba 2019
 
BARAZANI

Tumefiwa walimwengu: Mohamed Mlamali Adam (1944-2019)

Na Ahmed Rajab

SHEIKH Mohamed Mlamali Adam, aliyefariki dunia katika hospitali moja jijini London usiku wa Jumamosi iliyopita, akiwa na umri wa miaka 75 alikuwa mtu wa vipaji vingi. Alikuwa mwandishi, mtangazaji wa redio, mhariri wa magazeti, mkalimani (aliyezimudu vilivyo lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu), mfasiri wa riwaya na mhakiki wa mashairi.

Lakini watu wengi hususan Waisilamu wa Ulaya watamkumbuka kwa ushekhe wake na umahiri wake wa kutoa mawaidha ya kuwavutia watu katika dini

Mlamali hakuwa shekhe wa vilemba, kashda na majuba. Sana sana akivaa kofia ya mkono. Na hiyo akiivaa kwa nadra. Mara nyingi akenda kichwa wazi, akiwa amevaa shati, suruwali na koti. Akipenda kujificha, hakutaka ajulikane, akifuata moja ya miongozo ya tariqa yake ya Kisufi ya Ba ‘Alawi inayojulikana pia kwa jina la Tariqa ‘Alawiyya.

Ingawa mara nyingi kichwa chake kilikuwa wazi lakini ndani ya kichwa hicho mlikuwa bahari. Nayo ilikuwa shuwari, isiyochafuka. Na juu ya bahari hiyo pakielea ilmu, hasa ilmu ya dini ya Kiisilamu.

Tukimuona Mlamali akijiendea, kumbe akiibeba bahari iliyomgeuza naye awe bahari.

Kwa nilivyomjua ninathubutu kusema kwamba katika mwisho wa uhai wake Mlamali alikuwa ni “al Arif Billah”. Hii ni hii ni daraja kubwa katika tasawwuf (Sufism). Masufi wanaamini kwamba watu wenye kufikia daraja hii ni wenye kumjua Mwenye Ezi Mungu, siri na asirari zake.

Kwa mujibu wa mashekhe wa Kisufi watu wa aina hiyo ya Mlamali huko akhera Mungu huwajaalia yale ambayo macho yoyote hayakuwahi kuyaona, yale ambayo hayakuwahi kamwe kusikiwa na masikio yoyote, na yasiyowahi kuzipitia nyoyo za wanadamu (maa laa ‘aynun ra’at wala udhunun sami‘at wa laa khatara ‘ala qalbi bashar).

Tumeondokewa si na mtu bali na jitu la ilmu. Si mti bali gogo. Alikuwa kama ensaiklopidia Ukiwa na tatizo la kidini ilikuwa umuulize tu. Naye alikuwa tayari kukwambia wapi pa kukupatia jawabu yako ama kwenye Qur’an au kwenye vitabu vingine. “Hebu tazama kitabu fulani, mahala fulani, utapata jawabu.” Alikuwa ni mtu wa aina hiyo.

Ubongo wake ulikuwa mithili ya simaku. Alikuwa hodari wa kuhifadhi alichokisoma. Mfano ni dua zote za Al Habib Ali bin Muhammad bin Hussein al Habshi ambazo alizihifadhi kwa moyo. Dua hizo, ambazo ni nyingi mno, alikuwa akizisoma tangu utotoni kwenye msikiti wa Sharifu Abudu huko Vikokotoni, Unguja.

Katika kusaka kwake ilmu alikuwa akihudhuria darsa zilizokuwa zikiendeshwa huko saa za alfajiri. Wala hakuwa akiona taabu kuazimia vitabu vya dini kutoka kwa Prince Seyyid Haroub, mjukuu wa sultan wa enzi Seyyid Khalifa bin Haroub.

Mwana huyo wa kifalme alikuwa pia ni sufi naye na Mlamali wakikutana kwa Alhabib Omar bin Sumeit. Mlamali akimuitakidi sana pia Habib Swaleh bin Alwi Jamalul-leyl wa Lamu (1853-1932).

Miongoni mwa mashekhe waliomlea Mlamali katika mambo ya dini, ya kiroho, ni Alhabib Sayyid Omar bin Ahmed bin Sumeit, Sayyid Ahmed bin Hussein, Mwinyi Baraka na Sheikh Muhyiddin bin Omar ambaye katika zama za siasa alikuwa mmoja wa wasomaji dua kwenye mikutano ya chama cha Afro-Shirazi Party (ASP). Mlamali aliwahi kwa muda kukaa kwake na akihudhuria darsa zake wenye msikiti wake Baraste Kipande.

Pamoja na kutoa mawaidha katika mikusanyiko mbalimbali, jijini London alikuwa akiendesha darsa mbili. Iliyokuwa kubwa ilikuwa ile ya eneo la Wembley iliyoanzishwa katika miaka ya 1980 kwa idhini ya al Habib Ahmed Taha Mash-hur al Haddad. Darsa hizo akizitoa kwa lugha ya Kiingereza na zikihudhuriwa na wanaume pamoja na wanawake wa kabila mbali mbali.

Mwanzoni alikuwa akiziendesha kila baada ya wiki mbili, halafu zikawa za kila mwezi mara moja na mwishoni mwa uhai wake, hali yake ya afya ilipokuwa si nzuri, alikuwa akidarisisha kila baada ya miezi miwili.

Darsa nyingine ilikuwa ni ya kila Jumamosi aliyokuwa akiendesha nyumbani kwake. Hii ilikuwa ndogo, ikihudhuriwa na watu wachache aliowataka mwenyewe.

Miongoni mwa waliokuwa wakihudhuria ni Sheikh Abdal Hakim Murad, ambaye sasa ni profesa katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Murad ni Muingereza aliyesilimu alipokuwa kijana mdogo na sasa ni alim wa dini ambaye mihadhara yake huwavutia wengi.

Darsa za nyumbani kwake Mlamali zilikuwa zikianza kwanza kwa kiarabu, kwa wanafunzi wake waliobobea katika lugha hiyo. Halafu zikawa kwa Kiswahili kwa wanafunzi wake wa Afrika ya Mashariki.

Mlamali alikuwa akisomesha sana mambo ya fiqhi. Mara moja moja akigusia mambo ya “tasawwuf”.

Akishikilia watu waelewe mambo ya msingi katika dini kama kwa mfano namna ya kutawadha kabla ya kutaka kujua mingine.

Mlamali alikuwa akiwasomesha wanafunzi wake utadhani kama akiwashika mikono na kuwapitisha katika njia itayowafikisha kule alikotaka wafike, kwenye ucha ungu.

Mohamed Mlamali Adam alizaliwa Misufini, Unguja, Oktoba 8, 1944. Nyumba yao ilikuwa jirani sana na kwa kina Salim Said Salim, ambaye siku hizi ni miongoni mwa waandishi wakongwe wa Zanzibar. Tuliyekuwa tukimjua Mohamed Mlamali tangu miaka ya 1950 tumezoea kumwita kwa jina lake la pili, Mlamali, jina la baba yake.

Bwana huyo alikuwa akifanya kazi kwenye Jumuiya ya Walimaji Karafuu (CGA). Pembeni akinunua samaki kwa jumla, akiwakaanga na mkewe Bi Asha, mamake Mlamali, akiwauza.

Mlamali alikirithi kipaji cha ufasaha wa kusema na kuandika nyumbani kwao kutoka kwa bibi yake mzaa mama, Bi Mwanriziki, bibi wa Kingazija aliyekuwa ameolewa na bwana mmoja kutoka sehemu za shamba. Bibi huyo aliyekuwa na ustadi mkubwa wa lugha ya Kiswahili alimrithisha kipawa hicho Mlamali pamoja na mdogo wake Adam Mlamali aliyekuwa gwiji wa mashairi ya nyimbo za Taarab.

Mohamed Mlamali hakuwa akitunga mashairi ingawa alikuwa na ujuzi mkubwa wa mashairi hayo.

Utotoni alikuwa mbele yangu katika madrasa (chuoni Msikiti Barza), katika skuli ya msingi ya Darajani na pia katika skuli ya Sekondari ya King George VI ambayo sasa inaitwa Skuli ya Lumumba.

Miongoni mwa waalimu wake katika skuli ya Darajani walikuwa Ibrahim Kassim, Omar Ahmed Muhdhar (Sharif Mapanga) na Abdalla Kassim Hanga. Utotoni Mlamali akimhusudu Hanga kwa umombo wake na Hanga ndiye aliyemsaidia kukikuza Kiingereza chake.

Mlamali alikuwa hodari skuli lakini uhodari wake haukuwa wa kuzaliwa nao ila aliupata kutokana na jithada zake kubwa katika masomo. Yeye na kaka yake, Said Mlamali, waliruhusiwa kufanya mtihani wa kuingia skuli ya sekondari wakiwa darasa la saba badala ya la nane. Wote walifuzu.

Alipohitimu masomo ya sekondari Mlamali alipata kazi ya kuwa mkalimani mahakamani kwanza Unguja kwa kipindi kifupi na baadaye Chake Chake Pemba. Mapinduzi ya Januari 1964 yalimkuta Pemba.

Siku moja akiwa Unguja alikamatwa pamoja na baadhi ya mashekhe wakubwa. Walituhumiwa kuwa wakisoma dua kuiapiza serikali na kutaka kuipindua. Hakika ya mambo ni kwamba walikuwa wakikutana kila wiki kuomba dua. Walikuwa na ada hiyo hata kabla ya Mapinduzi. Walifungwa jela kwa muda bila ya kufanyiwa kesi.

Walipofunguliwa, Mlamali alihamia Dar es Salaam ambako kwa muda akifanya kazi katika ubalozi wa nchi moja ya Ulaya ya Mashariki. Nilimkuta Dar mwaka 1968 nilipokwenda kwa mapumziko kutoka London. Aliniuliza iwapo nikimjua mtu katika kitengo cha BBC kilicho Nairobi cha kunasa na kuzisajili taarifa za steshini za redio za baadhi ya nchi za Afrika na Mashariki ya Kati.

Nilimjulisha na Pat Edwards, Mwingereza aliyekuwa mkuu wa kitengo hicho na aliyewahi kuwa msimamizi wa vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London. Baada ya kufuzu mtihani aliopewa aliajiriwa na alifanya kazi Nairobi kwa takriban miaka sita akitafsiri kwa Kiingereza taarifa zilizokuwa zikitangazwa ama kwa Kiswahili au Kiarabu na steshini za redio za nchi za Afrika ya Mashariki na za Kiarabu.

Katika kufasiri taarifa za Kiarabu akishirikiana na kina Salim Bakhressa, Profesa Said Hamdun na Muhsin Attas.

Hatua nyingine ya maisha yake ilimfikisha jijini Cologne, Ujerumani kwenye stesheni ya Sauti ya Ujerumani (DW) alikoianza tasnia ya uandishi habari na utangazaji wa redio. Nafasi yake ya kazi Nairobi ikajazwa na Othman Miraji. Wawili hao baadaye wakafanya kazi pamoja DW.

Huko Cologne Mlamali alikutana na mwandishi maarufu wa Kinigeria, Peter Enahoro aliyekuwa mhariri DW na aliyekuwa pia akifanya kazi London kwenye jarida la Africa Magazine.

Enahoro na Mlamali walikuwa wakishiriki katika kipindi kimoja cha Kiingereza na ndipo Enahoro alipovutiwa naye. Enahoro alipohamia gazeti la New African akiwa mkurugenzi wa uhariri alimchukua Mlamali. Hapo ndipo ulimwengu usio wa Kiswahili ulipoanza kumtambua kwa uandishi wake mahiri.

Mwaka 1983 nilikuwa mtu wa kwanza kuajiriwa na kampuni moja iliyokuwa ikitaka kuanzisha gazeti jipya la kila mwezi kuhusu Afrika. Hatua yangu ya mwanzo ilikuwa kuwapata wenzangu wa kuliendesha gazeti. Nilifanikiwa bila ya tashwishi kubwa kumtoa Yusuf Hassan kutoka Idhaa ya Kiingereza ya BBC. Halafu tukaanza jitihada za kumtoa Mlamali kutoka Africa Now, gazeti alilolianzisha Enahoro, ili ajiunge nasi.

Hassan, siku hizi Mbunge wa Kamukunji, Nairobi, alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi katika gazeti la kila siku huko Baghdad, Iraq, kabla ya kujiunga na BBC.

Mimi nilikuwa na uzoefu wa kuhariri kurasa za Afrika na Mashariki ya Kati za jarida la Uingereza lililokuwa likichapishwa kila baada ya miezi miwili. Jarida hilo, Index-On-Censorship linahusika na uhuru wa kujieleza na wanafasihi wanaoingia matatani.

Mlamali pekee alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi kwenye gazeti la kila mwezi kama tulilokuwa tunalianzisha. Tulimbembeleza na kumbembeleza. Hatimaye alikubali na tukamwachia yeye, kwa sababu ya umri na uzoefu wake, awe mhariri wetu mkuu. Aliyetoa jina la gazeti jipya alikuwa Yusuf Hassan na muda si muda Africa Events likaingia mitaani Afrika nzima na nje ya Afrika likinguruma.

Peter Enahoro alinikasirikia kwelikweli kwa kumyang’anya Mlamali. Alinipiga simu na kunambia:

“Ahmed, ahsante sana kwa kutaka kutuua.” Akaibwaga simu.

Pamoja na umaarufu alioupata Africa Events wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC wakifurahikiwa sana na makala yake kwenye kipindi cha ‘Barua Kutoka London’.

Tangu aondoke Unguja hakurudi. Ingawa mwenyewe hakusema, inaweza kuwa sababu ni uonevu aliofanyiwa wa kutiwa jela bila ya kufanya kosa.

Atakumbukwa kwa mengi yakiwa pamoja na kazi zake za uandishi na tafsiri mbali mbali. Tafsiri yake ya “Things Fall Apart”, riwaya ya mwandishi wa Kinigeria Chinua Achebe, aliyoiita “Hamkani si shwari tena” ni tafsiri ya mwanzo ya Kiswahili ya kazi kubwa ya fasihi ya Kiingereza.

“Ikisiri ya Inkishafi” alichokiandika akitumia jina Muhamadi wa Mlamali kilichapishwa 1980 na shirika la uchapishaji vitabu la Longman huko Nairobi. Kwa “ikisiri” alikuwa na maana ya ufafanuzi. Na kitabu hicho kinaufafanua utenzi wa Kiswahili “Al Inkishafi” uliotungwa na Sayyid Abdallah bin Ali Nasir wa Lamu baina ya mwaka 1810 na 1820.

Kwa vile lugha aliyoitumia Mlamali katika ufafanuzi wake ni ya “babu kubwa” nikimtania kwamba panahitajika kitabu kingine chenye jina la “Ikisiri ya Ikisiri ya Inkishafi.”

Tukiviweka kando vitabu hivyo viwili vyote vingine alivyovifasiri vinahusika na dini. Miongoni mwavyo ni vya Habib Ali al Jifri, Imam Abdullah Alawi al Haddad na vya Al Habib Ahmad Mash-hur al Haddad. Pia ameandika kwa Kiingereza kitabu cha wasifu wa Al Habib Ahmad bin Zayn al Habshi Naf’an.

Mshairi mmoja wa Tanga, Hassan R. Hassan, aliposikia tu kuhusu kifo cha Mlamali alitunga shairi lifuatalo la beti tano alilolipa anuwani ya “Tumefiwa Waswahili”:

“Ai! Yabidi ninene, imenishinda nafusi

Msiba huu muone, ni mzito si mwepesi

Yu wapi tena mwengine, wa kuongoza kikosi

Aketi pa Mlamali, mpenzi wa Kiswahili

***

Yeye alikuwa bingwa, lugha aliihandisi

Hojaze hazikupingwa, alikuwa mdadisi

Watajwapo hakutengwa, alitajika farisi

Katutoka Mlamali, mpenzi wa Kiswahili

***

Isilamu yake dini, hakuitia mkosi

Alisoma yakini, akasomesha unasi

Hatunaye duniani, nani pake ajilisi?

Awe kama Mlamali, mpenzi wa Kiswahili

***

Kifoche kubwa ajali, tumeondokewa sisi

Na mtu aliye ghali, muungwana si mtesi

Ninakuomba Jalali, mpe mema majilisi

Akae pa watu wema, mpenzi wa Kiswahili

***

Beti tano kaditama, hapa ninasema basi

Moyo wangu waniuma, kwa zito liso kiasi

Shime tusirudi nyuma, tuliobaki ni sisi

Tumuenzi Mlamali, mpenzi wa Kiswahili”



Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter😡ahmedrajab
 
Poleni wafiwa, lakini mleta mada, huu uzi umekuwa mrefu mno
 
Hayo ndio mambo ya Barazani ndugu yngu bila shaka ww ni mwenyeji wa Bara sie Waswahili ndio mambo yetu ndugu yngu...
Ahsante, nimepakia gari bila kujua mwelekeo wake. Enjoy you stay
 
Hongera sana MoSaid, huwa inaburudisha sana kusoma makala zako. Mwenyezi Mungu akujalie nguvu na nafasi uendelee kuweka mambo sawa katika historia yetu, na uendeleze hayo mapambano kwa kutumia silaha hiyo ya kalamu. Nimecheka sana uliponikumbusha hadithi ya "Mzee wa Bahari", na kwa kweli nakubaliana na wewe kwamba viongozi wetu wa Afrika wamefanana sana na mzee huyo dhalimu.

Mimi ni Mkristu mzuri tu lakini najua lulu ninapoiona.

Mwenyezi Mungu pia asikie sala yako kumuombea huyo Mwalimu wako wa masafa, Mohamed Mlamali Adam. Amina.
 
Uandishi wa Ahmed Rajab kwenye kueleza tukio huwa fasaha na wenye mtiririko mzuri. Hauweki ubinafsi wa 'ukubwa' kwa kujificha hata kama kuna pahala dhahiri ameshiriki au kumshika Mtu mkono.

Kwa upande wa Mohammed Said, naye ni mwandishi mzuri lakini mara nyingi huongeza mistari mingi pasi sababu au kuonekana zaidi kwenye maandishi kuliko anayefanyiwa taazia. Hapa utaona kuna wakati ukiwa unasoma ukifika katikati unaweza kusahau kama hii ni taazia ya Mtu flani tena wa kutajika.

Huu ni mtazamo wangu

Rip Mzee Mlamali.
Nimekumbuka enzi za Bbc nikiwa na umri mdogo



Sent from my SM-G532F using JamiiForums mobile app
 
Kila nafsi itaonja umauti,Apumzike kwa Amani Mohamed Mlamali.
 
Uandishi wa Ahmed Rajab kwenye kueleza tukio huwa fasaha na wenye mtiririko mzuri. Hauweki ubinafsi wa 'ukubwa' kwa kujificha hata kama kuna pahala dhahiri ameshiriki au kumshika Mtu mkono.

Kwa upande wa Mohammed Said, naye ni mwandishi mzuri lakini mara nyingi huongeza mistari mingi pasi sababu au kuonekana zaidi kwenye maandishi kuliko anayefanyiwa taazia. Hapa utaona kuna wakati ukiwa unasoma ukifika katikati unaweza kusahau kama hii ni taazia ya Mtu flani tena wa kutajika.

Huu ni mtazamo wangu

Rip Mzee Mlamali.
Nimekumbuka enzi za Bbc nikiwa na umri mdogo



Sent from my SM-G532F using JamiiForums mobile app
nadhani sababu ni kwamba Mohamed Said ana moto wa volcano unatokota ndani yake. anajitahidi sana kuwa OBJECTIVE lakini hapa na pale ndimi za moto zinapenya na kuonekana mdomoni mwake. ukimwelewa, utafurahia maandishi yake
 
Mbona mnapenda kugawa sana watu?
Hamna mchango wa Waislam wala Wakristo, kuna mchango wa Watanzania
Kwa watu waliokomaa, wala sioni tatizo kuongelea Waislamu kama Jumuiya ya watu, yenye tamaduni zake na ada zake. mimi niliye Mkristu tena wa kutosha tu, siogopi kamwe. ni vizuri kuwajua wenzio ili mwende sawa.
 
Du!! mbona mimi nimeona fupi mno kwa utamu ule?? sisi tuliozoea kusoma vitabu kama THE CARPET BAGGERS, ANNA CARENINA, WAR AND PEACE, hapa angalau tunakata kiu

Sawa. Yalikuwa mawazo yangu tu. Si lazima tufanane kimawazo.
 
Sawa. Yalikuwa mawazo yangu tu. Si lazima tufanane kimawazo.
Kweli kabisa, na mimi lengo ni kukupa tu mtizamo mwingine, ili usifikiri kwamba tunafanana wote. Ila unaweza kujifunza kufurahia vitu virefu. vina raha yake ati. hasa kama siyo ugoro au MAPAMBIO kama tulivyozoea kuyasikia siku hizi kusifia viongozi kila kukicha.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom